Sanaa ni Utajiri, Kila msanii ni BOSS

Hussein Massanza

JF-Expert Member
Dec 26, 2012
918
1,994
Lazima msanii aishi maisha yake. Amiliki jumba au majumba mazuri, aendeshe magari ya kifahari. Akionekana barabarani iwe kero, maana atajaza umati utakaomzunguka kumshangaa. Wengine japo waguse ngozi yake.

Msanii ni tajiri, kipaji chake ni mashine ya fedha ambayo inamuwezesha kuishi anayotaka. Wewe ni msanii? Una kipaji? Umefanya sanaa kwa miaka mingapi? Unaishi kisanii au kawaida? Umewahi kujiuliza ni kwa nini mpaka leo bado hujaweza kuishi kisanii?

Manamuziki Joseph Haule ‘Prof. Jay' alighani "Sioni sababu za msingi kuomba kwenye mitaa, kama una kipaji iweje ufe na njaa", ni katika wimbo Mtazamo, ambao pamoja na fundi mwingine Msafiri Kondo ‘Solo Thang', walishirikishwa na galacha wa Hip Hop Tanzania, Suleiman Msindi ‘Afande Sele'.

Hapa Prof. Jay, alitumia stadi yake ya kimashairi kuiambia hadhira kuwa kipaji ni fedha, kwa hiyo hakuna sababu yoyote aliyejaliwa kipaji, kuwa ombaomba, kuhangaika mitaani au kufa njaa. Msanii mwenye kipaji kufa njaa ni aibu kwa taifa! Na labda dunia nzima!

Ni ukweli kwamba utajiri ni jitihada za mtu binafsi lakini inapotokea msanii amefanya kila alichoweza kuisimamisha sanaa yake na ikashindwa kumlipa, hilo ni tatizo kubwa! Ni mazingira gani ambayo yamewekwa kurahisisha maisha ya msanii?

Sanaa ni biashara! Serikali inapoamua kutambua sanaa kama sekta ya kibiashara, hunufaika moja kwa moja katika Pato la Taifa (GNP), hivyo kusaidia nafuu katika makadirio yake ya mapato na matumizi ya kila mwaka (bajeti).

Katika Serikali ya Marekani, ndani ya miaka ya hivi karibuni, sanaa imekuwa ikichangia dola bilioni 500 mpaka 600, sawa na shilingi trilioni 910 na trilioni 1100 (quadrillion 1.1) kwenye Pato la Ndani la Taifa (GDP), ikizidi mpaka sekta ya Usafiri na Utalii.

Kiwango hicho cha mapato kupitia Sanaa na Utamaduni ni sawa na asilimia 3.2 ya pato lote la ndani la taifa kwa mwaka 2012 nchini Marekani, huku sekta ya Usafiri na Utalii ikichangia asilimia 2.8. Hayo yanatokea pale ambapo serikali inatambua sanaa kama sekta rasmi na kuiwekea njia za kibiashara.

Kwa ufafanuzi ni kuwa mapato ambayo Serikali ya Marekani inapata kwa mwaka mmoja kupitia sekta ya Sanaa na Utamaduni, inatosheleza bajeti nzima ya Tanzania kwa miaka 58 ijayo, kwa kupigia mahesabu ya uwiano wa bajeti ya shlingi trilioni 19 ambayo iliidhinishwa na bunge Juni mwaka jana, mwaka wa fedha 2014-2015.

Ieleweke pia kuwa hizo ni fedha ambazo serikali inapata kupitia kodi inayowatoza wasanii na mapato yatokanayo na uwekezaji wake kwenye Sanaa na Utamaduni, kama vile vituo vya maonesho ya sanaa (arts galleries), kumbi na kadhalika.

Hapo hayajaguswa mapato hasa ya wasanii. Kwa nini wasiwe matajiri ikiwa makato tu kutokana na ingizo lao yanachangia taifa kwa kiasi hicho. Tambua kwamba hiyo ni Marekani, baba wa mataifa yaliyoendelea. Serikali yake ni tajiri inayojitosheleza kwa kila namna. Ila inaheshimu sanaa.

Si Marekani tu, kila nchi ambayo iliamua kwa dhati kabisa kutambua sanaa kama sekta rasmi na kuiwekea njia za kibiashara, inapata unafuu mkubwa wa kibajeti kila mwaka, kutokana na mchango wake katika Pato la Taifa.

Ukipofu wa Tanzania katika kuchangamkia sekta ya sanaa umesabaisha hasara kuu mbili. Mosi; ni serikali yenyewe kukosa mapato iliyostahili kwa muda mrefu. Pili; ni kuacha wawekezaji wa sanaa kufanya wanavyotaka mpaka kuamua mapato ya wasanii na maisha yao.

Kwa mfano; Nchi zenye mwamko wa sanaa, kila kazi inayotangazwa kwa kuoneshwa kwenye televisheni au kusikika redioni, msanii ndiye hulipwa gawiwo la faida (royalty) kulingana na wigo wa kazi yake ilivyooneshwa au kusikika, kwa sababu upo ukweli kuwa kazi za wasanii huongeza namba ya watazamaji (katika televisheni) au wasikilizaji (redioni).

Hapa Tanzania msanii hajui ladha ya royalty redioni wala kwenye runinga. Badala yake, kwa mfano ulio hai ni kwamba mwanamuziki ndiye hutozwa fedha ili wimbo wake usikike redioni au uonekane runingani. Hii ni rushwa ambayo katika lugha ya kimuziki huitwa payola.

Payola ni mpango haramu wa rushwa ambao hutumiwa na makampuni makubwa ya muziki, kuwahonga (kwa siri) watangazaji wa redio ili nyimbo zinazotoka kwenye studio zao zipigwe sana, hivyo kufanya biashara kubwa. More promo more money!

Payola hutumiwa kumtoa msanii. Yaani katika kalenda ya kampuni fulani, mathalan Universal Music Group wanataka kumtangaza mwanamuziki X ambaye albamu yake ipo jikoni, lengo likiwa kumuuza na kugonga platinum za kutisha, huhonga fedha kuhakikisha nyimbo zake zinapata upendeleo maalum.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Jimbo la New York, Marekani, Eliot Spitzer aliyafungulia mashtaka makampuni makubwa matatu ya muziki, Sony BMG Music Entertainment (Julai 2005), Warner Music Group (Novemba 2005) na Universal Music Group (May 2006).

Spitzer aliyafikisha mahakamani makampuni hayo kwa kujihusisha na rushwa (payola), kuhonga watangazaji na ma-DJ ili nyimbo au kazi zao zipate upendeleo maalum kwenye mzunguko wa vipindi. Makampuni hayo, yaliomba kesi iishe nje ya mahakama na kukubali kulipa faini.

Sony BMG Music Entetainment walilipa faini ya dola za Marekani milioni 10, Warner Music Group wao walitoa dola milioni tano na Universal Music Group ilibidi wagharamike dola milioni 12 (keshi) ndipo msala ukaondoka mahakamani.

Marekani haijaanza kampeni ya kupambana na payola leo, mwaka 1959, baada ya kamati maalum ya Bunge la Marekani (Congress) kuichunguza Radio WABC, ilibidi kituo hicho kimfukuze kazi DJ wake maarufu, marehemu Alan Freed, aliyebainika alichukua mshiko wa payola na akagoma kusaini hati ya kiapo kwamba hajachukua payola.

Kwa mtindo huo, hapa Tanzania, kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, litaamua kuitambua rushwa hii (payola), hivyo kuivalia njuga kwa kulifanyia uchunguzi wa kibunge, suala la wanamuziki kutozwa fedha ili nyimbo zao zichezwe redioni na kwenye televisheni, bila shaka tutakuja kusikia vituo kadhaa vya redio vinatolewa mapendekezo ya kufungiwa.

Kama Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru), itaamua kuiundia kikosi maalum cha uchunguzi, rushwa hii (payola), taifa litakumbwa na mshtuko mkubwa pale ambapo utitiri wa watangazaji, ma-DJ na hata waandishi wa habari watakaposimamishwa kortini kujibu mashtaka.

