Serikali ya Magufuli inaimarisha ndoa za vigogo!

Serikali ya Magufuli inaimarisha ndoa za vigogo!

Interest

JF-Expert Member
Joined
Apr 11, 2015
Posts
3,434
Reaction score
7,091
SOTE tulishuhudia timuatimua Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), vilevile lile agizo la Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa kwenda kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu la kukamata vigogo na mibuyu.
Hiyo mibuyu na vigogo, ni wale wale waliotengeneza mpango wa kutoroshwa kwa makontena 349 bandarini bila kulipiwa kodi na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 80.

Baada ya kushuhudia hayo yakitokea, nikamkumbuka mshkaji wangu, Mbunge wa Jimbo la Dilitown, Mheshimiwa sana Mchongo Bilioni-Si-Kitu, sisi huwa tunamwita Mutu-Ya-Pesa, si unajua upambe tena? Basi nilimpigia, mazungumzo yetu yalikuwa hivi-;

MHE BILIONI-SI-KITU: Haloo Luqman.

LUQMAN: Ndiyo mimi hapa, vipi Mutu ya Forbes, Mutu ya Nyota Tano, upo tajiri?

MHE BILIONI-SI-KITU: Nipo, nalipenda sana lile jina lako la The Gladiator.

LUQMAN: Unalipendea nini mheshimiwa?

MHE BILIONI-SI-KITU: Nataka niwe nalitumia bungeni wakati wa serikali ya Magufuli. Nitakuwa mnoko sana bunge la 2015-2020.

LUQMAN: Unoko wa nini wakati nakuaminia utakuwa waziri? Tena kati ya wizara zilezile ambazo uliniambia unataka mojawapo ili utishe katika serikali ya Rais John Pombe Magufuli.

MHE BILIONI-SI-KITU: Mimi uwaziri?

LUQMAN: Wewe hapo mheshimiwa, kwani nipo nazungumza na nani hapa?

MHE BILIONI-SI-KITU: Niwe waziri chini ya huyu Magufuli na Waziri Mkuu Majaliwa?

LUQMAN: Ndiyo hivyohivyo mheshimiwa, si unajua HapaKaziTu?

MHE BILIONI-SI-KITU: Hapana, mimi ubunge unanitosha sana.

LUQMAN: Umekuwaje leo Mutu ya Singita Hotel kila wikiendi? (Singita ni hoteli ghali na bora duniani, iliyowahi kushika namba moja kwa ubora ulimwenguni kwa miaka miwili mfululizo, ipo ndani ya Hifadhi ya Serengeti).

MHE BILIONI-SI-KITU: Maisha ya uwaziri yatakuwa magumu mno, binafsi sitaweza kufanya kazi na hao watu. Kasi yao inatisha halafu wanapenda sana sifa.

LUQMAN: Ila mheshimiwa Bilioni-Si-Kitu uliniambia unaitaka sana Wizara ya Uchukuzi ili ufanye yako kati ya mwaka 2015-2020, huitaki tena hiyo wizara?

MHE BILIONI-SI-KITU: Sikiliza Luqman, nimekuwa waziri kuanzia utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, akafuata Benjamin William Mkapa kisha Dk Jakaya Mrisho Kikwete, nimetosheka. Sitaki tena uwaziri, halafu huu ni muda wa kuwatumikia kwa nguvu sana wapigakura wangu wa jimbo langu la Dilitown.

LUQMAN: Ila sijapenda, wewe ni bonge la waziri. Halafu huwa unapendeza sana unaposimama mbele pale bungeni, unajibu maswali ya wabunge kwa pozi, na unapowasilisha hoja zako au kuzitetea na hata kuwasilisha miswada, huwa unapatia ile mbaya. Upo juu, kubali uwaziri.

MHE BILIONI-SI-KITU: Luqman wewe umenijua nikiwa mbunge na waziri, mimi nina familia yangu. Hawa jamaa Magufuli na Majaliwa hawana maana hata kidogo, wao ukifanya mpango wa kula hata tu-bilioni 10 tu, wanakuumbua, wanakuaibisha kisha wanakupeleka jela. Nani anataka hayo? Mimi nina familia na napenda kuwa uraiani.

LUQMAN: Sasa hapo kama nakupata hivi, kumbe huutaki uwaziri kwa sababu lazima ufanye ufisadi na utafungwa katika utawala wa Magufuli?

MHE BILIONI-SI-KITU: Acha maswali ya kitoto, unauliza tai kwa Mnyasa? Muulize hata Profesa Mpigaji, mbona alikuwa anaitamani Wizara ya Viwanda na Biashara baada ya Dk Abdallah Kigoda kufariki dunia lakini juzi kapigiwa simu akaulizwa apewe wizara hiyohiyo lakini alikataa kabisa. Mpigie umuulize, wewe si unaelewana naye?

LUQMAN: Sawa, nampigia kisha nitarudi kwako, siamini Mutu ya Kula Raha Singita Hotel na watoto wazuri kila wikiendi, leo hutaki uwaziri.

PROFESA MPIGAJI: Profesa hapa, nani wewe?

LUQMAN: Mheshimiwa Profesa, ni mimi hapa Luqman Maloto a.k.a The Gladiator.

PROFESA MPIGAJI: Ooh, The Gladiator, nipo hapa naandaa nondo za kuwashughulikia mawaziri wa Magufuli bungeni. Unajua hili Bunge la 11 chini ya Spika Job Ndugai na Naibu Spika Dk Tulia Ackson, nitatisha sana kwa mijadala ya kuisema serikali. Nitakuwa mwiba kuliko Tundu Lissu na Zitto Kabwe wa upinzani.

LUQMAN: Profesa kabla hujaenda mbali, nimeambiwa umepigiwa simu upewe Wizara ya Viwanda na Biashara umekataa, kwa nini?

PROFESA MPIGAJI: Wewe nani kakwambia hizo habari?

LUQMAN: Profesa wewe ni mtu wangu wa karibu na unajua mzunguko wa urafiki wetu, unapomwambia neno mmoja wa marafiki zetu halikawii kunifikia.

PROFESA MPIGAJI: Ni kweli nilipigiwa simu ila nilikataa.

LUQMAN: Ulikataa kwa nini? Wizara ya Viwanda na Biashara ni bonge la wizara, wengi wanaikimbilia. Wewe unaikataa kwa nini?

PROFESA MPIGAJI: Luqman umewahi kuumwa jipu?

LUQMAN: Nilishaumwa majipu mpaka mitaani nikawa naitwa mzee wa majipu.

PROFESA MPIGAJI: Unajua maumivu ya jipu hasa?

LUQMAN: Nayajua sana Profesa, kwani vipi?

PROFESA MPIGAJI: Unapokamuliwa jipu wewe huwa unafurahi?

LUQMAN: Nifurahi? Inauma hiyo Profesa!

PROFESA MPIGAJI: Kwa hiyo Luqman unataka mimi ndiyo niwe jipu, nitumbuliwe, halafu wewe ufurahi.

LUQMAN: Sina maana hiyo Profesa, wewe siyo jipu na huwezi kutumbuliwa.

PROFESA MPIGAJI: Usinitengeneze, mimi najijua mwenyewe. Ile wizara siiwezi chini ya Magufuli. Na kwanza siwezi wizara yoyote chini ya Magufuli. Mimi nataka ubunge tu, sitaki uwaziri tena.

LUQMAN: Profesa mbona unafanya uamuzi mgumu sana? Kubali uwaziri tafadhali.

PROFESA MPIGAJI: Luqman, kwa miaka mingi nikiwa waziri najua udhaifu wangu. Shida yangu ni moja, napenda sana teni-pasenti. Kila mkataba wa wizara lazima nitishe. Halafu mimi ni bonge la fisadi.

LUQMAN: Wewe ni fisadi, duh! Mpaka unajitaja Profesa.

PROFESA MPIGAJI: Hii nakwambia kwa sababu wewe ni rafiki yangu, najua huwezi kuwaambia watu wengine. Nina magari ya kifahari 66, na kila moja bei yake inaanzia shilingi milioni 400, hiyo ni thamani kabla shilingi haijaporomoka mpaka kuzidi shilingi 2,200 kwa dola moja.

LUQMAN: Profesa kumbe urafiki wetu hauna maana, yaani utajiri wote huo hata hatukumbakani? Mimi nakwea daladala, wewe magari peke yake thamani yake karibu shilingi bilioni 27?

PROFESA MPIGAJI: Tulia kwanza Luqman, nina majumba kwenye fukwe za Bahari ya Hindi kwa harakaharaka sikumbuki idadi, ila hazipungui 35, na kila moja thamani yake siyo chini ya shilingi bilioni tatu. Unadhani mali zote hizo ningezipata wapi bila kufanya ufisadi?

LUQMAN: Kwa hiyo Profesa? (akanikatisha).

PROFESA MPIGAJI: Usiwe na haraka Luqman. Sikiliza, mimi sifanyi biashara, wala sijawekeza kwenye soko la hisa kusema labda kuna gawio huwa napata, la hasha! Utajiri wangu umetokana na siasa, uwaziri umenifanya nile bata sana, ila kwa sasa hapana. Huyu Magufuli na mwenzake watakuja kuniumbua bure, halafu wapate sababu ya kunifilisi ?tumali twangu twote?.

LUQMAN: Profesa mimi nakuaminia, achana na mambo ya kupiga dili, wewe piga kazi kwa kasi ya HapaKaziTu.

PROFESA MPIGAJI: Luqman wewe unanijua kuliko ninavyojijua mimi mwenyewe? Mimi najijua zaidi, tatizo langu nikioni fursa ya dili siwezi kuacha. Ndiyo maana nimeamua kujihami kwa kuukataa uwaziri, maana nikipiga tu dili nitashtukiwa, Magufuli na Majaliwa wanafuatilia nyendo za watumishi serikalini utadhani wao ndiyo makachero wa Usalama wa Taifa. Naogopa sana, sitaki. Sitaki kuwa jipu!

LUQMAN: Dah, nimesikitika sana kwa uamuzi uliochukua. Unaogopaje kuwa waziri?

PROFESA MPIGAJI: Wewe sikitika tu, na kama urafiki wako kwangu ulisababishwa na uwaziri wewe achana na mimi. Ila kama ni mshkaji wangu wa damu basi tuendelee. Tena inabidi unisapoti ili ubunge wangu uende vizuri. Halafu nikwambie kitu?

LUQMAN: Niambie Profesa.

PROFESA MPIGAJI: Katika kipindi cha kati ya mwaka 2015-2020, maisha yatakuwa magumu sana, maana sitakuwa naingiza fedha kama zamani, kwa hiyo hata nyumba ndogo zangu nimeanza kuzipunguza, nina nyumba ndogo 44, nina makuwadi 21 Dar na wawili kila mkoa, makuwadi wote hao huwa nawalipa mishahara kila mwezi, nyumba ndogo nazihudumia kila siku.

LUQMAN: Profesa sikuwezi, wewe kiboko, nasema hivi wewe ni chiboko na siyo chibuku!

PROFESA MPIGAJI: Sikiliza, kazi ya hao makuwadi ni kunitafutia watoto wazuri wa kike kwa ajili ya kupumzika nao kila wanapopatikana. Kimsingi nilikuwa natumia fedha nyingi kwa ajili ya starehe ya wanawake na nyingine. Makuwadi wangu wanamiliki majumba na wanaendesha magari kwa fedha za serikali. Nyumba ndogo zangu zote zilizinunulia nyumba na magari. Halafu mimi ni mhongaji mzuri sana.

LUQMAN: Unataka kuniambia hizo starehe zote hizo ulikuwa unazifanya kwa fedha za serikali?

PROFESA MPIGAJI: Mbona unauliza kama unanichimba? Siri yako Luqman, baada ya kuona kasi hii ya Magufuli kisha nikaukataa uwaziri, sasa hivi nawekeza upendo wangu wote kwa mke wangu. Si unaona sasa hivi nipo nyumbani? Nina wiki mbili sijalala hoteli, sijasafiri na mapema sana narejea nyumbani baada ya kazi. Siku hizi nampenda sana mke wangu.

LUQMAN: Sasa hapo Profesa umenipa kitu, kumbe hii kasi ya Magufuli ya kudhibiti ufisadi kwa upande mwingine inasaidia sana kuimarisha ndoa za vigogo.

PROFESA MPIGAJI: Kabisa, Magufuli anasababisha vigogo tusipate fedha za fujo, kwa hiyo hatutaweza kuhonga kwa fujo. Na wanawake wa mjini wanapenda fedha, usiwapowahonga hakuna mapenzi. Hapo vigogo tunakuwa hatuna ujanja zaidi ya kurejea kwa wake zetu na kudumisha upendo na ndoa.

LUQMAN: Kama ni hivyo, naomba Magufuli awe rais miaka yote, nikiwa na maana hata Magufuli akimaliza muda wake, waje wengine kama yeye ili nchi inyooke na familia ziwe imara. Maana vigogo wamekuwa na kawaida ya kuvunja ndoa za watu, wanawarubuni wake za watu kwa fedha mpaka ndoa zinavunjika.

PROFESA MPIGAJI: Wewe Luqman umetumwa? Hii miaka mitano ya Magufuli naona kama jehanam, halafu wewe unataka iwe hivihivi miaka yote? Magufuli ni mzuri kwenu wananchi wa kawaida, ila kwetu sisi vigogo Magufuli hafai. Ila nataka nikupe siri moja.

LUQMAN: Niambie Profesa.

PROFESA MPIGAJI: Bila kuacha kitu ni kwamba wake zetu sisi vigogo wamekuwa wakiteseka sana. Tumekuwa tukisingizia wingi wa kazi kufanya fujo na wanawake mahotelini mpaka tunasafiri nao nje. Safari za nje nazo zimepigwa marufuku. Kwa muda mrefu mfumo wa utawala uliwafanya wake zetu kukosa amani ya kuwa mama wa familia, ila kwa sasa amani itarejea.

LUQMAN: Hili somo safi sana. Tena mnatakiwa muwanyenyekee sana wake zenu.

PROFESA MPIGAJI: Unajua usimuone kigogo kavaa suti, kwenye gari la bei mbaya mali ya serikali ukadhani ni mtu wa maana, mimi nakwambia wewe rafiki yangu. Mfumo wa kujichotea fedha serikalini kama kuvuna matunda kwenye shamba la bibi ulisababisha tuwe wendawazimu, tukachanganyikiwa, mapenzi ya familia yalipotea.

Ikafikia hatua mpaka watoto wetu waliona tulivyokosa heshima kwa mama zao. Magufuli na Majaliwa wanatunyoosha, mimi nimeshanyooka. I love my wife! Nyumba ndogo sitaki, sina pesa za kuwahonga. Hapa nataka wiki ijayo niwaambie makuwadi wangu wote tusijuane, na nyumba ndogo zangu zote zisinijue. Magufuli amenipa nidhamu ya kuongeza upendo kwa mke wangu. Luqman eeeh!

LUQMAN: Naam mheshimiwa Profesa.

PROFESA MPIGAJI: Naomba usimwambie mtu, katika hizi siku mbili nipo karibu na mke wangu, naona hata tabasamu lake limerejea. Halafu nimegundua mke wangu ni mzuri kuliko wale viruka njia waliokuwa wanani-keep busy bila mpango wowote. Nina bonge la mke, bonge la mama watoto, bonge la mama wa familia!

Hivyo ndivyo mazungumzo yangu na Profesa Mpigaji yalivyoisha. Katika kitabu changu cha simu (phonebook) nina rafiki mwingine ambaye ni kigogo, huyu ni Mheshimiwa Chivivu. Ikabidi naye nimpigie simu kupata maoni yake.

CHIVIVU: Kipindi chote cha kampeni hukunipigia simu, ulidhani nitakosa ubunge nini?

LUQMAN: Siyo hivyo mheshimiwa. Mimi nilijua tu lazima utusue, hakuna anayeweza kukutoa jimboni kwako. Vipi mambo ya uwaziri?

CHIVIVU: Uwaziri wa nini?

LUQMAN: Uteuzi, kwani hujapigiwa simu?

CHIVIVU: Nilipigiwa simu siku moja. Rais Magufuli alikuwa kwenye kikao na Majaliwa pamoja na Suluhu Hassan. Kiukweli nilijibu palepale kuwa afya yangu siyo nzuri, siwezi mikikimikiki ya uwaziri kwa kipindi hiki.

LUQMAN: Pole sana mheshimiwa, kumbe unaumwa?

CHIVIVU: Teh teh teh teh!!! Naumwa wapi? Niliwajibu tu vile ili kuwakatalia kisiasa, Magufuli ameharibu sana kufuta safari za nje. Unajua uwaziri bila safari haunogi.

LUQMAN: Ina maana umeukataa uwaziri kwa sababu tu ya safari.

CHIVIVU: Zipo sababu nyingi, unajua mimi asili yangu ni mvivu kama jina langu lilivyo. Sasa hizo hekaheka za serikali ya Magufuli nitaziweza wapi? Si bora nibaki tu na ubunge wangu kuliko kwenda kuumbuliwa na hao wapenda sifa Magufuli na Majaliwa?

LUQMAN: Mbona watu wanauogopa uwaziri katika Serikali ya Magufuli?

CHIVIVU: Kumbe wapo wengine pia wanaogopa! Sikiliza Luqman, hakuna mtu ambaye hajipendi. Kipindi cha nyuma uwaziri ulikuwa kuula, ila kwa hali iliyopo sasa ni kimeo, ukiwa waziri unabeba msalaba. Mfano mimi hapa, nikiwa waziri nilikuwa sifanyi kazi, majukumu yote nilikuwa namwachia Katibu Mkuu wa Wizara na naibu wangu ambaye naye alikuwa mvivu kama mimi.

LUQMAN: Sasa hapo kazi zilifanyikaje?

CHIVIVU: Hakuna kazi kufanyika, mtendaji alibaki kuwa Katibu Mkuu wa Wizara, mimi kazi yangu ilikuwa kutegea safari za nje, nasafiri na dogodogo kwenda majuu kula raha. Si unaona hata majibu nilikuwa sijibu vizuri bungeni? Ni kwa sababu kila kitu nilikuwa naandikiwa.

LUQMAN: Kweli wewe ni Chivivu, halafu kumbe unapenda dogodogo.

CHIVIVU: Siyo napenda dogodogo, nilikuwa napenda dogodogo, siku hizi nampenda sana mume wangu.

LUQMAN: Unataka kuniambia Magufuli amerejesha upendo wako kwa mumeo?

CHIVIVU: Sana, nampenda sana mume wangu. Tatizo humjui, ila ni bonge la handsome, uwaziri ulinifanya niwe namzidi kipato, kwa hiyo nikawa natumbua sana. Ila kwa sasa uwaziri siyo dili tena, pesa za kutumbua na dogodogo hazipo. Maslahi ya ubunge wangu nayatumia vizuri na mume wangu, tufanye maendeleo ya familia.

LUQMAN: Sawa mheshimiwa, sasa unaniachaje?

CHIVIVU: Nakuacha na hii, wale Magufuli na Majaliwa naona hawatumii macho ya kawaida. Nadhani wamepewa vioo vya jadi kutazama kila kinachoendelea serikalini. Kila kitu wanakiona. Wazee watakuwa wamewapa vioo vya kienyeji. Au wanatumia pembe ya nyati! Wanapiga ramli! Ukitegea kazi wanakuona, ukihujumu serikali wanakunasa, ukiiba wanakukamata. Mimi siyawezi hayo.

CHUKUA HII
Magufuli na Majaliwa wanafanya kazi kubwa sana. Ni hakika kuwa wanachokifanya kinapendwa zaidi na wananchi wa kawaida, kinachukiwa mno na vigogo ambao maisha yao yote yalitegemea mianya ya wizi serikalini.

Ni hakika kuwa Magufuli na Majaliwa wanahitaji kuongezewa ulinzi. Maana chuki dhidi yao ni kubwa. Wafanyabiashara wahuni wanaonufaika kwa mgongo wa watendaji wezi wana nguvu sana. Maana ukuaji wa utajiri wao umekuwa ukitegemea zaidi ukwepaji kodi. Hawa hawawapendi.

Ila tuendelee kuwatia moyo, maana wanafanya mambo mema kwa taifa letu. Tusiache kukubali ukweli kuwa kazi inayofanywa na Magufuli pamoja na Majaliwa, siyo tu kuwa inasaidia kudhibiti ufisadi bali pia inaimarisha ndoa za vigogo, maana watakuwa na nidhamu ndani ya familia zao. Mpunga unakata. Teh teh teh teh!

By Luqman Maloto
 
Katuni flan hivi ila bonge la ujumbe big up maloto.
 
Nimeipenda.Umenifumbua macho kwa kiasi fulani kwa sababu watu mtaani wanasema baraza la mawaziri linachelewa kutangazwa kwa sababu eti Magufuli anawachunguza sana wabunge kabla ya kuwateua katika baraza lake la mawaziri ili asijeteua mawaziri mizigo/Mafisadi/Wasio na maadili, kumbe ukweli unaweza kuwa baraza linachelewa kutangazwa kwa sababu kila anayeombwa kuteuliwa kuwa waziri anakataa.Hivyo baraza litachukua muda mrefu kabla ya kukamilika na kutangazwa.Tusubiri tuone.
 
Interest hiyo fasihi andishi mpaka uwe umezama kiasi ndo utajua kuna kipindi nipo sekondari hawa jamaa wa maigizo walikuwa na igizo lao tulikuwa kambi ya umiseta kila jioni tunawaona wanafanya mazoezi igizo halichekeshi wala halielewiki watu wakaenda kwa mwalimu kumwambia kama vipi watu wajiandae watengeneze igizo la kuchekesha ticha akakataa huwezi amini jamaa walitoboa kuanzia wilayani mpaka taifa wakaja kuwa washindi wa pili.
So fasihi ina uwanja mpana kwa wanauijua pamoja sana ndugu yangu INTEREST.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom