Nyufa zimezidi, nyumba hatarini kuanguka

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,044
Nyufa zimezidi, nyumba hatarini kuanguka

Johnson Mbwambo Aprili 23, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Kitendo

MARA kwa mara napenda kuwaambia marafiki zangu (wanapojali kunisikiliza) kwamba ‘kiama' kinachoonekana sasa Zimbabwe hakikuja siku moja. Kilikuja taratibu, na hatua kwa hatua. Kwamba mfumuko wa bei wa nchi hiyo haukuruka siku moja tu kutoka tarakimu moja hadi kuwa asilimia 165,000. Ulipanda taratibu na hatua kwa hatua.

Napenda kuwatolea marafiki zangu mfano huo wa Zimbabwe wakati tunapojadili hatima ya nchi yetu Tanzania, kwa sababu mbili kubwa. Kwanza ni kwa sababu nilipata bahati ya kutembelea vijiji vya nchi hiyo nikiwa mmoja wa waangalizi wa kimataifa wa Jumuiya ya Madola wa chaguzi mbili zilizopita za Zimbabwe ukiondoa huo wa majuzi, kwa hiyo naielewa kidogo nchi hiyo. Pili, napenda pia kuwatolea mfano wa Zimbabwe kuwakumbusha kwamba mambo yasiporekebishwa hapa nchini, nasi pia tunaweza kuishia ilikoishia Zimbabwe.

Kwa sababu ya Wazimbabwe kutochukua hatua pale ilipostahili kuchukua hatua kumdhibiti Rais Robert Mugabe na chama chake cha ZANU PF, alifika mahali akajenga kiburi cha ajabu kwamba ni yeye tu (na ZANU PF) anayeweza kuulinda ukombozi wa nchi hiyo kutoka kwa Wazungu.

Kwa sababu ya miaka mingi ya kuachiwa na Wazimbabwe afanye afanyacho bila kupingwa, akajenga baadaye tabia ya kutokubali kupingwa, tabia iliyokuja kuathiri kichwa chake na kumfanya ‘mtumwa' wa fikra potofu kwamba akiachia urais au ZANU PF kikiondoka madarakani, basi, Zimbabwe itakuwa tena koloni la Uingereza!

Vinginevyo, utaielezeaje hotuba yake ya wiki iliyopita ya maadhimisho ya miaka 28 ya Uhuru wa Zimbabwe? Anahutubia taifa katika kipindi ambacho wananchi wote wa Zimbabwe wanasubiri kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu ambayo yamecheleweshwa kwa zaidi ya wiki tatu kwa sababu ya yeye kushindwa na Morgan Tsvangirai, lakini hagusii kabisa suala hilo katika hotuba yake na badala yake anazungumzia hofu ‘hewa' kwamba akiondoka madarakani ukoloni wa Mwingereza utarejea.

Utamwelezeaje kiongozi ambaye nchi yake inaongoza duniani kwa mfumko mkubwa wa bei, inaongoza duniani kwa asilimia kubwa ya watu wasio na ajira (asilimia 80); nchi ambayo nusu ya raia wake wanaishi uhamishoni, nchi ambayo kikombe cha chai katika hoteli kubwa kinauzwa dola za Zimbabwe milioni 2.5, na bado akihutubia mkutano wa taifa katika maadhimisho ya miaka 28 ya uhuru ‘anaiota' tu Uingereza kwamba inaweza kuja tena kuitawala nchi yake?

Utamwelezeaje Rais au chama tawala ambacho kinamruhusu Rais wa nchi yenye wananchi wanaokufa kwa sababu ya ukosefu wa chakula na wengine milioni 4 wanaoishi kwa chakula cha msaada, aagize tani 77 za shehena ya silaha kutoka China badala ya chakula ambacho ni dhahiri kitakuwa cha shida mno kupatikana katika siku za karibuni kwa sababu ya kuanguka kwa uchumi wa dunia?

Kwa ufupi, Mugabe na ZANU PF waliachiwa kwa muda mrefu mno kuiongoza nchi bila kupingwa kiasi kwamba wameathirika vichwani kiasi cha kujenga fikra kwamba hakuna maisha Zimbabwe bila Robert Mugabe au bila ZANU PF.

Ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba kama Wazimbabwe wangechachamaa miaka ile ya mwanzo wakati Robert Mugabe na ZANU PF, alipoanza kuiendesha nchi hovyo, asingefikia hatua hiyo ya kuugua kifikra na pengine Zimbabwe isingefikia hapo ilipofikia. Lakini Wazimbabwe hawakuchachamaa na walipozinduka na kuchachamaa tayari kadikteta kadogo kalishaota pembe, na sasa kukatoa madarakani na chama chake cha ZANU PF, labda, kuwe na umwagaji damu wa pili baada ya ule wa vita ya ukombozi.

