Naisoma360
JF-Expert Member
- Jan 23, 2015
- 821
- 491
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangwala.
Serikali inapanga kuajiri watumishi wa sekta ya afya zaidi ya 10,000 mwaka huu wa fedha 2015/16, ili kukabiliana na uhaba wa wakunga na wauguzi wa zaidi ya asilimia 51 nchini.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kingwala, alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya uuguzi na ukunga katika Chuo cha Aga Khan, ambacho kimefanyiwa ukarabati na kuwekewa vifaa vya kisasa kwa ufadhili wa Ujerumani kwa gharama ya euro milioni 1.2.
Alisema serikali inaendelea na jitihada za kutoa elimu ya ukunga na uuguzi kwa kuongeza wanafunzi wengi katika vyuo vya serikali na binafsi ili kukabiliana na uhaba wa watumishi hao pamoja na kuwapangia kazi pembezoni mwa mikoa yote nchini.
“Kwa mwaka huu tutatoa ajira zaidi ya 10,000, haijawahi kutokea ni kwa mara ya kwanza, pia tutahakikisha watumishi hawa tunawapeleka maeneo yote ambako hakuna watumishi ili kukabiliana na uhaba tulionao,” alisema.
Dk. Kigwangala alisema serikali pia inaendelea na jitihada za kushirikiana na wakunga wa jadi kwa kuwapa mafunzo ya kitaalam ili waweze kutoa huduma bora za ukunga na kupunguza uhaba wa watumishi hao nchini.
Naye Makamu wa Rais na Ofisa Mkuu wa Fedha wa Chuo cha Aga Khan, Al-Karim Haji, alisema katika kipindi cha miaka 10, chuo hicho kimetoa elimu kwa wakunga na wauguzi 600 nchini na 21,000 kwa nchi za Afrika Mashariki.
Alisema wauguzi wa elimu ya stashahada na shahada wanawapata kutoka kazini katika hospitali mbalimbali nchini na kwamba wanawapa ruzuku ya asilimia 80 ili kukabiliana na gharama za ada.
“Ufadhili tuliopewa na Ujerumani umewezesha ukarabati majengo, kununua vifaa vya kisasa vya kufundishia kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu inayotolewa na chuo hiki pamoja na kuzaliwa wauguzi wenye viwango na sifa ya kutoa huduma bora,” alisema.
Naye Waziri wa Uchumi na Maendeleo wa Ujerumani, Dk. Gerd Muller, alisema serikali ya nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana nchini na kuendelea kutoa elimu ya ukunga hadi vijijini badala ya kuishia mijini pamoja na kubadilishana uzoefu wa masuala ya uzazi baina ya nchi hizi mbili.
Alisema pia serikali yake imetoa euro bilioni 7 kwa ajili ya kuzuia ugonjwa wa polio kwa watoto nchini.
CHANZO: NIPASHE