Nyumba ya jirani inaungua, yetu inateketea. | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nyumba ya jirani inaungua, yetu inateketea.

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by GWOTTA, Dec 8, 2011.

?

NANI MUASISI WA UDINI TANZANIA?

Poll closed Feb 6, 2012.
 1. JULIUS NYERERE

  0 vote(s)
  0.0%
 2. ALI HASSAN MWINYI

  0 vote(s)
  0.0%
 3. BENJAMIN WILLIAM MKAPA

  0 vote(s)
  0.0%
 4. JAKAYA MRISHO KIKWETE

  4 vote(s)
  100.0%
 5. KIGHOMA ALI MALIMA

  0 vote(s)
  0.0%
 6. FREDRICK SUMEYE

  0 vote(s)
  0.0%
 1. G

  GWOTTA Member

  #1
  Dec 8, 2011
  Joined: Jun 15, 2011
  Messages: 14
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  NYUMBA YA JIRANI INAUNGUA, YETU INATEKETEA.
  Tarehe 9 Desemba 2011 tutasherehekea miaka 50 ya uhuru wa nchi ya Tanganyika. Kwanza nianze kwa masikitiko kwa namna vyombo vya habari vinavyojitahidi kupotosha na wanaelekea kufanikiwa. Mara nyingi wamesikika wakisema kuwa ni uhuru wa miaka 50 ya Tanzania. Si kweli wala Tanzania haikuwahi kutawaliwa na mkoloni, iliyotawaliwa ni Tanganyika na ndiyo iliyopata uhuru kutoka kwa Muingereza. Juhudi za kulificha jina la Tanganyika ni kitendo kibaya kihistoria ambacho kinapaswa kukemewa na Watanganyika wote.

  Tanzania ilizaliwa Aprili 26 mwaka 1964 baada ya muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar. Kabla ya hapo kila nchi ilikuwa ni dola kamili iliyo huru na inayojitegemea. Kuja kwa muungano haikuwa ni kifo cha Tanganyika wala Zanzibar. Lengo la mfulululizo wa makala hizi itakuwa ni kueleza kinaga ubaga hali ya mahusiano ya kidini ilivyo hapa nchini na nini cha kufanya ili kuboresha mahusiano hayo, nini kitatokea kama hali iliyopo sasa itaachiwa iendelee kama ilivyo?, Nani atakayeathirika kutokana na kuachiwa huko mambo yajiendee kama yalivyo?.

  Watanzania tumekuwa ni mabingwa wakubwa wa kushughulikia migogoro ya nchi jirani na Alhamdulillah tumefanikiwa kwa hilo na pengine hakuna mpinzani wetu katika kushughulikia mambo kidiplomasia. Jambo linalonishangaza ni kwamba tunaona na tunakwenda kuzima moto katika nyumba za majirani zetu ilhali tunasahau nyumba yetu na kuiacha inateketea. Hizo nyumba za wenzetu zinaungua , ni bora zinazoungua unaweza hata kuokota vya kuokota kuliko ya kwetu inayoteketea. Tumeshiriki vema katika kutatua migogoro ya nchi kadhaa ndani na nje ya Afrika. Mgogoro wa Liberia, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo {DRC}, Comoro wakati wa kumtoa Kanali Bakari, Jimbo la Darfur nchini Sudan bila kusahau mgogoro uliopo Lebanon. Kwa umahiri wa vikosi vyetu vya ulinzi na usalama na kwa ushirikiano wa wanadiplomasia wetu, inatarajiwa kabisa kuwa tatizo lolote linaloweza kujitokeza hapa nchini linaweza kutatuliwa kidiplomasia humuhumu ndani bila kuhitaji msaada wa yeyote kutoka nje ya mipaka ya nchi yetu. Tutakuwa ni watu wa ajabu sana kama tutahitaji msaada wa nje katika kutatua matatizo yetu ilhali kila uchao na uchwao tunawasaidia wengine pindi wanapokumbwa na matatizo katika nchi zao.

  Alhamdulillah tunao wanadiplomasia wetu wa kimataifa; Dr. Salim Ahmed Salim, Rais mstaafu Benjamin William Mkapa, Dr.Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wengineo lukuki. Umaarufu wao nje ya nchi huenda ni mkubwa sana kuliko ulivyo hapa nchini. Dk.Salim Ahmed Salim anafahamika sana kwa kuwa msuluhishi wa mgogoro wa Jimbo la Darfur nchini Sudan, huenda utulivu mdogo uliopo huko una mchango mkubwa sana wa Dk. Salim.

