Pinda hakujikwaa ulimi wala hakuteleza

Pinda hakujikwaa ulimi wala hakuteleza

assadsyria3

JF-Expert Member
Joined
Apr 9, 2013
Posts
6,909
Reaction score
4,057
AZIZ Nesin alikuwa mwandishi mahiri Wakituruki aliyeiaga dunia 1995 akiwa na umri wa miaka 79. Aliandika vitabu zaidi ya mia moja vikiwa pamoja na vya hadithi za kubuni. Vitabu vyake vingi vimetafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza.
Alhamisi iliyopita niliikumbuka hadithi yake moja iitwayo ‘Waziri Mkuu Mpya.’ Niliikumbuka hekaya hiyo baada ya kuyasikia aliyoyatamka bungeni siku hiyo Mizengo Pinda, Waziri Mkuu wa Tanzania.
Matamshi ya Pinda yalinitisha. Yaliwatisha na wengi wengine pia. Yalikuwa matamshi ya vitisho. Nilisikitika kumsikia Pinda akiyasema aliyoyasema kwani hakustahiki kuyatamka.
Pinda alikuwa akimjibu Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu aliyelilaumu Jeshi la Polisi kwa nguvu linazotumia linapopambana na wananchi wanapokuwa wanaandamana.
Kukusanyika na kuandamana ni miongoni mwa haki za kidemokrasia za kila mwananchi. Badala ya kuziminya na kuzikandamiza serikali zinazojinata kwamba ni za kidemokrasia zinahitajika kuzihifadhi.
Lakini sidhani kama viongozi wetu wanaziamini kwa dhati nguzo hizo za kidemokrasia.
Pinda, mwenye shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alijibu hivi: “Ukifanya fujo umeambiwa usifanye hiki ukaamua wewe kukaidi utapigwa tu maana hakuna namna nyingine maana wote lazima tukubaliane nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria sasa kama wewe umekaidi hutaki unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ndio jeuri zaidi watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine maana tumechoka sasa.”
Kama nilivyokwishadokeza nilishtuka nilipoyasikia matamshi hayo. Si mahala pake kiongozi mwenye hadhi aliyonayo Pinda kuwaamrisha polisi watumie nguvu badala ya sheria.
Kweli polisi wetu wana uzoefu huo lakini lazima mikono yao ifungwe; sio wapewe nguvu zilizo kinyume cha sheria.
Nikajiuliza: “Hivi huyu Waziri Mkuu hana mshauri wa kumnasihi namna ya kujibu maswali?”
Hapo ndipo nilipoikumbuka ile hekaya ya ‘Waziri Mkuu Mpya’ ya Aziz Nesin. Hadithi hiyo inaeleza jinsi Waziri Mkuu mmoja alivyokuwa akipata fikra na mawazo yake yote kutoka kwa nyumbu.
Sultani aliyekuwa akitawala alichoshwa na tabia hiyo ya Waziri Mkuu wake na akaona kheri amteue nyumbu awe Waziri Mkuu mpya badala ya huyo mwenye kumtegemea nyumbu.
Kwa hivyo, si muhimu kuwa Waziri Mkuu awe na mshauri. Muhimu ni mshauri wa aina gani aliyenaye.
Tunaweza kuiendeleza mantiki hiyo na kusema pia kwamba si muhimu kuwa Rais awe na Waziri Mkuu. Muhimu ni Waziri Mkuu aina gani aliyenaye.
Pingine Pinda kweli amechoka si na waandamanaji tu lakini hata na kazi yake.
Labda wakati umefika kwa Rais Jakaya Kikwete kumpumzisha na kumteua Waziri Mkuu mwengine ili mradi asiwe nyumbu. Sijui Pinda anamfuata nani. Sidhani kama ni nyumbu. Labda anaufuata aina ya udikteta ambao watawala wetu wameuzoea.
Tunajigamba kwamba taifa linafuata misingi ya kidemokrasia lakini bado viongozi wetu na vyombo vyao vya dola wanajifanyia watakavyo.
Nimesema vyombo vyao kwa kusudi kwa sababu kwa namna vinavyotumika ni kama vyao wao. Na wanavitumia kuwakandamiza wenzao. Wananchi wale wale waliokula kiapo kuwatumikia.
Tuliangalie Jeshi la Polisi tu linavyofanya kazi. Ushahidi uliopo unaonyesha wazi kwamba polisi wanaona kuwa wametekeleza wajibu wao wanapokuwa wanatembeza mikong’oto yao wakati wa maandamano ikiwachapa na kuwatandika waandamanaji.
Wengine ambao polisi huhisi kuwa ni wakorofi huwafika mabaya zaidi ya hayo. Kuna neno moja ambalo hatulisikii sana siku hizi katika mazungumzo ya kisiasa nchini Tanzania: ‘muamala.’
Wafuasi wa chama kimoja huwa hawana muamala mzuri na wakinzani wao wa chama kingine. Wanasiasa wanaoongoza serikali hawana muamala mzuri na wananchi wanaowatawala.
Vyombo vya dola, hasa vile vya usalama, havina muamala mzuri na waandishi habari. Badala ya kuwako muamala mzuri tunaona kwamba siasa za Tanzania zinagubikwa na ufasiki wa kisiasa. Tabia za kihunihuni ndizo zinazojitokeza mara kwa mara katika majukwaa ya kisiasa.
Inavyoonyesha ni kwamba baadhi ya wanasiasa wetu siku hizi wamo mbioni kujenga utamaduni wa uhuni wa kisiasa.
Badala ya kuutumia utaratibu wa sheria uliowekwa na Katiba ya nchi wanasiasa hao wanavishajiisha vyombo vya dola vitumie nguvu na vitendo vya kihuni.
Wanayapuuza kabisa Mahakama ambayo ndiyo yenye kupaswa kutoa hukumu na kuwapa adhabu waandamanaji iwapo watapatikana na hatia ya kuvunja sheria.
Wanataka kuwatisha wananchi ili wananchi warudi nyuma wasizitumie haki zao.
Kwa namna walivyozipanga karata zao wanahisi kwamba hiyo ni njia moja ya kuwawezesha waendelee kutawala.
Hizo ni hila zilizowahi kutumiwa katika sehemu mbalimbali duniani. Kila zilikotumiwa zilishindwa kutimiza lengo. Zinaendelea pia kutumiwa hadi leo katika nchi Fulani Fulani lakini huko pia zinashindwa na zitashindwa. Wananchi wamekwisha kuwa sugu; hawatishwi tena wala hawatishiki na vitisho vya wanasiasa.
Hila hizo zitashindwa Tanzania pia madhali wananchi wataendelea kuzitumia haki zao za kidemokrasia. Siku hizi wananchi wanazijuwa haki zao na wanajua namna ya kuzitumia.
Hicho ndicho kitisho kikubwa kinachowakabili watawala. Na ndio maana watawala hao mara nyingine huonekana wakifanya mambo kama afanyavyo paka aliyezingirwa asiyejuwa pa kukimbilia na anayekuwa tayari kumrukia yeyote yule ili amparure apate mwanya wa kupenya.
Kwa namna siasa zinavyoibuka siku hizi nchini Tanzania tuna wajibu wa kuwaonya viongozi wawe waangalifu wa wanayoyasema.
Wanapaswa wawe na busara ili waweze kuepusha hasara. Wasipofanya hivyo wanaweza wakauwasha moto wasioweza kuuzima.
Naitoshe kuunukuu ubeti wa mwanzo wa shairi ‘Ulimi’ la Shaha wa Mombasa, Ahmed Sheikh Nabhany:
“Ulimi ni tamu, ukiutongowa
Waama ni sumu, yakusongonyowa
Uyuwe fahamu, namwisohuuwa…”
 
