Samson Mwigamba: "Nakwenda kuikamata Magu" | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Samson Mwigamba: "Nakwenda kuikamata Magu"

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Ntemi Kazwile, Jul 21, 2010.

 1. Ntemi Kazwile

  Ntemi Kazwile JF-Expert Member

  #1
  Jul 21, 2010
  Joined: May 14, 2010
  Messages: 2,145
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 135

  [​IMG]


  Mwandishi wetu


  “UFISADI umeishika nchi pabaya. Tukiendelea kuwa na wabunge legelege na madiwani legelege, watendaji wetu wa halmashauri wataendelea kufanya vitendo vya ajabu hujapata kuona. Tunahitaji kuongeza wapiganaji mithili ya Dk. Wilbroad Slaa, Zitto Zuberi Kabwe, Halima Mdee, Suzan Lyimo, Grace Kiwelu, na wengineo.
  “Ni kwa sababu hiyo, nimekubali wito wa wazee wa Magu walioniita na kuniomba nirejee nyumbani kuwasaidia. Ilikuwa niende masomoni mwezi wa tisa mwaka huu nchini Uholanzi kusoma Shahada ya pili ya uhasibu na usimamizi wa fedha, lakini wakaniomba niahirishe kwa kuwa wananihitaji sana hivi sasa, nami nimekubali wito wao. Elimu niliyonayo nimeipata kwa kodi zao na nilisoma kwa ajili ya kuwatumikia wao. Nakwenda kuiongoza Magu”.
  Hiyo ni sehemu ya tamko la Samson Mwigamba, alilolitoa kwa umma kupitia kalamu yangu nilipofanya naye mahojiano maalumu mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Magu.
  Mwigamba sio jina geni kwa wafuatiliaji wa mambo. Kwa Watanzania wengi hususan wasomaji wa magazeti, Mwigamba anafahamika kama mmoja wa wachambuzi mahiri wa masuala ya kisiasa katika gazeti hili, ambaye kwa muda mrefu sasa amekuwa akiandika makala za siasa kila wiki kupitia safu yake maarufu, “Kalamu ya Mwigamba”.
  Kwa wakazi wa Magu, anafahamika zaidi kama kijana wa nyumbani na kada machachari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye kwa zaidi ya miaka mitatu sasa amekuwa akifanya kazi ya mara kwa mara ya kukijenga na kukiimarisha chama chake katika jimbo hilo.
  Mwigamba ni mwanaharakati, mwanasiasa, mwalimu na msomi wa fani za uhandisi, uhasibu na usimamizi wa biashara, anayefanya kazi katika shirika moja la kimataifa lililopo mjini Arusha kama mtaalamu wa masuala ya bajeti. Huyu ndiye mwenyekiti mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Arusha aliyechaguliwa mwezi Machi mwaka huu.
  Kabla ya kushika wadhifa huo, mwanasiasa huyu kijana alikuwa Katibu Mwenezi wa chama hicho Wilaya ya Arusha Vijijini, Kaimu Katibu Usa river Arusha na Arumeru, kwa vipindi tofauti.
  Wakati akitangaza nia hiyo, Mwigamba alikuwa njiani akielekea jimboni humo kuendelea na shughuli za kukiimarisha chama chake. Akiifafanua nia hiyo, alisema mbali ya wito wa wazee wa Magu, pia kama mwenyeji wa Magu ameamua kugombea ubunge ili kushughulikia matatizo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii yanayowakabili wananchi wa jimbo hilo.
  Akiyaainisha baadhi ya matatizo hayo alisema:
  “Magu sawa na Tanzania nzima inakabiliwa na kuathiriwa na matatizo matatu ya msingi. Moja ni kukosa viongozi, pili ni ufisadi na tatu ni mfumo mbovu wa utawala wa nchi hii. Tuna tatizo kubwa la viongozi. Viongozi wengi tulio nao si viongozi. Uongozi ni kuonyesha njia, kwa hiyo pale kiongozi anapokuwa fisadi ni sawa na kuwatoa anaowaongoza kwenye njia iendayo kwenye maendeleo na kuwaingiza kwenye pori la ufukara uliopitiliza.
  Kiongozi anaposhindwa kufanya maamuzi sahihi wakati sahihi kwa watu sahihi anakuwa amewatoa watu njiani na kuwatokomeza gizani ambako hawatajua ni nini cha kufanya. Taifa leo halina uongozi. Serikali iliyoko madarakani na chama kinachotawala wote wamewekwa mfukoni na ufisadi.
  Hawana la kusema mbele ya ufisadi na wanatekeleza matakwa ya mafisadi na si wananchi.
  Mfumo wa utawala ndilo tatizo namba moja katika yote niliyoyataja. Ni ajabu hivi leo kwamba mkuu wa wilaya ama mkoa aliyepachikwa na rais wilayani kuwa kiongozi mara nyingine bila hata rais kumfahamu, ana mamlaka makubwa kuliko hata baraza zima la madiwani waliochaguliwa na wananchi wa wilaya husika.
  Naamini kwamba kuna wakuu wa wilaya ambao rais hata hawajui ingawa tumetangaziwa kwamba ni yeye kawateua.
  Wengine anaambiwa tu na marafiki zake kwamba mteue huyu na yeye anafanya hivyo. Tunahitaji kupigania mabadiliko ya mfumo wa utawala.
  Nikiingia bungeni nitakuwa mbunge wa kwanza kuleta hoja binafsi mbele ya Bunge kwa ajili ya kufanya mabadiliko makubwa ya katiba na kubadili kabisa mfumo uliopo wa utawala ili kuwezesha nchi hii kupiga hatua haraka ya maendeleo.
  Mambo hayo yanaonekana ya kitaifa zaidi lakini ni ya muhimu sana kwa kuwa mabadiliko yakitokea kitaifa, ufisadi ukaondoka, nchi ikapiga hatua kubwa ya maendeleo, pato la taifa likaongezeka wanaofaidika ni wananchi wanaoishi kwenye majimbo yetu ya uchaguzi. Kila Mtanzania (hata rais wa nchi hii) anaishi kwenye jimbo la uchaguzi, kwenye halmashauri fulani ya wilaya ama mji ama manispaa ama jiji. Kwa hiyo, mabadiliko yoyote yenye tija kitaifa humfaidisha Mtanzania huyu huyu akiwemo yule wa Magu. Uchumi ukipanda na ule wa mfukoni kwake utapanda, bei zikishuka pesa kidogo aliyonayo ataweza kufanya manunuzi mengi zaidi, kodi nyingi zikishuka mfuko wake utatuna na ataanza kufikiria kujenga nyumba, na kadhalika.
  Lakini pili, mambo hayo hayo yanayoonekana ya kitaifa zaidi bado pia yapo kwenye ngazi ya wilaya. Kwenye halmashauri zetu kumejaa wababaishaji wengi ambao hawafai kuwa watendaji na wanaweza tu kufanya kazi ikaonekana ikiwa kuna Mbwa wakali (watch dogs). Nikiwa kwenye kampeni zangu za ubunge wa Magu nitafanya juu chini kuwanadi madiwani wenye sifa na wenye uchungu na halmashauri yao kwa ajili ya kuja kuwa ‘watch dogs’ kwenye raslimali ya halmashauri yetu. Tutapiga vita kila aina ya ufisadi ili pesa za halmashauri zitumike kwa manufaa ya wananchi wa Magu”, alisema Mwigamba.
  Nilipomuuliza mbona mwaka huu Halmashauri ya Wilaya ya Magu imepata tuzo kwa kuwasilisha ripoti ya fedha kwa mujibu wa kanuni za kihasibu na hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwatunuku hati safi ya hesabu zao kwa mwaka wa hesabu 2008/2009, alijibu kama ifuatavyo:
  “Ni kweli Magu imepata hati safi mwaka huu lakini ndugu mwandishi napenda utambue kitu kimoja. Kutayarisha ripoti ya fedha kitaalam na kupata hati safi ni jambo moja na kubaini ubadhirifu wa mali ya umma ni jambo jingine. Halmashauri kupewa hati safi sio kigezo cha mwisho kwamba hakuna ubadhirifu katika halmashauri hiyo.
  “Ninamaanisha kwamba si ajabu mtu akapewa hati safi kwa kuwa alitumia pesa kununua gari ambalo lilipangwa kwenye bajeti, alifuata taratibu za ununuzi, na mkaguzi wa hesabu alikuta risiti ya malipo ya gari hilo lakini kumbe gari linalouzwa milioni 40 lilinunuliwa kwa milioni 80. Huo bado ni ubadhirifu wa mali ya umma. Nikiwa na shahada ya kwanza ya uhasibu, nitautumia vizuri utaalamu wangu kuanzisha ofisi ya mbunge itakayokuwa inawatumikia wananchi na kulinda haki yao kitaalamu.
  “Nitashirikiana na madiwani wa halmashauri yangu kwanza kuwapa elimu tosha ya mambo ya fedha na mambo ya kiutawala halafu kuwatia uchungu wa raslimali zao na kisha tusimamie kwa pamoja matumizi bora ya raslimali hizo kwa manufaa ya wana Magu. Ruzuku zinazotolewa kwenye ngazi ya kata na vijiji lazima zitumike kwa ajili ya wanavijiji na zitolewe taarifa za mapato na matumizi kwa wanakijiji wote, zikiwemo zile za shule za sekondari na msingi”, alifafanua Mwigamba.
  Pia aligusia masuala mengine kuhusu Magu kama ifuatavyo:
  Huduma ya maji
  “Kwa kiwango cha mapato ya halmashauri yetu, na kwa eneo la kijiografia la Halmashauri ya Magu, raslimali za wilaya zikisimamiwa vizuri wananchi wataondokana na umaskini. Tatizo la maji katika mji ambao uko chini ya kilometa 10 kutoka Ziwa Victoria ni jambo lisiloingia akilini. Nimeteseka sana na shida ya maji ya mji wa Magu kwa hiyo naijua vizuri sana. Nimeendesha sana baiskeli kuchota maji ziwani eneo la Bugabu na kwenye chemchemu ya Sawenge. Nalitambua vizuri tatizo hilo na najua namna ya kulitatua na tatizo hilo litakuwa historia kwenye maeneo mengi ya Magu.
  Kuboresha kilimo, upatikanaji wa chakula na kuondoa umaskini wa kipato
  Magu ina ardhi nzuri ya kilimo cha umwagiliaji na ukiachilia mbali maeneo mengi ya wilaya hiyo kuwa karibu na ziwa, pia yapo maeneo mengi tu yaliyopitiwa na Mto Simiyu ambao haukauki. Ni kiasi cha kuzingatia tu utunzaji wa mazingira na kuzalisha mazao na kuifanya njaa kuwa historia kwa wananchi wa Magu na kupata chakula cha ziada cha kuuza na kuingiza pesa.
  Ikiwa sera ya CHADEMA ni kuifanya Tanzania kuwa ghala la chakula la Afrika, mimi nanuia nikiwa mbunge nishirikiane na madiwani na watendaji wa halmashauri kuifanya Magu kuwa ghala la chakula la Mkoa mzima wa Simiyu na nje ya mkoa.
  Elimu
  Yako matatizo makubwa kwa upande wa elimu yanayoweza kutatuliwa kama Magu itapata mbunge makini atakayeshirikiana vema na wananchi. Matatizo kama ya nyumba za walimu, vifaa vya kufundishia na hata motisha kwa walimu ili waweze kukubali na kudumu kufanya kazi katika maeneo ya vijijini ambayo yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu.
  Mimi ni mwalimu, nimefundisha kwa miaka sita katika shule mbalimbali za sekondari, nazijua adha zinazowakabili walimu na wanafunzi kwenye mazingira ya shule. Nitashiriki kwa vitendo katika kutatua matatizo ya walimu na hata darasani nitaingia kufundisha kwa kuwa mimi ni mwalimu wa Hisabati na napenda kufundisha na nitafundisha maisha yangu yote.
  Lakini pia nataka kurudisha hadhi ya michezo ya Magu. Miaka ya tisini tulikuwa na timu kubwa mbili za mpira wa miguu na ule wa mikono. Timu ya mpira wa miguu Siba, ilifikia ligi daraja la pili kitaifa, ilivuma sana enzi hizo mojawapo wa washambuliaji akiwa ni mwalimu wangu wa hesabu shule ya Msingi Nyalikungu, Ramadhani Bernard Msengi.
  Wakati huo tulishuhudia timu kama Simba na Yanga zikija hadi Magu kwenye uwanja wa Mwanankanda kucheza na Siba.
  Nitafanya kila niwezalo na nina uhakika ndani ya miaka mitano timu zilizopo hivi sasa za Tinsela (ya wakubwa na ya watoto) zitakuwa tishio tena ndani ya ukanda huu kama ilivyokuwa Siba”, alisisitiza.
  Mwigamba alizaliwa Julai 7 mwaka 1975, ameoa na ana watoto wawili. Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Nyalikungu iliyopo mjini Magu, ambapo alifanya vizuri na kuendelea na elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Mazengo iliyopo Dodoma na baada ya hapo alijunga na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) ambapo mwaka 1999 alitunukiwa cheti cha juu cha ufundi mchundo katika uhandisi wa elektroniki na mawasiliano ya anga. Mwaka 2005 alijiunga na Chuo Kikuu cha Arusha ambapo alisomea shahada ya kwanza ya uongozi wa biashara (BBA) na kutunukiwa shahada mwaka 2008. Kwamba Mwigamba atakuwa mwakilishi wa Jimbo la Magu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu au la, hilo ni suala litakaloamuliwa na wakazi wa Magu, lakini kwa kutazama wasifu wa mgombea huyu, umahiri wake katika kujenga hoja na kazi kubwa aliyoifanya ya kukiimarisha chama chake jimboni humo pamoja na gumzo la kisiasa linaloendelea Magu, ni dhahiri kuwa Mwigamba ana matumaini ya msingi ya kuwa mbunge mpya wa Magu. Tusubiri tuone.
  Source: Tanzania Daima Jumatano 21 July 2010
   
 2. Ntemi Kazwile

  Ntemi Kazwile JF-Expert Member

  #2
  Jul 21, 2010
  Joined: May 14, 2010
  Messages: 2,145
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 135
  Hongera Samson kwa uamuzi makini. Ingawaje mimi siyo mpiga kura wa Magu lakini nakuunga mkono kutokana na misimamo yako ambayo umekuwa ukiionyesha kwenye makala zako mbalimbali.

  Kila la kheri
   
 3. Geza Ulole

  Geza Ulole JF-Expert Member

  #3
  Jul 21, 2010
  Joined: Oct 31, 2009
  Messages: 11,067
  Likes Received: 3,999
  Trophy Points: 280
  safii
   
 4. A

  Audax JF-Expert Member

  #4
  Jul 21, 2010
  Joined: Mar 4, 2009
  Messages: 444
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  tunataka mabadiliko kuanzia bungeni-sura mpya na mawaziri na wabunge wapy wanhitajika!!
   
 5. Mwanamayu

  Mwanamayu JF-Expert Member

  #5
  Jul 22, 2010
  Joined: May 7, 2010
  Messages: 7,945
  Likes Received: 2,090
  Trophy Points: 280
  Ni nzuri lakini angesema anakwenda kuwawakilisha wananchi wa Magu na sio kuikamata Magu!!!
   
Loading...