Rais Magufuli kuminya mpaka vipele baada ya majipu

Ashura9

JF-Expert Member
Oct 21, 2012
740
485
Magufuli kuminya mpaka vipele baada ya majipu



Rais John Magufuli akiwahutubia wananchi wa Mianzini mkoani Arusha alipokuwa njiani kuelekea Monduli kufunga zoezi la Onesha Uwezo Medani jana, lililokuwa likifanywa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. (Picha na Ikulu).


RAIS John Magufuli amesema ataendeleza kazi aliyoanza ya kutumbua majipu yanayonuka, yasiyoiva na vipele vidogo vidogo vinavyoota mpaka ndani ya vyama mbalimbali vya siasa, ikiwemo katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwani nako kuna majipu.

Alisema hayo jana jijini hapa, wakati akiwa njiani kwenda kufunga mazoezi la Onesha Uwezo Medani, yaliyoandaliwa na kutekelezwa na Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, ambayo ni sehemu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), katika eneo la Lang’arurusu nje kidogo ya Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli mkoani Arusha.

Mbali na uminyaji vipele, Rais Magufuli akizungumza na wananchi hao waliomsimamisha maeneo mbalimbali ili azungumze nao, alionya kuwa wilaya ama mkoa wowote ambao utakumbwa na njaa, itakuwa ni kipimo tosha cha kuonesha kuwa Mkuu wa Mkoa ama Mkuu wa Wilaya husika, hafai kuendelea na wadhifa huo.

Alisema kwa kuwa mvua zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi, viongozi wa wilaya na mikoa wana wajibu wa kuwahamasisha wananchi kuzalisha mazao ya chakula, ili wasikumbwe na njaa.

Rais Magufuli ameendelea kuwasihi wananchi wa Arusha Mjini kuwa uchaguzi umekwisha na kwamba kilichobaki sasa ni kazi huku akiwahimiza kufanya kazi za uzalishaji mali, ikiwemo kilimo.

“Naomba ndugu zangu mniombee, na ninapenda kuwahakikishia kuwa sitawaangusha. Yote niliyoahidi nitayatekeleza bila kubagua, nawaombeni mnipe muda na muwe wavumilivu,” alisisitiza Rais Magufuli.

Alirejea kauli zake alizotoa jana alipoingia mkoani Arusha kuwa ataendelea kuwashughulikia wezi, mafisadi na watendaji wote wa Serikali ambao wamekuwa wakijineemesha kwa kufuja mali ya umma kupitia kampeni yake ya ‘Kutumbua Majipu’ na amewaomba Watanzania wote waendelee kumuombea ili atumbue majipu yote hadi yaishe.

Rais Magufuli amelazimika kuzungumza na wananchi wa Arusha Mjini waliokuwa wamekusanyika kwa maelfu kando kando mwa barabara na kujikuta akisimamishwa na wananchi wa Sanawari, Tekniko, Ngarenaro, Kona Ya Nairobi, Mbauda, Majengo na Kisongo.

Akiwa katika eneo la Ngarenaro, wananchi wamelalamikia vitendo vya rushwa vilivyokithiri katika Mahakama ya Mwanzo ya Maromboso na pia katika eneo la Kona ya Nairobi wananchi wamelalamikia kero za kelele na uchafu wa kiwanda kilichojengwa kandokando mwa barabara ambapo Rais Magufuli ameahidi kufanyia kazi kero hizo.

Baadhi ya wananchi hao walimpongeza Rais kwa kuonesha kwa moyo wa kipekee jinsi anavyofanya kazi, ikiwemo kukusanya mapato ya Serikali, yaliyokuwa yakiibwa na watu wachache kunufaika na rasilimali za Taifa huku wengine wakishindwa kuona raha katika nchi yao.

Chanzo: Magufuli kuminya mpaka vipele baada ya majipu
 
Kwanza nianze na cheo cha Amir jeshi mkuu.

Kiuhalisia cheo hiki hakina hakina mahusiano yoyote na vyeo vinavyopatikana katika ngazi za kijeshi! Hiki hata mtu ambaye hajui nini maana ya jeshi akishakuwa rais wa nchi tu hupewa! Hakina mahusiano yoyote na vile vyeo vinavyopatikana ndani ya jeshi ambavyo mwisho wake ni Jenerali!

