Rais saidia kuleta fikra mpya

Msambichaka Mkinga

JF-Expert Member
Oct 22, 2015
1,649
2,911
Umadhubuti wa Taifa unatokana na kukamilika kwa jamii. Ukamilifu wa Taifa unatokana na uwepo wa watu wenye fikra, uwezo, vipaji na weledi wa aina mbalimbali.

Kila mmoja katika mchanganyiko huo wa wananchi, akitumika na kuchangia kikamilifu, mchango wake ndiyo huleta maendeleo katika Taifa. Na kila mmoja katika eneo lake, akifanya kwa kiwango kinachozidi ile kawaida, ni shujaa wa Taifa.

Kuna fikra mbaya imeanza kujengeka katika Taifa letu, ambapo tunaanza kuamini kuwa maendeleo ya Taifa, na watu walio muhimu sana katika Taifa na ambao wanastahili kupimwa na kutambulika kama wametoa mchamgo muhimu au hapana, ni wanasiasa pekee.

Hakuna nchi inayoweza kupata maendeleo yoyote yale kwa kutegemea wanasiasa pekee yao. Kwa kiasi kikubwa, viongozi wa kisiasa ni waratibu tu katika processes za kuleta maendeleo ya Taifa. Ni waunganishaji wa vipaji, taaluma, ujuzi, na maarifa ya watu mbalimbali katika Taifa.

Nchi ijenge mfumo wa kuwatambua mashujaa wa Taifa letu, watu ambao mchango wao siyo wa kawaida. Utambuzi wa namna hiyo utawafanya watu mbalimbali kufurahia taaluma zao, ujuzi na maarifa yao, vipaji vyao, n.k. badala ya kufikiria kuwa ili mchango wako uweze kutambulika na kusikika, ni lazima uwe mwanasiasa.

1. Tuwatambue madaktari bingwa ambao mafanikio yao yanazidi utendaji wa kawaida.

2) Tuwatambue wafanyabiashara na wawekezaji ambao mchango wao katika uchumi wa Taifa, ajira na ustawi wa jamii, vinazidi mategemeo yetu.

3) Tuwatambue wahandisi, wanajiolojia, wahasibu, wahadhiri, walimu, wanasheria, n.k. ambao michango yao inavuka viwango vya kawaida.

4) Tuwatambue wasanii na wanamichezo ambao michango yao kwa ustawi wa Taifa letu, imevuka matarajio yetu

Mara nyingi watu wa namna hiyo, tumependa kuwaita kuwa ni mabalozi wetu, lakini ukweli imebakia tu kuwa mabalozi wa maneno yasiyoweza kuamsha ari ya wengine kuwa kama wao. Hawa walistahili kupewa hadhi inayotambulika kisheria ili watu wajivunie vipaji vyao. Wenzetu kule Uingereza wapo watu wanaitwa 'Lord, Sir'. Title hizo zinaandamana na privilege fulani katika jamii.

Lakini jambo jingine muhimu, hivi karibuni tulikaribia kupotea. Kwa sababu nafasi nyingi, hata zile za kiutaalam, teuzi zake ziliegemea kwenye mlengo wa kisiasa badala ya weledi. Huu ulikuwa ni mwelekeo mbaya kabisa. Kazi zinazohitaji utaalam ni muhimu sana zikabakia kuegemea kwa 100% taaluma na ujuzi na siyo mwelekeo wa kisiasa.

Pongezi nyingi kwa Rais kuhusu kumrudisha James Mataragio kwenye nafasi ya Ukurugenzi wa TPDC. Huyu ni mtaalam, siyo lazima abakie kwenye nafasi hiyo hiyo, na hatuna uwezo wa kumlazimisha mwenye mamlaka ya kuteua kufanya hivyo, lakini muhimu tutakachoebdelea kukumbusha wakati wote ni kuwa nafasi zinazohitaji utaalam, uteuzi uzingatie utaalam na siyo vinginevyo.

Kila Mtanzania, katika nafasi yake, ana uwezo wa kuonesha uzalendo na ushujaa wake kwa Taifa, na Taifa ni sharti likautambua mchango wake.

Mheshimu Rais, ikimpendeza aendelea kuchekecha ili ofisi zote ambazo teuzi zake zilistahili kuzingatia utaalam, lakini kwa bahati mbaya zilizingatia ukada, makosa hayo yarekebishwe haraka. Tanzania ina watu zaidi 60m, tuna uwezo wa kuwapata watu sahihi wa kila mahali lakini siyo kweli kuwa kuna mtu anaweza kuwa sahihi kila mahali na kila wakati.
 
Back
Top Bottom