Penye nia pana njia

Asha Abdala

JF-Expert Member
Mar 21, 2007
1,130
44
Na Samson Mwigamba

MALALAMIKO ni mengi kutoka pande mbili. Lakini wanaolalamika zaidi ni wale walio mijini. Wanalia na wale walio vijijini.

Msomaji wangu aitwaye Aziza, wa Kitunda Dar es Salaam anasema: "Nakupongeza sana kaka Mwigamba kwa makala zako. Nimekuwa nikifuatilia makala zako lakini je, hili gazeti linafika vijijini? Nauliza hivi kwa sababu vijijini watu ni rahisi kurubunika na pipi za CCM.

Leo hii ukienda Singida Vijijini kuna watu ukiwauliza uchaguzi ujao watakuambia wanataka chama cha Nyerere. Napenda ufanyike utaratibu habari hizi ziwafikie pia.

Bwana Hajj anasema: "Gazeti lenu Tanzania Daima ni zuri siwezi kukosa nakala kila litokapo. Ila sasa najutia pesa yangu. Mnafanya kosa kubwa kuchapa makala za Tambwe Hizza, amewapa nini kikubwa?! Inasikitisha, inachukiza sana sana."

Huyu anaona kwamba waandishi wa aina ya Tambwe Hizza wasingeruhusiwa kabisa kuchapa makala zao kwenye gazeti hili kwa kuwa wanarudisha nyuma juhudi za kuwaamsha Watanzania katika usingizi wa kifikra.

Lakini anasahau kwamba gazeti makini, linalojali uhuru wa habari na fikra na lenye heshima kama Tanzania Daima, haliwezi kuzuia makala za waandishi wenye fikra tofauti na wengi hata kama fikra zao ni potofu. Ni kazi yetu wasomaji kuyapuuzia maandishi yao.

Msomaji mwingine aliniambia: "Hey, nashukuru kwa makala yako nzuri kwenye Tanzania Daima. Maoni yagu tuzidi kuhamasishana, tuna kiza kinene hasa vijijini, ndio wanatuangusha sijui kama makala yako inawafikia."

Nikiamini kwamba wanaowasiliana nami wengi wako mijini ambako wana nafasi zaidi ya kupata mawasiliano, ni dhahiri msomaji utakuwa umepata picha kwamba wengi walio mijini kilio chao kikubwa ni kwa wenzetu walio vijijini.

Inaonekana kwamba hawa hurubunika kwa urahisi zaidi kuwachagua mafisadi wale wale kwa sababu nyingi lakini kubwa ikiwa ni ukosefu wa elimu ya uraia na rushwa.

Inaonekana kwa wengi kwamba wachapishaji wa magazeti makini kama Tanzania Daima wangejitahidi kusambaza nakala za magazeti haya hadi vijijini ili wananchi wale waweze kusoma makala motomoto za kina Ansbert Ngurumo, Absalom Kibanda, Martin Malera, Happiness Katabazi, M.M. Mwanakijiji, Chris Allan, Yusuph Halimoja, Kitila Mkumbo, Gervas Zombe, Prudence Karugendo, na wengine wengi. Kwamba hii itawaamsha usingizini na watafanya mabadiliko.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa wengi, Bwana Magesa kutoka Mwanza aliniambia: "Tanzania ni ya vijana, ni kweli kabisa Mwigamba. Lakini vijana wataikomboa Tanzania wakati wengi wanajiunga UVCCM na kutetea ufisadi?"

Kwa maoni haya nadhani huyu sasa anatuambia kwamba si wananchi wa vijijini tu wanaokwamisha ukombozi wa pili wa taifa hili ambao ni wa kweli, maana ule wa mwaka 1961 na 1964 ulikuwa wa bendera tu.

Ametuonyesha kwamba hata mijini bado tunao vijana wanaojiunga kutetea ufisadi.