Mahakama imethibitisha Upumbavu wake ni baada ya kukosa ground ya kumshitaki sugu
 
Mahakama imesha qualify kauli ya Sugu kuwa Pinda ni Mpumbavu!
Naona watoto wanaimba mtaani kuwa Pinda ni Mpumbavu
 
Mahakama imethibitisha Upumbavu wake ni baada ya kukosa ground ya kumshitaki sugu

Kutumia polisi ni hatua ya mwisho kwa utawala uliochoka. Tulejee maneno ya Pinda mwenyewe. Amekubali kwamba "wamechoka" ila tukubaliane kwamba polisi wakija tu kwenye mikutano, ndo kunatokea vurugu. CCM wamechoka na mimi naona hata wakiwa na polisi upande wao, bado yatawashinda...with or without police, they are going down. Ndani ya polisi kuna nyufa. Si wote wanaopenda kutumika. Chadema sasa itoe alternative. Ijitofautishe na utawala wa kipuuzi kwa kuahidi kuliunda upya jeshi la polisi na kulifanya liwe la wananchi sio mafisadi. Kibaya zaidi, nina wasiwasi CCM watajilipua wenyewe ili wabambikize kesi watu wengine.
Uchaguzi Arusha wanataka kuiba kweupe. Walijua mwisho wa mwezi huu kutakuwa na ugeni wa Obama hivyo wakajua wakiiba, fujo zitatokea. Wakasogeza hadi July 14 kusudi wawe na mwanya wa kufanya unyama. Hawatakubali kuhesabia kura kwenye vituo vya kupigia kura. Masanduku yaishaandaliwa sehemu nyingine.
Hivi ebu tufikilie; wametwambia hali ya amani haijatulia Arusha hivyo uchaguzi upelekwe mbele week mbili. Hizo week mbili ndo amani itatulia? Amani gani hiyo? Wao si ndo wanavuruga watu?
 
"Reasonable force to control the situation" haimaanishi wapigeni au waueni wanaokaidi. Pinda, Nchimbi na Mwema wanapotosha ukweli wa sheria
 
Mahakama imesha qualify kauli ya Sugu kuwa Pinda ni Mpumbavu!
Naona watoto wanaimba mtaani kuwa Pinda ni Mpumbavu
Kauri ya pinda imewatesa sana hasa wafanya fujo na bado atafanya mkae kimya kabisa mda wa kucheza umeisha.
 
Kwa sasa pinda akigeuka tu wale magaidi wote mbio,pinda wapigwe tu.
 
Pinda ni msomi wa sheria ambaye hajawahi kuwa mwanasheria!
 
Sio vema kumnyooshea mikono Waziri Mkuu hasa kwa kejeli na maneno yasiyo mazuri.

Toa mawazo yako kuleta amani na upendo. Mfano Je tufanye nini ili tutunze amani yetu hapa Tanzania
 
Sio vema kumnyooshea mikono Waziri Mkuu hasa kwa kejeli na maneno yasiyo mazuri.

Toa mawazo yako kuleta amani na upendo. Mfano Je tufanye nini ili tutunze amani yetu hapa Tanzania
haki itendeke na hionekane ikitendeka ndo amani iatkuwepo
 
Back
Top Bottom