Kwa hiyo, leo tunaposononeshwa na ‘kiama' cha sasa cha Zimbabwe na tuiangalie nchi yetu na kujiuliza, kila mara, iwapo hatujakiachia chama tawala cha CCM na serikali yake muda mrefu wa kujifanyia mambo hovyo bila kukemewa na wananchi; kama vile Wazimbabwe walivyomuacha Mugabe na ZANU PF kuiharibu nchi hatua kwa hatua.

Miezi minane ijayo tutatimiza miaka 47 tangu kupata uhuru wetu. Na tujiulize; je bado tumesimama kama taifa imara lenye umoja, mshikamano na amani? Msingi mkuu wa umoja wetu, kama ulivyojengwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ulikuwa ni usawa na haki kwa wote. Je, leo tunaweza kuendelea kujivunia hayo au tumetetereka kwa sababu ya kukiachia chama tawala cha CCM na serikali yake kufanya kitakavyo?

Miaka minane iliyopita, Aprili 14, 2000, Jaji Joseph Sinde Warioba wakati akifungua warsha ya maadhimisho ya miaka 79 ya kuzaliwa Mwalimu Nyerere alitaja nyufa nne kubwa zilizokuwa zimejitokeza na kutishia umoja wa kitaifa. Miaka minane baadaye si tu kwamba nyufa hizo bado hazijashughulikiwa, lakini zimezidi kupanuka na pia zimejitokeza nyingine, na sasa nyumba ina nyufa nyingi na imo hatarini kuanguka.

Kwa kuzingatia matukio ya hivi karibuni hapa nchini, napenda kuzungumzia ufa mmoja tu kati ya nyufa nne alizozitaja Jaji Warioba miaka minane iliyopita – ufa wa ufa wa kukithiri kwa ufisadi nchini.

Akizungumzia ufisadi miaka minane iliyopita, Jaji Warioba aliainisha mahusiano ya kuongezeka kwa ufisadi nchini na kuongezeka kwa pengo kati ya matajiri na masikini.

Alisema hivi: "Kuna mwenendo usiopendeza wa kuongezeka kwa kasi kwa pengo kati ya matajiri na masikini. Siasa imetekwa na matajiri kwa kushirikiana na wasomi. Ufisadi na rushwa sasa ni vitu muhimu katika uchaguzi na si sera…..ufisadi unaigawa vipande jamii. Tunauzungumzia sana, tunaushutumu sana, lakini pia tunashiriki bila haya kuuendeleza."

Je miaka minane tangu Jaji Warioba atoe kauli hiyo hali ikoje? Kwa kuzingatia kashfa chache zilizoibuliwa za miaka ya hivi karibuni za IPTL, ununuzi wa rada, EPA, Richmond, Kiwira, Songas, Buzwagi, majengo ya BOT na hata uuzaji wa nyumba za serikali, ni wazi hali ni mbaya zaidi, na kama ni ufa katika nyumba, basi, umetanuka zaidi.

Kama alivyosema Jaji Warioba, hali hiyo ya wasomi kufungamana na wafanyabiashara na ‘kuiteka' siasa ndiyo chimbuko la kuongezeka kwa ufisadi nchini na pia ndiyo chimbuko la kuongezeka kwa pengo kati ya matajiri na masikini.

Ni katika kipindi hicho ambacho tumeshuhudia wingi wa wafanyabiashara wa Kihindi na Maburushi wakijiunga kwa wingi na CCM na kukubalika kama wafadhili wa chama; huku baadhi yao wakifikia hatua ya kugombea ubunge.

Lakini ni imani yangu kwamba hakuna Mhindi au Burushi hapa nchini anayeipenda CCM kwa dhati kiasi cha kutoa mwenyewe pesa zake mfukoni kuchangia chama hicho. Wala hakuna Wahindi au Maburushi waliojiingiza katika siasa kwa sababu tu wanapenda siasa au wanataka kuwahudumia wananchi kwa karibu; bali wote wanajiingiza ili kulinda biashara zao tu! Walioingia katika siasa ili kutumikia wananchi ni akina Amir Jamal ambao hatunao siku hizi.

Hivi sasa mfanyabiashara wa Kihindi au wa Ki-burushi akitoa pesa zake mfukoni kuisaidia CCM ni kwa sababu anatarajia huko mbele kuingiza kiasi kikubwa cha pesa isivyo halali kwa kukitumia chama hicho hicho alichokisaidia.

Kwa maneno mengine, Mhindi au Burushi anakupa kwa mkono wa kulia; lakini baadaye ‘atakuibia' na kurejesha alichokupa kupitia mkono wa kushoto. Tuliliona hilo (kwa mfano) katika ‘hadithi' ya Jeetu Patel na pesa za EPA.

Kwa hiyo, kwa mtazamo wangu, ni wafanyabiashara hao hao wakubwa waliopenyeza nchini dhana ya kutumia pesa kushinda uchaguzi kiasi cha kuifanya njia hiyo haramu ionekane ni ya kawaida si tu katika uchaguzi wa wabunge; bali hata wa urais. Nani (kwa mfano) hivi sasa anaweza kupinga kwamba sehemu ya mabilioni ya pesa za EPA yaliyochotwa na wafanyabiashara hao hayakutumbukizwa katika kampeni za urais za uchaguzi za CCM za mwaka 2005?

Ukweli ni kwamba kabla ya wafanyabiashara hao kujitosa katika siasa, kiwango cha matumizi ya pesa za rushwa na ufisadi mwingine katika chaguzi zetu kilikuwa kidogo, lakini walipoingia kwa wingi mwanzoni mwa miaka ya tisini, hali ilibadilika na kuwa ya kutisha kama tulivyoshuhudia katika chaguzi zetu mbili za mwisho.

Tumefika mahali ambako hivi sasa wengi wanaojitosa kugombea uongozi katika CCM ni wale wenye mapesa ya kuhonga, na wakishashinda uchaguzi kazi kubwa inayokuwa mbele yao ni kupanga namna ya kuyarejesha mapesa walioyatumia na kuongeza mengine – na njia ya mkato ni kujitosa katika ufisadi.

Wale wanaobahatika kupata nafasi za juu za uongozi baada ya kushinda ubunge hujitahidi mno kujiweka karibu na wafanyabiashara hao wa Kihindi au Kiburushi ambao ni wabunge wenzao ili "wafunzwe" dili za kuwatajirisha mapema kabla vipindi vyao vya uongozi havijaisha au kabla hawajang'olewa katika nafasi walizonazo.

Nikilitafakari jambo hili, ndivyo ninavyozidi kuamini kwamba ni wafanyabiashara hao waliofanikiwa kumshawishi Rais Mkapa kujitosa katika biashara angali Ikulu. Siamini kwamba Mkapa wa mwaka 1995 alikuwa akitamani kuwa milionea (mjasiriamali mkubwa); achilia mbali kufuata njia ya mkato aliyoifuata
kuupata utajiri huo.

Ninaweza kuapa kwamba haraka ya kuwa tajiri ambayo Mkapa aliionyesha miaka yake ya mwisho Ikulu, ina uhusiano na kuwa kwake karibu na baadhi ya wafanyabiashara hao waliojiunga na CCM na kupata uongozi (uwaziri, ubunge, ujumbe wa NEC na kadhalika).

Na kama ilivyokuwa kwa Wazimbabwe walioshindwa kumchachamalia Mugabe kungali mapema, nasi pia tumeshindwa kuichachamalia mapema CCM iache kuwakumbatia wafanyabiashara hao na kuwatosa wanyonge.

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alituonya zamani kabisa kuhusu suala hilo la Chama kuwasahau wakulima na wafanyakazi na badala yake kuwakumbatia matajiri katika hotuba yake aliyoitoa Oktoba 22, 1987 kwenye mkutano wa taifa wa CCM.

Alisema hivi: "Utajiri unaotokana na wizi wa mali ya umma na wizi wa fedha za kigeni na unyonyaji na uharamia wa aina mbalimbali, hautupunguzii umasikini wetu, bali unauongeza. Chama chetu hakiwezi kuwakubali matajiri wa aina hiyo na kikaendelea kuwa CCM, na wala wasitarajie kuwa wananchi watakikubali."

Lakini si Nyerere tu aliyeonyesha hofu ya matajiri hao kukivamia CCM; kwani hata Mkapa na Kikwete walizungumzia pia hofu hiyo katika hotuba zao ndefu za kwanza baada ya kushinda urais (1995 na 2005).

Tatizo ni kwamba ingawa wote wamezungumzia kukerwa na wingi wa matajiri hao katika CCM na matumizi makubwa ya pesa wakati wa uchaguzi, hakuna aliyekwenda mbali zaidi na kuidhibiti hali hiyo katika CCM. Si Mkapa na wala si Kikwete (angalau mpaka sasa hatujawaona wakifanya hivyo).

