Bongo tunapendwa sana na Mungu Baba Mwenyezi. Kuna vitu alituletea kwa njia za Roho Mtakatifu. Yaani alitubariki kwa utajiri wa vitu vilivyoshuka kimiujiza. Unakumbuka vichwa vya treni? Ghafla tu viliingia bandarini na kila mtu akijiuliza vya nani? Baada ya kukosekana muagizaji. Na uzuri wa Roho Mtakatifu vile vichwa aliviandika kabisa jina la shirika letu la reli.
Sisi tumebarikiwa. Halafu Roho Mtakatifu alihamishia makazi yake kwenye mwili wa Raia Namba Moja wetu. Kila alipotembelea bandarini alikutana na magendo yanayotoroshwa. Mara ya mwisho alikuta magari ya wagonjwa yamepaki kibao kama kumbikumbi na hayana mwenyewe. Mungu anatuhusudu sana. Unakumbuka kontena za makinikia?
Yeye alijiendea tu kukagua uendeshaji wa bandari mara akakutana na lundo la kontena kibao za Makinikia. Akayazuia kindava na kuibua balaa kubwa zaidi. Ni dhahiri pale tulioneshwa kupitia raia Namba Moja kuwa kuna 'maibilisi' kibao waliopo kwa njia ya uwekezaji wanaotorosha utajiri wetu ambao tumezaliwa tukaukuta umejaa bwerere kila kona ya nchi. Huyo ni roho mtakatifu jamani alitenda miujiza.
Ila mbona siku hizi miujiza hii imetoweka kabisa? Au roho mtakatifu ametususa? Maana hata kupona kwa Tundu Lissu ukijiuliza kwa umakini kabisa utagundua kuwa mbali na madaktari pia mkono wa Roho Mtakatifu ulihusika kwa asilimia 90. Kuna haja ya kurudi kwenye maombi ili tuendelee kutendewa miujiza. Kama tulikosea atusamehe, na safari hii Roho Mtakatifu kwa mapenzi yako tuletee bunge jipya kimiujiza.