Masaibu ya msaidizi wa Raila yazidi
Bw Eliud Owalo akiwa katika makao makuu ya CID, Nairobi Julai 17, 2013. Picha/STEPHEN MUDIARI
Na DAVE OPIYO Na ISAAC ONGIRI
Imepakiwa - Monday, July 22 2013 at 07:16
Kwa Mukhtasari
Masaibu ya msaidizi wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, yanaonekana kuzidi baada ya kubainika kuwa maafisa wawili wakuu wa usalama nchini wamemshtaki kwa kuwachafulia majina.
MASAIBU ya msaidizi wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga yalizidi jana baada ya kubainika kuwa maafisa wawili wakuu wa usalama nchini wamemshtaki kwa kuwachafulia jina.
Huku ikonekana kwamba Mkuu wa ulinzi Jenerali Julius Karangi, na mkuu wa ujasusi nchini Michael Gichangi, walighadhabishwa na madai ya Bw Eliud Owalo, kuwa walihusika na mpango wa serikali kuingilia shughuli na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Machi 4.
Wakati wa kampeni za uchaguzi wa urais, Bw Owalo alitoa taarifa na kudai ana ushahidi wawili hao walisimamia mikutano kadha iliyolenga kushawishi matokeo ya uchaguzi ambapo Uhuru Kenyatta ndiye alitangazwa mshindi.
Kwenye taarifa hiyo, alidai Jenerali Karangi alisimamia mkutano aina hiyo Februari 7, katika afisi yake iliyo makao makuu ya Idara ya Ulinzi.
Kwa upande wake, Bw Gichangi alidaiwa kuwa mmoja wa waliosimamia mikutano kadha katika maeneo tofauti, ikiwemo Hoteli ya Outspan, Nyeri, Disemba 15, na Pizza Garden, Nairobi, Disemba 20 mwaka jana, akiwa na lengo sawa na la Jenerali Karangi.
Kwenye barua tofauti zilizoonekana na Taifa Leo hapo Jumapili, mawakili wao walisema madai hayo yaliwapatia wateja wao sifa mbaya.
Wakili wa Jenerali Karangi, Bw Waweru Gatonye, alisema madai kuwa mteja wake alisimamia mkutano huo ni uongo, kwani hakuwa nchini, na alikuwa amesafiri Uganda kuhudhuria siku ya jeshi, iliyoadhimishwa Arua.
Kwa upande mwingine, Bw Mohammed Muigai, anayemwakilisha Bw Gichangi, alisema taarifa hiyo ilisambazwa kwa njia ovyo iliyoweza kuzua taharuki, ikiwa na nia mbaya.
Wakati huo huo, uchunguzi wa polisi unaomhusu Bw Owalo, umechukua mwelekeo mpya baada ya mwanaharakati Nairobi kuandikia Idara ya Upelelezi (CID) akidai yeye ndiye anamiliki vuvugu ambalo limetajwa katika kesi hiyo.
Kupindua serikali
Katika barua aliyomwanfdikia mkuu wa kitengo cha makosa ya jinai Bw John Kariuki, mwanaharakati Okiya Omtatah alidai kuwa yeye ndiye anamiliki vuguvugu linalojiita March 4 Movement (M4M) huku akidai vuvugu hilo halina nia yoyote ya kupindua serikali.
Bw Omtatah huenda akampatia afueni Bw Eliud Owallo ambaye amekuwa akihusishwa na vuguvugu hilo.
Omtatah alisema vuguvugu hilo linalenga kuendesha kampeni ya kutaka kuungwa mkono kwa pendekezo ambalo linataka kubadilishwa kwa kifungu cha 138 cha katiba kuhusu uchaguzi wa Urais. Pendekezo hilo linalenga kuzuia jamii zenye watu wengi 'kuzigandamiza' jamii zenye watu wachache.
"M4M ni kampeni ambayo inapigania kubadilishwa kwa kifungu cha 138 cha katiba ili kuondoa taifa hili kwenye 'mfumo wa wengi wape' hadi 'usalama wa wengi'," akasema Omutatah.
Kiongozi huyo wa M4M pia alikabidhi CID barua aliyomwandikia mwenyekiti watume ya uchaguzi (IEBC) Bw Ahmed Issack Hassan, mnamo Aprili 14 akimfahamisha kuhusu nia ya vuguvugu hilo.
http://www.swahilihub.com/habari/HABARI-ZA-SIASA/-/1310214/1922636/-/awbsmr/-/index.html