Riwaya Kali Sehemu ya 3

Riwaya Kali Sehemu ya 3

Man_Sai

Member
Joined
Aug 24, 2016
Posts
8
Reaction score
8
1473144895139.jpg



RIWAYA: Jina
NA: Frank Masai
SEHEMU YA 3.

ILIPOISHIA.

Pale alipoirusha, alijikuta akitumia nguvu nyingi ambazo zilimfanya asogee mbele kidogo ya Frank, na kwa kuwa alimkosa mtu aliyekusudia, basi ikawa adhabu kwake.
Frank baada ya kupinda kwenda nyuma na fimbo ile kupitiliza, alijiinua kwenda mbele huku mguu wake akiurusha kwa nguvu kwenda kwenye kifua cha yule mrusha fimbo. Teke kali likamkuta yule jamaa, na bila kutegemea, hata yule wa nyuma yake ambaye alikuwa kashika fimbo, naye alikumbwa na mwili ukiopigwa teke na Frank Masai.
Hapo wale waenyeji wengine ndipo walipoamua kuinuka huku kila mmoja akitayarisha silaha yake hasa visu na viti. Na bila kuchelewa wakamvamia Frank kwa fujo nyingi, lakini walichokutana nacho, sidhani kama maishani mwao wamekisahau.

ENDELEA.
Walipata mapigo ya kushtukiza ambayo kwa mtu anayejua mapigano, anaweza akahisi mtu anayepigana naye ni mchawi au labda ni Ninja.
Wakati jamaa wale wanakuja kwa kasi kumvamia Frank, ndipo Frank alichomoa vitu kama nyota kutoka nyuma ya mgongo wake. Nyota zile alizirusha kiustadi na kuhakikisha kuwa haziwadhuru sana wale wanaomvamia. Alikuwa hana haja ya kuwaua, hivyo alizirusha zile nyota ambazo zilikuwa na makali kama ya wembe, alihakikisha zinatua kwenye miguu yao na kutoboa kidogo ili wayasikie maumivu.
Jamaa wale ambao walikuwa kama kumi na tano, walijikuta wakishindwa kumvamia Frank na kubaki wakichechemea na kutoa kilio kikali cha maumivu. Kilio hicho kikaibua walinzi wengine ambao walikuwa wanafanya ufuska kwenye vyumba vilivyopo kwenye Casino lile.
Ghafla eneo alilo Frank likajaa mijamaa iliyokuwa imejaa miili yao mithili ya watunisha misuli. Hapo Frank ndipo alipowaonesha kuwa yeye si mtu wa kawaida katika tathnia ile ya mapigano.
Kabla wale jamaa waliokuja mara ya pili hawajakaa vizuri, Frank alikimbia hatua fupifupi hadi pale walipo na kuanza kuwapa mapigo ya kushtukiza.
Alikuwa anapiga mateke pamoja na ngumi za nguvu kwenda kwenye mabega yao, ambayo nayo yalisaliti amri bila tabu kwa kutenguka.
Yalikuwa ni mapigo ya hatari ambayo kwa akili ya wale walinzi, walihisi wanaweza kuyaona kwenye video tena Jet Li au Donnie Yen ndiye awezaye kuyapiga. Lakini haikuwa hivyo, yote yalikuwa ni kweli, mapigo hayo yaliwaingia vema mwilini na kujikuta wakiteguka mabega yao.
Dakika chache mle kwenye casino watu wakawa wanagalagala kwa maumivu makali yaliyo miilini mwao. Frank akawa kasimama wima huku akiwa kaangalia chini na kukunja ngumi yake ya kulia iliyokuwa inategua mabega kama haina akili nzuri.
Akili ya Frank ikaona tayari kishaondoa vikwazo ambavyo vilikuwa vimemkabili. Akanyanyua uso wake na kuangalia mbele tayari kwa kuelekea katika ule mlango aliokuwa kadhamiria tangu mwanzo kwenda.
Aliponyanyua uso wake, hapo alikutana na sura nyingine ya kivietnam lakini hii ilikuwa kidogo imetulia na kujiamini. Haikuwa na mwili mkubwa kama za wale jamaa, na wala ilikuwa haina papara au kujishauri kama wale jamaa wa kwanza. Huyu alikuwa akimtazama Frank kwa macho ya utulivu na ya kijanja zaidi. Frank kama kawaida yake, akadharau na kurudisha macho yake chini.
Kitendo cha kurudisha macho chini kwa Frank, ni kama anavuta kasi, na mtindo huo aliupata kwa mkufunzi wake wa mapigano. Yule bwana akiyekuwa kasimama umbali mdogo toka pale kwa Frank, alishausoma huo mchezo kabla hata Frank hajafika pale. Kifupi jamaa yule, anazijua mbinu za Masai.
Frank alipoinamisha kichwa chake chini, jamaa kwa spidi ya ajabu, alichomoka huku viatu vyake vya raba vikiwa havitoi sauti wala mshindo wakati anakimbia.
Mwanaume kuja kuangalia mbele, akakutana na mateke mawili yaliyopigwa juu kwa juu na bwana yule. Na mateke hayo yalitua kifuani na kumfanya Frank kuyumba kidogo kabla hajakaa sawa. Lakini wakati anahangaika kujiweka sawa, ndipo alipokutana na zimwi lilelile linalokuja kasi kama mzimu.
Ngumi tatu zikatua kifuani na tumboni kwake. Akarudi nyuma huku maumivu ya mapigo yale yakiwa yaneingia vema mwilini mwake. Ikabidi sasa awe macho kuliko kutumia mtindo wa kuangalia chini mbele ya jitu linalosogea kwa hatua za haraka kama treni ya umeme.
Akajiweka sawa Masai, na kisha akakunja ngumi tayari kwa mpambano na mtu yule ambaye ni wazi Frank alijua tayari kakutana na size yake.
Jamaa yeye alikuwa hakwepeshi macho katika uso na mwili wa Frank. Hata pale Masai aliposogea mbele ili akamvae, naye alisogea mbele tayari kwa kumvaa mwaume wa shoka.
Miili ya wababe wale, ikakutania katikati ya ukumbi wa casino lile. Frank akarusha ngumi moja ya kwenda mbele (straight punch), jamaa yule akaikwepa kwa kuinama kidogo. Akawa kafanya kosa kubwa kupita maelezo, kwani mkono mwingine wa Frank ulinyanyuka kwa kasi na kwa nguvu na kumfumua jamaa chini ya kidevu, ngumi ile mitaani wanaiita KATA FUNUA au BLOCK BUSTER . Ilimkuta kidevuni yule jamaa na kumfanya apae juu kama kindege kilichopigwa jiwe la manati. Hata kabla hajatua chini, kidume akawa kafika eneo ambalo yule jamaa atatua. Na pale alipotua, jamaa alijikuta akichezea mtama mzito ambao ulimfanya adondokee mgongo.

