Rais Kikwete na Maendeleo ya Michezo na Sanaa

Supermwanangu

Member
Apr 18, 2012
12
1
Je tumemtumia vizuri Rais Kikwete katika kuinua kiwango cha Maendeleo ya michezo na Sanaa?
Rais Kikwete ni rais ambaye kati ya marais wa awamu zote nne amekuwa mwanamichezo na mpenda michezo kwa kiasi fulani kushinda marais wengine. Sababu nitazieleza hapo baadae. Kufuatana na asili yake,tabia zake, namna alivyoingia madarakani na jinsi anavyotekeleza na kuendesha kazi zake kama kiongozi wa nchi, mimi binafsi namfananisha na watu ambao katika jamii yetu tunawaita Bwana au Bi Shughuli. Bwana/Bi Shughuli uishi kwa kutegemea matukio au shughuli mbalimbali kwenye jamii. Shughuli na matukio kama majanga, misiba, harusi, sherehe, ugomvi na mitafaruku mbali mbali ya ndani ya jamii uwapa ulaji na umaarufu hawa jamaa. Bwana/Bi Shughuli kwa kutumia mbinu mbali mbali ujipenyeza katika shughuli hiyo na kuhakikisha anaiteka au anapewa majukumu maalum ambayo yatamwezesha yeye kutekeleza azima yake ambayo kwanza ni kuingiza chochote mfukoni. Bwana/Bi Shughuli anaishi mara zote bila mkakati na mipango ya muda mfupi na mrefu maana anajua kuwa shughuli au matukio mengine yanatokea ghafla hivyo lazima ajiandae kishughuli wakati wowote hivyo atakuwa tayari kubadilisha ratiba yake saa yeyote na mahali popote ili ahudhurie shughuli mahali popote. Bwana/Bi Shughuli wana tabia ya kujipendekeza kwa kila mtu, pia upenda kutengeneza mitandao ndani ya jamii ili waweze kutaarifiwa kila jambo litendekalo na sana sana upenda umaarufu kwa kujichanganya katika kila jambo ambalo litamletea umaarufu kwenye jamii hasa hasa michezo, sanaa na siasa. Mara nyingi viongozi wetu wa michezo na siasa wamekuwa ma Bwana/Bi Shughuli wazuri sana.
Tumemshuhudia Rais Kikwete akitekeleza majukumu yake ya kuongoza nchi kama Bwana Shughuli na hii imejitokeza katika changamoto nyingi zinazoikabili nchi yetu chini ya Utawala wake. Amekuwa mstari wa mbele katika kuhudhuria matukio na shughuli ukilinganisha na kasi yake ya kufafanua kwa kina namna gani atatekeleza ahadi na ilani ya uchaguzi ya chama chake. Maamuzi magumu, mikakati/mbinu mbadaala na ubunifu wa Miradi mpya ya kukwamua hali ya maisha ya mtanzania kufuatana na changamoto zilipo haitoshelezi hali halisi katika Serikali yake hii-hamna jipya kabisa.Safari za nje za Rais Kikwete ni hulka yake ya u Bwana Shughuli hivyo isionyeshe ugeni kwani ndivyo hawa jamaa wa shughuli walivyo. Kama nilivyoeleza hapo juu kuwa Bwana/Bi Shughuli ni mpenda umaarufu na mojawapo ya shughuli zinazoleta umaarufu wa haraka sana ni michezo na sanaa, hoja yangu hii inajikita katika kuleta mjadala wa kuwa tumeshindwa kumtumia Rais Kikwete katika kuwekeza na kujenga misingi imara ya Maendeleo ya michezo na sanaa na kuhakikisha Michezo na Sanaa inazalisha ajira za vijana zilizo katika mfumo rasmi na endelevu nyingi na za kutosha.
Rais Kikwete alipoingia madarakani katika hotuba yake ya kufungua bunge 2005 alieleza mkakati wake wa kuiendeleza sekta ya michezo na sanaa kwa kuanza na kuandaa kongamano la kitaifa litakalo jadili na kuelekeza mwelekeo wa sekta ya michezo kitaifa. Mpaka sasa hivi halijawahi kufanyika na hakuna ambaye anauliza mpaka sasa hivi. Ujio wa Kocha Maximo na Makocha wengine wa Netball and ngumi ni mojawapo ya harakati za Rais Kikwete katika kutekeleza azima yake katika Maendeleo ya michezo. Sakata la Studio ya Kisasa ya kuredi mziki aliyoahidi na ambayo ilikuwa na mgogoro na wasanii wa bongo fleva na hip pop na pia mashindano ya dunia ya kumtafuta Miss Utalii alipoingilia baada ya waandaaji kushindwa kumudu ni mifano bora ya harakati zake za kusaidia sekta ya sanaa nchini. Kwa wapenzi wa soka kumbuka na zingatia mchango wa Rais Kikwete katika kuhudhuria michezo mbali mbali pale uwanja wa taifa(Mkapa kwa miaka yake 10 hakuwahi kuhudhuria mechi hata moja) na pia misaada ya hali na mali kwa timu zetu za taifa ambazo alizozitoa. Ni Serikali yake iliyorudisha michezo mashuleni kwa kurudisha mashindano ya UMISETA na UMISHUMTA. Ni mambo mengi ambayo siwezi kuyaandika yote ambayo Rais Kikwete amefanya katika sekta hii ya michezo na sanaa. Ninaleta hoja kuwa hayo yote aliyoyafanya na atakayoyafanya katika kipindi chake kilichobaki( kama atamaliza) atayafanya kwa kuzingatia hulka yake ya Bwana Shughuli sio vinginevyo. Na hapo ndipo kwenye msingi wa hoja yangu kuwa kama tungekuwa makini, wabunifu,washirikishaji na wanamkakati wa Maendeleo ya michezo na sanaa tungetumia Rais Kikwete katika awamu hii ya nne na tungeweza kuwekeza na kujenga misingi imara ya maendeleo ya michezo na sanaa. Nawakumbusha kuwa kuwekeza katika michezo na sanaa ni jambo ambalo matunda yake yatapatikana baada ya miaka 10-15 sio kwa kipindi kifupi kama wengine tunavyodhani. Sekta ya michezo na sanaa imetelekezwa miaka nenda rudi katika awamu zote za uongozi.Mfano mzuri ni ujenzi wa viwanja bora vya michezo mikoani na wilayani ambapo ni uwanja mmoja(Modern Stadium) wa kisasa uliojengwa ndani ya miaka takribani 30. Jamii ndani ya Serikali kwa kutumia ilani za uchaguzi na sera za chama tawala imeshindwa kutoa maelekezo yakinifu ya nini kifanyike katika kuwa na Maendeleo endelevu katika sekta hii. Hakuna maandalizi makini na ya kina yanayofanywa na jamii kuielekeza Serikali ya awamu inayofuata kuhusu nini kifanyike katika kuboresha sekta ya michezo na sanaa. Hivyo hoja yangu ni kutoa chamgamoto kwa Great Thinkers kubadilishana mawazo na kuanza kuwa na mkakati wa kimawazo kwa awamu ya Tano ya Utawala kuhusu sekta hii nyeti ya Michezo na Sanaa ili fursa ikitokea isipotee hivi hivi. Kumbuka kuwa sekta hii haipewi nafasi kujadilika kwa sababu ya nyingi zitakazojitokeza kadri tutakavyokuwa tunajadili hivyo muhimu tukaipa msukumo wa kuichambua na kujadili kwa kina na upana zaidi. Namalizia kwa maswali machache ambayo yakipata majibu yake yatazalisha hoja nyingine ambazo zitaendeleza mijadala na pia kupanua wigo wakujadili na mwisho mbele yake uelewa utakuwa mpana kwa wanajamvi kwa ajili ya Maendeleo ya watanzania.Majibu ya maswali haya yatabeba ujumbe na maelekezo kwa awamu ya tano ya uongozi ambapo ilani za uchaguzi, sera,sheria na mikakati ya utekelezaji itapangwa kwa umakini ili kuepuka yaliyojitokeza katika awamu za kwanza, pili, tatu na nne za uongozi.
Maswali yenyewe ni haya hapa: Je tungemtumia vizuri Rais Kikwete angeweza kujenga misingi bora ya Maendeleo ya Michezo na Sanaa? Je Michezo na Sanaa ina nafasi gani katika kukuza uchumi wa Taifa? Changamoto gani za msingi zinaikabili sekta ya Michezo na Sanaa nchini? Nini mchango wa sekta ya Habari katika Maendeleo ya Michezo na Sanaa nchini? Je tumeainisha na tumejifunza changamoto zilizosababisha michezo ikafutwa mashuleni? Tufanye nini kuhakikisha kuwa sekta ya Michezo na Sanaa inakuwa ni Nguzo tegemezi ya uchumi wa Taifa kwa kuzalisha ajira za kutosha na kuongeza pato la taifa? Fursa zipi na sehemu gani za kuwekeza katika sekta hii? Ni tegemeo langu kuwa Wanajamii mnayo maswali mengine ya kuongezea. Naomba kutoa hoja na pia nakaribisha mjadala.
 
Back
Top Bottom