Na matokeo ya udhaifu huo si tu kushamiri kwa ufisadi katika chaguzi zetu lakini pia kila kona ya maisha na mienendo ya viongozi wetu. EPA, Kiwira, Buzwagi, Richmond ni mifano michache tu kati ya mingi iliyopo.

Kitu kibaya zaidi ni kwamba hali hiyo ya CCM kuwakumbatia matajiri imeifanya ajenda ya uongozi isiwe tena kuwasaidia wananchi wapambane na umasikini, bali ni kujitajirisha zaidi na zaidi; hata ikibidi kuiba pesa za wananchi hao hao masikini.

Kwa hakika, haiingii akilini kwa Serikali kumchangisha masikini wa Bariadi pesa za ujenzi wa madarasa wakati inaachia kina Jeetu Patel na wenzake kunyakua mabilioni ya umma katika BOT, pesa ambazo zingetosha kujenga madarasa hayo bila kulazimika kumchangisha masikini yeyote.

Kosa hilo la CCM la kuwakumbatia matajiri na kuwatosa wanyonge ndiyo chanzo cha viongozi wetu kuingiwa na kiwewe cha kuusaka utajiri kwa udi na uvumba, na ndiyo pia chimbuko la nchi yetu kuwa na viongozi wenye utajiri wa kiwango cha kutisha kama Waziri wa Miundo Mbinu aliyejiuzulu mwishoni mwa wiki, Andrew Chenge ambaye pamoja na umasikini wa watu wa jimbo lake la Bariadi bado anaziona dola milioni moja alizonazo katika akaunti ya nje ni ‘vijisenti' kidogo.

Kwa hakika, kauli ya Chenge unaweza tu kuifananisha na ile ya mke wa Mfalme Louis wa 16 wa Ufaransa, Marie Antoniette ambaye aliishi maisha ya kifahari na kushindwa kuona dhiki za Wafaransa wengine kiasi kwamba aliposikia watu wanalalamika kwa kukosa mikate akasema wapewe keki!

Na kama ilivyokuwa kwa Zimbabwe hatukifika hapa tulipo mara moja. Tulifika hatua kwa hatua. Kama ilivyokuwa kwa Wazimbabwe walioshindwa kumdhibiti mapema Mugabe na ZANU PF yake mpaka ‘kiama' kikaingia, nasi pia tulishindwa kuichachamalia CCM kuhusu ufisadi pale ilipostahili kuichachamalia, na sasa imejenga usugu.

Nasema hivyo kwa sababu tatizo la ufisadi, licha ya kuitikisa nchi, halijadiliwi kwa undani ndani ya vikao vya juu vya CCM au Serikali, na ndiyo maana hakuna hatua zozote kali zinazochukuliwa. Na kisingizio ni kwamba kufanya hivyo ni kuunufaisha upinzani.

Katika Zimbabwe wananchi wanagilibiwa kwamba kumdhibiti Mugabe ni kutoa ‘ushindi' kwa Uingereza na katika Tanzania nako tunagilibiwa kuwa kuwatimua mafisadi chamani na serikalini ni kuupa nguvu upinzani!

Ni shinikizo tu la wahisani, vyombo vya habari, vyama vya siasa vya upinzani na wabunge kadhaa wakiwemo wachache wa CCM kulikowafanya kina Lowassa, Karamagi, Msabaha na sasa Chenge, wajiuzulu; lakini si utashi au mapenzi ya chama tawala na serikali yake.

Unapokuwa na waziri anayetoka jimbo lenye masikini wengi kama Bariadi na anayeona dola milioni moja alizozipata kwa njia zinazodaiwa ni za kifisadi ni ‘vijesenti' na unapokuwa na Waziri anayediriki kusema kwamba wananchi wale majani lakini ndege ya rais inunuliwe, ujue hakika twaweza kuishia ilikoishia Zimbabwe.

Kwa kumalizia, Jaji Warioba, mwaka 2000, aliutaja ufisadi kama moja ya nyufa nne kubwa zinazoliangamiza taifa letu akiwa ameuweka katika nafasi ya tatu. Miaka minane baadaye nadiriki kuuweka ufisadi katika nafasi ya kwanza katika orodha ya nyufa zitakazosababisha anguko la nyumba yetu zisipozibwa. Tafakari.

Email: mbwambojohnson@yahoo.com
 
Back
Top Bottom