Mdakuzi mkuu
JF-Expert Member
- Dec 27, 2016
- 212
- 719
Arusha. Mgogoro wa pori tengefu la Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro umechukua sura mpya baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kutangaza kuendelea kwa majadiliano ya kutafuta suluhu, wakati tayari Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alishatangaza uamuzi.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari akitoa taarifa za utendaji wa Serikali za robo mwaka, zilizotolewa na idara za serikali na mashirika ya umma, Gambo alisema kamati aliyounda kutafuta suluhu inaendelea kama alivyoagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Gambo alisema tamko ambalo linaonekana kama limehitimisha kazi ya kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa Loliondo uliodumu kwa zaidi ya miaka 25 ni maoni tu.
“Serikali inakwenda kwa itifaki anapotoa maelekezo Waziri Mkuu, mtu anayeweza kuyapinga maelekezo yake ni Makamu wa Rais ama Rais, lakini mtu mwingine yeyote anapotoa maelekezo yake sisi kama viongozi wenzake tunayachukulia kama sehemu yake ya ushauri katika kupata suluhu,” alisema.
Gambo alisema mgogoro wa Loliondo ulikuwa umefikia hatua mbaya, lakini tangu kuanza kwa majadiliano yaliyohusisha wadau wote wakiwamo wananchi hali ya utulivu ilirejea.
Alisema katika kupata suluhu mambo matatu yalikuwa yanazingatiwa ambayo ni kuilinda ikolojia ya Serengeti, hifadhi ya Ngorongoro, hatma ya wananchi wa Loliondo na suala la wawekezaji ambao wanachangia mapato kwa Taifa .
Gambo alisema kwenye majadiliano ambayo yanaendelea, kulikuwa na mapendekezo matano, lakini mawili ndiyo yamepitishwa kufanyiwa kazi na timu ya wataalamu.
Alisema mapendekezo hayo ni kuanzishwa Hifadhi ya Jamii (WMA) ama kuwa na pori tengefu lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,500 na sasa timu ya wataalamu itapita katika eneo hilo kulipima.
“Tukakubaliana tuunde timu ya wataalamu wa sekta zote na kushirikisha jamii husika na kwenda kuona eneo la pori tengefu ni lipi na linatoka wapi hadi wapi,” alisema.
Gambo alisema kuna sehemu muhimu ambazo zilielezwa na watu wa maliasili na utalii, kwa ajili ya uhifadhi nazo zitatazamwa.
Alisema kumekuwa na maoni ya wananchi kuwa, eneo ambalo linatengwa inaonekana ni kubwa kwa tarafa moja tu.
“Hatuwezi kufanya maamuzi kutenga pori tengefu bila kujua hatma ya wananchi watapata wapi malisho, watapata wapi maji,” alisema.
Msimamo wa Wizara ya Maliasili na Utalii
Profesa Jumanne Maghembe mapema wiki iliyopita, akitoa msimamo wa wizara hiyo, alitangaza kutengwa eneo la kilomita za mraba 1,500 kwa ajili ya pori tengefu la Loliondo.
Alisema kilomita za mraba 2,500 ambazo zilikuwa sehemu ya pori tengefu Loliondo, zinarejeshwa kwa wananchi na lengo ni kuhifadhi Ikolojia ya Serengeti ambayo sasa ipo hatarini.
Profesa Maghembe alisema eneo hilo la kilomita za mraba 1,500 ndipo kuna vyanzo vya maji vya hifadhi ya Serengeti na Mto Mara na Ngorongoro na ndipo kuna mazalia ya wanyamapori, lakini sasa limeharibiwa.
Aliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), kuweka mipaka katika eneo hilo na itakuwa ni marufuku kuingiza mifugo katika eneo hilo ili litunzwe kwa masilahi ya Taifa.
Kwa zaidi ya miaka 25 kumekuwepo na mgogoro wa Loliondo, ambapo mawaziri kadhaa na viongozi wa Serikali wamekuwa wakitofautiana katika kupata suluhu.
Chanzo: Mwananchi