RC Adam Malima ashauriwe aachane na ubabe unaowaumiza wananchi

Jul 23, 2018
46
66
JINSI MGOGORO WA RC ADAM MALIMA NA HALMASHAURI YA WILAYA YA TARIME UNAVYOWAUMIZA WANANCHI WANYONGE KIMAENDELEO.

Tangu kumetokea kashfa ya kile kinachoitwa "wizi" wa fedha za mgodi wa Nyamongo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mara ndg. Adam Malima, Mimi kwakuwa ninakipenda chama changu *CHAMA CHA MAPINDUZI* na kukiamini kama chama kinachosimamia ukweli, basi niliamini yote aliyoyasema ndg. Malima kuwa ni ya kweli.
Pamoja na kwamba nilikaa kimya bila kuandika chochote juu ya suala hili,nilikuwa nikisubiri kuona hatima yake. Lakini nilikuwa nikilifuatilia chini kwa chini bila watu wengi kujua.
Pia nilikuwa nikisubiri ripoti ya uchunguzi ya Kamati aliyoiunda ndg. Adam Malima juu ya suala hili ambalo alisema Shilingi Bil. 9.5 zimeliwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Nimejaribu kufanya uchunguzi wangu kama mwanachama wa CCM kwa kuwauliza wahusika na kuwatumia watu (bila wao kujua), nimezungumza na baadhi ya watumishi wa Halmashauri, nimezungumza na Mbunge (Mimi mwenyewe na kwa kutumia watu), nimezungumza na baadhi ya madiwani (wa vyama vyote) juu ya jambo hili.
Kuna mambo ya muhimu sana niliyoyapata ambayo yapo nyuma ya pazia hili la kashfa ya Bil. 9.5

Moja ya mambo niliyokutana nayo ni pamoja na haya;

01. RC Malima amewahi kuwa na ugomvi na aliyekuwa DC Tarime ndg. Glorious Luoga kwasababu ya hizo fedha za mgodi. Iko hivi, Malima alitaka kupata "share" katika fungu la Mgodi linaloingia ndani ya Halmashauri ya Tarime, lakini Luoga alimkatalia kuwa hizi fedha ni za Tarime tu haziwezi kwenda mkoani. Suala hili lilipelekea Malima kumchukia sana Luoga na hata kupelekea kumpa taarifa Rais kuwa Luoga anahujumu maendeleo hapa Tarime na kukihujumu chama chetu cha Mapinduzi.
Mpaka kutenguliwa kwa Luoga ndg. Malima alichochea kwa zaidi ya 70%. Maelezo haya niliyapata katika Ofisi moja hapa Halmashauri na Kiongozi mmoja wa chama changu cha CCM.
Lakini pia, Malima aliwahi kwenda mgodini Nyamongo na kuzungumza na uongozi wa Mgodi akiwaomba waingize fedha hizo mkoani ili yeye awe anazigawa, lakini uongozi wa mgodi nao ulimkatalia kwa kusimia maelekezo na matakwa ya sheria ya madini. Hakuchoka, akaendelea kutafuta mbinu nyingine.

2. Nimezungumza na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mhe. John Heche (bila yeye kuifahamu itikadi yangu) na nikawatuma watu watatu ili kuongea nae lakini jambo la ajabu ni kuwa, Mhe. John majibu aliyonipa Mimi ndio yale yale aliyowapa hao watu watatu.
Msimamo wa Mhe. Mbunge ni kuwa *"hakuna hata senti moja iliyoliwa ndani ya Halmashauri"* na amesema *"hakuna hata senti moja itakayotoka nje ya wananchi wa Tarime kwa matakwa ya mtu fulani, ilihali bado wananchi wa Tarime wana upungufu mkubwa wa huduma za kijamii"*

Mhe. Mbunge anasema, ikiwa RC Malima anaamini watu wamekula pesa, basi (kwa ushahidi alionao) aagize vyombo vya dola kuwakamata watu hao na kuwafikisha mahakamani, hata kama ni Mbunge mwenyewe.
Nilipopata majibu haya nililazimika kumtafuta M/Kiti wa Halmashauri ndg. Moses Matiko Misiwa (Yomami) na kumuuliza juu ya hilo.
Nae alisema, kama kuna fedha zimeliwa watu hao wakamatwe na wafikishwe mahakamani, akadai hakuna mtu anaemtetea mwizi.
Lakini akasema, wakati hayo yakifanyika fedha zitolewe wananchi waendelee kupata huduma badala ya kuzuia fedha na wananchi wataabika huko.

Katika mazingira haya ya viongozi wa wananchi hawa kujiamini hivi, katika hatua za awali kabisa unaweza kutambua kuwa Halmashauri hii haina tatizo kabisa, bali ni hujuma tu za kisiasa.
Maana mtu hawezi kula fedha halafu akusaidie kukushauri kumpeleka mahakamani.

3. Nimeambiwa Kamati ya LAAC wamekuja hapa Halmashauri wamefanya ukaguzi wao wa miradi iliofanyika na kwa thamani ya pesa iliyotumika, wakaridhika.
-Pia, nakumbuka Waziri Mkuu wa Serikali ya chama changu cha CCM amewahi kufika hapa Tarime na akapongeza viongozi wa Halmashauri ya Tarime kwa usimamizi mzuri sana wa fedha katika ujenzi wa Vituo vya Afya kikiwemo kile cha Sirari, tofauti na alivyokosoa kule Rorya (ambapo sisi tunaongoza Halmashauri na tuna Mbunge).
-Pia, kwa takribani miaka mitatu mfululizo ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Halmashauri ya Wilaya ya Tarime imekuwa ikipata hati safi kwa miaka mitatu mfufulizo.
Lakini pia, wakati suala hili la "kashfa" lilipoibuliwa na RC Malima, Ofisi ya Waziri Mkuu ililazimika kutuma timu yake ya wataalam kuja kuchunguza suala hili hapa Tarime. Timu ilipewa ushirikiano kutoka Ofisi ya Mkurugenzi, M/Kiti wa Halmashauri, Ofisi ya Mbunge na Madiwani lakini mpaka wamemaliza, taarifa zilizopo mpaka sasa ni kuwa *hakuna wizi waliobaini*.

Jambo hili linasikitisha sana, tena sana. Na ninabaki kujiuliza, ikiwa kuna wizi umefanyika hapa kwanini Ofisi zote nilizotaja hapo juu hazijabaini wizi huo?
Jambo hili la RC Malima lipo kisiasa zaidi. Linakosa uhalisia wenyewe.
Nadhani ni vyema Malima akasema nia yake ni nini katika hili, kuendelea kuegemea kashfa ya wizi ni kuendelea kuupotosha umma bila sababu.

Jambo la kushangaza sana kwa RC Malima ni kuendelea *kuzizuia zile fedha za Halmashauri zisitoke ili zifanye maendeleo* na *kusimamisha vikao vya Kamati ya fedha na Vikao vya Halmashauri kinyume cha sheria*.
Lakini pia, hata sheria ingempa mamlaka hayo, ni lazima ajiulize "hivi ninaposimamisha vikao hivi wananchi watapataje maendeleo?".
*Katika hili binafsi pamoja na kuwa Malima ni mwana CCM mwenzangu lakini sikubaliani nae kabisa*.
Na inashangaza sana kusikia na kuona viongozi wangu wakubwa wa chama wanaunga mkono suala hili. Jambo hili litatumaliza ninawaambia!!.

Wiki iliyopita nilipata bahati ya kufika msibani pale Kata ya Gwitiryo ambapo ndg. Mrimi Zabron alikuwa amefiwa na mama yake Mzazi.
Bahati nzuri, Mbunge alikuwepo Mhe. Heche.
Alipopata nafasi ya kuzungumza, aliongea akasema mpaka sasa alichofanya na chama chao lakini pia akagusia suala hili la RC Malima kuzuia fedha hizi kwenda kwenye miradi ya maendeleo.
Kwa jinsi Mbunge alivyolielezea suala hili, lilijenga dhana mbaya kwa wananchi kukidharau na kukisema vibaya CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM).
Heche alisema hayupo tayari kuona hata senti moja ya fedha za wananchi ikiliwa, na hayupo tayari kuona hata senti moja ya Tarime ikienda nje ya Tarime wakati wananchi wa Tarime bado wana shida. Wananchi walilipuka kwa makofi na na vigelegele.
Baada ya hotuba yake fupi, kwakweli wananchi walimsema vibaya sana Malima na chama changu. Ni dhahiri kuwa sikupenda kusikia chama changu kikisemwa vibaya vile lakini sikuwa na namna yoyote.

Juzi tena, nimefanikiwa kufika msibani kwa Mzee Gimunta pale Nyamwaga. Viongozi mbalimbali wa serikali na kisiasa walipata fursa ya kuzungumza. Suala hili likaibuka tena, ambapo Diwani wa Nyamwaga ndg. Yomani aliliibua na kuonesha masikitiko yake kwa fedha za wananchi kuzuiliwa, vikao vya Halmashauri kusimamishwa na hivyo kupelekea baadhi ya miradi ya wananchi kusimama kwa muda mrefu sasa. Yomami aliitafsiri kuwa hii ni njia ya *"kukwamisha maendeleo kwa wananchi"*.
Baadae, waliposimama viongozi wangu wa CCM wakaharibu kabisa hali ya hewa. Mwenyekiti wa CCM Wilaya ndg. Ngicho aliharibu kabisa katika hotuba yake. Baadae akaja Mwenyekiti wa CCM Mkoa ndg. Samwel Kiboye "No.3" huyu ndiye aliyeharibu zaidi. Yaani viongozi wangu walikoswa hekima ya kuwajibu CHADEMA pale msibani badala yake wakajibu kwa panic kubwa sana.
Haileti maana kwa kiongozi wa CCM kumwambia kiongozi wa CHADEMA na wananchi kwamba "tumieni ruzuku ya chama chenu kufanya maendeleo". Huu ni ujinga wa kiwango kikubwa sana!! Wananchi wana masikio na wanasikia. Hapa ndipo tunapowapatia CHADEMA ushindi asubuhi na mapema.

Na walivyongumza pale msibani, watu wenye akili timamu walielewa nini haswa alichomaanisha Yomami aliposema "watu wanakwamisha maendeleo".
Viongozi wa chama changu sijui wanashindwa nini katika hili. Wanashindwa kutambua kuwa, kwa sasa wananchi hawahitaji kumsikia tena Malima,, maana wameamini kuwa yeye ndie adui yao, kwahiyo unaposimama kwenye hadhara na ukamuunga mkono Malima kwa kuzia fedha hizo, nawe unaingizwa kwenye kundi hilo pamoja na chama chako (CCM).

Hivi chama changu cha CCM hakijui kwamba kuendelea kupamba jambo hili ni kukiangamiza chama?
Kwamba wananchi watakichukia chama chetu kwasababu ya mtu mmoja, kweli chama changu hakioni hili?
Kwanini tunawapa CHADEMA agenda za kutupigia kwa wananchi?
Kwanini tunaruhusu CHADEMA kupata agenda za kuonewa huruma na wananchi?

Nimeambiwa kuna miradi mingi sana ya Wananchi ndani ya Halmashauri imesimama. Ipo miradi mipya na iliyokuwa inaendelea..
Kuna miradi ya kujenga zahanati, shule, kukarabati barabara, kuezeka majengo ya shule, usafi wa soko mfano ni soko la Sirari n.k
Haya mambo yote yanawagusa wananchi.
Hivi leo hii CHADEMA wakiamua kuzunguka Wilaya nzima ya Tarime kwa ajili ya kutushtaki sisi CCM kuwa tumewanyang'anya fedha za maendeleo ndio maana miradi imesimama, mnafikiri tutazipeleka wapi nyuso zetu sisi wana CCM?

Hapana, tuweni fair katika hili!! Kwakuwa wananchi waliwaamini CHADEMA mwaka 2015 wakawakabidhi Jimbo na Halmashauri basi tuwaache wamalize miaka yao mitano. Hayo mengine tusubiri mwaka 2020 tutawashitaki kwa wananchi, kisha wao wataamua.
Sikubaliani kabisa na hizi figisu ambazo hazina tija kwenye jamii yetu ya Tarime.
Kabla ya Malima kuja, Wilaya ya Tarime hatujawahi kuwa na mgogoro na Wilaya zingine jirani zetu na Mkoa kwa ujumla, ila shetani huyo ameibuka sasa ili kutugombanisha. Tukatae.
Ndugu Malima ni mtu wa muda hapa Mara, atakaa muda ukifika ataenda kwingine au ataenda kwao, halafu sisi tutaendelea kuwepo hapa miaka yote. Hebu tujenge umoja wa kuliliana na kushikamana katika maendeleo ya Tarime yetu.
Sisi CCM tumewahi kuongoza Wilaya hii na Halmashauri lakini hatukuwahi kusema pesa hizi ziende Mkoani, kwanini sasa?

Ninamshauri Mkuu wa Mkoa wangu wa Mara ndg. Malima aachane na mgogoro huu kisha, aruhusu pesa hizo ziendelee kutumika na pia aruhusu vikao vya Madiwani viendelee.
Ninakishauri chama changu kiepukane na mgogoro huu, maana hauna tija yoyote kwa chama chetu. Badala ya kujisafisha sasa, tunajichafua.
Yangu ni hayo kwa leo, mwenye kusoma na aelewe.
Mwenye kusikia na asikie.
Mwenye kuwiwa na atende.

NI MIMI MWANACHAMA (KADA MTIIFU) WA CHAMA CHA MAPINDUZI.
MZALIWA NA MKAZI WA TARIME.
 
Malima atumie busara sana kufanya kazi katika mkoa wa Mara hasa wilaya ya Tarime na Serengeti. Hao 'mamura' huwa wanajielewa sana na hawaongozwi kwa kuburuzwa bali kwa maridhiano!
 
Back
Top Bottom