Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
Wakati bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17 iliyopitishwa bungeni mjini hapa juzi, imeshuka kwa Sh. bilioni 4.6 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka huu ambayo ni Sh. bilioni 24.957, Bunge limetaarifiwa na wizara hiyo kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, haitalipa tena mishahara ya mkocha hao.
Akihitimisha mjadala wa makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha, Waziri Nape Nnauye aliliambia Bunge mjini hapa juzi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imechukua uamuzi wa kutolipa mishahara ya makocha wa timu za taifa baada ya kubaini kuwa michezo iliyopo nchini ni mingi.
Alisema jukumu la kulipa mishahara ya makocha wa timu za taifa litabaki kuwa la vyama vya michezo husika.
"Ni kweli Serikali ya Awamu ya Nne ilikuwa inalipa mshahara ya kocha wa timu ya taifa ya mpira wa miguu. Uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kutolipa mshahara huo," alisema na kufafanua zaidi:
"Kwa sababu michezo iko mingi katika nchi yetu na sisi hatukuona busara ya kulipa kwa kocha mmoja na kuiacha michezo mingine. Kwa hiyo, uamuzi huu umeshapita, ni kazi ya vyama vya michezo. Serikali tutaviwezesha kuwatengenezea mazingira mazuri vyama vya michezo vipate uwezo wa kupata mapato ya kulipa makocha wake badala ya serikali kubagua na kulipa makocha wachache na michezo mingine ikaachwa nje ya wigo."
Waziri huyo alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) kuhoji wakati wa mjadala wa bajeti hiyo kwanini serikali haijalipa mishahara ya Kocha wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa zaidi ya Sh. milioni 200 ilhali Bunge liliidhinisha fedha za mshahara wa dola 12,500 kwa mwezi katika mwaka huu wa fedha (2015/16).
SAKATA TFF, TRA
Katika hatua nyingine, Nape alisema mgogoro kati ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) uko mbioni kumalizika baada ya serikali kubaini kuwa shirikisho hilo halihusiki na ukwepaji wa kodi unaolikabili.
Hivi karibuni TRA ilifunga akaunti zote za TFF na kukamata magari matano ya shirikisho hilo kwa maelezo kuwa shirikisho hilo limekwepa kodi ya Sh. bilioni 1.6 ambazo zilitokana na kutokatwa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika mechi ya Taifa Stars dhidi ya Brazil iliyoingiza Sh. bilioni 1.8 kwenye Uwanja wa Taifa 2010 pamoja na kutokatwa kodi ya PAYE katika mishahara ya makocha wa Stars; Mbrazil Marcio Maximo na Wadenmark Jan Poulse na Kim Poulsen.
Kwa mujibu wa Nkamia aliyeliibua sakata hilo bungeni juzi, TRA imechukua fedha zote zilizokuwamo kwenye akaunti za TFF kiasi cha Sh. milioni 407 na kwamba deni lililobaki ni Sh. bilioni 1.16.
Akitoa ufafanuzi kuhusu sakata hilo, Nape alikiri serikali inapaswa kulaumika kwa kutokata fedha za PAYE katika mishahara ya makocha ambao walikuwa wanalipwa na Hazina. "Tatizo ni la serikali. Mshahara ulikuwa unalipwa na Hazina, TFF na Hazina walitegeana kukata kodi ya PAYE.
TRA anamjua mteja wake ni TFF ndiyo maana imekuwa ikimfuata mara kwa mara na kuchukua fedha. Hata pesa za mechi ya Brazil, TFF haihusiki. Kulikuwa na kamati iliyoundwa kuratibu mechi hiyo (kamati hiyo ilikopa Sh. bilioni tatu NMB kufanikisha mechi hiyo). Tumekubaliana aliyepaswa kuilipa, ailipe na serikali inalisimamia vyema jambo hili," alieleza zaidi Nape.
Source: Nipashe