Ridhiwani anajaribu kuziba ombwe? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ridhiwani anajaribu kuziba ombwe?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Ortega, Jan 27, 2011.

 1. Ortega

  Ortega Member

  #1
  Jan 27, 2011
  Joined: Jan 4, 2011
  Messages: 63
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 15
  Msomaji Raia

  WIKI iliyopita baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa Ridhiwani Kikwete, mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) alitoa shutuma nzito kwa CCM.

  Mapema UVCCM ilikuwa imetoa tamko mbele ya waandishi wa habari, na wenye hekima walidhani hilo lingetosha kuwakilisha maoni ya Jumuia hiyo.

  Hatua ya Ridhiwani Kikwete kutoa shutuma za ziada haiwezi kuchukuliwa kuwa ni kwa niaba ya UVCCM; maana UVCCM ilikwishakutoa tamko lake. Hatua yake, yaweza kuwa ni katika wadhifa mwingine ambao baba yake aliwahi kuukana kuwa haupo; yaani ubia wa urais wake.

  Naelewa watoto wa ma rais wana maisha binafsi na utashi wa kusema na kufanya lolote kama raia wengine. Lakini hatua ya Ridhiwani kukishutumu Chama cha Mapinduzi (CCM) kinachoongozwa na baba yake, kwangu mimi, ni zaidi ya uhuru huo wa mtoto wa rais. Nitaeleza.

  Ridhiwani anatuhumu uwepo wa makundi ndani ya CCM. Hata ukimwuliza kipofu ndani ya Taifa hili atakueleza kuwa mwanzilishi wa makundi haya ndani ya CCM ni baba yake Ridhiwani. Hata Rais mwenyewe anasema kuwa baada ya kura za urais wake kutokutosha mwaka 1995, hakukata tamaa, bali alirudi nyuma akaanza kujipanga upya hadi 2005.

  Mikakati yake ya kuingia Ikulu ndicho chanzo cha makundi anayoyalaani mwanawe Ridhiwani Kikwete. Kwa maana nyingine, Ridhiwani anamlaumu baba yake. Makundi yote tuliyo nayo ndani ya CCM yana asili yake katika madhara na athari za mtandao uliomwingiza Kikwete madarakani.

  Baada ya kuingia Ikulu mwaka 2005, Kikwete aliunda Serikali ya kiswahiba; huku akiwaengua aliodhani si wana mtandao uliomwingiza Ikulu. Lugha ya huyu si mwenzetu kwa mara ya kwanza ikaanza kutumika ndani ya CCM baada ya kutumika dhidi ya watu walio nje ya CCM.

  Serikali hiyo ya kiswahiba iliyotanda kutoka mawaziri, manaibu, makatibu wakuu, wakuu wa vyombo vya fedha, wakuu wa mikoa na wilaya, n.k badala ya kufanya kazi ilianza kusherehekea ushindi wa kishindo.

  Sherehe hizo zisizoisha ziliasisi mmomonyoko wa maadili ya utendaji kazi serikalini na kwenye chama. Rushwa na ufisadi vikashamiri vikikosa kiongozi wa kuvikemea na kuvichukulia hatua; maana, maswahiba hawawezi kukemeana.

  Hata pale baadhi ya watendaji walipoamua kuwajibishana, kazi ya Kikwete ikawa ni kusafiri mikoani kusuluhisha migogoro ya watendaji usiku kucha; huku akitumia msemo wake wa "tunajenga nyumba moja, tusigombanie fito". Msemo huu, hauvunji makundi bali unayaimarisha na Ridhiwani anaposhutumu makundi anamshutumu baba yake aliyeyaendeleza.

  Baada ya miaka mitano ya awamu yake ya kwanza, Kikwete akaasisi mtindo mwingine wa kuongoza nchi ambao pia hauvunji makundi bali unayaimarisha. Akaamua kutumia familia yake kufanya kampeni za kurudi madarakani na hatimaye kuongoza nchi.

