RIWAYA-MWALIMU WA ZAMU

RIWAYA-MWALIMU WA ZAMU

MSHILWANOGI

Member
Joined
Jun 5, 2011
Posts
11
Reaction score
7
Hii ni riwaya mpya ambayo itakuwa inawajia hapa kila ifikapo saa tatu usiku. Inaitwa MWALIMU WA ZAMU mwandishi wake ni JOHN WISSE


SEHEMU YA KWANZA

Usingizi unamruka. Anaamka na kuketi kitandani. Anatafakari mengi, lakini jicho lake linaishia kwenye saa iliyo ukutani. Ni saa kumi na nusu—bado nusu saa tu ifike saa kumi na moja alfajiri. Tabasamu linamtoroka utadhani katekenywa. Nusura kicheko cha nguvu kimtoke ila tu anakizuia baada ya kutambua pembeni yupo mkewe aliyelala fofofo.
Wakati anatafakari, mkewe pale kitandani kwanza ndo anageuka na kuutuma mkono upande ambao mmewe alikuwa kalala. Patupu! Anakumbana na mto ukiwa umejaa huzuni kwa ukiwa. Anazungusha tena mkono kama alivyozoea, lakini hakukuwa na mtu. Mke anaangaza macho upande wa pili wa kitanda. Anamwona mmewe kaketi upande wa pili wa kitanda—kwenye ncha pembeni kabisa akiwa kifua wazi.
“Bravius, mbona unanifanyia hivyo?” anauliza Benigna.
“Kukufanyia nini?” Anafoka utadhani kachomwa mkuki jichoni.
“Jamani mme wangu, leo siku ya ngapi? Si lolote—si chochote! Unatatizo?” Anahoji tena Benigna. Anaketi kitandani na kusogea kwa mumewe. Anaegama mgongoni na kumpapasa huku akipumua kwa huba. “B’ unajua nipo taabani, siwezi kuvumilia.” Anatazama ukutani. Mishale ya saa inamstaajabisha kabisa. “Hivi Bravius, tayari kumekucha ama saa inaniongopea?”
“Kumeshakucha tayari! Too late Benigna!”
“Hapana! Bado saa moja na nusu—muda huu unatosha kabisa kuzipunguza shida zangu.” Anamvuta Bravius. Anambusu na kubaki taabani kamganda. “Please B’ naomba jamani…!”
“Heee! Nimesema it’s too late Benigna. Nawahi kazini mpenzi. Unajua nipo zamu na inanipasa niwahi kuliko wote. Wiki hii yote nivumilie tu. Ikiisha nitakuwa sawa. Sipo sawa kisaikolojia kabisa—wajua kazi za watu zinavyotia uchovu. Unasimama mwanzo mwisho na hakuna muda wa kupumzika. I have no feelings honey! Please, ngoja mwisho wa wiki nimalize zamu.!”
Benigna anabaki njiapanda. Chozi linatoroka machoni. Anauchukua mto na kuurusha kama mtu aliyepandwa wazimu. Analia tena na tena. Anajikunja kama paka wakati wa baridi. Kilio cha kimyakimya kinamvaa. Bravius hana habari. Anamtazama mara moja kisha anasimama. Anapiga hatua hadi kwenye taulo lake. Anaondoka na kuingia bafuni kwenda kuoga.
Baada ya kuvaa kisha kujifukiza manukato ayapendayo, Bravius anachukua mkoba wake wenye vitabu na madaftari. “Baby—tutaonana jioni!” Anapiga hatua kutaka kuondoka. Benigna ananyanyua kichwa kumtazama.
“Hivyo ndivyo huwa unaniaga Bravius! Si vizuri kunipa adhabu kama hii. Unajua fika nilitoka kwetu si kwa ajili yoyote zaidi yako.” Bravius anamtazama tu na kuurudisha mlango, unajibamiza. Anatoka na kwenda ikiwa saa kumi na moja kasoro robo. Benigna anabaki akiugulia kitandani kwani anaamka na kuizima taa kisha anarudi kulala akiwa kajawa joto la huba lisilopozwa na barafu wa moyo wake.
Bravius analazimika kutembea kwa miguu, kushoto kisha kulia anaharakisha. Anayo nia yake kuu moyoni na kule aendako. Je, anawahi kweli kwenye zamu yake ama ana mahali anakwenda? Maswali hayo yanajibiwa kwa simu anayoipokea Bravius. “Hello Be’lle!”
“Unakuja ama bado umeatamiana na huyo kiberenge wako?”
“Come on Be’lle! Hivi huwezi tu kusema jambo bila kumtaja?” Anasema Bravius.
“Jibu—unakuja ama la!” Anafoka Be’lle.
“Nipo njiani, nakaribia—jiandae tu!”
“Ushaoga ama nikuandalie maji?”
“Kila kitu tayari. Nimeoga nawe--!” Anajibu Bravius. Anasindikiza kwa busu jibu lake. “Be’lle, usiku mmoja utadhani mwaka vile. Naona kama nachelewa vile,” anasema Bravius.
“Acha maneno mengi. Nakungoja ujue. Mlango uko wazi, just push it utanikuta nipo tayari kukungoja,” anajibu Be’lle.
Bravius anakazana kutembea utadhani katiwa gia miguuni. Anapiga kona ya kwanza na kuzipa kisogo nyumba za majirani na pale aendapo. Anavuka barabara na kuchepuka upande wa pili. Anatazama kule atokako—kote hakuna dalili ya mtu yeyote. Jimbi wanasikika kuwika kutokea mbali na mji, bado giza li zito. Baridi ya masika inatambaa na radi zinalichana anga.
Bravius anapiga hatua ndefundefu, anaingia kwenye kichochoro na kuambaa hadi kwenye nyumba moja iliyo kama mabehewa ya gari moshi. Anasimama kwenye chumba kimoja cha katikati. Anasukuma mlango na unakubali kufunguka. Anaingia lingali giza wala hakuna umeme tena kwani hali ya hewa imetishia na umeme umekatika.
“Brav--!” Anaita Be’lle.
“Naam! Nimefika.” Anaufunga mlango. Anapopiga hatua moja kwenda pembeni kidogo, anagonga ndoo zilizokuwa pembeni. Anawasha tochi ya simu yake na kuona. Hapo anavua viatu baada ya kukitua kimkoba chake cha daftari kwenye kochi moja lililo pembeni.
“Umeme tena umekatika, loh!” anauliza Bravius.
“Heri wakate tu ili usiku uzidi kuwa mkubwa. Kwanza natamani tu hiyo mvua ishuke na itandike hadi saa nne ama saa nane kabisa,” anasema Be’lle.
“Ili iweje sasa? Hutaki niende kazini?”
“Utaenda ikikatika. Unadhani wao hawajui kama kuna mvua?”
“Acha porojo bwana.” Be’lle ananyanyuka na kumfuata Bravius alipo. Anamvua shati na kila alichokivaa na kumkokota kama mbuzi kwenda kitandani. Tochi ya simu anaizima na giza linakimeza chumba. Kelele hakuna tena zaidi ya ala za mdomo na ndimi zasikika gizani. Muziki wa chaga za kitanda kibovu kilichozidiwa uzito wa watu wawili unasikika utadhani kuna mtu anaendesha baiskeli iliyokauka grisi kwa muda mrefu. Pumzi kama zile za gari moshi na wakati kama kinanda zinasikika. Hakuna kingine kinachosikika sasa zaidi ya sambo za kama mzazi auguliaye uchungu na mara kadhaa miguno ya fisi walao uozo kwa siri zinasikika. Hatimaye kimya! Hakuna mtikisiko zaidi ya pumzi za watembea mbio kutoka mbali. Wanastarehe baada ya safari ya huba kwa takribani kilomita saba wakiwa barizini.
Baada ya dakika kupita, mmoja anagutuka. “B’ acha nitoke nje kwanza.”
“Nje—na giza hili?” anasema Bravius. Be’lle kanyanyuka tayari na kuikwapua simu baada ya kupapasa.
“Nahisi mkojo umenibana hatari!”
“Fanya haraka bwana kabla wazungu hawajapandwa mashetani!” anasema Bravius akiwa na lepe la usingizi. Be’lle anatoka na simu ya Bravius akielea nje kuliko na maliwato ya pamoja katika nyumba hiyo. Anakikopo cha maji mkononi na simu inayommulikia mkono mwingine. Anaurudishia mlango na Bravius anaendelea kulala akitafakari namna alivyoupanda mlima na kuushuka.
