Tubandikie tuisome tuweze kujadili
Ridhiwani: Viongozi
CCM hawawajibiki
*Asema tatizo lao ni kukwepa lawama
*Atamani CCM ya Mwalimu Nyerere
*Amsifu Mzee Msekwa kwa ukomavu
*Azungumzia sakata la malipo Dowans
Na John Daniel
MIEZI michache baada kumalizika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka jana, Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Ridhiwani Kikwete, amesema hali ndani ya chama hicho si shwari kutokana na viongozi wake kushindwa kutimiza wajibu wao kwa kukwepa lawama.
Akizungumza na gazeti hili wiki hii katika mahojiano maalumu Bw. Ridhiwani ambaye pia ni mtoto wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alitaja mambo mengine yanayotishia mustakabali wachama hicho kuwa ni ubinafsi na kushuka kwa nidhamu ndani ya chama.
Alisema kutoka na hali ilivyo sasa ndani ya chama hicho anatamani CCM ingekuwa ile aliyoiacha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
"Katika kampeni za mwaka jana nilijifunza mambo mengi mazuri, lakini kikubwa zaidi ni kwamba chama (CCM) kinahitajia mabadiliko makubwa, nawaomba sana viongozi watusaidie wanapeleka wapi nchi? Watusaidie sisi vijana,"alisema Bw. Kikwete.
Aliendelea,"Mfano rahisi wakati tunaanza kazi ya kuzunguka nchi nzima, yalikuwa ni maamuzi ya UVCCM na tulikuwa na makundi manne moja likiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Beno Malisa, Nyingine Katibu Mkuu Martin Shigela na nyingine Bw. Mfaume.
Lakini baadaye yalianza maneno mara ooh! chama kimebinafsishwa, hakuna hata kiongozi aliyesimama kutoa ufafanuzi huo wa kweli, matokeo yake wanachi wakajenga dhana mbaya, sasa hii tunaelekea wapi? Alihoji.
Alisema kutokana na hilo alijifunza kwamba viongozi wa CCM wanakwepa majukumu yao na wanaogopa aidha kulaumiwa kwa kusema ukweli.
Alitaja jambo la pili alilojifunza kuwa ni viongozi wengi kushindwa kueleza mazuri yaliyofanywa na serikali katika kipindi cha miaka mitano hivyo kuwafanya wananchi kuelewa kwa usahihi matunda ya utawala.
"Mfano barabara nyingi zimetengenezwa, mikopo imetolewa, ruzuku ya mbolea na zana mbalimbali za kilimo pamoja na mbegu bora zimetolewa kwa fedha nyingi lakini vijana wamekaa vijiweni wanasema hawana ajira.
Kilichotakiwa ni viongozi kuwaelimisha kuwa serikali imefanya hayo ili sasa wao wenyewe sasa waongeze uzalishaji na kujiajiri, kama mtu alikuwa akizalisha tani moja na kuuza kwa bei ya chini sasa azalishe tani 10 na kusafirisha na kuuza kwa bei ya juu maana miundombinu imeimarishwa,"alisema .
Alisema kutokana na viongozi kushindwa kuwaelimisha wananchi mambo yaliyofanywa na serikali na kutoa mwanga wa jinsi wanavyoweza kujinasua katika umasikini, vijana wengi wamebaki na wimbo wa kukosa ajira.
Alisema amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya viongozi kugongana kauli katika tukio la maandamano yaliyozuiliwa Arusha huku akimwagia sifa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Bw. Pius Msekwa kwamba majibu yake ndiyo yaliyoonesha ukomavu wa uongozi katika suala hilo.
"Mimi ni kijana niliyekulia ndani ya CCM, nimeanza kushiriki mambo ya chama nikiwa shule ya msingi kama chipukizi, mtu asije akadhani nimeanza jana wala leo.
"Siku zote CCM inatoa kauli kupitia vikao, Mzee Msekwa peke yake ndiye aliyejibu vizuri kuhusu sakata la Arusha kuwa 'tusubiri kikao kitatoa kauli' wengine walitoa kauli za ajabu ajabu huku wakipingana wao kwa wao, natamani sana CCM aliyoacha Mwalimu Nyerere, kwani wakati huo kila kitu kilisemwa kupitia vikao,"alisema
Alitaja changamoto nyingine aliyojifunza katika uchaguzi wa mwaka jana kuwa ni wagombea kushindwa kuvunja makundi yao na kuyahamishia kujenga uadui ndani ya chama.
"Katika maeneo yote tulioshindwa mfano Mwanza, Arusha mjini, Iringa Mjini,Maswa na maeneo mengine CCM ndio ina wanachama wengi zaidi, kilichotokea ni mgawanyiko ndani ya chama,maeneo mengine tulikuta Kamati za siasa zenyewe zimegawanyika.
"Maeneo mengine tuliambiwa kuwa waliochaguliwa ni chaguo la viongozi wa wilaya si wanachama, hali kama hii ni hatari kwa chama, mimi kama kijana nasema tunahitaji mabadiliko makubwa, "alisema.
Alisema angependa kuundwa kikosi maalum cha uchunguzi ambacho kitapita kila eneo kutathmini hali halisi ya wanaoomba kuteuliwa kugombea ili kuhakikisha kila anayeteuliwa ndiye changuo la wananchi.
"Uchunguzi wetu kama UVCCM na hata mimi mwenyewe unaonesha wazi kuwa Watanzania wanaipenda sana CCM, tatizo ni mabadiliko tu,"alisema na kuongeza.
"Mimi tangu nizaliwe sijaona CCM ikitikiswa kama kipindi hiki, ni lazima tukae chini tujiulize tunakwenda wapi, dira na malengo ya chama chochote ni kuongoza, ni lazima tukubali kubadilika,"alisema
Alisema chanzo cha matatizo mengi ni ubinafsi ndani ya viongozi badala ya kufikiria kwanza wananchi.
Alisema licha ya Serikali ya Awamu ya Nne kujitahidi kuboresha maisha ya wananchi wake bado kunahitajika juhudi kubwa za kuelimisha wananchi kuboresha makazi yao kwa kutumia fursa zilizopo.
Bw. Ridhiwani ambaye aliweka wazi kutotaka cheo chochote kikubwa ndani ya chama hicho au serikali kwa maelezo kuwa anapenda kujifunza, alisema vijana wengi wa kitanzania wanahitaji kubadilika kifikra ili kuondokana na umasikini.
Alisema hata serikali kuu ikitoa matrekta madogo (power tillers) kwa ajili ya wakulima iwapo vijana hawatatambua kuwa hiyo ni fursa ya kujiendeleza bado umasikini utaendelea.
Kuhuusu malipo ya sh. bilioni 94 kwa Kampuni ya Dowans, alisema yeye kama mwanasheria anawaomba viongozi kuacha kufanya suala hilo ajenda ya kisiasa, badala yake waisaidie serikali kulimaliza.
"Sisi wanasheria taratibu zetu zinaanza baada ya mahakama kutamka hukumu, sasa katika hili serikali inapaswa kuangalia nafasi yake kama ni kukata rufaa au kulipa, lakini si watu kulifanya la kisiasa,"alisema.
Hata hivyo alisema hatua yoyote ya serikali inaweza kuanza baada ya Dowans kukazia hukumu hiyo Mahakama Kuu ya Tanzania.