Serikali isizibe masikio malalamiko, madai haya | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Serikali isizibe masikio malalamiko, madai haya

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by kilimasera, Apr 15, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Apr 15, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  Wiki iliyopita serikali iliwasilisha bungeni muswada wa kupitia katiba kwa nia ya kuundwa tume ikakayoratibu mchakato wa kupata Katiba Mpya na iliamua kutoa nafasi kwa wananchi na wadau mbalimbali watoe maoni yao.
  Mara baada ya kuanza kwa mchakato huo kumetokea ubishi mwingi, malalamiko na maneno mengi kuhusu udhaifu wa muswada huo.
  Katika maeneo yote kulikofanyika mikutano ya wananchi kutoa maoni, yaani ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, ukumbi wa shule ya Haile Sellasie Mjini Zanzibar na ukumbi wa Pius Msekwa Dodoma, kulitokea rabsharabsha baina ya wananchi na viongozi.
  Kwa upande wa Zanzibar walikwenda mbali kwa kuuchanachana muswada huo mbele ya Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, wakilalamika kuwa haukuzingatia hadhi ya nchi yao na hawakushirikishwa katika hatua za awali za uundwaji wake.
  Rabsharabsha zote hizi zinaonyesha kuwa serikali inapaswa kujipanga na kujiweka sawa ili kuhakikisha zoezi la ukusanyaji wa maoni linakwenda vizuri na malengo tarajiwa yanafikiwa.
  Kwa kuwa serikali imeitisha maoni ya wananchi ili Katiba Mpya itakayopatikana iwe na ridhaa yao, tunadhani lazima serikali itilie maanani yale yanayosemwa na wananchi ili kuepusha manungÂ’uniko siku za usoni.
  Serikali iwe sikivu, ichukue maoni ya wananchi kuhusu masuala yote yanayolalamikiwa, iyachambue kwa kina na kuyafanyia kazi ili mchakato wa maoni na hatimaye katiba itakayopatikana iwe na ridhaa ya wananchi kweli.
  Tunadhani hilo haliwezi kuwa jambo gumu kwa serikali kwani yenyewe ndiyo iliamua kuanzisha mchakato na kutoa fursa kwa wananchi washiriki katika mjadala wa kuundwa wa katiba yao baada ya vuguvugu la kudai Katiba Mpya kuanza kushika kasi nchini.
  Kwa kuwa serikali imeamua kufanya hivyo, basi kuna umuhimu kwa viongozi kuwa na utashi wa dhati wa kisiasa wa kuchukua maoni ya wananchi, kuyafanyia utafiti na kisha kuyajumuisha ikiwezekana kwenye muswada wa kuundwa kwa tume ya kuratibu mchakato wa Katiba Mpya.
  Bila serikali kuwa makini na kuchambua maoni ya wananchi kuhusu tume itakayoundwa ni dhahiri kazi yake itakuwa ngumu kwani wananchi wengi hawatakuwa na imani nayo kama ambavyo tayari imeonekana katika mijadala Tanzania Bara na Visiwani.
  Kuna mambo mengi ambayo wananchi wamekuwa wakilalamikia ndani ya muswada wa sasa kama vile madaraka ya Rais kutohojiwa na masuala ya Muungano, jambo ambalo limeonekana kuwakera wananchi wengi.
  Hata hadidu za rejea za muswada husika lazima ziwekwe wazi na zieleweke kwa wananchi walio wengi ili kurahisisha kazi ya tume itakayoundwa.
  Kwa kuwa serikali haikuwashirikisha wananchi wakati wa kuandaa muswada huu wa kuunda tume basi ni vyema isidharau maoni yao na badala yake iwe na dhamira ya dhati ya kuyasikiliza, kuyachambua na kuyajumuisha kwenye muswada huo.
  Kuna mambo mengi ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi na hata viongozi kuhusu Muungano, baadhi ya wananchi wa pande hizi mbili wanaona hawafaidiki na muungano huo hivyo hii ni fursa nzuri ya kuwaacha watoe yaliyo moyoni mwao.
  Ushahidi kuwa suala la Muungano linapaswa kujadiliwa ulijitokeza wakati wa mjadala wa Zanzibar ni nchi au si nchi mwaka mmoja tu uliopita kwani hadi baadhi ya mawaziri wa serikali ya SMZ walitoa kauli kali kwenye vyombo vya habari zikionyesha kuwa wanakerwa na muungano.
  Baadhi ya mawaziri walitamka kuwa wamechoka na kuendeshwa na serikali ya Muungano na wanataka Zanzibar iendeshe mambo yake kwa uhuru, yaani hawataki kuburuzwa na Bara.
  Kauli hizo zinadhihirisha kuwa kuna umuhimu wakati wa kuundwa kwa tume hii wananchi wakaachwa waseme yaliyomo mioyoni mwao kwani wao na baadhi ya viongozi wana dukuduku hivyo waachwe waseme.
  Wakati wa serikali kujifungia ndani na kufanya mambo bila kuwashirikisha wananchi umepita na tunatarajia serikali katika suala hili itawasikiliza wananchi kwa umakini na hatimaye kuchukua maoni yao ili katiba ichukue mambo wanayoona yana maslahi kwao.
   
Loading...