Rais Magufuli safari moja nje, Kikwete kumi

lebraza

Senior Member
Jan 8, 2013
124
114
Inaweza kuwa kitu cha kawaida, lakini kwa kulinganisha na viongozi wa awamu mbili, si jambo la kawaida kwa rais kuwa amesafiri mara moja tu kwenda nje ya nchi katika kipindi cha miezi sita.

Ndivyo ilivyo kwa Rais John Magufuli, ambaye sera zake za kupunguza matumizi yasiyo ya lazima zimemfanya awe amesafiri mara moja tu tangu aapishwe Novemba 5 mwaka jana.

Na safari yenyewe ilikuwa ya kwenda Rwanda Aprili 6 kuhudhuria Maadhimisho ya Mauaji ya Kimbari, yaliyotokea mwaka 1994 na kupoteza maisha ya maelfu ya watu kwenye nchi hiyo ndogo iliyo kaskazini magharibi mwa Tanzania.

Zaidi ya hapo, Rais alikuwa akitokea mpakani mwa nchi hizi mbili alikokwenda kuzindua daraja la Mto Rusumo. Kwa hiyo si ajabu kwamba mkuu huyo wa nchi alikwenda kwa barabara iliyompa fursa ya kusalimiana na wananchi waliomchagua Oktoba 25, 2015.

Katika kikao chake cha kwanza na watendaji wa Serikali, Rais alieleza mkakati wake wa kukusanya mapato ya Serikali na kubana matumizi yasiyo ya lazima, akipiga marufuku safari za nje isipokuwa kwa kibali cha Ikulu.

Na wafanyakazi wa Takukuru waliothubutu kwenda nje bila ya kibali, walisimamishwa kazi kuonyesha kuwa Rais hafanyi utani katika hilo.

Ni ajabu kwa mkuu huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano kuwa amesafiri mara moja tu katika kipindi cha miezi sita, kwa kuwa mtangulizi wake, Jakaya Kikwete alikuwa ameshasafiri zaidi ya mara 10 katika miezi hiyo ya kwanza.

Kikwete alianza safari zake Januari 19-25, 2006 alipokwenda Khartoum, Sudan kuhudhuria mkutano wa nchi za Afrika (AU). Katika kipindi kama hicho, Magufuli hakuhudhuria mkutano wa AU uliofanyika Addis Ababa nchini Ethiopia badala yake alimtuma Samia Suluhu Hassan.

Machi 23, 2006 Kikwete alifanya ziara ya siku moja ya kiserikali nchini Rwanda kujitambulisha.

Machi 22 alikwenda Kampala, Uganda kwa ziara ya siku moja ya kujitambulisha. Machi 24 alikwenda Nairobi, Kenya na Aprili 19-20 alikuwa Lesotho na Swaziland na Aprili 21-22 Aprili alikuwa ziarani Maputo, Msumbiji.

Aprili 28, Kikwete alikuwa Harare na Bulawayo, nchini Zimbabwe; Aprili 6 alikuwa Gaborone, Botswana. Alikuwa ziarani Namibia kuanzia Aprili 10-12; Mei 7-9 alikuwa Pretoria, Afrika Kusini; Mei 12 alianza ziara ya wiki mbili katika nchi za Uganda (13 Mei), Arabuni (Mei 15), Ufaransa (Mei 16-19) na Marekani (Mei 21-26).

Akiwa na nafasi tofauti kwenye taasisi za kimataifa, safari za Kikwete ziliongezeka kiasi cha kuanza kuzua maswali mengi, na wapinzani wakashika usukani kulalamikia hilo.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari Dar es Salaam mwishoni mwa mwaka jana, mbunge wa Vunjo, James Mbatia alidai kuwa katika kipindi cha miaka 10 ambacho ni wastani wa siku 3,650, Kikwete alikuwa amesafiri mara 409 na alikuwa akikaa nje ya nchi kwa wastani wa siku tano katika kila safari, hivyo alikuwa nje kwa takriban siku 2,045.

Alisema siku hizo ni sawa na asilimia 56 ya muda wake wote akiwa madarakani hadi siku hiyo ya mkutano wa Mbatia.

Kilio hicho cha viongozi wa upinzani kilisikika kwa Magufuli ambaye katika hotuba ya kufungua Bunge la Jamhuri ya Muungano Novemba, 2015 alitaja mikakati ya kudhibiti matumizi ya fedha za umma akitaja safari za nje ya nchi kuwa miongoni mwa mambo atakayoyashikia bango.

Katika kusisitiza hilo, Rais Magufuli alisema safari za nje kati ya mwaka 2013/14 na 2014//2015 ziligharimu Sh356.3 bilioni, kati ya hizo posho za kujikimu zilikuwa Sh104.6 bilioni.

“Hizi fedha zingeweza kutumika vizuri kuboresha huduma za wananchi wa maisha ya chini, kama afya, maji, elimu na umeme,” alisema.

Kwa kutekeleza hilo, Rais Magufuli hajaenda nje kuhudhuria vikao kama vya wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) mjini Gaborone, Botswana ambako alimtuma Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Mbali na safari hiyo, Rais Magufuli aliwahi kuamuru watu wanne tu kusafiri wakitokea ofisi ya ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza kwenda kumwakilisha katika mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola uliofanyika visiwa vya Malta, badala ya msafara wa watu zaidi ya 50 kama ilivyozoeleka.

Hata hivyo, Bernard Membe, waziri wa zamani wa mambo ya nje, alisema nchi haiwezi kuwa kama kisiwa na hivyo Rais hana budi kwenda nje kwenda kutia uzito kwenye masuala ambayo Tanzania inayataka.

Akizungumzia suala hilo, kada mkongwe wa CCM, Njelu Kasaka alisema kila mtawala ana uamuzi na mikakati yake katika kuongoza nchi, hivyo uamuzi wa Rais Magu-fuli kwa sasa ni sahihi.

“Kwa maoni yangu, Rais Magufuli kwanza alipaswa kujifunza kuhusu Serikali anayoiongoza mara tu baada ya kuingia madarakani, kuliko kuanza na safari tu. Kuna sheria na mambo mengi ambayo rais anapaswa kuyajua hivyo atatumia muda mwingi kuwa nchini,” alisema Kasaka.

Hata hivyo, alisema, “Kusafiri nje ya nchi nako ni muhimu kuliko tu kusema unaokoa hela. Inategemea umuhimu wa jambo unaloliendea. Safari zinapimwa na umuhimu wake,” alisema Kasaka.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho alisema uamuzi wa Rais Magufuli ni wa muhimu kwa sababu umeokoa fedha nyingi. “Ni uamuzi mzuri kwa sababu ni kweli safari za nje zilitumia fedha nyingi sana, ndiyo maana Magufuli aliamua kubana fedha kwa ajili ya matumizi muhimu,” alisema.


Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom