Obama na JK wanavyochagua Mawaziri | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Obama na JK wanavyochagua Mawaziri

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Sumaku, Jul 30, 2009.

 1. S

  Sumaku Member

  #1
  Jul 30, 2009
  Joined: Feb 17, 2009
  Messages: 53
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Na Born Again Pagan

  KATIKA toleo lililopita tuliangalia suala la itikadi katika vyama vya siasa: Amerika na Tanzania. Nilidokeza kero ya kushindwa kuelewa tofauti mbadala (fundamental differences) za ki-itikadi kwa vyama vyetu vya siasa!

  Kwa bahati nzuri mwandishi mwenzangu, Andrew Mushi, amenidokezea kuwa hapo awali aliandika makala yenye sehemu ya jibu kwa kero yangu katika toleo la Raia Mwema (Aprili 1 - Aprili 7, 2009).

  Makala ya leo yana malengo mawili: Kutamatisha sehemu iliyobaki ya suala la itikadi; na jinsi ma-Rais wanavyochagua Kabineti zao, Amerika na Tanzania.

  Kwetu Tanzania vyama vingine, huenda, vikaishiwa mafuta ya siasa (political gas), kama gari barabarani au hewa kwa mnyama (asphyxiating)! Vingine, huenda, vikajiimarisha kwa kuungana.

  Kama nilivyoelezea katika makala yaliyopita, vyama vya siasa vinatubagua kati ya sisi na wao! Na sijui kama kweli tutaachana na hayo ya sisi na wao! Serikali inaundwa lakini ubaguzi huu unabakia. Hii inasambaratisha maslahi makubwa ya taifa na kuyafinya ya ki-vyama!

  Hii inawakareketa wananchi wengine kushauri kwamba wakati wa kupigakura tuzingatie (au wa-Bunge wakiwa vikaoni wazingatie) maslahi ya taifa na kuachana na tofauti za ki-vyama!
  Je, tunaweza kujenga maslahi ya taifa yavukayo tofauti zetu za vyama? Je, kila mwanachama ataacha kujigamba kuwa chama chake ndicho chenye majibu-dhamiria kwa matatizo yaliyopo katika Tanzania yetu tuipendayo wote?

  Mimi huwa nafikiri kuwa tulijaliwa kuwa na vichwa kwa ajili ya maslahi ya Tanzania! Tuwe wa Chama-Tawala au wa Upinzani ni lazima tutumie hivyo vichwa vyetu.

  Tusijali kupigania kubakia madarakani; wengine kupigania kuwang’oa hao waliomo madarakani. Tusijali kujidai kuwa sisi ndio tulipewa mandate ya kutawala (maana kuna siku tutang’olewa). Tusijali kungojea kwanza tushike madaraka ndipo waone kali yetu (maana inaweza kuchukua zaidi ya miaka 20 hivi kabla ya kuingia Ikulu au kutoingia kabisa Ikulu hiyo)!

  Je, mikakati hii ndio kujenga nchi?

  Tunaweza kabisa kuyapunguza haya majambo kwa kubadili mfumo wa siasa yetu kuhusu haki ya wapigakura! Ndio, tunaweza! Tunaweza kuwakilisha maslahi ya taifa kutokana na kubadilisha mfumo wa kupigakura:

  Tuachane na mfumo wa paliamentary democracy – mfumo wa “wengi wape” wenye kuwajibika mbele ya Serikali ya Chama-Tawala. Twende mfumo wa proportional representation, wenye kupendelea maslahi yote ya jamii katika taifa. Tume ya taifa ya Uchaguzi inafaa kuliangalia hili jambo; tunalitumia katika kuchagua akina mama wa-Bunge, eti!

  Pengine, hili ni kati ya mambo muhimu ya kujifunza kutoka Demokrasia na Chaguzi Kuu (Rais) za hapa Amerika, kama nitakavyoeleza badaye.

  Nchini Amerika, ingawa kuna vyama viwili vikubwa vinavyoshindania utawala/uongozi, wenyeviti wa vyama hivi hawajitokezi kuwa wagombea kinyang’anyiro cha wadhifa wa kisiasa wa juu – u-Rais, kama ilivyo huko Uingereza.

  Nchini Amerika mtu yeyote mwenye sifa zitakiwazo anaweza tu kujitokeza kuwa mgombea nafasi hiyo aidha kwa kuchagua chama ama binafsi. Lakini uwezekano wa vyama vidogo na mtu binafasi ni mdogo sana!

  Mtawala/kiongozi wa chama cha siasa nchini kwetu anachaguliwa na ndiye anakuwa mstari wa mbele kugombea kinyang’anyiro cha u-Rais wa nchi.

  Vyama vya siasa vinakuwa kama kampuni binafsi za biashara!Lakini naona vyama vingine vinaandamwa na mvuto wa kukaribisha mwanachama yeyote kuwania nafasi hiyo. Pengine vinafanya hivyo tu kwa sababu wenyeviti waliopo wamekuwa wakishindwa (lost hopes) katika Chaguzi Kuu!

  Suala la itikadi halipewi uzito mkubwa kiasi cha vyama vyetu vya siasa kukoswa maono au mweleko kwa siku za usoni. Vyama vya siasa vinapambana kuokoa yaliyopo; njaa ya kutaka kuingia Ikulu tu!

  Sasa tuangalie jinsi ma-Rais wanavyochagua Kabineti zao, Amerika na Tanzania. Tuanze na Amerika, ambayo kiini chetu kinatutaka tujifunze angalau lolote la ki-demokrasia kutokana na Uchaguzi Mkuu uliopita nchini hapa.

  Rais-Mteule wa Amerika anayo madaraka ya kuweza kumchagua yeyote anayempenda awe katika timu yake ya uongozi. Anaunda Baraza la ma-Waziri nje ya wa-Bunge au chama chake, hata kabla ya kuapishwa. M-Bunge anayechaguliwa kutoka chama anachotoka Rais inambidi aache wadhifa wake.

  Rais anaweza pia kuchagua Waziri kutoka vyama vya upinzani, kama Rais Barack Obama alivyofanya kwa kumchagua Waziri-Mteule Seneta wa New Hampshire Judd Gregg (Biashara) kutoka Chama cha Republican. Lakini huyo Waziri-Mteule alijitoa baadaye kutokana na tofauti za ki-itikadi.

  Baada ya kuteuliwa, ma-Waziri hao huchunguzwa na Kamati ya wa-Bunge na wakati mwingine baadhi yao hukataliwa.

  Sisi tumezoea baada ya kumtangaza mshindi wa Uchaguzi Mkuu na kumpata Rais, basi Rais huyo huunda Baraza la ma-Waziri kutoka kwa wa-Bunge walioshinda ama wanaokubalika ki-Katiba kuteuliwa naye. Hapa pia kuna kasoro ya Rais wetu kuweza kuchagua walio karibu naye na/au marafiki zake!

  Wa-Bunge ma-Waziri wanabakia na u-Bunge wao. Rais hawezi kuchagua Waziri kutoka vyama vya upinzani!

  Ma-Waziri wetu wengi wana ma-jimbo yao ya uchaguzi. Wengine huchaguliwa na Rais kuwakilisha jamii.
  Mwingiliano ni wapi pa kuwajibika: kwa wapigakura au serikali, ni suala ambalo Mheshimiwa m-Bunge Fred Mpendazoe (CCM-Kishapu) aliligusia katika mahojiano yake na Raiamwema hivi majuzi. Hasara yake kuna kulindana sana.