Hatuoni hayo yakitendeka kwa sababu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijawa na nia ya dhati ya kuifanya sanaa kuwa sekta muhimu kwa mchango wa Pato la Taifa (GNP) na kwa hivyo, wasanii wanabaki kuwa wavuja jasho wasiothaminika, kutambulika wala kuheshimika.

Serikali iliamua kukaa mbali, hivyo wadau wakaona wawe wanajiamulia tu; vituo vya televisheni vikawa vinachezesha tamthiliya za Watanzania bure, hawawalipi wasanii. Televisheni inaingiza fedha kupitia matangazo, tena watangazaji wenyewe wanakuwa wamevutiwa na kazi za wasanii.

Hili ni tatizo ambalo lilisababisha wasanii kukimbia kufanya maonesho yao kwenye televisheni na kuamua kujiajiri kwa kutengeneza filamu japo nako hawanufaiki inavyotakiwa, ila angalau wanapata ndogondogo za kupunguza njaa. Basata ipo na wasanii walinyonywa na vituo vya televisheni bila chochote kutokea.

Wanasiasa wamekuwa na uswahiba mkubwa na wasanii zinapofika nyakati za uchaguzi. Hapo ndipo huona umuhimu wao na kutambua kama siyo kuthamini nguvu iliyopo ndani ya wasanii. Ni kipindi hicho huambatana nao katika mikutano yao ya kampeni kwa kuwa wasanii ni kivutio, huongeza umati pia hurahisisha upatikanaji wa kura.

Siku moja nikiwa kwenye mazungumzo ya kawaida na Mkurugenzi wa Utafiti na Uzalishaji Vipindi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tanzania House of Talent (THT), alinieleza hofu yake kwa wanamuziki wa THT kushiriki matukio ya kisiasa.

Aliniambia kuwa kupotea kwa mwanamuziki aliyetikisa nchi kwa nguvu na uwezo mkubwa, Lawrence Marima 'Marlaw', ni baada ya wimbo wake Piii Piii (Missing My Baby), kubadilishwa na kuimbwa kwa ajili ya kampeni za CCM katika Uchaguzi Mkuu 2010.

Hii ni Tanzania peke yake; mwanamuziki anakubali kupoteza soko lake kwa sababu ya fedha za msimu, kusimama jukwaani na kukata mauno kukifanyia kampeni chama fulani. Hii inasababishwa na njaa pia kukosa uwezo wa kutafakari na kuliona soko lake la kesho.

Uchaguzi Mkuu wa Marekani mwaka 2012, tulishuhudia wanamuziki wengi maarufu kama Sean Combs ‘P. Diddy', Shawn Carter ‘Jay Z', Beyonce Knowles na wengine wengi wakimfanyia kampeni Rais Barack Obama. Silaha waliyotumia ni maneno tu, wakijenga hoja ni kwa nini wanaamini Obama alistahili kuongezewa muda.

Haikwa kutumia nyimbo zao au sanaa yao kumfanyia kampeni Obama. Nawashauri wasanii wa Tanzania kutumia umaarufu wao kwenye kampeni za kisiasa pale wanapoona kuna ulazima wa kutumika. Hata siku moja wasithubutu kutumia sanaa zao katika kampeni. Gharama yake ni kubwa sana.

MAISHA YA MSANII;
Msanii kufa maskini ni kwa bahati mbaya ambayo inaweza kusababishwa na mambo matatu. La kwanza ni kufilisika kutokana na matatizo. Kuibiwa haki zake na la mwisho ni kuchezea fedha zake na utajiri wake. Hiyo ni bahati mbaya!

Msanii stahili yake ni kufa akiwa tajiri. Kufa maskini ni bahati mbaya kama ilivyomtokea marehemu Egon Schiele, raia wa Austria aliyefilisika akigharamia matibabu yake na mkewe, waliposhambuliwa na Mafua ya Kihispania, ugonjwa ambao ulikuwa janga lililogharimu maisha ya watu zaidi ya milioni 20 barani Ulaya.

