TTCL yahitaji Sh bil. 322 kujikwamua
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 22nd December 2010 @ 23:15
ILI ijipanue na kupambana na ushindani wa kibiashara uliopo, Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), inahitaji mtaji wa zaidi ya Sh bilioni 322 na kwa kuanzia Sh bilioni 70, zinahitajika kwa haraka.
Pamoja na mtaji huo, pia kampuni hiyo inakabiliwa na changamoto sugu ya taasisi za serikali kutolipa huduma wanazozitoa hasa simu ambapo mpaka sasa inazidai taasisi za serikali pekee Sh bilioni 7.2.
Hayo yalibainishwa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Said Said alipojibu maswali ya waandishi wa habari wakati wa mkutano baina ya Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa na watumishi wa kampuni hiyo.
"Si kwamba hatuwezi kujiendesha, tunajenga minara, tunalipa mishahara, lakini ili kuweza kujipanua kibiashara tunahitaji Dola za Marekani milioni 230, lakini fedha hizo kwa kampuni yoyote ni nyingi, kwa uchache wake tukipata Dola milioni 50, tutapanuka katika soko," alisema Said.
Mkutano huo ni sehemu ya ziara ya Waziri huyo kutembelea idara na taasisi zilizopo katika wizara yake baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni.
Said alitoa ufafanuzi huo baada ya waziri awali kueleza kuwa mkutano wake na watumishi wa TTCL (waandishi hawakuwepo), umebaini kuwa kampuni hiyo pamoja na kufanya vizuri katika mawasiliano mpaka sasa, inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo madeni na mtaji.
"Nimefika hapa kufahamiana na wafanyakazi, lakini pia kupitia changamoto zilizopo na kuona namna ya kukabiliana nazo, matumaini ya shirika hili kwa serikali ni makubwa, shirika lina matatizo ya mtaji, lakini tayari suala hilo liko serikalini na utaratibu kupata fedha," alisema Profesa Mbarawa bila kufafanua zaidi.
Aidha, katika kufafanua hilo, Waziri huyo alisema pamoja na hitaji la mtaji pia taasisi za serikali zinadaiwa na kwamba utaratibu unafanywa ili katika kipindi kifupi kijacho madeni hayo yawe yamelipwa.
Hata hivyo, hakuweka wazi kipindi hicho pale alipoulizwa kwa madai kuwa fedha za serikali zina utaratibu wake.
Waziri huyo pamoja na kufafanua namna serikali ilivyoanzisha kitengo cha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) kinachojiendesha tofauti na TTCL, alizitaka kampuni za ndani na nje ya nchi kutumia mkongo huo ili kurahisisha mawasiliano na kuingiza taifa mapato.