SEHEMU YA 61
Alihangaika kumtafuta kwenye kila pembe ya shamba la Fuad huku akijua hakika hawezi kumwona.
Baada ya muda mrefu Kijakazi alirejea kwa Fuad akamkuta amekaa ukumbini.
“Sikumwona Bwana!”
“Hukumwona? Ng’ombe we! Nimekwambia usirejee hapa mpaka umwone!”
“Lakini, Bwana......”
“Lakini, lakini, lakini nini?”
“Lakini, Bwana, nimemtafuta kila pahala sikumwona!”
“Umekwenda kibandani kwake?”
“Nimekwenda kila pahala, Bwana! Hakuna pembe ya shamba hili niliyoibakisha, lakini sikumwona!”
“Ahaa! Hukumwona sio? Mwachilie mbali! Lazima amekimbia hapa na mimi nitakwenda kumwona baba yake. Mzee Sharwan, nimuhadithie kila kitu,” Fuad alisema, lakini sasa kwa sauti ya chini.
“Umari je, umemwona po pote?”
“Umari nimemwacha kule bondeni anapalilia mpunga,” Kijakazi alijibu.
“Nenda kamwite basi!”
Kijakazi alikuwa amechoka lakini, ndio yumo katika utiifu; kumtii Bwana wake. Bila ya kupoteza wakati alikwenda mpaka kule alikokuwa Umari.
Alimkuta Umari ameshughulika, tumbo wazi. anapalilia mpunga.
“Umari, Bwana anakwita.”
Umari aliinuka na kujiuyosha, kijasho kinamtoka. Ali mtazama Kijakazi na halafu akatikisa kichwa.
“Kwani Kijakazi hunioni kama mimi nina kazi mkononi?” Umari aliuliza.
“Nimemwambia kuwa unapalilia mpunga lakini kanituma nije nikwite,” Kijakazi alijibu.
“Nenda kamwambie sitaki,” Umari alisema.
“Ah! Mimi sitoweza kumjibu hivyo!” Kijakazi alisema.
“Usiogope, Kijakazi, nenda kamwambie hivyo hivyo. Usimwogope yule, Kijakazi: wakati wake umekwisha, na sote hapa tunangojea siku ifike tuondoke. Labda utabakia wewe peke yako hapa, Kijakazi.” Umari alisema huku akitabasamu,
Mbio, Kijakazi alirudi na alipofika alimkuta Fuad amekaa pale pale ukumbini.
“Yuko wapi?” Fuad aliuliza kwa hamaki.
“Anasema... anasema...” Kijakazi hakuweza kusema kama alivyoambiwa.
“Anasema nini?” Fuad aliuliza huku amesimama baada ya kuondoka kwa ghafla juu ya kiti alichokuwa amekalia. “Anasema nini?”
“Arasema hataki!” Kwa khofu Kijakazi alijibu.
“Hataki? Anathubutu. kujibu hivyo? Mwachilie mbali; leo ndio mwisho wake ndani ya shamba hili.”
“Basi, wewe Kijakazi nenda ukafanye kazi zako na huyo Umari akija tutaonana mimi na yeye.”
Kwa hakika Fuad mwenyewe alikwisha kuelewa kwamba siku zake zimekwisha ila alijikaza kisabuni tu. Kila mmoja katika watanyakazi wake alikwisha yajua hayo isipokuwa Kijakazi.