Kwa kawaida msanii anaishi kwa kanuni hii; Kipaji – Umaarufu – Fedha – Utajiri – Maisha ya Kisanii – Kifo – Mazishi ya Heshima (Mazishi ya Kifahari).

Maisha ya kisanii, haina maana ya wale wajanjawajanja wa mjini, wanaoishi kwa kutapeli, la hasha! Hapa namaanisha maisha ya msanii yalivyo ambayo hutawaliwa na burudani, starehe, mbwembwe na purukushani za kila aina.

Katika kanuni ya maisha ya msanii, kiungo cha katikati ni fedha, kwa hiyo mwanamuziki anapokuwa na uhakika wa fedha ndipo hapo hujiona usanii wake umekamilika. Hiyo ndiyo hali halisi. Dhiki na sanaa, hiyo inakuwa imepotea njia. Imeingilia uani. Kwa msemo wa wana wa mjini, hiyo dhiki inakuwa imeingia choo cha kike!

Tumeona hali halisi ya vifo vya akina Juma Kilowoko ‘Sajuki', Albert Mangweha ‘Ngwair', Nasma Hamis Kidogo, Said Ngamba ‘Mzee Small' na wengineo, hakika vifo vyao havikuwa kwenye mkondo wao, japo mazishi yao yalibeba thamani yao kama wasanii. Ila haikutosha!

Hapo sikumtaja marehemu Steven Kanumba kwa sababu angalau yeye alikuwa na nafuu kubwa wakati roho yake ilipoagana na mwili wake, ila kiukweli naye alistahili zaidi ya kila alichopata na alichoacha kutokana na kazi kubwa aliyofanya. Tatizo ni Tanzania na dharau yake kwenye sanaa.

Nasma Hamis Kidogo, mwanamke mkubwa sana Tanzania unapozungumzia ulimwengu wa Taarab, lakini alifia Hospitali ya Temeke, hata taarifa za kuumwa kwake hazikutolewa. Zilitoka taarifa za ghafla tu kwamba "hatunaye". Hakuwahi kuishi maisha ya msanii!

Ukipita mstari kwa mstari katika tungo za marehemu Ngwair, utagundua kwamba alitamani sana kuishi maisha ya msanii. Maskini ya Mungu, hakuwahi kupata! Alikuwa na kipaji kikubwa, alikuwa na bidii ya kuandika, kubuni na kuimba, akaukwaa umaarufu hasa ila hakuzifikia fedha, hakuwahi kuuona utajiri, kwa maana hiyo hakuwahi kuishi kisanii.

Kanuni ya msanii wa Kitanzania ni hii: kipaji – Umaarufu – Dhiki – Umaskini – Maisha ya Kuganga Njaa – kifo – Mazishi ya Kifahari.

Hii ndiyo hali halisi, hata Mzee Small ambaye aliteseka sana wakati akiumwa na aliomba msaada, akisisitiza wasanii wenzake kwenda kumjulia hali bila mafanikio, alipofariki dunia, siku ya mazishi, mtaa wa nyumbani kwake ulikuwa mdogo. Umati mkubwa, viongozi na watu wengi maarufu walijazana na kusongamana.

UMARUFU KWENDA UTAJIRI;
Kwa kuangalia kanuni ya maisha ya msanii wa Kitanzania, jawabu lipo wazi kwamba kizingiti kikubwa cha msanii kuufikia utajiri na kuishi maisha anayotaka, kama ilivyo kwa wasanii wa nchi nyingi duniani ni fedha. Umaarufu unapatikana kirahisi lakini fedha ni majanga.

Imeshaonekana kuwa mfumo wa ufanyaji sanaa Tanzania ndiyo tatizo la msingi kwa maendeleo ya wasanii na sanaa yenyewe kwa jumla, basi yapo mambo ambayo kama msanii unataka kufanikiwa inabidi uyashughulikie kwa bidii kubwa. Bidii kwa sababu kuendelea kama msanii Tanzania ni vita.

Upambane ukielewa kuwa walikuwepo magwiji wa muziki nchini kama marehemu Marijani Rajab ambaye aliitwa Jabali la Muziki, Mbaraka Mwinshehe, Muhidin Maalim Gurumo, TX Moshi William, Hemedi Maneti na wengine wengi, na hapa juzi aliondoka Shem Karenga. Walifanya kazi kubwa ila walikufa na dhiki.

Wakati unapoamua kuvaa joho la mapambano, utambue kuwa wakongwe hao si kwamba walikuwa wavivu au wazembe, wala usidhani walichezea fedha, na utakosea sana ukiamini kazi zao hazikuingiza pesa. Elewa kuwa mfumo haukuwa rafiki wa sanaa yao.

Zingatia kwamba kufanya sanaa Tanzania ni mateso makubwa, kwa sababu inakutaka utengeneze njia zako mwenyewe. Hakuna kitu ambacho msanii atakikuta kipo tayari. Marehemu Bibi Kidude (Fatma Baraka), aligeuzwa maonesho nyakati za mwisho za uhai wake.

Kipindi ambacho bibi wa watu alistahili kupumzika kwa sababu ya uchovu wa uzee, kisha ale matunda ya sanaa yake aliyoifanya kwa takriban karne nzima, akawa mara arudishwe Zanzibar, mara apelekwe Bara. Wadau walimtumikisha na uzee wake. Angefanya nini na fedha hana?

TUMIA AKILI YA ZIADA;
Kwa Tanzania, unaweza kuanza sanaa kawaida lakini ukishapata umaarufu, hapo inabidi gia yako ibailike. Elewa kwamba ili uishi maisha yako, hatua inayofuata ni muhimu sana. Ni hatua inayohusu fedha. Ukifeli hapo, basi tena!

Usilaumu wala kupiga sana kelele, maana ukifanya hivyo, utawazindua walioshika meno yao na watakubana na kukung'ata vilivyo. Ni mapambano, maana unapoona msanii hanufaiki kwa kazi yake, ujue wapo ambao wanatengeneza fedha kwa mlango wa nyuma. Shamba la msanii, anayevuna mfanyabiashara!

Cheza na akili ya walioshika mpini; kwa maana kwamba wakati unaongeza thamani ya soko lako, wakati mwingine simama kati kwa kati. Zipo nyakati itakubidi ukubali matakwa yao, wasikuone mbishi sana. Muda mwingine waoneshe kuwa huyumbi unaposimamia maslahi yako.

Msimamo wako utakufanya usiwe mtumwa, hata pale unapokubali matakwa yako, wataheshimu kwamba umekubaliana nao kibiashara na siyo kwa nidhamu ya woga, eti ukikataa utapotezwa kisanii. Ndiyo maanaa hapa muongozo ni kutumia akili. Usiwe mnyonge, usiwe mtata, simama kati.

FANYA KAZI YENYE UKUBWA WA BAHARI;
Upo msemo kuwa huwezi kulinda bahari, kwamba ukiweka ulinzi wako Coco Beach au Sea Vew, watu watakuwa wanaogelea Ununio, Bagamoyo na maeneo mengine mengi. Fanya kazi yako iwe kubwa, hapo utaona jinsi utakavyozidi fitina za wabanaji.

Wewe ni mgumu kutoa rushwa, lakini kazi yako ni kubwa. Radio au TV fulani wakigoma kucheza kazi yako, kutokana na ubora wa sanaa uliyofanya, vipo vituo vingine ambavyo vitacheza tu. Na kwa sababu vyombo vya habari vinaendeshwa kwa mashindano siku hizi, hata wale waliobana, itabidi wacheze kwa shingo upande ili kuvutia watazamaji au wasikilizaji.

Kipengele hiki kinamgusa pia msanii chipukizi. Unahaha kutoka na mlango unakuwa mgumu, unachotakiwa kufanya ni kunoa ubongo wako ili ufanye sanaa kubwa ambayo itakurahisishia kupenya na kukupa umaarufu kabla yakuzifikia fedha ambazo zitakuvusha mpaka kwenye utajiri.

Katika mazingira magumu ya kupenya sokoni na kuzifikia fedha, msanii anafanya kazi ya kawaida, hapo matarajio ni kufeli tu. Sanaa ya Tanzania inahitaji wasanii wanaoumiza kichwa zaidi ya kiwango cha kawaida. Ukifanya kawaida, hutafanikiwa kuifanya sanaa yako kuwa mashine ya fedha. Utabaki maskini.

Ukifanya kazi kubwa, unastahili malipo makubwa kulingana na ukubwa wa ubunifu pamoja na usanifu wako. Hapa namaanisha sanaa ya aina yoyote ile. Maana kila sanaa inaleta umaarufu, fedha, utajiri na maisha ya kisanii. Muhimu kuzingatia ni jinsi unavyoifanya sanaa yako. Fanya sanaa yako kibiashara.

SANAA YAKO NI UTAJIRI WAKO;
Jarida la Sayansi na Utafiti la Neuroimage la Uholanzi, liliandika mwaka 2014 kisha Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kuripoti habari hiyo kwamba msanii ana akili ya juu kuliko binadamu mwingine ambaye hajishughulishi na sanaa.

Utafiti huo unabainisha kuwa sababu ya msanii kuwa na akili kubwa ni kwamba anatumia nguvu kubwa kufikiri na kubuni kazi, hivyo kuifanya akili yake kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi kuliko binadamu wengine ambao siyo wasanii.

Kama wanasayansi wanaweza kutafiti na kutoa majibu kuwa wasanii wana akili sana, hilo ni jawabu kwamba wanastahili kilicho bora. Yaani kuwa matajiri na kuishi kama mabosi. Msanii ni mwajiri. Msanii ni kiwanda, ni malighafi, ni bidhaa, ni kampuni.

Msanii ndiye mkurugenzi, anamwajiri meneja na maofisa wengine mbalimbali ambao huhusika na majukumu ya kila siku wakati yeye anakuwa ‘bize' na masuala ya kurekodi, mazoezi au mpangilio wa maonesho yake. Mambo ya biashara na promosheni hushughulikiwa na waajiriwa wake.

Msanii kazi zake zinapokuwa kwenye mzunguko mzuri, anaweza kutengeneza ajira za watu 200 na kuendelea. Kwa maana hiyo ni vizuri msanii akajiamini kila siku. Ajipende na kujikubali kutokana na kipaji chake. Hatakiwi kukata tama kabisa.

Serikali inapaswa kutafakari upya na kubadili mfumo wake, kwani sekta ya sanaa siyo tu kuwa inaweza kusaidia kuongeza Pato la Taifa, hivyo kufidia changamoto za bajeti kila mwaka, vilevile inaweza kuisaidia serikali kutokana na janga la upungufu wa ajira.

Hapa serikali haina kazi kubwa sana, wajibu wake ni kutengeneza njia za kuwezesha mazingira rafiki ya ufanyaji sanaa. Angalau wasanii wapunguze kunung'unika na kunyongeka. Hiyo itasaidia kufanya akili za wasanii kutulia na kufanya kazi zaidi. Ni hapo jamii itashuhudia ubosi wa vijana wenye vipaji. Maarufu walio na hulka ya kutumia. Ndiyo zao wasanii.

Na Luqman Maloto
 
Tukiwa wakweli...ni lazima tuwaambie watoto zetu na wadogo zetu kuwa kwa Tanzania

ni bora usome uwe mwalimu au daktari kuliko kujifanya unaendeleza kipaji

sanaa ya Tanzania ni ngumu saana na wanaofanikiwa ni wachache mno.....

Msanii mkubwa mno kama Marehemu Kanumba aliacha nini kikubwa?
kuna mali zozote za maana alizoacha?

ulichukua walimu 20 wa sekondari waliofanya kai miaka 10
na wasanii wakubwa 20 waliofanya kazi miaka 10 nani utawatamani?

halafu hii mifano ya Marekani ndo mnazidi kuwadanganya kabisa na kuwapotosha watoto

Marekani ni kitu kingine kabisa kiuchumi kulinganisha na Tz....

