Paul Makonda: Shisha na ushoga ni tatizo, lakini si vipaumbele vya Dar

Mchanya

JF-Expert Member
Jul 29, 2015
976
1,525
Kwa mtazamo wangu usalama wa wakazi wa jiji na mali zao ndio kipaumbele cha kwanza katika ajenda za kutokomeza kero za jiji, na si matumizi ya shisha na masuala ya ushoga.

Salamu kwako Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar Salaam. Ningekutana nawe uso kwa uso, swali langu la kwanza ningetamani uwaambie wakazi wa jiji la Dar Es Salaam nini hasa vipaumbele vyako katika kulisimamia jiji hili la Dar, tena ningekwenda mbali zaidi kutaka kujua ungefanyaje ili kuweza kuvifikia vipaumbele hivyo.

Umesikika na kunukuliwa mara kadhaa ukisisitiza kwamba hutaki masuala ya ushoga na shisha yawepo katika mkoa wako, na unataka masuala hayo yatokomezwe kabisa na wahusika washughulikiwe ipasavyo.

Nakubaliana kabisa kwamba shisha na ushoga ni tatizo lakini sikubaliani masuala haya yanavyopewa kipaumbele kana kwamba Dar Es Salaamu hakuna kero zingine za kutokomezwa. Pia nakerwa na nguvu kubwa inayotumika kushughulikia shisha na ushoga wakati nguvu hizi zingeweza kutumika vizuri na kuzaa matunda katika kutokomeza kero zingine ambazo ni vilio vikubwa sana kwa wakazi wa jiji.

Tatizo la shisha na ushoga kunahitajika mikakati na mjadala mpana kuliko inavyoshughulikiwa sasa. Shisha na ushoga ni matokeo ya tatizo lililojificha katika jamii, hivyo namna ya kushughulikia kunahitajika busara, hekima na mikakati ya hali ya juu. Leo sitaki kuingia ndani zaidi kwenye hili, maana linahitaji mjadala unaojitegemea.

Hebu fanya utafiti mdogo wewe pamoja na watendaji wako, jaribu kuwauliza wasaidizi wako wawili watatu, kila mmoja wao akutajie kero tatu ambazo angependa zitokomezwe hapa Dar Es Salaam, nina hakika shisha na ushoga hazitakuwemo katika tatu za mwanzo.

Usalama wa wakazi wa jiji na mali zao ndio kiwe kipaumbele cha kwanza katika ajenda za jiji na si uvutaji wa shisha na ushoga.

Jiji la Dar es Salaam na wakazi wake wanaishi katika mazingira yasiyo salama kwa kiwango cha kutisha. Wakazi wa Dar es Salaam wanahitaji sana amani na usalama wao na wa mali zao kuliko chochote kwa sasa. Mifano michache ya uhalifu ni pamoja na vibaka/wezi wanaovamia na kuiba fedha, simu, tv majumbani hasa usiku wa manane.

Wizi kwa mtindo wa makundi kama Panya Road, na wengineo, wizi wa kutumia boda boda au hata hizo boda boda nazo kuibiwa, wizi wa kutumia silaha majumbani, madukani, mabenki na biashara zingine kubwakubwa, hasa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka ambapo wengi wako likizo na katika maandalizi ya sikukuu za mwisho wa mwaka.

Gharama za kujilinda dhidi ya uhalifu hasa wezi, vibaka zinazidi kuongezeka na kuwa kama kitu cha kawaida. Mfano alarms za magari, nondo, grilsl za milangoni na madirishani, nyaya za umeme majumbani, ulinzi wa wamasai na utitiri wa kampuni za ulinzi ni ushahidi tosha kwamba suala la usalama linapaswa liwe ajenda yenye kipaumbele kwa jiji la Dar Es Salaam.

Sisi wakazi wa jiji tutafarijika sana tukikusikia ukitoa matamko yanayoashiria kutokomeza uhalifu jiji Dar Es Salaam. Nguvu, uwezo na mamlaka ya kutokomeza uhalifu hapa jiji unayo. Tumeiona nguvu hiyo ulipohimiza upandaji wa miti katika baadhi ya barabara na mitaa ya jiji, tumeona jinsi ulivyowahenyesha watendaji wazembe wa jiji katika ziara zako za hivi karibuni, tumeona ulivyomchongea Kamanda Siro kwa Waziri Mkuu kuhusu shisha, hivyo ukiamua unaweza.

Kazi yako ya ukuu wa mkoa haina dhamana, unaweza kukaa madarakani kwa muda mrefu au utashangaa siku moja kuwa umeondolewa bila kutarajia. Ushauri wangu kwako ni kwamba, kuna kero nyingi sana hapa jijini, jipange uchague chache ambazo unaweza kushughulika nazo ili hata ukiondoka madarakani, sisi wakazi wa jiji tukukumbuke angalau kwa kero moja tu ambayo umewaondolea wakazi wa jiji.

Zifuatazo ni baadhi ya kero ambazo kwa mtazamo wangu nimeziweka kwa mpangalio wa umuhimu wa kipaumbele ziondolewe, nawe au na wengine wanaweza kuwa na mawazo tofauti.

1) Uhalifu (Hasa wizi, vibaka, panya road, ujambazi)
2) Uhaba wa Maji (Wakazi wengi wa jiji hawapati/hawatumii maji safi na salama)
3) Barabara mbovu na mifumo mibovu ya majitaka hasa wakati wa mvua

4) Uchafu uliokithiri wa vyoo vilivyopo katika shule za msingi, sekondari, mahospitalini (Mfano Mwananyamala), masokoni, migahawani, sehemu za starehe, na hata baadhi ya ofisi za serikali. Vyoo ni vichafu mno kiasi kwamba unaweza kuahirisha haja zako ukiona uchafu huo.

5) Ukiukwaji wa sheria wa vijana waendesha bodaboda, hadi kujiona wako juu ya sheria, juu wa waendesha magari na wata watembea kwa miguu.

6) Kundi kubwa la vijana kukaa bila kufanya kazi za uzalishaji kwa kujitakia, wakitegemea kupata fedha kwa njia za mkato kama, kucheza Pool, kucheza kamari na michezo ya kubahatisha (Beting), kutumia muda mwingi kuwaza na kuangalia mpira hasa ligi za ulaya.

7) Huduma mbovu, rushwa, uzembe na kukosa ubunifu na uwajibikaji kwa watendaji wengi wa manispaa za jiji la Dar Es Salaam na taasisi zake.
8) Ujenzi holela
9) Kukosekana kwa mfumo unaoeleweka kwa wanaomiliki ardhi (viwanja, nyumba) kupata nyaraka za umiliki ardhi jijini.

10) Ufutaji bangi, shisha, matumizi ya mdawa za kulevya, ukahaba na ushoga
11) Makelele yanayosababishwa na muziki mnene/mkubwa wa katika kumbi za starehe, baadhi ya makanisa, n,k.

12) Wafanya bisahara ndogondogo kutotengewa maeneo maalum ya kufanyia biashara zao

Sisemi kwamba ufanye yote haya, la hasha chagua moja au mawili unayoyamudu yafanyie kazi kwa umakini na hapo utakuwa umelitendea jiji letu la Dar haki, vinginevyo utakuwa unapita tu.
 
kuna pambano kali kaandaa kati ya bela na banana ,mshindi anaondoka na milioni 50,huoni kama wa na dsm wanahitaji burudani pia?mpongeze kwa hilo basi
 
Back
Top Bottom