Bibianna
JF-Expert Member
- Jun 6, 2025
- 400
- 135
View: https://youtube.com/shorts/gQOZqg8blW0?si=-lRtUNLB63qZPj_X
Katika taarifa yake kwa wanahabari mkuu huyu wa mkoa wa Tanga amesema kuwa Kukamilika kwa maboresho ya Bandari ya Tanga kumeleta mageuzi makubwa katika ufanisi wa utoaji huduma bandarini, jambo lililoinua ushindani wa bandari hiyo ndani na nje ya nchi. Moja ya mafanikio makubwa ni kupungua kwa muda wa kuhudumia meli, ambapo kabla ya maboresho meli zilihudumiwa kwa wastani wa siku 5, lakini sasa huduma hiyo inakamilika kwa siku 2 tu. Hii imesaidia kupunguza gharama kwa wamiliki wa meli na kuongeza mzunguko wa kibiashara bandarini.
Kiasi cha meli zinazotumia Bandari ya Tanga kimeongezeka kutoka meli 198 mwaka 2021 hadi meli 307 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 55. Shehena ya mizigo inayopakiwa na kupakuliwa bandarini imeongezeka kutoka tani 888,130 mwaka 2021 hadi tani 1,191,480 mwaka 2025, ongezeko la zaidi ya tani laki tatu ndani ya miaka minne. Aidha, idadi ya makasha yaliyoshughulikiwa bandarini (TEUs) imepanda kutoka makasha 7,036 hadi 7,817, hali inayoashiria ongezeko la shughuli za biashara ya kimataifa kupitia bandari hiyo.
Maboresho haya pia yameleta ongezeko la mapato kwa Bandari ya Tanga, kwani ongezeko la shehena na idadi ya meli limeongeza malipo ya tozo, ushuru, na ada mbalimbali. Taarifa zinaonesha kuwa mapato ya bandari hiyo yamepanda kwa zaidi ya asilimia 40 ikilinganishwa na kipindi kabla ya maboresho. Zaidi ya hayo, maboresho yamefungua fursa za ajira kwa vijana wa Kitanzania, ambapo ajira za muda mfupi (za mikataba) na muda mrefu (ajira rasmi) zimeongezeka hususan kwenye sekta ya upakuaji mizigo, usafirishaji, usimamizi wa maghala, usalama, na huduma za kiufundi.
Kwa sasa, Bandari ya Tanga inachukuliwa kama lango muhimu kwa biashara ya kikanda, hasa kwa nchi zisizo na bandari kama Rwanda, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara na reli inayounganisha bandari hiyo na mikoa mingine ili kuhakikisha mizigo inasafirishwa kwa haraka zaidi.
Mafanikio haya ni ushahidi thabiti wa maono ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji wa mizigo Afrika Mashariki.