SERIKALI ya Rais Jakaya Kikwete imeshindwa kuanza kulipa madeni ya walimu kuanzia Desemba mwaka huu kama ilivyoahidi, Tanzania Daima Jumatano imebaini.
Endapo serikali itashindwa kulipa madeni hayo hadi Desemba 31, mwaka huu, walimu wametishia kuitisha mgomo nchi nzima hadi walipwe madai yao.
Hadi sasa walimu wanaidai serikali zaidi ya sh bilioni 48 ambazo iliahidi kuanza kuzilipa kwa awamu, na kwa kuanzia, mwezi huu iliahidi kulipa sh bilioni 20.
Ahadi hiyo imekuwa ikitolewa kwa nyakati tofauti na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo na hivi karibuni aliifafanua tena wakati wa mahafali ya 47 ya Chuo cha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), ambapo wahitimu wengi ni walimu.
Katika mahafali hayo, Waziri Mulugo alisisitiza kuwa kuanzia Desemba, serikali itakuwa imelipa sh bilioni 20 kati ya 48, sawa na asilimia 44, inazodaiwa na walimu na sh bilioni 28 sawa na asilimia 56, zitalipwa mapema mwakani.
Kwa mujibu wa naibu waziri huyo, malipo hayo yangeingizwa kwenye mishahara wa walimu hao Desemba mwaka huu.
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa ahadi hiyo ni sawa na changa la macho kwani hakuna mwalimu aliyeanza kulipwa kama ilivyoahidiwa na serikali.
Baadhi ya walimu waliozungumza na gazeti hili, walisema hawakuona nyongeza yoyote ya fedha kwenye akaunti zao kama walivyoahidiwa.
"Nilimsikia naibu waziri akikaririwa mara mbili kwamba madeni ya walimu yanaanza kulipwa mwezi huu. Hadi sasa hakuna aliyelipwa," alisema mwalimu mmoja wa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano kwa njia ya simu jana, Katibu wa Chama cha Walimu nchini (CWT), Gratian Mukoba, alisema serikali imeamua kuwachezea walimu mithili ya watoto wadogo.
"Alisema kila wakati imekuwa ikiahidi inalipa, lakini hailipi. Kwa mfano walituambia wataanza kutulipa Novemba, ilipofika wakahamisha deni hadi Desemba, nayo hakuna kitu. Kwanini watuchezee wakati hizo ni hela zetu?" alihoji Mukoba.
Kwa mujibu wa Mukoba ambaye hakupenda kutoa msimamo wa CWT, alisema kuwa siku chache zijazo, watatoa msimamo mzito dhidi ya Serikali kwani hawaoni sababu za kudang'anywa kama watoto.
"Kwanza hela tunazodai ni zetu, zilitokana na makosa yao wakati wa kulipa mishahara maana kama ulitakiwa kulipwa sh 10,000 wao walikuwa wanalipa sh 1,000. Sawa wamehakiki, wameona walikosea, wanachopaswa kufanya ni kuturudishia fedha zetu na si kuhamisha deni kila wakati," alisema Mukoba.
Vyanzo vyetu vya habari kutoka Wizara ya Fedha na Uchumi, vilirejea kauli ya mara kwa mara ya hivi karibuni kuwa serikali haina fedha kiasi cha kushindwa kulipa mishahara kwa wakati.
Habari zaidi zinasema kuwa serikali haina fedha kwani hadi sasa imeshindwa hata kulipa ruzuku ya vyama, kikiwamo Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuvifanya vishindwe kuendesha shughuli zao.
Kabla ya Waziri Mulugo kutangaza tarehe ya kuanza kulipa madeni ya walimu, CWT ilikutana na serikali na kukubaliana kuanza kulipa madeni hayo wakati wowote.
Wakati walimu wakicharuka walipwe madeni yao, kwa upande wake serikali iko taabani kifedha kwani haina uwezo wa kuajiri watumishi wapya wala kupandisha vyeo wale waliopo.
Kutokana na ukata huo, tayari imeagiza ajira zote serikalini katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 zipunguzwe kwa asilimia 50. Vilevile upandishaji vyeo upunguzwe kwa kiwango kilekile.
Kwa hatua hii, serikali inabadilisha maamuzi ya Bunge lililoidhinisha mapato na matumizi yake Juni mwaka huu.
Serikali imekiri kutokuwa na uwezo wa kutekeleza bajeti iliyopitishwa na Bunge, kuwa na vipaumbele tofauti na mashaka na vyanzo vyake vya mapato.
Utekelezaji wa hatua hiyo ya serikali ulianza rasmi Novemba mwezi uliopita.
Waraka wa serikali umesainiwa na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejementi ya Utumishi wa Umma, Habu Mkwizu na kupelekwa kwa makatibu wakuu wote wa wizara, wakuu wa idara na taasisi zake nyingine.
Matokeo ya uamuzi huu, waraka unaeleza: "Ni kwamba kila mwajiri sasa atalazimika kuandaa upya mahitaji yake ya ikama (taratibu za ajira na malipo) kwa kuzingatia ukomo uliorekebishwa wa bajeti uliotolewa na wizara ya fedha kwa mwaka 2011/12."
Kila mwajiri amepelekewa jedwali la viwango vya ajira mpya, mishahara na nyongeza; na kutakiwa kufuata mkondo huo wakati wa kuwasilisha maombi mapya ya vibali vya ajira mpya kwa mwaka huu wa fedha.
Waraka unaagiza waajiri kuweka kipaumbele katika kutenga "nafasi za kutosha kwa ajili ya wataalamu wa sekta za Elimu, Afya, Kilimo na Mifugo."
Aidha, upungufu huo wa kifedha, umeibua hofu ya kukwama kwa miradi ya maendeleo na ahadi nyingine zilizotolewa na Rais Kikwete wakati wa kampeni za urais muhula wa pili, zikiwamo ahadi za ujenzi wa barabara za ghorofa, ununuzi wa meli, viwanja vya ndege, bandari na reli.
|
|