Rais Magufuli njoo NEMC majipu kibao

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
KUNA Majipu mengi kutumbuliwa Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC). Kwa hakika kuna kero nyingi zinazotukabili katika mazingira ya kazi. Kero hizi zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka huku viongozi wakionyesha kutokukerwa kwani hakuna ufumbuzi wowote uliopatikana mpaka sasa.Masijala

Ofisi ya Masijala: Tuna kila sababu kusema kwamba wafanyakazi wa ofisi ya Masijala hawana ustadi wa kazi ya idara hii nyeti. Kwa mfano, kiongozi wa ofisi hii alikuwa mhudumu tu wa kawaida. Kufumba na kufumbua, amepelekwa Masijala. Kana kwamba hiyo haitoshi, wafanyakazi wengine wa Masijala hawana vigezo / ujuzi wowote wa kufanya kazi hapo.

Kwa kifupi wamewekwa tu kwa sababu ni ndugu, jamaa na marafiki wa baadhi ya wafanyakazi wa Baraza. Kwa ufupi hakuna mwenye fani ya kufanyakazi hapo, na haishangazi kwamba barua zinapotea kila uchao. Mbaya zaidi ni pale barua zinapokuja kwa lugha ya kigeni.

Kutokana na tatizo la lugha, barua hizo hazipelekwi katika Idara/Kitengo husika au kuwekwa katika mafaili husika. Matokeo yake huduma kwa wateja inachelewa bila sababu za msingi. Hatuelewi kwa nini Mkurugenzi Mkuu au Mkurugenzi wa Fedha na Utawala hawaoni kikwazo hiki.

Idara ya EIA;
Idara hii pia ina mapungufu yake mengi isipokuwa tutajikita kwenye makubwa matatu. Mosi ni rasilimali watu. Baraza lina upungufu wa wataalamu wakati miradi inayosajiliwa ni mingi. Wafanyakazi wa idara za DEICO, DEPR na Kanda hawafanyi kazi za idara zao. Watu wanakwenda kazini lakini hakuna kazi za kufanya.

Huku hili likitokea watu wa idara za EIA wamezidiwa na kazi, wanakaribia kuzama nazo. Mtu angedhani hawa wasio na kazi nyingi, aidha, wawezeshwe au wapewe fursa ya kusaidia miradi mingine ya EIA nk. Kuachia kazi za EIA kwa idara hii iliyozidiwa kunaleta ucheleweshaji wa kazi za wawekezaji.

Kwa mfano, kuna miradi kama ya minara ya simu, miradi ya ujenzi wa majengo marefu, ujenzi wa miradi ya mahoteli, yote hii ingeweza kufanywa na wataalamu wa idara nyingine. Lakini hali haiko hivyo kwa sababu ya maslahi ya kifedha. Wanashikilia miradi yote na kusabibisha kucheleweshwa kwa upatikanaji wa vyeti kwa wawekezaji.

Waziri January Makamba alitoa tamko mbele ya wandishi wa habari kuhusu ucheleweshwaji na upatikanaji wa vyeti, hapa tungependelea sana aongee na wafanyakazi afahamishwe sababu halisi ya hili tatizo, kamwe menejimenti haiwezi kusema ukweli.

Pili, mbali na upungufu huo, tunafanya kazi kwenye mazingira magumu sana. Kwa kawaida maofisa ndio hufanya ukaguzi na baada ya hapo huandika ripoti.

Utaratibu ni kwamba ripoti ikiwa tayari mkaguzi/ wakaguzi huitisha kikao cha wataalamu kutoka taasisi husika za serikali pamoja na wawekezaji wenye mradi kujadili ripoti ile. Baada ya hapo inabakia jukumu lake/ lao kufuatilia mpaka cheti kitoke. Lakini cha kushangaza ni kwamba, mabwana wakubwa ambao wanashinda kivulini ndio wanaofaidika na zoezi hili kipesa.

Kwa taarifa, wakubwa ni kama wanajilipa mishahara miwili kwa njia mbalimbali. Wamo Mkurugenzi Mkuu, Mkurugenzi wa EIA, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Maafisa wa Utawala, wahasibu na wakuu wa idara za EIA. Kwa mfano, kwa kila mradi unaosajiliwa katika Baraza wanajilipa shilingi 130,000 (yaani shilingi 50,000 ya sekretariati wakati hawajaenda field wala kuandika ripoti; shilingi 50,000 ya kusoma kitabu na kutoa maoni; shilingi 30,000 ya kuhudhuria kikao) kila mmoja.

Piga hesabu. Kwa wastani Baraza linafanya vikao vya miradi saba kwa wiki. Hiyo ni sawa na shilingi 910,000 kwa wiki au shilingi 3,640,000 kwa mwezi, au shilingi 43,680,000 kwa mwaka kwa kila mmoja. Hiyo na sawa na kusema kuwa jumla ya shilingi 262,080,000 zinaingia mifukoni mwa watu. Fedha hizo wanapokea hata wasipokuwapo ofisini.

Kama wakurugenzi wana nia njema na Baraza, na kutaka ofisi mpya basi kama wangeokoa hizo shilingi 262 milioni kwa miaka mitano ingepatikana zaidi ya shilingi bilioni moja ya kujenga ofisi za kisasa. Mawaziri kadhaa wamewahi kutembelea Baraza. Hata hivyo, hawakuwahi kuingia ofisini kujionea hali halisi. Wengine hatuna viti wala madawati.

Asilimia 95 ya wafanyakazi wote wanatumia kompyuta mpakatato binafsi kwa shughuli za kikazi. Cha kushangaza zaidi, ofisi kubwa kama ya Baraza haina mashine ya kutolea nakala mtu inabidi uende nje ya ofisi.

Kana kwamba hiyo haitoshi, mashine ya kuchapa inayotumika kwa idara zote nne za Baraza ni moja tu, kama ilivyo kwa kompyuta moja tu inayotumika kwa idara zote nne za Baraza kufanyia kazi. Tumechoka kila siku kuambiwa Baraza halina fedha wakati tunaona kwa macho yetu wakigawiana fedha. Kwa nini wasiboreshe ofisi?

Tunaomba sana mawaziri waweke mikutano na wafanyakazi kwa ufafanuzi zaidi wa hali hii si Menejimenti. Kwa upande mwingine tunaomba Takukuru na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali wakague mahesabu ya fedha zinazotumika kwenye idara ya EIA. Kwa mfano, kwenye bajeti inayopelekwa kwa mwekezaji kuna sehemu inasema “internal review”.

Ukweli ni kwamba hakuna internal review yoyote inayofanyika NEMC. Huwa kuna kikao kimoja tu cha wataalamu ambacho hakizidi watu 20. Lakini bajeti anayopelekewa mwekezaji inasema tuna vikao viwili na wanauhudhuria vikao ni watu 25. Hiyo pesa yote ya ziada inagawanya kwa wakubwa na wengine. Kwa hesabu za haraka haraka kila mwekezaji anatozwa takribani shilingi 1,500,000 hela ya ziada, yaani ulaji wa watu wachache pale ofisini.

Pesa za kazi ya Minara

Kuna kazi za minara zimefanyika na Baraza yaani Vodacom, Airtel, Halotel na Helios. Mwekezaji amepelekewa bajeti ambayo ilipitishwa na uongozi. Bajeti inaeleza utaratibu wa kazi utakavyofanyika hivyo basi malipo yafanywe watu waanze kazi. Bajeti inatengenezwa na maafisa wa Baraza wanaohusika na hiyo miradi na mkurugenzi wa idara ya EIA anapitisha.

Cha kushangaza ni kwamba baada ya pesa kulipwa, uongozi umeshindwa kuwalipa wataalamu waliofanya kazi hizo kama ilivyoelezwa kwenye bajeti iliyokwenda kwa mwekezaji. Kwa mfano, Vodacom wamelipa Baraza wastani wa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kufanya tathmini ya minara yao.

Katika pesa hizo bajeti ya wataalamu ilikuwa wastani wa shilingi milioni sita, lakini wakalipwa wastani wa shilingi milion tatu tu. Je, hizo nyingine zimeenda wapi?

Chanzo:Raia Mwema
 
... Kwa mfano, Vodacom wamelipa Baraza wastani wa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kufanya tathmini ya minara yao. Katika pesa hizo bajeti ya wataalamu ilikuwa wastani wa shilingi milioni sita, lakini wakalipwa wastani wa shilingi milion tatu tu. Je, hizo nyingine zimeenda wapi?
...
Kuweka wazi hii pesa ni kutaka JPM aifute hata hiyo ndogo waliyopewa kwa kigezo cha 'kubana matumizi' au kigezo cha 'ni majukumu yao wanayolipwa mshahara'
 
Back
Top Bottom