  Mwaka 2007 Desemba Kenya walifanya uchaguzi mkuu, uchaguzi ambao uliiishia katika umwagaji wa damu. Wanadiplomasia wengi walijaribu bahati yao lakini hawakusikilizwa, pindi alipoingia Dk.Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mambo yote yalikaa sawa na hatimaye ikawa ni uundwaji wa serikali ya mseto ambayo tunaiona hadi hii leo.
  Ushughulikiaji wa matatizo ya hao wenzetu unatokana na matatizo makubwa mojawapo ni ukabila na pili ni udini. Kwa hakika tumefanikiwa sana katika kuwasaidia, shida ni kwamba tunagawa chakula huku tukijisahau kuwa nasi tuna njaa tena njaa ya kufa mtu.
  Tatizo lililopo nchini kwetu lakini halitajwi kwa kinywa kipana na hata likitajwa hupuuzwa. Udini ni moja kati ya matatizo makubwa sana linaloikabili nchi yetu lakini hakuna anayeshughulika nalo kuhakikisha nasi hatufiki kule walipofikia wenzetu Rwanda, Burundi, Kenya n.k. Tatizo hili ni kubwa sana lakini kwa upofu wa wananchi wa Tanzania wakiongozwa na wasomi wao wanalifumbia macho suala hili na kuwa ni mabingwa wa kuchangia mada katika redio na runinga za ndani na nje ya nchi kuhusu matatizo ya ukabila na udini yanayowakabili wananchi wa nchi zingine kama Rwanda, Burundi , Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lebanon, Liberia n.k.
  Nitumie fursa hii kuwapongeza Waislamu wote walioshiriki kwa nguvu zao na mali katika kutembea nchi nzima kuwaelezea Watanzania kuhusu hatari kubwa inayoikabili nchi yetu nayo si nyingine bali ni hatari ya serikali ya Tanzania kuukumbatia MFUMO KRISTO. Ilikuwa ni 15 Januari 2011 ndani aya ukumbi wa Diamond Jubilee hadi 16 Oktoba 2011 tena ndani ya ukumbi huohuo ambapo Kamati ya maandalizi ya makongamano ilizindua na kuhitimisha safari ndefu ya nchi nzima ya kuwafahami sha wananchi. Wengi wa Watanzania leo wanafahamu nini maana ya MFUMO KRISTO na ushahidi wake wa namna serikali inavyopelekwa puta na viongozi wa dini ya Kikristo badala ya kuongozwa na viongozi wa serikali kwa kuzingatia sheria na kanuni.

  Lakini inasikitisha kuendelea kuwapo watu, mbaya zaidi wengine ni Waislamu nao wapo wasioona hali hii ya ubaguzi na dhuluma dhidi ya Waislamu na upendeleo wa wazi kwa Wakristo. Waislamu hawa na Watanzania wengine wanapaswa wakae chini na kutafakari upya, wapitie marejeo yenye tafiti za kisomi kisha wataweza kubaini ukweli unaozungumzwa na wanaharakati wa kutetea haki za Waislamu. Watanzania tunapaswa kufahamu kwamba kutengemaa kwa mahusiano mema baina ya Waislamu, serikali na waumini wa dini zingine haitakuwa ni kwa faida ya Waislamu pekee bali ni kwa faida ya Watanzania wote, na kama hali ya amani ikitoweka watakoathirika ni Watanzania wote na si Waislamu pekee. Katika historia ya mwanadamu hakuna mahali ambapo dhuluma ilidumu, wanaodhulumiwa walisema pindi ambapo hawakusikilizwa waliamua kutafuta namna nyingine nzuri ya kuondokana na dhuluma wanayofanyiwa. Mfano wa Wahutu ni mzuri sana kuuzingatia kwa namna walivyobaguliwa na kutengwa na serikali iliyohodhiwa na Watutsi. Watutsi walihodhi mamlaka ya nchi utadhani wanaishi peke yao, kumbe kuna wengine pia. Kilichotokea mwaka 1994 kila mtu anakifahamu, tutakijadili siku nyingine.
  Hivi karibuni niliwasiliana na ofisa mmoja wa chombo kimoja cha habari cha serikali, nilimuomba kuwasilisha mada yangu. Aliniuliza kuhusu maudhui yaliyomo katika mada husika, nilimwambia kuwa itahusu hali ya mahusiano ya kidini baina ya Waislamu, serikali na waumini wa dini zingine. Alinikatalia kwa kusema kwamba dini ni suala nyeti ambalo halipaswi kuwasilishwa katika vyombo vya habari hususani vya serikali maana itaweza kuibua hisia hasi za mgawanyiko miongoni mwa hadhira kama ilivyo na inavyozidi kutokea katika nchi zingine. Akanikaribisha kushiriki kwa kuwasilisha mada zingine tofauti na nilivyomuomba awali. Haya, tazameni ndugu Watanzania, kumbe tatizo linafahamika lakini waheshimiwa hawataki lizungumzwe, je, wanachotaka wao ni nini hasa? Tafakari. Hao hao wanaokwepa kuzungumzia tatizo la udini hapa nchini ndiyo hao hao wanaoongoza mijadala katika vyombo vyao vya habari kuhusu matatizo ya ukabila na udini katika nchi zingine. Kama kweli tunafahamu kuwa ubaguzi wa aina yoyote ule mwishowe ni mpasuko mkubwa katika jamii, je, sisi twangojea hadi utokee huo mpasuko? Kwanini tusizibe ufa mapema? Chonde tusithubutu kujaribu kungojea kujenga ukuta maana gharama yake ni kubwa kuliko tunavyojaribu kuikwepa. Waislamu wa Tanzania hatutaki makuu ndiyo maana kila siku twaongea na kuandika ili kila mtu afahamu hali ilivyo hapa nchini, ili siku likitokea la kutokea tusianze kuulizana yalianzia wapi.

