Papaa Mobutu, Tikala Libela, Lokuta Monene! ( Makala, Raia Mwema) | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Papaa Mobutu, Tikala Libela, Lokuta Monene! ( Makala, Raia Mwema)

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by maggid, Apr 23, 2011.

 1. m

  maggid Verified User

  #1
  Apr 23, 2011
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,084
  Likes Received: 397
  Trophy Points: 180
  Na Maggid Mjengwa,  WAKONGO wa Kinshasa na kwengineko wanaujua wimbo huu; ”Papaa Mobutu ee, lokuta monene, oy'akanisaka, MPR ekokufaha, wayahaa, Tata Marechal, tikala libela, tata Mobutuee, tikala libela, ...!”


  Makala yangu ya juma lililopita imepelekea baadhi ya wasomaji wangu, na hususan vijana, kutaka kufahamu zaidi habari za Joseph Mobutu. Kuna aliyeniandikia akisema; kwa anavyoiangalia jamii yetu hii, kuna anayojifunza kutoka kwa yaliyomkuta Mobutu.


  Naandika zaidi kuhusu Joseph Mobutu, maana, nami naamini, Mobutu ni kielelezo kizuri cha hulka za watawala wengi wa bara letu.
  Na Afrika utazionaje dalili za chama cha siasa kinachokufa? Jibu; ni pale ’Kiongozi Mkuu’ anapoanza kujitenga na umma, kwa kauli na matendo. Kuna wenzake wachache pia ndani ya Chama watakaokuwa na hulka hiyo. Chama cha siasa huonekana kuwa mbali na watu. Hakikidhi matakwa , mahitaji na matarajio si tu ya wanachama wake, bali ya umma. Afrika chama cha siasa hutekwa kirahisi na wachache.


  Je, Mobutu huyu ni nani? Joseph Desire Mobutu; baadae akaja kujiita Mobutu Sese Seko Nkuku Ngbendu wa Za Banga. Inasemwa kuwa Sese Seko ina maana ya milele, na Nkuku Ngbendu wa Za Banga ina maana ya mtu anayepita na kuacha nyuma yake alama za moto . Naam. Ni Mobutu wa milele na anayeacha alama za moto nyuma yake!


  Joseph Mobutu alizaliwa mwaka 1930 na alifia uhamishoni, Rabat, Morocco, mwaka 1997. Kwa matendo yake alipokuwa madarakani, Mobutu aliishia kuzikwa kama njiti ya kibiriti katika makaburi ya Ughaibuni. Mazishi yake yalihudhuriwa na watu wachache sana. Hayakufanana na ufahari aliojijengea alipokuwa hai na mwenye madaraka.


  Kule Kongo Mobutu alishasikia kilio cha Wakongo cha kutaka mabadiliko, akapuuzia. Wakongo katika mitaa ya Kinshasa, Lubumbashi, Kisangani na kwingineko walianza kunong’ona kuwa MPR, inakaribia kufa. MPR- Popular Movement Of The Revolution- kilikuwa ni chama kilichoanzishwa na Mobutu na wenzake mwaka 1967. Hatimaye Wakongo wakaacha kunong’ona, wakawa wakiongea kwa sauti mitaani, sokoni na kwenye vilabu vya pombe kuwa, “MPR inakufa!”


  Katika hali ya kujinusuru, Mobutu akawanunua hata wasanii ili wamuimbe yeye na chama chake. Hiyo hapo juu ni moja ya nyimbo za kumtukuza Mobutu na chama chake. Tafsiri yake; ”Baba Mobutu, utakaa udumu, wanasema sana , kuwa MPR itakufa, haiwezekani! Naam. Leo tunaona kuwa Mobutu hakukaa akadumu, MPR imekufa. Imewezekana! Na ndivyo wahenga wetu wanavyotwambia; ” Kila lenye mwanzo lina mwisho”.


  Nimepata kuandika kuwa katika nchi, vyama vya siasa vinakuja na kupita, lakini nchi hubaki daima. Kwa wanasiasa ni hivyo hivyo. Wanasiasa huja na kupita kwa maana ya kufa, lakini nchi huziacha. Na inakuwaje basi chama cha siasa kinapokaribia kufa?


  Jibu; ni kama simba mzee anayekaribia kufa. Hupoteza uwezo wa kuona, kunusa na kusikia. Kiongozi Mkuu’ na wenzake katika Chama hushindwa kusoma alama za nyakati. Hushindwa kuona kwa uhalisia mazingira yanayowazunguka. Hushindwa kusikia yanayosemwa mitaani na vijijini kumhusu ’ Kiongozi Mkuu’ na wenzake katika Chama kinachoongoza.


  Na katika kufa huko, ’ Kiongozi Mkuu’ na chama chake huhangaika sana kwa kuulisha umma kauli za propaganda. Wataonyesha kuwa kila kitu ni shwari. Zamani enzi za akina Mobutu walihakikisha watatumia vyombo vya dola vya wazi na vya gizani kuwatesa, kuwasweka magerezani na hata kuwaua wapinzani wa kisiasa wa ‘Kiongozi Mkuu’ na chama chake.


  ’Kiongozi Mkuu’ na wenzake katika Chama, na kwa kutumia vyombo vya habari watajitahidi sana ili umma usiamshwe kwa kupata habari za mapinduzi ya umma yanayofanyika nje ya mipaka ya nchi hiyo. Kuna wakati Mobutu alimfokea waziri wake wa Habari na Utangazaji, kisa? Waziri huyo aliruhusu televisheni ya Taifa kurusha hewani tukio la Mapinduzi ya Umma na kukamatwa na kupigwa risasi kwa dikteta Nikolai Nicolae Ceausescus wa Romania. Kwa Mobutu, Ceausescus hakuwa na tofauti kubwa na yeye ( Mobutu).


  Siku hizi macho ya jumuiya ya kimataifa yanaangaza sana kwa ’ Viongozi Wakuu’ wa Afrika na vyama vyao. Hivyo, wengi wa ’ Viongozi Wakuu’ Afrika wamebadilisha mbinu za ukandamizaji. Leo Afrika, ’ Kiongozi Mkuu’ hamnyongi wala hamsweki gerezani mpinzani wake wa kisiasa. Mbinu ya kwanza; Atamkumbatia ’kirafiki ’ hadi akose pumzi - afe. Hii inaitwa hugging to death! Ikishindikana mbinu ya kwanza, ’Kiongozi Mkuu’ Afrika atamhujumu au atawahujumu wapinzani wake wa kisiasa ’kimya kimya!’.


  Msingi wa yote hayo ni huu; watawala wengi Afrika , ndani ya mioyo yao, HAWAIPENDI demokrasia , wanaichukia. Masuala ya demokrasia, ikiwamo Katiba, inayotokana na watu na kugawana madaraka ina maana moja kwao; kuwa wao kuwa katika hatari ya kupoteza mamlaka na hata kufikishwa mahakamani na kusekwa magerezani kwa wizi wa mali ya umma. Katika mazingira hayo, watawala wengi Afrika watapambana kuhakikisha wanazuia mazingira ya kutokea hali hiyo niliyoielezea hapo juu. Na msingi wake ni ubinafsi na uchoyo wa viongozi hao.


  Lakini, hali hiyo haiwezi ikabaki ikiendelea tu bila ukomo. Hatimaye, walio wengi huamka usingizini. Humnyoshea kidole ’Kiongozi Mkuu’, na chama chake pia. Hapo ’Kiongozi Mkuu’ na chama hutafuta ’ wachawi’ ndani na nje ya chama, na pengine nje ya nchi. Husikika kauli kama ’ Njama za Mabeberu’! Umma hupotoshwa, huonyeshwa adui wa umma asiye adui.  Ukweli hubaki kuwa huu; adui wa umma huwa ni ’Kiongozi Mkuu’ mwenyewe, na chama chake. Mara nyingi kosa kubwa kwa ‘Kiongozi Mkuu’ na chama chake huwa ni kupungukiwa, si kuishiwa hekima na maarifa. Mobutu ni moja ya mifano ya ‘Viongozi Wakuu’ wa Afrika aliyepungukiwa na hekima na maarifa. Anguko la Mobutu lilitokana na hayo mawili, basi.


  Na Afrika ’ Kiongozi Mkuu’ kupungukiwa hekima na busara ni pamoja na kiongozi huyo kusahau kuwa , kama binadamu wengine, iko siku naye atakufa. Hataishi milele. Mtawala Afrika hajisumbui na swali lifuatalo; Baada ya kuondoka hapa duniani, Je, ningependa nikumbukwe kwa lipi?


  Inauhusu ’legacy’; yaani kile unachokiacha nyuma yako ambacho ungependa ukumbukwe nacho. Ndio, tofauti na viongozi wa nchi za wenzetu zilizoendelea, mtawala Afrika mara nyingi ni mbinafsi sana. Atajiangalia yeye, familia yake na wachache wengine katika nchi anayoitawala. Anapowania madaraka atajinadi kuwa ni mtetezi wa walio wengi, anapoingia madarakani, haraka sana , hulewa madaraka. Hugeuka kuwa ‘mlevi’ wa madaraka. Na katika ulevi wake wa madaraka, hutokea hata akatoa kauli za kuwatukana watu wake, wanyonge walio wengi waliomwingiza au waliomuunga mkono alipotwaa madaraka.


  Mobutu bado ni mfano wa kujifunza. Ikafika mahali Wakongo wakachoka, pamoja na kukandamizwa kote, walionyesha wazi kuwa wamemchoka Mobutu, na chama chake pia. Na chama cha Mobutu cha MPR- Popular Movement Of The Revolution ambacho twaweza kukiita kwa Kiswahili; Chama Cha Mapinduzi ya Watu, kikawa kimepoteza mwelekeo. Kimsingi, MPR hakikuwa chama wala hakikuleta mapinduzi kwa watu wa Kongo. MPR lilikuwa ni ’genge’ la Mobutu na wenzake wachache.


  Na ndio maana, siku Mobutu alipoikimbia Kinshansa ndio siku ambayo Laurent Kabila aliapishwa urais wa Kongo. Mobutu alipaa angani kuelekea uhamishoni Morocco, na kwenye mabegi yake, yumkini alibeba pia ’Katiba’ ya chama chake. Naam. Ndio, MPR ilikufa rasmi siku ile Mobutu alipoikimbia Kinshasa.


  Kumbe walioimba; ”Papaa Mobutu, tikala libela, lokuta monene!” walimdanganya ’ Kiongozi Mkuu’. Mobutu hakuwa mtu wa kukaa na kudumu. Na walicho-lokuta monene Wakongo kuwa MPR inakufa, ndio ukweli wenyewe. Kuna cha kujifunza.


  Maggid,


  MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo
  0788 111 765
   
 2. b

  bulunga JF-Expert Member

  #2
  Apr 23, 2011
  Joined: Oct 24, 2010
  Messages: 290
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 35
  Mbona husemi MPR ni sawa na CCM, nakumbuka yule kiongozi wa Romania Ceausescus alikuwa royala mdel wa Kingunge, ilikuwa ni baada ya Ziara ya mhesimiwa Kingunge akitokea Romania alirudi hapa nchini akawapa watanzania somo kuwa aliyoyaona huko Romania yalikuwa ya kuigwa na aliisifia sana nchi hiyo na kiongozi wake, haikupita hata mwezi moja Rais wa Romania alipinduliwa na hiyo ikawa ndiyo mwisho wa siasa za kijamaa nchini humo, ukiangalia Zaire na Tanzania, utakuona hata slogan za vyama vyao zinafanana, KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI,ZIDUMU FIKRA ZA MWENYEKITI na upuuzi mwingi tu, Leo TBC imekuwa ndo chombo cha propoganda cha CCM, wapinzani hawasikiki kwa hoja zao isipokuwa kwa mabaya yao, siioni tofauti ya Tido mhando na yule waziri wa Zaire aliyefokewa na Rais Mobutu kwa kuruhusu habari za mapinduzi ya Romania kwenye TV za taifa ya Zaire, tutakukumbuka Mhando
   
 3. m

  matawi JF-Expert Member

  #3
  Apr 23, 2011
  Joined: Mar 29, 2010
  Messages: 2,055
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 135
  Hii imenyooka sana magid, big up
   
Loading...