Phd Hewa
JF-Expert Member
- Oct 3, 2016
- 572
- 466
MBUNGE wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), ameoinyoshea kidole Serikali na kuitaka kuja na majibu ya kuridhisha ya namna ya kukomesha migogoro ya ardhi nchini.
Kutokana na hali hiyo amesema licha ya kuishauri Serikali kila mara bungeni lakini bado waziri mwenye dhamana ameshindwa kuyatekeleza, hali inayochangia kuongezeka kwa migogoro ambayo imekuwa ikileta maafa kwa Taifa.
Kauli hiyo ya Ridhiwani imekuja siku mbili baada ya kutokea mapigano baina ya wakulima na wafugaji mkoani Morogoro ambapo mkulima Augustino Mtuti alipigwa mshale mdomoni na kutokea shingoni.
Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, Ridhiwani alisema mara nyingi wabunge wamekuwa wakitoa maoni yao juu ya nini kifanyike ili kupungua tatizo hilo, lakini waziri mwenye dhamana ameshindwa kutekeleza jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa migogoro hiyo ambayo sasa inaanza kuleta maafa kwa Taifa.
Alisema, yapo mambo ambayo unaweza kupuuzia au kufanyia utani, lakini mengine huwezi kufanya hivyo kutokana na kugusa maisha ya watu.
“Hivyo basi kwa hali ilivyo, lazima Serikali iamke na kutoa uamuzi sahihi na siyo kufanya mzaha. Serikali inatakiwa kujua pale tunaposema kuwa kuna migogoro ya wakulima na wafugaji tunamaanisha nini.
“Ukifanya utani unaweza kuhatarisha maisha ya watu, hivyo basi ifike wakati Serikali ichukulie suala hili kwa umakini wa hali ya juu,” alisema Ridhiwani.
Mbunge alisema aliwahi kuzungumza bungeni kuhusu migogo ya ardhi iliyopo jimboni kwake, ambayo imesababisha baadhi ya wananchi kupigwa, kuvunjwa mgongo na wengine kupigwa na mishale, lakini waliopewa dhamana walidhani ni utani.
Alisema mapigano hayo ya migogoro ya ardhi sasa yameanza kushika kasi nchini ambapo awali lilitokea Mvomero mkoani Morogoro na kwamba litaendelea kutokea pangine kama Serikali itashindwa kuweka nguvu ya ziada ya kulishughulikia.
“Serikali inapaswa kusikiliza kilio cha wananchi na kuja na majibu ya kuridhisha ambayo yanaweza kupunguza ukubwa wa tatizo au kumaliza kabisa.
“Wanyonge wanategemea kilimo ndiyo kiinua mgongo chao, hivyo Serikali inapaswa kusimamia sheria ya mpango bora wa matumizi wa ardhi ili iweze kutenga maeneo ambayo yatatumika kwa ajili ya wakulima na mengine yatatumika kwa ajili ya wafugaji,” alisema.
Ridhiwani alisema kitendo cha kukaa kimya bila ya kutoa uamuzi wowote kinaonyesha wazi kuwa kuna jambo limefichwa.
“Ilianza Mvomero, ikaja Chalinze, Handeni, Kiteto na sasa Mikumi katika baadhi ya maeneo, jambo linaloonyesha wazi kuwa tatizo hilo linaendelea kukua siku hadi siku,” alisema
NAIBU WAZIRI NASHA
Naye Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha alisema katika kukabiliana na migogoro hiyo, Serikali imeunda timu ya watalaamu inayoshirikisha wizara tano kwa ajili ya kufanya tathimini ya kumaliza tatizo la wafugaji na wakulima.
Nasha alizitaja wizara hizo kuwa ni Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na TAMISEMI.
“Ili kupata ufumbuzi wa tatizo hili ambalo limedumu muda mrefu, Serikali imeunda tume maalumu inayoshirikisha wataalamu wetu wa nyanja mbalimbali ambao sasa karibu miezi mitano wanafanya kazi hii…tunategemea watakuja na majibu ya msingi ambayo mamlaka husika zitayafanyia kazi.
“Tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji inahitaji ufumbuzi wa kudumu, na kuhakikisha kwamba Serikali imejipanga vizuri katika hili, ingawa bado kuna matukio yanatokea,” alisema Waziri Nasha.
Alisema kama ripoti ya wataalamu hao ikiwasilishwa serikalini, basi ni wazi kazi ya kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji itafanyika haraka.
“Jambo hili si la siku moja, kosa ambalo tumelifanya kama Taifa, zamani mifugo ilikuwa michache na maeneo yalikuwa yanajulikana tofauti na sasa.
“Ukiangalia vizuri mikoa ya Kanda ya Ziwa hakuna mapigano ya aina hii kwa sababu wakulima na wafugaji wameishi kwa muda mrefu tofauti na mikoa kama Morogoro na Tanga ambako wafugaji wamekuwa wakihamia,”alisema.
Kuhusu tukio la kikatili lilitokea juzi wilayani Kilosa mkoani Morogoro, Waziri Nasha alisema hali imetulia na mpaka sasa vyombo vya dola vinaendelea kuwasaka wahusika.
“Hali ya Kilosa imetulia na vyombo vyetu vya dola vinaendelea kuwasaka wahusika wote wa tukio hili… nawasihi wananchi waache tabia ya kujichukulisha sheria mkononi,” alisema.
Source: Mtanzania