Seif atabiri kuanguka kwa CCM

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,299
33,080
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad ametabiri kuanguka kwa CCM katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba, kufuatia mazingira mazuri ya kisiasa, yaliyotokana na maridhiano kati yake na Rais Amani Abeid Karume.
Maalim Seif alitoa kauli hiyo nzito muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kugombea Urais wa Zanzibar kwa mara ya nne tangu kuanza mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini humo katika tawi la CUF Mtoni Zanzibar jana.
Alisema hivi sasa Zanzibar kuna mazingira mazuri ya kisiasa yanayoonesha dalili za uchaguzi huru na haki na ndio maana anaona kuna kila sababu ya kuibuka mshindi katika uchaguzi huo.
Akizungumza katika tawi la CUF, Mtoni mara baada ya kuchukua fomu alisema chaguzi zilizopita zilikuwa na kasoro nyingi, ikiwemo ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi ulio huru na haki na kusababisha matatizo makubwa ya kisiasa visiwani Zanzibar.
“Kauli ya Rais Karume alipozindua umeme kisiwani Pemba kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa tofauti na chaguzi zilizotokea inatupa matumaini kwa chama chetu kushinda katika uchaguzi ujao,” alisema Maalim Seif.
Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo amesema mbali na yeye kuchukua fomu ya kuwania Urais Zanzibar, hakuna mwanachama anayezuiliwa kuwania nafasi hiyo na ile ya Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Kauli hiyo ya Katibu Mkuu wa CUF, ni ngeni tangu kuingia kwenye maridhiano na Rais Karume, ambapo amekuwa muangalifu sana na kujiepusha kuzungumzia ushindani wa kisiasa na wapinzani wao CCM, Zanzibar.
Katika hatua nyingine Maalim Seif ametaka viongozi wa vyama vya siasa kuonyesha ustaarabu katika harakati za kampeni zitakapoanza na kushindana kwa hoja.
“Tufanyeni kampenzi za uchaguzi bila ya kutumia maneno machafu katika majukwaa, ili wananchi watoe ridhaa zao za kuchagua kiongozi wanaemtaka kuwaongoza katika nchi yao,” alisema.
Hivi karibuni Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Salum Bimani alisema kuna watu 16,000 wamenyimwa haki ya kuandikishwa kuwa wapiga kura kutokana na kukoseshwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.
Kuhusu sakata la kung’olewa wasaidizi wake wa karibu kuwania Ubunge kisiwani Pemba, Maalim Seif alisema hali hiyo ilitokana na baadhi ya wananchi katika majimbo hayo kutoridhika na utendaji wa wabunge wao.
Katika mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho kisiwani Pemba wabunge 12 kati ya 18 wameanguka, akiwemo muasisi wa chama hicho, Fatma Maghimbi.



CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
 
Hivi Kauli ya Rais Karume peke yake inatosha kuufanya uchaguzi uwe huru na wa haki? Mimi nafikiri kuna kazi ya kupambana na wahafidhina wengine wanaofikiria kwamba nje ya CCM hakuna kiongozi anayestahili kuitawala Zanzibar.
 
Hivi Kauli ya Rais Karume peke yake inatosha kuufanya uchaguzi uwe huru na wa haki? Mimi nafikiri kuna kazi ya kupambana na wahafidhina wengine wanaofikiria kwamba nje ya CCM hakuna kiongozi anayestahili kuitawala Zanzibar.

Ni kweli Seif anafikiria Karume tu ndio anaweza kuleta mabadiliko, hajui kuwa nyuma yake kuna wahafidhina wengi wasiopenda mabadiliko na hasa kutoka bara. Watu hao wanajua kuwa CCM iking'olewa Zanzibar itaanza kuandaliwa kaburi pia hata huku bara kwa sababu wananchi wataona inawezekana bila CCM. Kwa sababu hiyo uchaguzi wa Zanzibar hautakaa uwe huru kwa mazungumzo ya mezani tu.....
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom