Pumzika Kaijage, umetuachia pengo

Pumzika Kaijage, umetuachia pengo

karama kaila

Senior Member
Joined
Jan 30, 2015
Posts
122
Reaction score
60
Hatimaye kwa majonzi na huzuni kubwa jioni ya leo 19/11/2016 tumekupumzisha kwenye nyumba yako ya milele ndugu yetu, mpiganaji na mzalendo Joshua Kaijage Kilembwe.

Tangu tulipopokea taarifa ya kifo chako sote tuliokufahamu tumekuwa katika hali ya majonzi na huzuni kubwa. Wengi wamekulilia na wengi wamesikitika kwa kukupoteza MTU uliyejitoa sana kwa kutenga muda na maarifa yako katika kuhakikisha unapigania kujengwa kwa misingi imara na ustawi wa demokrasia ndani na nje ya chama chake.

Kwa familia ya ACT Wazalendo ulikuwa shujaa, kiungo muhimu na mpambanaji wa dhati na daima hukuchoka wala kukata tamaa kusimamia kile ulichokiamini. Hakika tumebaki na pengo kubwa.

Ulikuwa Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo jimbo la Kasulu mkoani Kigoma lakini mapenzi, moyo wa kujitolea na utendaji wako ulikufanya ufahamike sana katika medani za siasa za kitaifa. Wengi walikufahamu kwa maandiko yako kila mara ukikitangaza chama chako bila woga na kukitetea kila pale ilipobidi kufanya hivyo. Hakika utendaji wako ulitukuka.

Ulishiriki kikamilifu kwenye kazi mbalimbali za chama ikiwemo za kitaifa kama vile uzinduzi na ziara ya kukitambulisha chama katika mikoa mbalimbali nchini na ni hapo ambapo ulidhihirisha utendaji wa hali ya juu kwa kuhakikisha unawahabarisha wanachama na watanzania kwa ujumla kila hatua iliyofikiwa. Hakika ulikuwa MTU wa kipekee.

Jimboni Kasulu uliendelea kuwa kiungo muhimukwa chama na wananchi na ulishiriki kikamilifu kazi za kampeni na uenezi wa chama bila kusita. Hakika ulijitoa kwa dhati ya moyo wako.

Tunakumbuka, Mwalimu ulisafiri na kufika Dar es Salaam tarehe 23/10/2016 kwa ajili ya matibabu yako na tarehe 24/10/2016 tulikushauri tuanze matibabu Kwenye Hospitali ya Serikali ili kama italazimika kutakiwa matibabu na uangalizi zaidi wa kitabibu iwe rahisi kupata rufaa kwenda hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mwenyewe ukapendekeza tuanzie Hospitali binafsi ya Agha Khan ambapo tuliafiki na ukafanyiwa vipimo vya awali na kumuona Daktari Bingwa ambaye alishauri ufanyiwe kipimo maalumu ambacho tulilipia na kikafanyika.

Baada ya majibu ya kipimo kupatikana Daktari akatueleza kuwa gharama za matibabu ni takribani Tsh 1,450,000 na ukaruhusiwa kurejea nyumbani kusubiri matibabu rasmi.

Wakati tunajipanga kwa ajili ya matibabu hayo ulizidiwa ghafla usiku na ukapelekwa na kulazwa Hospitali ya Temeke ambapo asubuhi yake tulifika na baada ya kuona hali halisi ilivyo tukaomba rufaa na kukuhamishia Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako ulipata Huduma ya vipimo ikiwemo CT-Scan na ukalazwa ukiendelea kupatiwa matibabu. Na baada ya siku kadhaa ukaruhusiwa

Kwa kushirikiana na familia yako pamoja na madaktari wa hospitali ya Muhimbili tulianza mipango ya kukusafirisha kwenda Marekani ambako kaka yako kifamilia yupo nchini humo ili kupata matibabu zaidi

Baadae kwa sababu za ushauri wa kitabibu, taratibu za kuingia nchini humo na hali halisi ya afya yako ikabidi tubadili uamuzi na kuanza mawasiliano na hospitali kadhaa nchini India ili ukapate matibabu huko.

Wakati tunaendelea kushughulikia hilo ukalazimika kurejea Kigoma ambako ulikuwa umeitwa kwa ajili ya kuripoti katika ajira yako mpya ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR Wilayani Kibondo.

Bahati mbaya ulipofika Kigoma ulizidiwa tena na kulazwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Maweni wakati huo na sisi tukiwa tumekwisha pata treatment plan and costs na kumalizia taratibu za mwisho ili usafiri kuja Dar es Salaam tayari kwa kuelekea nchini India kwa matibabu.

Kwa bahati mbaya zaidi wakati tukikutarajia usafiri kuja Dar es Salaam tukapata taarifa umefariki Dunia. Hakika lilikuwa ni pigo kubwa sana kwetu kama chama cha siasa, pigo kwa familia yako, Ndugu, Jamaa, Wanachama na wapenda Demokrasia waliokufahamu. Hakika umetuachia pengo lisilo zibika.

Na leo tumehitimisha safari yako ya maisha hapa Duniani kwa kukihifadhi katika nyumba yako ya milele kijijini Kagunga, mkoani Kigoma.

Tutakukumbuka na kukuenzi Daima.

Bwana alitoa na Bwana ametwaa Jina lake lihimidiwe.
 
R.I.P Mwalimu Kaijage....

Kule kwenye Uzi wa Mchange alisema kafia Muhimbili, hapa mnatuambia kafia Kigoma bila kutaja hospital na kwamba "mipango ya kwenda India ilikuwa kamili". Mnayapa nguvu maneno ya Mibangi Sele Msindi.

NB: Badala ya kueleza hiyo milioni mliyoilipa pale Agha Khan bora mngeeleza wasifu wa Marehemu tujue alizaliwa wapi na kama ameacha familia inayomtegemea na alikuwa na umri gani. Hizi figisu nyingine kuonyesha chama kilimpigania kumuuguza kwa ahadi za India na Marekani hazina maana
 
Back
Top Bottom