  Mwanzoni mwa mwezi Septemba Ndugu Mohamed Said aliandika makala kwenye Jamii Forum, makala hiyo ilihusu mchango wa Waislamu katika kupigania uhuru wa Tanganyika na namna Waislamu walivyotengwa baada ya uhuru hadi hii leo. Kwa upofu wa wachangiaji wengi wao wenye majina yanayonasibiana na Ukristo nami natumai kuwa ni Wakristo, walimpuuza mwandishi na kusema kuwa wameshayazoea maneno yake ni yale yale kila siku. Sijui zikoje akili za Watanzania hawa, badala ya kujadili kwa kina kuhusu mada husika, waliamua kumpuuza kwa kuwa wanaozungumzwa ni Waislamu na kwa mtazamo wao watu hao ni watu wasio na thamani yoyote hapa nchini wala mchango wao wowote hauna haja ya kukumbukwa wala kuthaminiwa. Mimi nasema kwamba vyovyote iwavyo Waislamu walipigania uhuru au hawakupigania uhuru bado wanastahili haki zote sawa na wananchi wengine. Hawastahili kubaguliwa kwa aina yoyote ile na ubaguzi huo ni dhuluma kubwa sana inayopaswa kujadiliwa kitaifa na hatimaye dhuluma hii ifike mwisho na wananchi wote tuishi kwa kutakasiana nafsi badala ya sasa ambapo Waislamu tuna dhiki kubwa katika nyoyo zetu kutokana na dhuluma kubwa zisizokoma tangu kabla ya uhuru na hata baada ya uhuru hadi sasa. Kupigania au kutopigania uhuru si sababu hata kidogo ya kuwabagua Waislamu au kuwapendelea Wakristo. Utu wa mtu unapaswa kuzingatiwa kuliko kitu kingine.
  Kupuuzwa malalamiko ya Waislamu dhidi ya kuabaguliwa kidini; Kutofanyiwa uchunguzi wa mauaji ya Waislamu Masjid Mwembechai Jijini Dar es salaam mwaka 1998 Februari, Kuzuiliwa kitabu kilichoelezea kwa kina mauaji ya Waislamu Mwembechai: Mwembechai Killings and the Political Future of Tanzania kilichoandikwa na Dr. Hamza Mustafa Njozi [sasa Profesa], Kuzuiliwa Tanzania isijiunge na OIC ilhali Mheshimiwa Bernard Membe waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa alitutangazia bungeni kuwa suala la kujiunga ni muhimu na halina tatizo lolote. Ghafla tukaambiwa kuwa haitowezekana, sijui ilikuwa ni amri ya kutoka ikulu Magogoni au ni amri kutoka Kanisani?. Kupigwa zengwe la kutoruhusiwa mahakama ya Kadhi ni aina nyingine ya kupuuzwa malalamiko ya Waislamu.
  Makala haya ni utangulizi wa mfululizo wa makala zitazokuwa zinaelezea hali ya mahusiano ya kidini baina ya Waislamu, serikali na waumini wa dini nyingine. Hivyo basi matukio nitakayoyaorodhesha hapa nitayafafanua kwa kina katika makala zitazofuatia. Msomaji uwe mtulivu ili upate ufafanuzi wa kina wa mifano hiyo ni mingine mingi nitakayoitumia.