Tz angalau mtoe mifano ya South Africa kidogo tunaweza kuiga huko baadhi ya vitu


mwisho tu niseme sasa teknolojia imeshafanya hizo kazi za sanaa kama nyimbo au filam zipatikane bure kabisa
hivyo ni pigo lingine kwa wasaniii......

taifa la watu masikini wakiwa na access ya kupata bure kazi yako usahau kabisa uwezekano wa kuwa tajiri that much
sana sana ujitahidi uweze kufika middle class tu ambayo madaktari na walimu wapo huko
 
Kwenye Taaluma nako ni kama kwenye sanaa, Ukiritimba mwingi na hakuna UBORA wa elimu kwa 'masikini', so pia tukianza kupachambua tutapata yale yale yanayowakumba wasanii, japo inaweza kuwa ni kwa different dimensions!

Haina maana watoto wakifanya sanaa wasiende masomoni, la hasha! Ila ni vema wasanii wafanye sanaa yao kulingana na wakati na kwa ubora. Watu watanunua tu kazi zao, kama si kazi zao, basi walau products zitakazotokana na wao ikiwa tu watafanikiwa ku-brand majina yao. Mifano Ipo!


I wonder kama umenielewa
ni hivi ukitoa mfano wa Marekani mtu akishatoa album na ika hit
swala la kupata millions ni given...labda ashindwe mwenyewe tu ku manage pesa yake

shida ya TZ hata ukiwa na hit album haiku guarantee kipato


ili useme tasnia fulani ina mafanikio unapaswa utazame kwa ujumla wake
sio mifano ya watu wawili au watatu....


huwezi kusema TZ kuwa designer wa nguo inalipa kwa mifano ya Eve collection na Sheria Ngowi...

kwa ufupi tu TZ hakuna kabisa 'fashion indusrty'
waliopo wanabangaiza tu......

Usitoe mfano wa Diamond bila kumtazama waliofanya nae kazi
kuanzia producers wa nyimbo zake hadi wabeba camera wa video zake bongo....
 
kama una kipaji iweje ufe na njaa
ha ha ha ha
huu mstari umekudanganya

Ngurumo kaimba mpaka amestaafu hakuwa na gari
Tx moshi alinunuliwa gari na friends of simba

Mziki wenyewe huu baadhi ya vyombo vinawapa airplay wasanii wanaowamanage

Wanaandaa mabeef ili wamkuze asiye mkubwa
Mandojo na domokaya wamepiga show nchi za watu kama vichaa walichoambulia duka la nguo
Saida Karoli yupo wapi ??
kwa nini wasanii wanaukimbilia ubunge ?

Kufanikiwa kwenye mziki ni shida sana kuliko kazi yeyote
 
Makala kama hii ni ya maana sana, tatizo ni pale unapokuta imewekwa katika gazeti lenye picha za uchi na mafumanizi ya kutunga ukurasa wa mbele. Ukurasa ambamo makala ipo pana chombezo la 'Kisamvu cha Kopo'...
1907992_904406732925532_2452450695315734965_n.jpg
 
Ni mfumo tu ndugu! Hao wakina Gurumo ni miongoni wa wahanga wakubwa wa Mfumo kutokuwa makini na kuichukulia poa sanaaa.. Sanaa ni Industry, kwenye industry tunatarajia uzalishaji wa bidhaa, zikiwa bora zitauzwa kuanzia nchini na kuvuka mipaka, Ni suala la serikali kuithamini na kuweka njia nzuri ya kukusanya mapato na kulinda maslahi ya wazalishaji wa hizo bidhaa.

Ukitaka kubaini kuwa Sanaa inalipa, tazama wajanja wa kihindi wanavyotajirika kupitia hizi hizi sanaa za wasanii wa Tanzania. Wanatajirika si mchezo na nachelea kusema 'wanakula sahani moja na wenye dhamana ya usimamizi wa sanaa', Ni ukiritimba tu!

Mziki utalipaje wakati unatumia kudownload mziki bure ??

wale wadosi siku hizi hawana habari na mziki

tanzania itabidi ichukue miaka 200 ndio mziki ulipe ambapo siwezi kumshauri mwanangu afuate kipaji chake nitamwambia fuata masomo ambayo hayo masomo napo yatakua hayalipi

kuandika ni rahisi kuliko utekelezaji
 
Back
Top Bottom