Send to a friend Wednesday, 02 February 2011 21:08
Fidelis Butahe na James Magai
MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe jana alikutana uso kwa uso na Rais Jakaya Kikwete ikiwa ni mara ya kwanza tangu chama hicho kilipotangaza kutotambua ushindi wa Kikwete uliompa fursa ya kuwa rais kwa kipindi kingine cha miaka mitano kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka jana.Tukio hilo la aina yake kutokea tangu kuanza kwa mwaka huu, liliwakutanisha Mbowe na Rais Kikwete katika maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo walisalimiana kwa kupeana mikono.
Mbowe na Kikwete walikutana uso kwa uso ikiwa ni siku 85 tangu Mbowe alipowaongoza wabunge wa chama chake kususia hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la 10, Novemba 18 mwaka 2010 kutokana na msimamo wa chama chake kutotambua matokeo ya urais.
Mwaka jana, Mbowe alitangaza chama chake kutotambua matokeo ya rais huku akitoa madai mbalimbali kuhusu taratibu zilizotumika kumwingiza kiongozi huyo madarakani.
Madai ya Chadema ambacho mgombea wake wa urais Dk Willibrod Slaa alishika nafasi ya pili ni pamoja na kutaka kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi, kuandikwa kwa katiba mpya na kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyomweka madarakani Rais Kikwete kwa mara ya pili baada ya kupata kura 5,276,827 ukiwa ni ushindi wa asilimia 61.17.
Katika uchaguzi huo, Dk Slaa alipata kura 2,271,941 sawa na asilimia 26.34 huku Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF akipata kura 695,667 sawa na asilimia 8.06.
Mbali na kutohudhuria hafala ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo, wabunge wa Chadema pia walisusia sherehe za kumwapisha Kikwete zilizofanyika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na pia zile za kuapishwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda zilizofanyika katika viwanja vya Ikulu Ndogo ya Chamwino, Dodoma.
Mbali na Sherehe hizo, pia viongozi wa Chadema hawakuonekana katika maadhimisho ya miaka 49 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Desemba 9, 2010.
Katika maadhimisho ya jana yaliyofanyika nje ya Mahakama Kuu Dar es Salaam, Mbowe alikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria katika maadhimisho hayo, akiwa ni kiongozi pekee wa chama cha upinzani huku Rais Kikwete akiwa mgeni rasmi.
Tukio hilo lilivuta hisia kwa washiriki wa maadhimisho hayo ya siku ya Sheria nchini ambapo Mbowe aliwasili katika maadhimisho hayo akiwa peke yake huku akiwa amevaa mavazi maalumu ya chama hicho maarufu kwa jina la kombati pamoja na miwani myeusi.
Baada ya kuwasili alikwenda kukaa katika viti vya mbele karibu na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa.
Katika tukio la kupiga picha za pamoja ndipo Mbowe alikutana uso kwa uso na Rais Kikwete ambapo walisalimiana kwa kupeana mikono na kupiga picha pamoja huku wote wakiwa na tabasamu pana.
Alipotafutwa na gazeti hili ili kuzungumzia tukio hilo, saa kadhaa baada ya kumalizika kwa sherehe hizo, Mbowe alisema alikwenda katika sherehe hizo kwa kuwa zilikuwa ni za mahakama na kwamba hata kungekuwa na tofauti gani kusingemzuia yeye kusalimiana na Kikwete.
"Sherehe zile si zangu wala Rais Kikwete hivyo siwezi kuwa na chuki na mahakama, ni 'Birthday' ya Mahakama yenyewe ni mhimili wa dola," alisema Mbowe.
Mbowe alisema kuwa katika maadhimisho hayo alialikwa kama mwenyekiti wa Chadema na kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni.
Hatuwezi kuwa na chuki na mahakama, pale mihimili yote mitatu ya nchi ilikuwepo, ile haikuwa 'Birthday' yangu wala ya Rais Kikwete, alisema Mbowe.
Mbowe alisema kuwa madai waliyotoa baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana haikuwa na maana kwamba hawaitambui Serikali wala kutaka Rais Kikwete angoke madarakani.
Alisema kuwa mambo mawili kati ya matatu yaliyokuwemo katika dai lao yameshaanza kupatiwa ufumbuzi kwa namba moja au nyingine ambayo ni katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.
Rais azungumzia imani ya wananchi kwake
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Rais Kikwete alisema kuwa baadhi ya wananchi wamekosa imani naye kutokana na msimamo wake wa kukataa kuingilia uhuru wa Mahakama wanapomtaka atengue maamuzi mbalimbali ya korti.
Kikwete alikuwa akizungumzia uwelewa wa wananchi juu ya sheria mbalimbali na nafasi ya Mahakama ambapo alisema kuwa wananchi hawana budi kufahamu jinsi Mahakama inavyofanya kazi.
Rais alitoa wito kwa Mahakama kushirikiana na wadau mbalimbali vikiwamo vyombo vya habari katika kutoa elimu kuhusu sheria.
Naye Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman alisema kuwa ingawa ni msingi wa sheria kuwa kila mtu anatarajiwa kujua sheria, lakini kwa bahati mbaya uwelewa wa wananchi kuhusu Mahakama na sheria ni mdogo na kwamba kutokujua sheria sio kinga.
source:Mwananchi