Kufikia hapo utakubaliana nami kwamba bado tunayo kazi kubwa katika harakati za kulikomboa taifa hili mara ya pili. Na kama una imani ndogo unaanza kupoteza matumaini na unaweza kujikuta ukiungana na wale wanaodhani 'Chama Cha Mafisadi' kitaendelea kutawala (si kuongoza) kwa miaka 100 ijayo.

Lakini nataka nikuhakikishie kwamba tumaini lingalipo. Kama nilivyosema katika makala yangu iliyopita, sababu za kufanya mabadiliko ya uongozi wa nchi hii tunazo, uwezo wa kufanya hivyo tunao, na nia ya kufanya hivyo tayari tunakuwa nayo, tutawang'oa.

Tunahitaji kunuia. Na kinachotufanya tunuie ni zile sababu zetu tulizozitaja huko nyuma. Kwa nini tuendelee kuwaangalia hawa wazee wakiharibu nchi yetu na sisi vijana tupo tumetulia na njozi zetu ambazo zinaweza kufanya maajabu. Nawahakikishia vijana tukishika uongozi wa nchi yetu tutafanya makubwa ndani ya miaka mitano ambayo yamewashinda wazee hawa kufanya kwa miaka karibu 50 ya uhuru wa nchi yetu.

Matatizo yanayotukabili zaidi ni matatu. Kwanza, hatuna uongozi bora. Baadhi ya viongozi wetu ni wala rushwa tena jina lao halisi ni mafisadi.

Fikiria kiongozi mkubwa serikalini kama waziri. Hata kama alisoma darasa la saba tu tena lile ambalo tulikuwa tukisoma sisi kule Mwibara chini ya mwembe mkubwa na viti vikiwa ni mawe, anawezaje kusaini mkataba wa IPTL ukiwa na kipengele kwamba TANESCO watawalipa sh bilioni 3 kila mwezi kama hawakuzalisha umeme na kama wamezalisha basi watalipwa hiyo bilioni 3, jumlisha gharama ya umeme waliozalisha? Ni waziri wa kawaida kweli huyu?

Halafu rais aliyechaguliwa eti kwa kura za kimbunga, tena akarudia mara kwa mara kuwaahidi wananchi kwamba hatawaangusha, anatangaza hadharani kwamba anawafahamu wala rushwa kwenye wizari zote ila anawapa muda wajirekebishe. Huo ndio uongozi? Tena badala ya kujirekebisha wakaamua kula rushwa tena wakasaini mikataba mingine mibovu kama ile ya Richmond na nduguye Buzwagi, halafu rais katulia!! Kikubwa anachoweza kufanya ni kuwabadilisha wizara!

Kituko zaidi ni kauli ya mkuu huyu wa nchi. Majuzi amenukuliwa akisema anawafahamu vigogo waliojigawia miradi ya wanachi. Akawataka wajirekebishe la sivyo atawataja hadharani. Hiki nacho si kituko?

Hivi kuna kigogo serikalini ambaye anamshinda ubavu rais kiasi kwamba anaweza tu kumtaja hadharani? Anataka kufanya kazi ya Dk. Slaa ameona inalipa?

Hapana, huu ni usaliti wa hali ya juu wa kiongozi wa nchi kwa wananchi alioahidi kuwa hatawaangusha. Katiba ya nchi imempa madaraka makubwa kiongozi wa nchi. Ana uwezo wa kuanzisha (establish) ofisi yoyote ya serikali au kuivunja (abolish) bila kuhojiwa na mtu au chombo chochote.

Anaweza kumstaafisha kiongozi au mtumishi yeyote ndani ya serikali kwa manufaa ya umma. Kwa ujumla katiba inasema, mamlaka yote ya kuongoza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yako mikononi mwa rais.

Wengine wote wanafanya kwa niaba yake. Kitendo cha yeye kusema atawataja tu hadharani ni ushahidi kwamba amefungamana nao na hawezi kuwafanya lolote. Uongozi wa aina hii hautufai asillan.

Kukosa uongozi bora wapendwa wasomaji ni kasoro na sababu kubwa ya umaskini wetu. Fikiria mabilioni yaliyochotwa Benki Kuu kwa ajili ya kuwawezesha waheshimiwa kushinda kwa kimbunga.

Yangejenga hospitali ngapi ili kuzuia mama zetu kufa wakijifungulia kwa wakunga wa kienyeji? Au yangepeleka wanafunzi wangapi waliokosa kuingia chuo kikuu kwa sababu ya kutokuwa na pesa na wakakataliwa mikopo eti kwa sababu bodi ya mikopo haina pesa ya kutosha?

Au yangejenga visima vingapi kule vijijini na kuwaepushia mama zetu kutembea umbali mrefu? Na yangeweza kupeleka umeme kwa wilaya ngapi na kuwarahisishia wananchi maisha? Msikilize Bwana Brown, msomaji wa Tanzania Daima aliyeko China anavyosema:

"Kaka Sam mimi nafuatilia sana gazeti la Tanzania daima, nalisoma kila siku. Imefikia sasa naamini kwamba Tanzania Daima, Hakielimu na wachache walio wazi kuibua na kujenga hoja juu ya hali zinazotugawa Watanzania karibu tutashinda, sauti ya wengi ni sauti ya Mungu.

Nimeifuatilia sana makala yako, imenigusa sana. Mimi nimezaliwa kijijini Mdasi, Njombe lakini toka utotoni nimeishi pia Kijiji cha Msolwa Ujamaa, Wilaya ya Kilombero. Hivyo naelewa vizuri maisha ya vijiji vya Wilaya ya Njombe na Kilombero pia. Hali ni ngumu mno.

Hata nilivyoweza kusoma, namshukuru Mungu, hakika nikikueleza utashangaa ingawa unajua vizuri hali za Watanzania vijijini.

Kaka Sam, ninaamini kwamba mageuzi yanawezekana, vijana tunaweza ila kasumba. Kule vijijini hasa Mkoa wa Morogoro, wilaya za Kilombero na Ulanga watu wanakoboa mpunga kwa kinu, hawaijui mashine.

Mimi mwenyewe nimetwanga mpunga sana. Kilombero ndiko liliko Bwawa la umeme la Kidatu, lakini watu wanakoboa mpunga kwa kutwanga kwenye kinu. Utakuta kijiji hata line za umeme hazipo, wakipata fedha kidogo wanakwenda kukoboa kilomita 20 - 30.

Kilombero hasa kata za Sanje, Kidatu na majirani, vifo vya watoto chini ya miaka 5 ni vingi mno. Kaka ukiweza tafuta takwimu pale Hospitali ya Kilombero au Ifakara. Kisa, malaria. Kuna mbu balaa lakini watu hawana 'net' nyumba zenyewe haziwezi kuwasitiri kwani hata milango ni ya nyasi.

Watanzania hawa wanalipa kodi kibao. Kodi hizo zingetumiwa vizuri (walaji wangetumia nishati wanayopata kubuni mbinu na mikakati) wangeondokana na umaskini huo unaotisha.

Matokeo yake walio madarakani hawaoni kwamba hilo ni tatizo nyeti, linahitaji kuwekewa mikakati inayotekelezeka.

Umaskini wa Watanzania hasa wa vijijini, hauwaumizi watawala. Kwa kuwa hawaumii, hawaoni kama kuna jambo linatakiwa kutendeka, wanaamini kwamba kadiri siku zinavyokwenda kila mmoja (as an individual, tena bila kuwezeshwa) atapata maendeleo, na wale wanaoshindwa basi hayo ndiyo maisha yao ya milele duniani.

Kaka Sam, naitegemea kalamu yako, hata sasa inasaidia kuwaamsha wanyonge waliokufa ganzi na kutoona maumivu juu ya hali iliyopo.

Naamini kwamba maneno yako hayasaidii sana walioko madarakani kwani mwenye nia ya kuleta mabadiliko huonekana tangu mwanzo, na wala hakurupushwi akiwa katikati ya safari.

Juzi hapa tumetangaziwa kwamba mama mmoja kafiwa mtoto huko Tabora kwa kukosa tu kulipia dozi ya shilingi 12,000 kwenye hospitali ya serikali.

Wakati hayo yakitokea, vigogo wanaruka majuu kwenda kuangalia afya zao na kuteketeza mamilioni ya pesa za walipa kodi hao hao wanaoshindwa kulipa elfu kumi na mbili.

Maovu ya waliotutawala kwa miaka mingi sasa ni mengi mno.. Yatosha tu kusema vijana tukiwang'oa wazee hawa na kuwanyang'anya kila mali ya umma waliyojilimbikizia kama vitalu vya uwindaji, machimbo ya madini, miradi ya wananchi, magari ya kifahari yalionunuliwa kwa mamilioni ya serikali na yanayolipiwa gharama na serikali hata wakienda nayo baa, na tukawalazimisha kulipia gharama za huduma kama umeme na maji, tutakuwa tumeiwezesha nchi kupiga hatua kubwa sana kiuchumi.

Tuelewe kwamba wakati vigogo hawa wamejilimbikizia mali namna hiyo, ndio wanaoongoza kwa kutolipia umeme na maji.

Na matumizi yao ya maji na umeme ni makubwa kupindukia. Kwani mama na watoto wao watatumiaje maji na umeme kwa kiasi wakati hawalipi?

Matokeo yake mashirika ya huduma hizi yanalazimika kutupandishia gharama za maji na umeme kina yakhe, ili kufidia hasara wanayopatiwa na vigogo.

Kwanza, wameshatupandishia gharama ya umeme na maji kwa kusaini mikataba mibovu kama ile ya IPTL na City Water. Halafu wanatupandishia kwa matumizi ya hovyo ya huduma hizi wasizolipia. Tutaponea wapi? Tuwang'oeni mwone huduma hizi zitakavyoshuka bei maana kila mtu atalipa hata rais wetu.

Tatizo la pili ni sera mbovu za kiuchumi. Ndani ya katiba imeandikwa nchi ni ya Ujamaa na Kujitegemea. Tunachoshuhudia ni ubepari, tena usio na mipaka. Badala ya soko huria tunaendeshwa na soko holela. Tukishika vijana tutawapatia kazi wataalamu wa uchumi watufanyie mchanganuo wa falsafa zote za kiuchumi, faida zake na hasara zake.

Kisha tutachagua ile itakayotufaa katika mazingira ya sasa. Tutaisimamia hiyo na kuitekeleza kivitendo.

Hawa waliopo madarakani hawawezi kufanya hivyo maana humo kwenye soko holela ndimo wanamopatia masilahi makubwa kwa faida yao na watoto wao. Wanajiita wajasiriamali hata wakiwa Ikulu. Wanasaini mikataba mibovu eti walikuwa wanawahi muda maana wamezoea sana kwenye ujasiriamali muda ni kitu cha muhimu sana.

Hakuna taifa lililoendelea bila kuwa na falsafa yake ya uchumi ambayo wanaitekeleza vilivyo, tena kwa kuitungia sheria za kuongoza mfumo huo wa uchumi.

Hata kama tumeamua kuendesha uchumi wetu katika mfumo wa soko huria, lazima tuwe na sheria za kuusimamia mfumo huo. Lazima sheria zetu ziweke nafasi ya serikali kuingilia kati ili kuweka ushindani stahili (fair competition). Wazee hawa watawala wameshindwa kufanya hili. Watuachie vijana.

Tatizo la tatu ni mfumo wa utawala. Nchi hii ni kubwa mno. Haiwezekanai kuiongoza kwa kutumia serikali kuu (central government) iliyoko Dar es Salaam.

Katika makala mojawapo huko nyuma niliwahi kuhoji kitendo cha waziri anayeishi Dar es Salaam kusaini mikataba ya machimbo kule Buhemba, North Mara, Kahama, Buzwagi, Tulawaka, Geita, Bukombe, Muheza, Mererani, Mwadui, Kiwira, Mchuchuma, na kwingineko.

Maeneo mengine naamini hajawahi hata kuyaona tu kwenye ramani ya Tanzania. Hajui taabu inayowapata wanachi wa huko. Tangu nimezaliwa hadi leo, kijiji chetu cha Nakatuba hakijawahi kutembelewa na waziri wala naibu waziri yeyote, wala katibu mkuu wa wizara yoyote na hata mkurugenzi wa idara yoyote katika wizara yoyote.

Halafu leo pagunduliwe madini au maliasili yoyote ya thamani kubwa, utasikia eti waziri anasaini mkataba. Halafu hajui watu wa pale wanavyolala kwenye ngozi za ng'ombe, wanavyofulia majani ya mipapai, wanavyomulika kwa vizinga vya moto wa kuni usiku kwa kukosa mafuta ya taa, wanavyotembea umbali mrefu kutafuta kuni na maji, wanavyokufa kwa malaria kwa kukosa dozi ya shilingu elfu moja tu, na masahibu mengine mengi.

Vijana tukiwang'oa hawa wazee tutaanzisha utawala wa majimbo ili kusogeza uongozi kwa wananchi na kuwapatia wanachi mamlaka ya kuongoza maeneo yao na kusimamia rasilimali zao.

Gavana wa jimbo la Ziwa Victoria kwa mfano, asingekubali kusaini mikataba tata ya madini iliyotapakaa mikoa ya Mara, Mwanza, na Shinyanga isiyo na masilahi kwa wananchi.

Hivi sasa machimbo ya Buhemba yamefungwa, kilichobaki ni mashimo. Je, unajua hali ya wananchi wa vijiji vya Buhemba, Magunga, Matongo, Busegwe na Mlazya vinavyozunguka machimbo hayo?

Wananchi wale wamebaki na umaskini wao uleule, tena tunaweza kusema umezidi. Kwa sababu sasa wameongezewa shida ya ajali zinazowapata kwa watu kuanguka kwenye mashimo yale na kufa hasa wakati wa usiku.

Hadi naandika makala hii tayari vifo vya watu wawili vimeripotiwa. Na si watu tu bali hata mifugo kama ng'ombe, mbuzi na kondoo nao wanakufa katika mashimo yale na kuwaachia umaskini zaidi wananchi wale. Na si hivyo tu, bali sasa kumezuka ugomvi wa kikabila baada ya wananchi wa maeneo mengine ya mkoa ule nao kuingia kule, lengo likiwa ni kufukua fukua mle ndani ili kujaribu kubahatisha chochote. Maisha gani haya kwa wananchi walioishi jirani na mgodi mkubwa wa dhahabu?

Kama gavana anayeishi nao huko angeshirikiana na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya husika tena mkataba ukiwa umepitia kwenye Bunge lao la jimbo na hatimaye Baraza la madiwani la halmashauri hiyo, wangesaini mkataba huo laghai uliowaongezea umaskini wananchi badala ya kuwaondolea umaskini? Vijana tutafakari kama hakuna haja ya kunuia kufanya mabadiliko.

Matatizo haya matatu ndiyo makubwa zaidi ambayo tutatakiwa kuyarekebisha haraka baada ya kuwang'oa wazee hawa.

Haya ndiyo huzaa matatizo mengine yote tunayoweza kuyataja katika nchi yetu yanayotuletea umaskini wa kupita kiasi. Ni sababu tosha inayotufanya tunuie kufanya mabadiliko ya uongozi wa nchi yetu tena si mbali bali ni katika uchaguzi wa mwaka 2010.

Naam! Kwa maneno hayo sasa vijana tumenuia kuleta mabadiliko. Kinachofuata ni kujadili kwa kifupi namna tutakavyoleta hayo mabadiliko.

Kwanza , nashauri kwamba ingawa wametudhibiti kwa ngazi ya urais, lakini tunuie kumchagua mgombea urais atakayekuwa na umri mdogo hasa chini ya miaka 50.

Huyu atakuwa bado ananukia ujana na mara baada ya kushika uongozi, tutafanya mabadiliko ya katiba na kufuta kifungu kinachomlazimisha mgombea urais kuwa na umri wa kuanzia miaka 40.

Mtu yeyote mwenye miaka 18 ni mtu mzima ambaye kama wananchi watakuwa wamemwamini na kumkabidhi uongozi wa nchi, sioni kwa nini azuiliwe na katiba.

Pili, tunuie kuingiza vijana wengi kadiri tutakavyoweza ndani ya Bunge. Tuwachague wabunge vijana wengi zaidi kuingia bungeni wakashirikiane na kina Zitto Kabwe kuleta mageuzi.

Tukumbuke katiba ya hawa wazee imeshatubana kwamba hatuwezi kugombea ubunge au urais au udiwani bila kupitia chama chochote cha siasa (jambo tutakaloliondoa kwenye mabadiliko ya katiba na kuruhusu wagombea binafsi baada ya kushika uongozi).

Hivyo hatuna budi kuchagua chama tawala au upinzani. Uchambuzi wangu siku zote na ujumbe wenu kwangu wasomaji wangu, umeonyesha dhahiri kwamba chama tawala ndicho kilichotufikisha hapa.

Tena tumeona jinsi chama hicho kinavyowabana vijana wasishike nafasi za juu za uongozi si tu kwenye chama bali pia serikalini.

Kule, kupata nafasi ni lazima jina lako la pili (surname) liishie na herufi kama –ete, -cela, -kamba, -wawa, -wassa, -wiru, -kapa, -winyi, -rume, n.k, na bado utaishia tu kwenye ujumbe wa NEC, ukuu wa wilaya, n.k.

Lakini upande wa pili umetuonyesha njia. Tumeona jinsi kina Zitto Kabwe, John Mnyika, Erasto Tumbo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare, Maharagande (CUF), Benedicto Mtungirehi, Godbless Lema (TLP), James Mbatia (NCCR) na wengineo wengi, walivyoaminiwa na vyama vyao na kukabidhiwa nafasi za juu za uongozi. Matokeo yake sasa tunayaona.

Upinzani sasa unajiimarisha na kukua kuliko watu walivyodhani na hili hata CCM wanalijua na hawalali wakipanga mipango ya kuubomoa upinzani.

Lakini maadam upinzani umegundua siri kwa kuwakabidhi vijana uongozi wa juu katika vyama vyao, upinzani utazidi kupeperusha bendera ya matumaini mapya kwa Watanzania.

Tena mambo karibu yote niliyojadili hapa kama matatizo ya nchi yetu tayari yameingizwa kwenye ilani za vyama hivi. Tutakuwa na urahisi sana kutekeleza mikakati yetu maana hatutatakiwa tena kutumia muda mwingi kuwashawishi wazee wa vyama hivi kukubali kubadili katiba, kubadili mfumo wa utawala wa nchi yetu, kuweka msimamo mpya wa maadili ya uongozi, kutengeneza falsafa mpya ya uchumi tunayoihitaji, n.k. Tayari mambo hayo yamo ndani ya sera za vyama hivi. Kinachohitajika tu ni uwezo wa vijana wa kuyatekeleza.

Pesa ni tatizo. Wazee hawa wamejilimbikizia mali zote na kutuacha vijana tukiwa maskini.

Lakini hawajatunyang'anya umoja wetu na nguvu zetu na wingi wetu na nia yetu. Tutavitumia hivyo kuleta mabadiliko. Najua umuhimu wa pesa.

Hatuhitaji pesa za kutoa rushwa na kuiita takrima. Lakini tunahitaji pesa kwa ajili ya kuzunguka huku na huko na kuwaelimisha vijana wenzetu na wananchi wengine waelewe chanzo cha umaskini wao ili nao wanuie kufanya mabadiliko.

Magazeti hayafiki vijijini, ni kweli. Na tusitarajie kwa sasa chini ya utawala huu kwamba wenye magazeti watayafikisha vijijini. Kwa barabaara zipi? Kwa usafiri upi na bei ya petroli ikipanda kila siku? Na je, ni wananchi wapi watapata shilingi mia tatu angalau kila wiki ya kununua nakala ya Tanzania Daima? Na je, wenye gazeti hili watawezaje kuligawa bure ikiwa ushuru wa makaratasi unapaa, bei ya petroli inapaa, na VAT kwenye kila nakala ikiwa palepale? Ni ngumu.

Tunahitaji sisi wenyewe vijana wa mijini kupeleka ujumbe kwa wale wa vijijini. Hakuna asiye na kwao kati yetu sisi tunaoweza kuhamasishana kwa njia hii. Hebu tunapotembelea vijijini kwetu au vijiji vyovyote vile, twende na ujumbe wa matumaini kwa wale watu.

Tuwaambie umaskini unaweza kutoweka ukiamua. Tuwahamasishe na mtashangaa watakavyobadilika. Kote barani Afrika walikoamua kuleta mabadiliko ilikuwa ni kwa njia hii.

Natoa wito maalumu kwa vijana walio vijijini lakini wakiwa na nafasi ya kufika mijini na kupata habari mbali mbali. Wakisha kuamka, wawaamshe na wenzao walioko huko vijijini wanakotoka. Nimepokea ujumbe kutoka kwa vijana wengi wa vijijini wakilalamikia hali ya nchi yetu. Hebu fanyeni hii kazi, na mabadiliko yatakuja. Lakini tunao pia vijana wengi walimu wa shule za msingi na sekondari wanaofundisha shule za vijijini.

Msikubali hali hii iendelee. Waelimisheni wananchi hata wasiojua kusoma na kuandika kwamba wakati wa wokovu wao umefika.

Wakati wa kuwakomboa kutoka katika lindi zito la umaskini. Kwamba kazi yao ni kutuunga tu mkono vijana katika mapinduzi ya kifikra na kiuongozi.

Ili tupate pesa ya kutuzungusha huku na huko wakati wa kampeni, nashauri tuunde network. Kila kijana mwenye uchungu na nchi yetu katikaTanzania yote na nje ya nchi, aruhusiwe kujiunga.

Nasi tutakuwa na viongozi wa network hii watakaoratibu nchi nzima na katika mikoa mbalimbali.

Hawa watasimamia akaunti maalumu ambayo kila kijana mwanachama na asiye mwanachama, atachangia kila mwezi kadiri ya uwezo wake na kuingiza mchango wake wa pesa katika akaunti hiyo.

Mwaka 2010 ndipo pesa hiyo itatumika kuwasaidia vijana wanachama wa network yetu watakaogombea ubunge na udiwani sehemu mbali mbali za Tanzania.

Kwa mahesabu ya haraka haraka, tukifika vijana 4,000 tu, na hao tukaweza kuchangia sh 10,000 kila mwezi, kufika mwaka 2010 wakati wa uchaguzi tutakuwa na sh 700 milioni kuwasaidia vijana watakaogombea ubunge na udiwani maeneo mbali mbali. Penye nia pana njia. Tusikate tamaa, maana sisi ndio wapiganaji kwenye mstari wa mbele katika kuiletea nchi hii uhuru wa kweli na maendeleo ya kweli. Viva Tanzania, aluta continua.

smwigamba@yahoo.com
0784 815 499
0712 012 514

Kutoka: http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/12/5/makala7.php
 
Back
Top Bottom