  Viashiria vichache vya ubaguzi wa kidini; Kupumzika Jumamosi na Jumapili, ingekuwa ni kupumzika Ijumaa pekee na kufanya kazi Jumamosi na Jumapili- Wakristo nchini wangeandamana usiku kucha, Kutoruhusiwa kuswali Ijumaa katika shule nyingi na maofisi mengi hapa nchini, Wanawake kutoruhusiwa kuvaa Hijabu hali ya kuwa Watawa wa Kikristo wanaruhusiwa, Tukio la hivi karibuni la jijini Mwanza Waislamu walipigwa kwa mabomu ya machozi nje ya mahakama, Utendaji wa watumishi ambao ni Wakristo kutawaliwa na chuki zao za kidini badala ya sheria na taratibu za kazi, mfano Polisi waliokwenda kutekeleza mauaji ya Mwembechai walikusudia kuwaadabisha Waislamu na wala hawakwenda kutuliza ghasia, pia walikwenda kutokana na amri ya Paroko Camilius Luambano wala si amri ya kitaalamu ya mambo ya ulinzi na usalama, Wasomi wa Kikristo na viongozi wa dini ya Kikristo kupinga ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Shule za kata, Walifanya haya si kwa mapenzi ya nchi bali ni kwa chuki zao za kutowapenda raia wenzao ambao ni Waislamu. Tarehe 25 Novemba 2011 Chuo cha usimamizi wa fedha IFM pamoja na Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM vilifanya mahafali ya kuwatunukia shahada wanafunzi wake ilikuwa ni siku ya Ijumaa tena muda wa swala ya Ijumaa kwa Waislamu; je inawezekana kufanya mahafali ya chuo kikuu siku ya Jumapili hapa nchini? Kwanini ifanyike Ijumaa na isifanyike Jumapili? Mgawanyo mbaya wa ajira na nafasi za uteuzi wa madaraka ya umma ambapo Waislamu wanaminywa na Wakristo wanapendelewa, Nafasi za kielimu kuanzia sekondari hadi chuo kikuu bado Waislamu wanagandamizwa na Wakristo wanapewa upendeleo.

  Kushindwa kujibiwa hoja zilizotafitiwa zinazodhihirisha ubaguzi wa kidini ambapo Waislamu wanabaguliwa kutokana na Uislamu wao; Kitabu cha Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara kilichoandikwa na Dr. John Sivalon, Maisha na Nyakati za AbdulWahid Sykes {1924-1968} Historia iliyofichwa ya Harakati za Waislamu dhidi ya Ukoloni wa Waingereza kilichoandikwa Mohamed Said, The Partner-ship kilichoandikwa na Mzee Aboud Jumbe Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Justice Rights and Worship- Religion and Politics in Tanzania kilichoandikwa na REDET, Development and Religion in Tanzania kilichoandikwa na Jan P.Van Bergen, Mwembechai Killings and the Political Future of Tanzania kilichoandikwa na Dr. Hamza Mustafa Njozi, Historia ya Kuhuisha Uislamu Tanzania 700 hadi 2009 kilichoandikwa na Islamic Propagation Centre, Muslims and the State in Tanzania kilichoandikwa na Dr.Hamza Mustafa Njozi. Vitabu hivi vimeelezea kinaga ubaga hali ya mahusiano ya kidini ilivyo baina ya Waislamu, serikali na waumini wa dini zingine na namna Waislamu walivyobakishwa nyuma kimaendeleo kwa makusudi. Mfululizo wa makala hizi nimekusudia kuwakumbusha wanaofahamu na kuwaelimisha wasiofahamu kuhusu hatari itakayoweza kujitokeza kama kundi linalokandamizwa ambalo ni Waislamu watakapoendelea kukandamizwa, je muitikio wao utakuwa namna gani. Pia nitatazama somo muhimu kutoka Rwanda na Burundi ambao wao walifanikiwa kupambana na ubaguzi lakini walishachelewa, walirekebisha baaada ya mauaji ya halaiki ya mwaka 1994. Pia nitachambua mbivu na mbichi zilizomo katika Waraka wa Waislamu kwa Viongozi na Wapenda Haki Tanzania-MFUMO KRISTO NA DHULMA DHIDI YA HAKI ZA WAISLAMU NCHINI kilichozinduliwa siku ya tarehe 16 Oktoba 2011 katika hitimisho la makongamano maarufu kama makongamano ya MFUMO KRISTO. Tukutane wiki ijayo katika muendelezo wa makala hizi.

  Imeandikwa na RAHIM GWOTTA
  1. rgwotta@yahoo.com, gwottajunior@gmail.com
  2. 0784 232957, 0756 232957.
   
Loading...