RAIA MWEMA: Waasi wa Kikwete hadharani | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

RAIA MWEMA: Waasi wa Kikwete hadharani

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Jul 29, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Jul 29, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 64
  Trophy Points: 145
  Waandishi Wetu
  Dodoma
  27 Jul 2011
  Toleo na 196

  [​IMG]
  • Jumuiya za chama zahusishwa
  • UVCCM watofautiana mkutanoni
  • Baadhi wakejeliwa kujipendekeza kwa JK

  MTANDAO wa viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wakiwamo wa jumuiya za chama, umejitokeza na unapingana na uongozi wa juu wa chama hicho akiwamo Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, Raia Mwema limethibitishiwa.

  Taarifa za hivi karibuni zinawataja viongozi wa CCM wa baadhi ya mikoa na wilaya, viongozi wa Jumuia za chama za Vijana (UVCCM), Wazazi na Wanawake (UWT) kuwa tayari wameanza kutoa matamko ya wazi kupingana na maamuzi ya vikao vya juu vya chama hicho na kuwakejeli viongozi wake wa juu akiwamo Mwenyekiti wao, Kikwete, Katibu Mkuu, Wilson Mukama na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.

  Hiyo inatokana na nguvu kubwa waliyonayo viongozi waliotakiwa na NEC ya CCM ‘kujivua gamba'; kwa maana ya kujitoa katika uongozi kutokana na kutajwa katika kashfa mbalimbali za ufisadi.

  Tayari Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, amekwishakutekeleza agizo hilo, na sasa wanasubiriwa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambao wamekuwa wakiwekwa katika kundi moja na Rostam. Uchunguzi wa Raia Mwema unaonyesha ya kuwa kuna uasi wa chini kwa chini wa muda mrefu, lakini ambao umeibuka dhahiri zaidi siku za karibuni kwa baadhi ya viongozi kujitokeza hadharani kupingana na maamuzi ya vikao vya juu vya CCM; huku baadhi ya vijana wakidiriki kujeli moja kwa moja kwa kuwaambia wenzao kuwa wanajipendekeza kwa Kikwete.

  Hoja ya sasa ambayo imeanzia katika vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho kuhusiana na kuwachukulia hatua baadhi ya viongozi na kupewa msemo wa ‘kujivua gamba' ndiyo iliyochokoza hisia za makundi ya kishabiki ambayo yanapingana.

  Katika kikao cha UVCCM cha mwishoni mwa wiki, mjini Dodoma, baadhi ya vijana wanaotajwa kuwa karibu na kundi la wanaotakiwa kujivua magamba waliwashambulia wenzao wanaounga mkono kujivua magamba hayo wakisema wanajipendekeza kwa Rais Kikwete, na wao kujibu mapigo kwa kusema kutoridhia uvuaji gamba ni kuzubaisha umoja huo kama kuku aliyenyeshewa mvua. Hata hivyo, pamoja na tambo hizo za kila kundi, hatimaye Baraza Kuu la UVCCM limeunga mkono mchakato wa kujivua gamba unaoendelea.

  Hali hiyo ya vijana hao kunyoosheana vidole hadi kufikia hatua ya kuhoji uraia wa mwenzao mmoja aliyewahi kutangazwa si raia, ilijitokeza wakati wa majadiliano ndani ya kikao cha Baraza Kuu la UVCCM-Taifa, Julai 23, mwaka huu, mjini Dodoma.
  Kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka katika kikao hicho cha siku moja kilichofunguliwa na Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, shinikizo kubwa liliibuliwa na baadhi ya vijana wakitaka kikao hicho kiunge mkono uamuzi wa NEC wa ‘kujivua gamba', na wenzao wanaodaiwa kuathiriwa na utekelezaji wa uamuzi huo wakipinga hadharani, wakiongozwa na James Millya ambaye ni Mwenyekiti wa UVCCM – Arusha na Hussein Bashe ambaye ni mjumbe wa baraza hilo. Millya amesuluhishwa hivi karibuni na Katibu wa CCM, mkoani Arusha, Mary Chatanda, baada ya tofauti zao zilizoibuka wakati wa mchakato wa uchaguzi wa mbunge wa Arusha Mjini.

  Shinikizo kuridhia uvuaji gamba
  Inaelezwa kuwa ni kutokana na shinikizo hilo ambalo, hata hivyo, licha ya kupingwa na akina Millya na Bashe, uongozi wa UVCCM, akiwamo Kaimu Mwenyekiti, Benno Malisa, walikuwa wazito kuridhia kikao hicho kitoe tamko la kuunga mkono kujivua gamba. Vyanzo vya habari kutoka ndani ya kikao hicho, vinamnukuu mjumbe wa baraza hilo kutoka mkoani Mbeya, Asajile Mwambambale, kuwa alichukua tahadhari ya mapema akiandika barua rasmi kwa uongozi wa UVCCM kuhakikisha kikao hicho kinaazimia kuunga mkono falsafa ya kujivua gamba.

  Raia Mwema imefanikiwa kupata barua hiyo ya Mwambambale ya Mei 5, mwaka huu, ikielekezwa kwa Katibu Mkuu wa UVCCM, Martine Shigella, ikiwa na kichwa cha habari "Mapendekezo kwa UVCCM kuchukua hatua za kuunga mkono hadharani maamuzi ya NEC katika utekelezaji wa CCM kujivua gamba."

  Mbali na barua hiyo kupendekeza suala hilo liingizwe kama ajenda kwenye kikao hicho, lakini pia ilipendekeza UVCCM kutathmini utendaji wake katika idara, makao makuu na kamati ya utekelezaji na hoja ya uwakilishi wa wabunge wa viti maalumu UVCCM.
  Mtego kwa wapinzani wa uvuaji gamba Katika barua yake, Mwambambale anasema: "Ni vema nikaweka wazi kuwa pamoja na mambo mengine yaliyochangia CCM kupoteza umaarufu wake, suala la ufisadi na ukosefu wa maadili kwa baadhi ya wanachama na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake yamechangia kwa kiwango kikubwa zaidi.

  "Katibu Mkuu UVCCM, ninapenda kuweka wazi kuwa binafsi sijaridhishwa na mapokeo na mwenendo wa UVCCM kama jumuiya ya CCM katika kushiriki kwake katika utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa na chama.

  "Tangu kufikiwa kwa maamuzi ya CCM kujivua gamba Dodoma na kuundwa kwa sekretariati mpya, UVCCM imekuwa kimya na kunywea kabisa kama kuku aliyelowana katika mvua ya masika. Kimya hiki kinatia shaka kwamba labda UVCCM wana mtazamo tofauti, na kutounga mkono maamuzi hayo (ya uvuaji gamba) ni uasi.

  "Sekretariati mpya imeachwa kama yatima ijitambulishe kivyake pasipo uungwaji mkono wa karibu wa jumuiya zake ikiwamo UVCCM. Naipongeza Sekretariati kwa kuanza vizuri na kasi kubwa licha ya ukimya wa Jumuiya za Chama. Sitaki kuleta hoja za kuanza kudadisi kuwa labda UVCCM haiungi mkono maamuzi hayo kwani hata kama ndivyo ilivyo, UVCCM ikiwa jumuiya ya CCM ni jeshi la CCM na hivyo inawajibika kushiriki kikamilifu katika kusimamia utekelezaji wa maamuzi halali ya CCM pasipo kujali kama miongoni mwa wana-UVCCM wapo wasiounga mkono.

  "Ni vema wasiounga mkono wakae pembeni ili wasiathiri mwenendo wa Jumuiya. Tunayo kazi moja tu kama jeshi la CCM, nayo ni kwenda kutekeleza maamuzi ya CCM. Ni kufuatia mapungufu haya, ninaleta kwako mapendekezo yafuatayo kwa UVCCM Taifa ili kuweza kurejea katika dhana ya msingi ya UVCCM kuwa Jumuiya ya Chama.

  Anashinikiza umoja huo kutoa tamko akisema; "UVCCM itoe tamko la kuunga mkono maamuzi ya CCM yaliyofikiwa katika vikao vyake vya CC na NEC vilivyofanyika Aprili mjini Dodoma. Ikizingatiwa kuwa hakuna tamko la kitaasisi lililotolewa mpaka tarehe ya andiko langu kwako. UVCCM isitoe mwanya wa CCM kushindwa katika dhana ya kujivua gamba."

  Malisa akwepa hoja, achangamkiwa

  Akitambua alikwishawasilisha barua hiyo lakini mwenendo wa kikao chini ya Malisa na Shigella unakwepa kujadili na kupitisha azimio kuunga mkono dhana ya kujivua gamba, Mwambambale aliomba kuzungumza katika kikao akisema: "Ni wakati muafaka sasa kwa vijana wa CCM kwa kauli moja kuunga mkono dhana hii muhimu ya kujivua gamba ukizingatia kuwa Rostam Aziz amejivua gamba na kuonyesha njia kwa wengine kama Edward Lowasa na Andrew Chenge."

  Hapo ni kama alichokoza hisia za vijana wanaowaunga mkono wanasiasa waliotajwa na ndipo wapinzani wa kuvua gamba walipojitokeza.

  Wapinzani wa hoja hiyo walianza kuwashambulia viongozi wanaojitaja kuwa vinara wa sasa wa falsafa ya kujivua gamba kama Samuel Sitta, Dk. Harrison Mwakyembe na Nape Nnauye na wengine wenye msimamo dhidi ya ufisadi katika CCM.

  Katika mashambulizi hayo, walijaribu kushawishi bila mafanikio kutumia UVCCM kushinikiza CCM kiwaite na kuwahoji kina Sitta kwa kauli walizotoa hivi karibuni mkoani Mbeya katika mkutano wa hadhara ambako Sitta alisema tatizo la umeme si tu linachangiwa na mikataba ya ovyo lakini pia ni ufisadi wa baadhi ya viongozi.
  Mchangiaji mwingine alisema: "Kama ambavyo hajawahi kusikia vijana wakipinga suala la falsafa ya kujivua gamba hivyo ndivyo na mimi sijawahi kusikia vijana wa CCM wakiunga mkono falsafa hiyo ya kujivua gamba. Hivyo huu ni wakati muafaka kwa vijana wa CCM kuunga mkono kwa kauli moja falsafa hiyo ya kujivua gamba."

  Mjumbe mwingine kutoka Mkoa wa Mara, aliinuka na kusema; "Hoja hii (kujivua gamba) ni ya msingi sana ni vema baraza hili likaona busara ya kuipa uzito wa pekee; maana jumuia ya vijana ya CCM ni moja ya mihimili muhimu sana ya chama. Na hii itampa nguvu sana mwenyekiti wa chama kuendelea kufanya mageuzi ndani ya chama na serikalini."

  UVCCM Kigoma wavuana gamba
  Katika mwendelezo wa falsafa ya kujivua gamba, Baraza Kuu la UVVM mkoani Kigoma limemsimamisha uenyekiti, Mwenyekiti wa UVCCM wilayani Kibondo, mkoani Kigoma, Toyi Butono. Kwa sasa Butono anasubiri hatima yake katika vikao vya juu vya chama hicho.

  Akizungumza na Raia Mwema kutoka Kigoma, Katibu wa Chipukizi na Uhamasishaji wa UVCCM Kigoma, Nicholaus Zacharia, alisema Butono amesimishwa katika kikao cha baraza kilichoketi Jumatano wiki iliyopita, kwa tuhuma za kusaidia kufanikisha ushindi wa ubunge kwa mbunge wa upinzani, badala ya CCM. Wengine walioadhibiwa katika falsafa ya kujivua gamba ni Joel Rububura, wakati Asia Dodo akiwekwa chini ya uangalizi. Akizungumzia uamuzi huo, Zacharia alisema lengo ni kuwashughulikia wote waliokisaliti chama wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
   
Loading...