Serikali idhibiti mfumko huu wa bei | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Serikali idhibiti mfumko huu wa bei

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by kilimasera, Jan 5, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Jan 5, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  TUMESHTUSHWA na mfumko wa bei uliolipuka nchini siku za karibuni kwa kila kitu kupanda.
  Yalianza mafuta yakapanda, gesi nayo ikapanda, kabla ya kutangazwa kupanda kwa bei ya umeme na sasa hata kabla Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Summatra), haijaridhia kupanda kwa nauli za mabasi tayari wamiliki wameshapandisha wenyewe kwa maelezo kwamba mafuta yamepanda.

  Bidhaa nyingine zilizopanda kinyemela ni pamoja na vyakula, wakati wa kipindi cha sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, kilo moja ya nyama ilifikia hatua ya kuuzwa shilingi 7,000 kwa kilo.

  Bidhaa kama sukari, vinywaji baridi na kibaya zaidi hata wamiliki wa daladala jijini Dar es Salaam, nao wanafikiria kutaka kupandisha nauli za mabasi yao.

  Wachambuzi wa mambo ya uchumi mwishoni mwa mwaka jana, walichambua mwenendo wa hali ya uchumi na kubaini kuwa kuanzia mapema Januari mwaka huu, karibu kila kitu kitapanda na kusababisha kuongezeka kwa ugumu wa maisha. Na hicho ndicho kinachotokea sasa kabla hata ya mwezi huu kufika katikati.

  Tunachukua nafasi hii kuitaka serikali iuangalie mfumko huo wa ghafla wa bei vinginevyo hali itazidi kuwa mbaya kwa Mtanzania ambaye kipato chake bado kimebaki kile kile.

  Tunachukua nafasi hii kuitaka serikali itambue kuwa hali ya maisha ya Watanzania hata kabla ya kupanda kwa bidhaa hizo ilishakuwa mbaya na ongezeko la sasa la bei litazidisha makali ya maisha kwao.

  Hili ni jambo la hatari kwa usalama na utulivu wa taifa letu kwani tunaamini hakuna amani kama wananchi hawawezi kupata mahitaji yao muhimu kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, huku wachache wakimudu maisha kwa fedha za ufisadi.

  Tunaikumbusha serikali kutambua kwamba haijapandisha mishahara ya watumishi wake wa umma au wale wanaofanya kazi kwa watu binafsi.

  Kwa upande wa wakulima hali ndio mbaya kabisa maana hawana chochote mkononi achilia mbali kuongezeka kwa chochote ambacho wangekuwa nacho.

  Kwa sababu hiyo ni kumuumiza Mtanzania kumpandishia bei wakati pato lake halijapanda.

  Tunatambua kwamba kuna vitu ambavyo huongozwa na soko la dunia kama mafuta ambayo yaweza kuathiri bei ya vitu vingi nchini zikiwamo nauli na bidhaa na huduma zingine.

  Lakini serikali sikivu na inayowajali wananchi wake kwa kuzingati ukweli tuliousema hapo juu, inatakiwa kuchukua hatua kwa kupunguza kodi kwenye bidhaa adimu kama hiyo ya mafuta ili kushikilia bei yake isipande na kupandisha bei ya bidhaa zingine.

  Tunahitimisha kwa kuitaka serikali kuchukua hatua sasa ili kudhibiti upandaji huu wa bei kwa lengo la kupunguza ukali wa maisha, vinginevyo ahadi za maisha bora kwa kila Mtanzania iliyotolewa na viongozi wakati wa kampeni, haiwezi kutimia.
   
Loading...