  Ingawa wapigakura Amerika wana kura moja, mtu mmoja katika kumchagua Rais, sio kusema kuwa chama chenye kura nyingi kitashinda, kulingana na usemi, wengi wape. Rais wa Amerika hachaguliwi na wingi wa kura za wapigakura (popular votes). Anachaguliwa na kile wakiitacho, electoral college votes, kulingana na kila Jimbo linaruhusiwa kuwa na kura ngapi.
  Amerika ina mfumo-kubalika kati ya kura za mpigakura mmoja, kura moja, kwa siri (popular votes) na uchaguzi wa wawakilishaji wa wapigakura (the representatives of the electorate). Ma-Jimbo mengine yana kura zaidi (proportional representation). Ndio kusema kuwa wananchi wa kawaida wapigakura huwachagua wawakilishi wao wachache, ambao humchagua Rais wa nchi.

  Kwetu sisi Rais huchaguliwa kwa wingi wa kura za mpigakura mmoja, kura moja, kwa siri (popular votes). Tume ya Uchaguzi inayoangalia mchakato wa chaguzi kila baada ya miaka mitano. Tume hii inaweza kubadili majimbo ya kura kila baada ya miaka kumi pamoja na yale ya wanawake, uandikishaji wa wapigakura, michakato ya upigaji kura na kutangaza matokeo.

  Tume hii huchaguliwa na Rais na haingiliwi na mtu yeyote. Lakini kuna malalamiko mengi kutoka upande wa upinzani wa mwingilio wa chama-tawala na serikali yake, wakati mwingine kupitia vyombo vya usalama.

  Uandikishaji wa wapigakura unafunguliwa wakati wote; na ni wajibu wa Tume, kwa kushirikiana na NGOs, kuwaelemisha wapigakura. Lakini pia uandikishaji na orodha ya wapigakura navyo vinatia upinzani wasiwasi.

  Lakini sisi mgombea wa wadhifa wa u-Rais anapendekezwa na Chama, analipa arabuni na kuungwa mkono na wapigakura 200. Kila mgombea huteuliwa kupitia chama chake cha siasa na kuungwa mkono na wapigakura 25 wa jimbo lake la kupigakura.

  Serikali haigharamii matumizi ya vyama vya siasa katika shughuli za uchaguzi u-Bunge na wawakilishi wetu wa serikali za mitaa, pia tunachaguliwa na chama ni nani wa kumpigia kura mithili ya mfumo wa ma-super-delegates wa Democratic Party cha Amerika! Pengine, tungewaachia wapigakura wenyewe wachague watawala/viongozi wao moja kwa moja kuliko kuchaguliwa na ma-super-delegates!

  Demokrasia ni watu (kwa mfano, wanachama); si chama kuchagua watawala/viongozi! Pengine, ndio maana sasa CCM imebadili mtindo wake kutoka kwa huo wa ma-super-delegates kwa kuwawezesha wananchama wake kuchagua watawala/viongozi wao moja kwa moja! Vyama vingine vinafaa kufuata mfano huo wa CCM!

  Lakini hili la CCM nalo lina utata wake. Ni dawa ya kuwapaka wanachama wajione kuwa CCM kiko karibu nao. Lakini kauli ya mwisho itakuwa ya ma-super delegates wa Wilaya!
  Lakini tusisahau Amerika ina zaidi ya miaka 200; sisi ni chini ya miaka 50!

  Makala yatakayofuata yataangalia suala la vyombo vya habari/mawasiliano Amerika na Tanzania. Kwetu Tanzania suala hili ni muhimu kwani linajitokeza wakati huu wa malumbano makali baina ya serikali, kwa upande mmoja, na wamiliki au wadau wa vyombo vya habari/mawasiliano, kwa upande mwingine.

  Malumbano hayo yametokana na serikali kutaka kuandika rasimu ya marekebisho ya sera ya habari ya mwaka 2003 katika muswada wa sheria. Wadau wanadai kuwa muswada huo unadhamiria kunyonga uhuru wa vyombo vya habari/mawasiliano nchini na kuwakomoa mataikuni wachache wamiliki.


  romuinja@yahoo.com

  CHANZO: http://www.kwanzajamii.com
   
Loading...