Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
- Awatema rasmi aliowaahidi kuwapangia kazi
- Mmoja abubujikwa machozi, asema hakujiandaa
Chanzo cha habari kimetonya kuwa idadi ya makatibu na manaibu katibu wakuu waliopewa barua hizo za kustaafishwa inakadiriwa kufikia 15.
“Mimi sijafikisha umri wa lazima kustaafu kisheria lakini kwenye barua ile nimeambiwa kwamba nistaafu kwa hiari kwa sababu kisheria naruhusiwa kufanya hivyo.
“Sikuwa nimejipanga kwa ajili ya kustaafu lakini kwa sababu nimeambiwa hivyo, maana yake ni kuwa sasa itabidi nistaafu kwa hiari lakini kwa lazima. Barua nimepata tayari,” alisema Katibu Mkuu mmoja kwenye serikali iliyopita ya Rais Kikwete.
Moja ya barua ya kustaafishwa huko iliyofanikiwa kuonekana, imeonekana ikiwa imepigwa muhuri wa siri, ikimaanisha kuwa kilichomo ndani ya barua ile ni cha siri.
Kwa mujibu wa maelekezo ya barua hizo zenye muhuri wa siri; waliokuwa makatibu wakuu wa wizara kwenye serikali ya rais Jakaya Kikwete ambao Rais Magufuli aliwaacha na tayari wamefikisha miaka 60 wametakiwa kustaafu kwa mujibu wa sheria, huku wale wenye miaka 55 na kuzidi wakitakiwa kustaafu kwa hiari.
Maelekezo hayo ya Ikulu ni kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi Namba 3 wa mwaka 2002 unaoeleza kuhusu umri wa kustaafu kwa watumishi wa umma.
Ingawa imekuwa ni kawaida kwa marais wapya kubadili makatibu wakuu wakati wanapoingia madarakani, baadhi ya waathirika wa mara hii wametonya kwamba hii ni mara ya kwanza kwa watumishi hao kustaafishwa kwa lazima.
Mmoja wa makatibu wakuu wastaafu waliowahi kuzitumikia serikali zote zilizotawala Tanzania tangu kupata Uhuru ameeleza kwamba hatua ya kuwastaafisha makatibu hao inaweza kuwa na athari kwa serikali.
“Serikali ya Magufuli ni mpya na angehitaji uzoefu wa watumishi hawa wa umma hata kama si katika nafasi walizokuwa wakishikilia awali. Mabadiliko yoyote katika nchi yanaletwa na a very strong civil service (watumishi imara wa umma).
“Sidhani kama hatua hii ni nzuri sana. Mimi nimefanya kazi serikalini wakati wa Nyerere, Mwinyi, Mkapa na nikastaafu wakati wa Kikwete lakini sikuwahi kuona kitu kama hiki,” alisema Katibu Mkuu mstaafu huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Kwa mujibu wa chanzo cha taarifa hiyo ni kwamba, makatibu wakuu waliokuwa na umri chini ya miaka 55 wametakiwa kustaafu mapema ingawa wanaofanya hivyo wana hatari ya kupoteza sehemu ya mafao yao.
Baadhi ya makatibu wakuu maarufu wanaotajwa kuguswa na barua hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, wa Miundombinu, Omar Chambo na wa Uhusiano wa Afrika Mashariki, Dk. Joyce Mapunjo.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa Kikwete, Jumanne Sagini, Jumatatu wiki hii alitangazwa na Rais Magufuli kuwa Katibu Tawala mpya wa Mkoa wa Simiyu na hivyo yeye si mmoja wa waliokumbana na rungu hili la Magufuli, mbali na yeye mwingine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donan Mmbando, ambaye naye Jumatatu wiki hii aliteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo mkoani Dodoma.
Source: Raia Mwema