Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,809
- 34,193
Asema uhuru wa kuamua nani wa kuwaongoza kama ulivyokuwa ukisisitizwa haupo
Zanzibar. Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad amesema hadhani kama kuna muasisi yeyote wa Muungano angekuwa hai leo angekubaliana na kile alichodai uhuni unaofanywa kwa sasa kuhusiana na demokrasia visiwani hapa.
Maalim Seif aliyasema hayo jana nyumbani kwake Chukwani nje kidogo ya mji wa Unguja alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na maadhimisho ya miaka 52 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Muungano ni wa wananchi na siyo wa dola na watawala wake, kuheshimu uamuzi na matakwa yao ndiyo utekelezaji sahihi wa dhana ya Muungano,” alisema Maalim Seif.
Seif aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika Serikali ya Awamu ya Saba, alisema lengo la Muungano lilikuwa ni kujenga na kuimarisha haiba ya kila upande na kukuza uelewa na uwezo wa kujiletea maendeleo kwa pande zote mbili, jambo ambalo alidai kwa sasa linakiukwa na viongozi walioko madarakani.
Katibu mkuu huyo, alikuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia CUF katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, analalamikia kupokwa ushindi baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi huo na kutangaza uchaguzi wa marudio ambao ulifanyika Machi 20, mwaka huu.
Hata hivyo, CUF waligomea uchaguzi huo wa marudio ambao ulimpa ushindi mgombea wa CCM, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Alisema: “Dhana ya Muungano hasa wakati huu wa maadhimisho yake ya kimyakimya, isitafsiriwe kwa thamani ya kutumia majeshi ili kubatilisha kile wananchi walichokiamua, kitaendelea kuwa hivyo kwa Zanzibar.”
Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano kwa Umma wa CUF, Salim Abdalla Bimani alisema kumbukizi ya Muungano inawakumbusha Wazanzibari namna wanavyoendelea kupokwa haki yao na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwachagulia viongozi wanaotaka wawaongoze.
Bimani ambaye alirejea nchini hivi karibuni akitokea nje alikokwenda kutibiwa alisema: “Tunaikumbuka hii siku ya Muungano kwa maana pana zaidi kwetu sisi Wazanzibari ya kupinduliwa kwa demokrasia na uamuzi halali ambao umma ulikwishaamua kwenye sanduku la kura, Oktoba 25, mwaka jana.”
Alisema Tanganyika na Zanzibar ziliungana Aprili 26, 1964 chini ya waasisi wake, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume kwa lengo la kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “Lakini lengo hili linapinduliwa na watu wasiopenda uhuru na demokrasia ya kweli,” alisema Bimani.
Hata hivyo, wakati haya yakijiri kwa viongozi hao wa CUF, jana hali katika mitaa yote ya Unguja na vitongoji vyake ilikuwa shwari na watu wengi waliendelea kuyatumia maadhimisho hayo kwa kufanya shughuli zao na kujipumzisha.
Chanzo: Mwananchi