Frank kwa hasira, akanyanyua mguu wake wa kulia ili amkinde yule jamaa pale chini alipolala baada ya ule mtama. Lakini hilo likawa kosa kwa kwake. Yule jamaa akatumia nafasi hiyo kuharibu mpango wake wa kuendelea kumuumiza.
Mguu wa Frank ukiwa juu, jamaa akategua mguu uliokuwa umekanyaga chini na kumfanya Masai naye adondoke. Pale alipodondoka, jamaa akarusha teke lingine zito akiwa palepale chini. Teke hilo lilikwenda kifuani na kumfanya Frank aserereke kama kwenye barafu, kitendo kilichofanya wale jamaa wengine waliokuwa wanagalagala kusogezwa pembeni wakati mbabe wao anavoserereka.
Mwisho wa safari ya Frank ulikuwa ni kufikia chini ya pool table. Yule jamaa akajibetua kiustadi kwenda mbele, na hapohapo akasimama tayari kwa kumkabili tena mwanaume ambaye alikuwa anagugumia kwa maumivu.
Hatua za haraka haraka, zilipigwa na yule jamaa na kitendo bila kuchelewa, Masai alijikuta akichezea mateke mengi ya tumboni huku bado akiwa pale pale chini ya meza ya kamali.
Hali ikawa mbaya kwa kijana yule wa Kiafrika mbele ya yule Muasia. Na kama angeendelea kulemaa, basi yule Mvietnam angempasua bandama au angevunja baadhi ya mbavu. Akili ya haraka ikamwijia na kujikuta akidaka mguu wa yule jamaa, na kwa haraka akaurusha kwa nguvu kama anamkata mtama kwa kutumia mkono. Hapo jamaa alipaa juu na kwa bahati nzuri akadondokea mgongo juu ya lile pool table. Kitendo bila kuchelewa, Masai akanyanyuka haraka na kumkuta yule jamaa akigaa pale juu ya pool table. Akaruka sarakasi ambayo sarakasi hiyo ilikuwa pigo la hatari kwa yule mvietnam. Kwa sarakasi ile, Frank alijikuta mgongo wake upo juu ya kifua cha jamaa yule ambaye alianza kukohoa kwa maaumivu aliyokuwa anayapata kifuani. Frank akazidi kumpa kisago yule boya wa Kievitnam. Safari hii alisimama juu ya pool table lile na kisha akampiga teke ambalo kama ulifanikiwa kumwona alivyompiga, waweza sema jamaa kampiga kama mpira wa miguu.
Mvietnam akalanda kama feni baada ya kupigwa lile shuti, na moja kwa moja akaenda kudondokea kwenye meza ambayo ilikuwa imejaa vinywaji vya bei ya ghali. Hata kabla jamaa hajayakimbia maumivu ambayo alikuwa nayo, alijikuta bado yupo mikononi mwa Frank ambaye alishuka pale juu ya pool table kwa sarakasi ya upande upande iliyodhihirisha jamaa kaiva si kitoto.
Jamaa akiwa pale juu ya meza, alishuhudia teke lingine kali likitua kifuani kwake na kumpeleka mbali zaidi kuliko lile teke la mwanzo.
Frank akasimama wima na kumsibiri yule kichaa anyanyuke. Na jamaa ni wazi alikutana na jitu la hatari. Sidhani kama kawahi kupapambana na mtu mweusi ambaye anapiga mkono kama Frank Masai. Angekuwepo leo, tungesema Ni Shida.
