Polisi kumkamta Mbunge kwa nguvu

Zimmermann

JF-Expert Member
Sep 28, 2010
2,789
1,231
Jeshi la Polisi mkoani Mwanza huenda likamkamata Mbunge wa Busega kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Titus Kamani, ili kumhoji kuhusiana na tuhuma za kutaka kumuua aliyekuwa Mbunge jimbo hilo, Dk. Raphael Chegeni.
Tayari Jeshi hilo limekwisha kumwandikia barua Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Thomas Kashillilah, kumtaka mbunge huyo kwenda Mwanza kuhojiwa kuhusiana tuhuma hizo zinazomkabili.

Jeshi hilo limesema kuwa endapo Dk. Kamani ataendelea kukaidi amri ya polisi ya kwenda jijini Mwanza kutoa maelezo, linaweza kutumia nguvu kumkamata kwa mujibu wa sheria.

Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Mwanza (RCO), Deusdedith Nsimeki, alisema juzi jijini hapa kuwa mtuhumiwa huyo bado hajafika polisi kutoa maelezo yake dhidi ya tuhuma zinazomkabili licha ya polisi kumtaka kufanya hivyo.
Inadaiwa kuwa Mei 31, mwaka huu, Jeshi la Polisi mkoani Mwanza liliiandikia barua katika Ofisi ya Bunge kumtaka Dk. Kamani kwenda Mwanza kwa ajili ya mahojiano maalumu na jeshi hilo dhidi ya tuhuma hizo.
Nsimeki alithibitisha kuwa hadi sasa Dk. Kamani hajafika Mwanza kutoa maelezo kwa Jeshi la Polisi.
Alisema kuwa ikiwa mbunge huyo ataendelea kukaidi amri hiyo halali, wataomba kibali kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), ili watumie nguvu kumkamata.
Jeshi hilo liliandika barua Mei 31, mwaka huu, yenye Kumbukumbu No. MZR/CID/SCR/105/2011/4 iliyotumwa kwa Katibu wa Bunge ikimkata kumruhusu Dk. Kamani kwenda Mwanza kutoa maelezo polisi katika Jalada No. MW/IR/2607/2011-MR-CC.28/2011 lililofunguliwa kwa kosa la kula njama na kutaka kumuua Dk. Chegeni.
Watuhumiwa wanne tayari wamekwisha kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza kujibu tuhuma hizo.
Waliofikishwa mahakamani na sasa wako nje kwa dhamana ni Dismas Zacharia Ndaki, Erasto Kazimili Kombe, Queen Joseph Bogohe na Ellen Joseph Bogohe.
Kesi yao imepangwa kutajwa Julai 6, mwaka huu.
Dk. Chegeni aliangushwa katika kura za maoni na Dk. Kamani kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana.
NIPASHE ilipowasiliana na Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, jana jioni, kuhusiana na suala hilo, alisema kuwa wanachofahamu ni kuwa Dk. Kamani alikuwa Mwanza na kuongeza kuwa kama hajafika Polisi ni kitu kingine.
"Sisi hatupendi masuala kama haya yawasumbue wabunge, lakini la kwake (Dk. Kamani) ni gumu kuliingilia," alisema Joel.
Alipoulizwa kama ofisi ya Bunge ilipokea barua kutoka Polisi ikitaka Dk. Kamani kwenda kuhojiwa Mwanza, Joel alisema hana uhakika kwa kuwa wakati huo hakuwepo katika ofisi hiyo na kusisitiza kuwa anachokifahamu ni kuwa mbunge huyo hivi karibuni alikuwa Mwanza.
CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom