SEHEMU YA 29
“Basi Bwana Marijani nd’o kama tulivyokwisha zungumza huko ofisini kwako. Sisi tunakusubiri hapa kwa hamu kubwa na siku ya leo ni siku ambayo tumeisubiri siku nyingi. Wenzangu wana mengi wanayotaka kujua, kwa hiyo, baada ya kuwazungumza nafikiri bado watakuwa na maswala mengt ya kukuuliza.”
“Sikilizeni,” alianza Marijani, amezungukwa, amewekwa kati kati kila mtu ana hamu ya kumsikiliza atasema nini. “Shida mlizo nazo nyinyi nd’zo shida walizo nazo wakulima wote nchini. Kuna wengine, shida zao zimezidi zenu kwani wao washafukuzwa mashambani. Mimi mwenyewe kwetu ni shamba, kule Donge, na ijapokuwa sasa naishi mjini wazec wangu bado wako huko huko na nawatembelea kila wiki. Kwa hiyo, matatizo yenu nayaelewa vizuri.”
“Lakini Bwana...” alisema mkulima mmoja lakini mara Marijani alimkatiza maneno yake.
“Sikilizeni tafadhali msiniite Bwana, Mimi ningelipendelea mniite ndugu, man’ake naona fahari zaidi kuitwa hivyo.”
Marijani aliendelea na maneno yake. “Sisi tuna mipango madhubuti kuhusu maisha ya wakulima kwa jumla Si kama tunataka kukudaeni kwa mabwana shamba halafu wao wakuoneeni huruma, hasha. Wao hawana huruma, na haina maana kuzitaka huruma pahali zisipokuwa. Tuna mipango mizuri zaidi ya hapo baadaye, lakini habari hii tutazungumza tukisha fahamiana vizuri. Jambo muhimu ambaio napenda mlijue ni kwamba wakulima wote waliofukuzwa mashambani washapata ardhi na wanaendesha maisha huko na kila atakaye fukuzwa kutoka kwa bwana shamba atapatiwa ardhi ya kumtosha.”
Wote walikuwa wakisikiliza kwa hamu, wamemfumbul’a macho ili wamwone katika giza lililokuwa limetawala usiku huo. Kimya; mara moja moja tu ilisikika sauti ya bundi au ya komba, wakiimba baada ya kunyvva tembo. Marijani pekee ndiye aliyekuwa akisema. Kila alipopita mtu kwenye mkutano wao wa siri Marijani aiikatisha mazungumzo yake mpaka mtu huyo atoe salam, ajibiwe na aende zake.
“Mnajua ndugu; sasa sina budi niondoke nirejee mjini mana’ke wakin.’ona napita usiku huu pale polisi Mwera wataanza matala yao,” Marijani aliwaambia wenzake.
“Nani hao walakaokufanyia matata?” aliuliza Vuai.
“Askari wanatutabisha sana, lak’ni haidhuru!”
“Basi ye yote katika nyinyi akipata nafasi anaweza kupenya na kuja mjini siku yo yotc ile,” alisema Marijani huku akiwashika mikono na kuaga.
Marijani na Vuai walikutana tena na tena hapo Kijangwani na walipanga mipango mingi. Kila alilozungumza na Marijani, Vuai aliwaarifu wenzake na mahusiano kati ya ofisi kuu ya wakombozi wa wananchi yalikuwa mazuri.
Haya yote yalifanyika kwa siri bila ya Fuad kujua. Si kama kwamba hakuielewa ile chuki iliyokuwapo kati ya wakulima na mabwana shamba katika nchi kwa jumla. Aliloshindwa kufikiria tu ni kwamba lingekuwapo vuguvugu la mwamko wa wakulima na zaidi ya hivyo kwamba hilo vuguvugu lingewakumba hata watwana wale shamban’ kwake.
Baada ya mwezi tu tokea Marijani kuonana na kikundi cha wakulima wa huko Koani, wakombozi wa wananchi walitangaza kuwapo kwa mkutano mkubwa hapo hapo Kijangwani mbele ya ofisi yao. Siku hiyo Fuad naye alikuwa na safari ya kwenda mjini, sio kwa sababu ya kuhudhuria mkutano huo, bali kwa sababu ya kufuatia starehe zake.