Mfano ingetokea kama rais Kikwete (enzi akiwa rais) leo angevaa vazi la jeshi basi angevaa katika ngazi ya ukanali ila kwa rais (e. g
angekuwa Kikwete) cheo chake cha Amir jeshi mkuu kingebaki palepale na angetambulika kwa cheo chake cha Amir jeshi mkuu!

Ni amri ya jeshi kuwa mtu anapokuwa katika vazi la jeshi basi awe kirasmi! Kuendana na cheo chake. Ila hii haiondoi maana kuwa mtu akivua lile vazi basi cheo chake hakitambuliki! La hasha! Ila msisitizo ni pale unapokuwa ndani ya lile vazi basi uwe rasmi ndani ya mfumo wa jeshi la wananchi!

Mathalan Mwamunyange akiwa kiraia bado ni mkuu wa majeshi na anapewa sifa zote za ukuu wa majeshi! Ila akiwa ndani ya vazi la jeshi ni lazima awe ndani ya vazi rasmi linalotambua cheo chake ndani ya mfumo wa jeshi (Jenerali)

Kwanini rais Magufuli hakuwa sahihi?
Mbali na kuwa bado ni Amir jeshi mkuu, rais Magufuli hana cheo chochote ndani ya mfumo wa jeshi! Hajawahi kuwa ndani ya jeshi la wananchi kama mwana jeshi! Lile vazi ni la mwanajeshi wa kawaida ndani ya jeshi la wananchi! Kwa maana nyingine rais Magufuli pale alikuwa ndani ya mfumo wa jeshi! Labda tuambiwe kuwa alipoenda Monduli naye alitunukiwa cheti cha kufuzu mafunzo ya kijeshi ndani ya JWTZ!

Vinginevyo rais atakuwa amevaa lile vazi kama wanavyofanya kina Diamond ambapo ni kinyume na taratibu za jeshi na ndo maana wanapigwa marufuku!

Nadhani mmekuwa mkimwona Kikwete enzi akiwa rais alikuwa akitoa saluti kwa viongozi wenzake! Pale alikuwa akitumia mfumo rasmi wa jeshi kwa wakubwa zake kijeshi (Ingawa cheo chake cha Amir jeshi mkuu kilikuwa palepale) hivyo alikuwa hakosei kufanya hivyo!

Narudia tena: cheo cha Amir jeshi mkuu hakipo ndani ya mfumo rasmi wa jeshi. Hata mtoto mdogo akiwa rais wa nchi basi cheo hicho kinafuatia palepale!

Pia inashauriwa kuwa si vyema sana rais wa nchi ambaye amechaguliwa kwa kura kuwa ndani ya mavazi rasmi ya kijeshi kutokana na cheo chake! Hii inazua mkanganyiko wa heshima za kijeshi zinazotolewa! Mathalan Kikwete leo angeamua kuvaa vazi rasmi la kijeshi huku akiwa rais basi angeishia cheo cha kanali! Hapo yupo ndani ya vazi rasmi la jeshi kisha anapokea saluti kutoka kwa jenerali! Hii siyo sawa! Rais wa nchi anabaki kuwa Amir jeshi mkuu hii haijalishi kuwa amepita na/au hajapita jeshini! Kinacholeta mkanganyiko ni lile vazi rasmi la jeshi!

Huwa wanasema "ukiwa nje ya lile vazi utaheshimiwa kwa cheo chako kijeshi, ukiwa ndani ya vazi utaheshimiwa kutokana na vazi" na ndo maana mtu akiwa ndani ya lile vazi basi anawekewa vyeo vyake kijeshi lakini akiwa nje ya vazi hawekewi vyeo vyake ila bado anatambulika maisha yake yote!

Kwa hiyo kuna mawili! Eidha rais Magufuli ameanza rasmi mafunzo ya kijeshi na ana cheo cha chini kabisa kijeshi na/au alivaa lile vazi kama watu wengine! Ikiwa hilo la pili ni kweli basi hakuwa sahihi kutokana na kuvaa vazi rasmi la JWTZ bila kuwa ndani ya mfumo wa jeshi!
Ikiwa hilo la kwanza ni sahihi basi yuko sawa na cheo chake cha Amir jeshi mkuu bado kipo palepale ila kwa hapo yupo ndani ya mfumo rasmi wa jeshi!

G Sam
 
Back
Top Bottom