Msalani simu inaita. Be’lle anaipokea na baada ya kuwa kaongea ndipo anabaini kuwa kafanya kosa kubwa. Anatazama aliyepiga baada ya kuikata na kujua fika kuwa ni Benigna anapiga. Anaiminya na kuizima kabisa kuepa kukatishwa starehe yake. Anaendelea kufanya yake kwenye kigiza hapo na radi zinakazana na kummulikia. Kwa bahati, umeme unarudi. Bravius ananyanyuka na kujivisha kibukta chake. Anaelekea kwenye kapu lililopo pembeni ya kitanda kile. Anafukunyua harakaharaka, akitafutacho ajua yeye. Hatimaye macho yanakutana na kikasha cha ‘Rough Rider!’ Anastaajabu! ‘Hii sijawahi kuitumia mimi, nani kaitumia na imebaki moja tu?’ Anajihoji Bravius wakati akizidi kusinyaa na joto kumshuka. Taharuki fikrani.
Pekupekua yake inamkutanisha na kadi ya kliniki. Anaichukua na kuisoma haraka baada ya kuigeuzageuza. Ni kadi ya kliniki ya mwathirika wa UKIMWI. Bravius upekupeku wa kumchungua bata sasa unampa kiwewe. Anahisi joto kali linamkaba. Baridi haihisi tena! Kacheza kigodoro cha huba kama mswaki mdomoni. Anaposikia mlango unalalama kuwa Be’lle anarudi, haraka anarudisha kila kitu mahali pake.
Anajilaza kitandani. Be’lle anaingia na kuzima taa. Anatembea hadi kitandani na kuketi kwa sekunde chache kisha anapapasa na kushika kopo la losheni na kujipaka rasharasha. Anaingia kitandani akiwa na mzuka wa kusafiri tena kama awali.
“B’ nipo sawa sasa. Dereva kazi kwako safari kunifikisha salama!” Anasema Be’lle. Kimya! “Baby, umelewa na kulala ama!” anauliza.
“Heri ningelewa, ila nimeelewa!” anajibu Bravius. “Basi tu—!” Anakuwa mnyonge.
“Mbona unaonekana kuwa mnyonge tena? hujafurahia ama kuna nini? Na huko kuelewa umeelewa nini tena?” Anadodosa Be’lle.
“Sikia Be’lle! Nilipolala kidogo hapa na kutaka kuchukuliwa na usingizi, nimeota ndoto mbaya sana,” anasema Bravius kwa unyonge. Be’lle anampapasa na kumkumbatia.
“Mahabuba—nini umeota tena?”
“Nimeota kuwa una mtu mwingine zaidi yangu—mwanaume.”
“Mwanaume!” anastaajabu Be’lle.
“Ndiyo—nimeota kuwa una mwanamme mwingine. Na katika maisha yako nayeye huwa mnakutana nikiondoka na mnatumia mipira! Nimeota nimekukuta naye tukapigana sana ukaniaibisha kwa watu hapa mtaani.”
“Oh! Pole mpenzi. Hiyo ni ndoto tu mbaya,” anasema Be’lle!
“Hapana, huwa sioti ndoto burebure! Jambo lililoniumiza zaidi ni katika kupigana kwetu, ukanichamba sana na ukaniambia kuwa wewe ni mwadhirika wa UKIMWI,” anasema Bravius. Be’lle anashituka.
“Bravius! Hivi una nini leo?” Wewe ni mchawi ama ni nini?”
“Niambie ukweli Be’lle! Kuna mambo unanificha,” anasema Bravius.
“Bravius nakupenda sana. Lazima nitakuwa muwazi kwako. Nilikuwa na mtu kweli kabla sijakupata. Lakini tangia hapo sijawahi kuwa na mtu tena, ni wewe tu!” anajitetea Be’lle.


Je, kweli Be’lle ni mgonjwa wa 'Juliana' ama kuna namna tofauti na vile Bravius anawaza.
Je, Bravius atachukua hatua gani? Je, atapandwa wazimu na kufanya kitu kibaya ama atafurahia baada ya kuujua ukweli uliojificha.

TOA MAONI YAKO KAMA UNAHISI ITAKUWA NA MANUFAA KUITOA HAPA ILI JAMII IPATE KUJIFUNZA.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom