Jindal Singh
JF-Expert Member
- Sep 9, 2015
- 1,857
- 1,538
SERIKALI ya Ujerumani imeipa Tanzania msaada wa ndege mbili kwa ajili ya kufanya doria za angani katika Hifadhi ya Serengeti na Pori la Akiba la Selous ili kudhibiti uwindaji haramu.
Msaada huu umekuja siku chache tu baada ya watu wanaodhaniwa kuwa majangili kuitungua helikopta iliyokuwa ikifanya doria kwenye maeneo ya Pori la Maswa, karibu na hifadhi Serengeti, na kumuua rubani huku msaidizi wake akijeruhiwa vibaya. Majangili hao pia waliua tembo watatu na kunyofoa meno ya wanyama hao.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alikabidhiwa rasmi moja ya ndege hizo, aina ya ‘Aviat Aircraft Husky A-IC’ na Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Konchake katika eneo la Seronera, ndani ya Mbuga ya Serengeti ambayo ni ya pili kwa ukubwa nchini.
Akizungumza katika makabidhiano hayo jana, Balozi Konchake alisema nchi yake imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa masuala ya uhifadhi duniani yanatiliwa umuhimu na kwamba zaidi ya Dola za Marekani milioni 300 zimewekezwa kwa shughuli hizo pekee.
Ndege hizo mbili zina thamani ya Sh bilioni 1.2 na tayari zimeanza kufanya kazi, na watu wanne watuhumiwa wa ujangili wamekamatwa wiki hii, kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu wa Serengeti, William Mwakilema.
Profesa Maghembe alisema zaidi ya ndege hizo, Serikali ya Ujerumani pia imeisaidia Tanzania Sh bilioni 80 kwa ajili ya masuala ya uhifadhi katika kipindi cha miaka mitano ijayo, ikiwemo kuanzishwa kwa Mamlaka maalumu ya Ulinzi wa Wanyamapori (TAWA).
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Dk Allan Kijazi aliishukuru Serikali ya Ujerumani kwa ndege hizo na misaada mingine huku akibainisha kuwa ilikuwa vigumu kufanya doria ndani ya eneo la Serengeti lenye ukubwa wa kilometa za mraba 14,700 kwa kutumia magari au askari wa miguu pekee, ila sasa kwa uwepo wa ndege hizo kazi imerahisishwa.
Chanzo: HabariLeo