Monasha
JF-Expert Member
- Apr 2, 2011
- 561
- 422
Kwa miaka ya hivi karibuni, eneo la bonde la Ngorongoro limekuwa likikumbwa na migogoro ya aina mbalimbali hasa ya migongano ya maslahi. Maslahi haya ni kati ya wenyeji waishio katika eneo hili na hifadhi ikiongozwa na Mamlaka ya hifadhi ya eneo hili. Kumekuwa na uibukaji wa sheria mbalimbali za kuwabana weenyeji hawa katika eneo lao hili ambalo ndo hutegemea kwa maendeleo yao. Uongozi wa sasa umeanzisha sheria ya kuwazuia wenyeji kutofika na kufanya shughuli yeyote katika baadhi maeneo (NO GO ZONE).
Kuanzishwa kwa No Go Zone siyo tatizo, tatizo ni pale uongozi husika unapoamua kuanzisha makatazo bila ya ushirikishwaji. Ikumbukwe kwamba wenyeji hawa wana viongozi wao wa kiserikali na viongozi wa kimila. Katika uongozi wa awamu zilizopita, hakujawahi kutokea ubabe wa aina hii wa kuwapuuza wenyeji katika ushirikishwaji wa mambo mbalimbali yahusiyo eneo lao. Daima kumekuwepo na ushirikishwaji ulioleta usawa katika kufanya maamuzi juu eneo hili. Lakini cha kushangaza, uongozi uliopo ukiongozwa na Fredy Manongi (Mhifadhi Mkuu) umekuwa ukifanya maamuzi bila ya ushirikishaji kabisa. Hili limeleta mtafaruku na taharuki kubwa sana miongoni mwa wananchi hawa.
Jana tarehe 13/07/2019 jamii ilikutana kuyaongelea haya kuonyesha msimamo wao hasa juu ya uongozi wa bwana Manongi ambapo kiuhalisia bila kumumunya maneno, Manongi na uongozi wake hawahitajiki katika eneno lile. Na wakiendelea kuwepo basi watahatarisha maisha na shughuli za eneo la bonde la Ngorongoro. Ifike mahali Rais aliingilie hili kati maana licha ya viongozi wa chama tawala kufika katika eneo hili mara kwa mara, bado hakuna suluhisho lililopatikana. Suluhisho pekee tunaloliona kwa sasa ni Rais kutoa tamko juu ya matendo ya uongozi uliopo katika eneo hili.
Tunaomba sana, kwakuwa Rais Magufuli toka aingie madarakani hajawahi kulitembelea eneo hili na kujionea yanayoendelea, hakika afike siku moja na ninaimani kwamba atajiuliza kwanini hakufanya maamuzi ya kulitembelea eneo lile mapema sana.
Hapa unaweza kuona malalamiko toka viongozi wa kimila kuhusu uongozi wa Manongi. Kikubwa utagundua kwamba mahusiano kati ya managementi ya NCAA na wananchi inapungua mwaka hadi mwaka. Ndio maana tunataka angalau kiongozi wa nchi aliingilie hili kati ingali mapema maana tunakoelekea ni kubaya sana.
Kama ni kwamba wenyeji hawa hawatakiwi tena katika eneo lile basi liwekwe wazi na siyo kuendelea kuwanyanyasa. Hawa ni wananchi kama walivyo wananchi wa maeneo mengine Tanzania. Wanahitaji huduma zote za kibanadmu katika maendeleo yao. Fikiria mpaka wananyimwa kujenga shule na miundo mbinu zingine hata kwa nguvu yao wenyewe. Je vizazi vyao vijavyo vitaishi vipi?