  Kwa njia hii akayapa mwanya mkubwa makundi ili yapate fursa ya kupanga na kutekeleza mipango yao. Alipounda Serikali, hapakuwa na dalili zozote za kuvunja makundi bali kuyaongezea uchungu; kwani alichukua mahasimu wa kundi moja akawaweka serikalini; huku akiliacha kundi jingine nje ya Serikali.

  Matokeo ya njia hii ya kitoto, ni kuanza kukanyagana na kutuhumiana ndani na nje ya Serikali. Uhuru anaodai anautumia kukisema chama cha Mapinduzi nje ya vikao, ndiyo huo uhuru ambao baadhi ya mawaziri wanautumia kutoa dukuduku zao dhidi ya Serikali.

  Kwa utamaduni wa Taifa letu, serikali iliyo madarakani huongozwa na chama tawala. Na kama alivyotuasa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwa chama legelege huzaa serikali legelege, ni wazi msemo huu umetimia.

  Chama chetu cha CCM sasa si legelege tu, bali ni dalali na kuwadi wa tunu za taifa letu. Ukiwa na viongozi wanaoendekeza makundi, udini, uswahiba, ushirikina, visasi na jeuri ya utu uzima, huwezi kuwa na chama kinachoweza kuidhibiti serikali ili iwe na nidhamu.

  Matokeo ya kukosekana kwa mwongozo wa chama, sasa chama na Serikali kinakemewa na mtoto wa Rais, hatujui baadaye ataibuka nani naye aje na shutuma nzito dhidi ya chama na Serikali.

  Kwa waliobahatika kuiona Tanzania kabla ya Uhuru, wakati wa Uhuru, baada ya Uhuru, kabla ya CCM na sasa CCM, wana hazina ya kusema mengi. Hatujawahi kuwa na chama dhaifu kama wakati huu.

  Sasa imefika wakati hata Mtendaji Mkuu wa chama ananun'gunika mitaani kuwa Mwenyekiti wake "ana maneno matamu tu" lakini matendo hawezi.

  Hivi sasa moto unawaka kila mahali. Vyuo vikuu migomo inarindima, mabarabarani majambazi wamecharuka, mikoani maandamano ya vyama yamekuja juu, mitaani shilingi haina thamani, maofisini mishahara itagawiwa madirishani kwa sababu haina thamani, kwenye shule za kata watoto wamefukuzwa kwa kukosa michango iliyopigwa marufuku na Serikali, kwenye shule hizo hakuna walimu wakati wahitimu wa ualimu wanarandaranda kwenye korido za maofisi wakitafuta ajira, na wilaya na mikoa haina wakuu kwa visingizio visivyojaa kwenye kiganja. Mjadala wa Katiba unashawishi wengi wakati dereva wa kuuendesha ameamua kuutia mdomo wake kufuli.

  UVCCM wanasema Dowans isilipwe, Kamati Kuu inasema ilipwe. Wabunge wanasema isilipwe. Wastaafu wanasema watashangaa Dowans ikilipwa, watendaji wakuu wasio wanasiasa wanasema fedha zilipwe kutoka wapi wakati jungu kuu limekosa ukoko!

  Je, haya yote ni sababu ya makundi ya CCM au makundi haya yamekosa dereva mahiri? Kwa nini mwanzilishi wa makundi hataki kuyaendesha makundi yake mpaka yafike salama?

  Nimekuwa napokea shutuma kutoka kwa wasomaji wa safu hii kuwa mbona wakati wa Rais Benjamin Mkapa sikuwahi kuyasema haya? Jibu ni wazi kwanza mazingira ya wakati ule si haya ya leo. Kila zama na kitabu chake; lakini pia Serikali haikuwa dhaifu kama ilivyo sasa wakati wa Mkapa.

  Watanzania wamefikishwa mahali pa kutamani fisadi mchapa kazi atawale kuliko watawala ambao hata kupeleka wezi wa kuku mahakamani hawawezi


  Source:Raia Mwema
   
 2. AMARIDONG

  AMARIDONG JF-Expert Member

  #2
  Jan 27, 2011
  Joined: Jun 24, 2010
  Messages: 2,506
  Likes Received: 48
  Trophy Points: 0
  anataka uraisi 2020
   
Loading...