Kwa hasira, jamaa akapiga sakafu aliyoilalia ngumi nzito kuonesha hasira, na kisha akanyanyuka na kuanza kumfata mtoto wa Masai pale alipo.
Ile kumfikia, akaanza kurusha mateke ya nguvu ambayo yalikuwa yanalenga zaidi uso wa Frank. Lakini ni kama alikuwa anajichosha tu. Mateke mengine yalipiga hewa na mengine yalipanguliwa kiustadi na Masai.
Teke la mwisho kwa jamaa yule alilirusha lakini Frank aliliona na yeye akarusha lake kiustadi kama jamaa alivolirusha, mateke yakakutana juu kwa juu na kufungana kama kamba.
Pale jamaa alipojaribu kuuchomoa mguu wake, hakuweka kuutoa kwa kuwa Masai aliudhibiti kwa kuubana.
Jamaa baada ya kuona zoezi lake limebumba, akaanza kumrushia Frank ngumi ambazo kama kawaida yake, alizitolea nje huku bado kaubana mguu wa mpinzani mwenye hasira.
Sijui alijichanganya vipi yule jamaa, akarusha ngumi ambayo Frank aliikwepa na kisha mtoto huyu wa Masai akarusha yake kwa nguvu na kumpiga puani. Damu zikatapakaa puani kwa jamaa. Hata bado hajatokwa na mawenge ya ngumi ile nzito, alijikuta mguu wake uliobanwa ukivutwa na bila kupenda ukavutika. Hapo Frank aliuachia mguu ule huku akiruka kwa teke lile lililochini na kumpiga nalo kifuani na jamaa akapaa kama kapigwa bomu au kombora.
Frank akatua chini na kujiweka sawa huku begi lake bado likiwa mgongoni na mkononi akiwa katanguliza ngumi ya kulia ambayo ilimmwaga mchuzi yule Mvietnam.
"Pa pa pa pa pa. Umewiva Chude Bobo." Ni sauti iliyoongea kwa Kiswahili fasaha ikija baada ya makofi kadhaa yakiyopigwa kumpongeza.
Frank akashtuka baada ya kusikia Kiswahili katika eneo lile la Kivietnam. Na mbaya zaidi kaitwa jina ambalo ndilo linawafanya FBI, CIA na FISSA wasilale.
Akanyanyua uso wake kuelekeza kule ambapo palitokea sauti ile. Hapo alipata hamaniko baada ya kuiona sura ambayo alikuwa anaijua sana tu.
"Ni wewe Malocha?" Frank akamuuliza yule mtu aliyemuita.
"Hakuna chuki mbele ya upendo. Hakuna upendo mbele ya chuki. Chuki huja....." Yule jamaa aliyeitwa Malocha, alianza kuongea hayo. Na kabla hajayamaliza, Frank akayadakia na kwa pamoja wakajikuta wanayatamka kwa pamoja.
".......Huja baada ya upendo wa ukweli kupotea baina ya mioyo ya watu. Chuki ni kimelea kibaya ambacho kama kikiingia mwilini mwako na kumea, basi mwisho wake huwa mbaya. Mwanzo wa chuki huwa ni upendo uliopitiliza kwa watu fulani kuliko watu fulani. Mwanzo wa chuki huanza kutokana na matabaka ambayo binadamu tunayajenga." Wakamaliza kuyaongea maneno hayo ambayo yalimfanya Frank kusogea mbele kwenda kwa Malocha huku kachanua tabasamu la haja.
Akaruka watu kadhaa ambao walikuwa wanaendelea kuuguza mle ndani. Na alipomfikia Malocha, akamkumbatia kwa nguvu na wote kwa pamoja wakawa wanacheka kwa furaha

Watch Out Part 4
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom