Nyerere katika macho ya profesa Ahmed Muhidin (raia mwema)

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,916
30,259
NYERERE KATIKA MACHO YA PROFESA AHMED MUHIDIN

Gazeti la Raia Mwema Machi 25 - 31, 2020 wamechapa makala ya Prof. Ahmed Muhidin akimzungumza Mwalimu Julius Nyerere.

PROF. AHMED MUHIDIN ANAMUELEZA MWALIMU NYERERE

Katika maisha yangu nimekutana na watu ambao kwa muda mchache sana wa mazungumzo sikuchukua muda mrefu kutambua kuwa mbele yangu nina kisima cha elimu kubwa na mimi kazi yangu ni kuchukua kata na kuanza kunywa.

Nikishamaliza kunywa nichukue maji yale nitilie udhu hapo mimi nitakuwa sina jingine ila kushukuru.

Miaka mingi imepita na hivi leo ninaponyanyua kalamu kuandika (ukweli ni kuwa siandiki kwa kalamu ni keyboard lakini hatuwezi kukitupa Kiswahili chetu) natazama nyuma nawaona upya watu hawa na wengi wao wameshatangulia mbele ya haki.

Kitu ninachokiona kwao ni unyofu wao kiasi mtu unaweza kusema kuwa ukiona mtu anajikweza na ana vishindo basi hakikisha ni debe tupu.

Hiyo ndiyo nembo yao kuu.

Namkumbuka Peter Colmore na Jim Bailey.

Kuwaeleza Wazungu hawa wawili inataka muda maalum kwani akili zao na ''intellect,'' zao si za kawaida.

Nimebahatika kuiona maktaba ya Peter Colmore nyumbani kwake Muthaiga, Nairobi na sikuona aibu nilimuuliza uso kwa macho ile hazina itakwenda wapi atakapofariki?

Colmore akanijibu akaniambia itakuwapo kwenye mikono salama kwa watu kuitumia.

Jim Bailey Collection kutoka gazeti lake la Drum iliyopo Johannesburg ipo na inafahamika.

Imekusanya mengi katika historia ya Afrika kuanzia miaka ya 1950.

Jim Bailey niliyemjua kupitia kwa Ally Sykes amenipa picha za Mwalimu Nyerere ambazo sikupata kuziona kabla.

Bailey ndiye aliyenipatia picha ya Sheikh Suleiman Takadir yuko juu ya jukwaa na Julius Nyerere miaka ya mwanzo ya TANU na picha ya Bi. Chiku bint Kisusa, Tatu bint Mzee na Bi. Titi Mohamed wanamsindikiza Mwalimu Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam safari ya kwanza UNO mwezi February, 1955.

Naogopa kumtaja Prof. Ali Mazrui kwani wala sikuhitaji kukutananae kujua kuwa alikuwa, ''mkali,'' ila tulipokutana siku moja Kampala Hilton nami nikamfuata kumsalimia na kumweleza kuwa mimi ni rafiki ya mwanafunzi wake Dr. Harith Ghassany aliyemsomesha Michigan, akanishika mkono tukae pembeni tuzungumze.

Kwa siku nilizokuwa na Prof. Mazrui katika mkutano nilimfaidi sana nikikiangalia kila kitu chake, mavazi yake, anavyozungumza, anavyosikiliza wengine wakizungumza nk.

Baada ya kuwa nimemsoma Prof. Mazrui kwa miaka yangu yote na baada ya kukutana na Prof. Mohamed Khalil Timamy ambae ndiye aliyenijulisha kwa Prof. Ahmed Muhidin na yeye kumsikia akizungumza, nimejaaliwa kuchungulia ndani ya wasomi hawa kutoka Mombasa.

Kitu kimoja ambacho kimejitokeza kwangu mara moja ni ule ujuzi wao wa kucheza na maneno.

Huenda labda haya yanatokana pia na ule ujuzi uliopo pwani wa lugha ya Kiswahili na uandishi wa mashairi kiasi kuwa haiwi tabu kwao kutengeneza maneno yanayopiga miungurumo ya radi hata kwa Kiingereza.

Nimekaa na Prof. Khalil nyumbani kwake tumebarizi ananieleza kuhusu ''paper,'' yake moja aliyoandika, ''The Nature of the Plundering Beast.''

Namsikiliza kisha najiuliza moyoni huyu ''Beast,'' ni nani kama vile simfahamu.

Nacheka najiuliza ''Beast,'' atajisikiaje atakaposoma paper hii?

''Beast,'' Kiswahili chake ni ''Nyang'au" na hii ikanikumbusha kipindi, ''Mazungumzo Baada ya Habari,'' Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) katika miaka ya 1970 wakati wa uhasama baina ya Kenya na Tanzania kipindi hiki akikiendesha Mkuregenzi mwenyewe wa RTD, Paul Sozigwa.

Kuna paper nyingine ya Prof. Khalil na iko huko huko kwa wanyama wakali, ''Africa in the Lions's Den.''

Bingwa wa kukoroga maneno ni Prof. Mazrui.
Mwaka wa 1967 Prof. Mazrui alikuja na neno, ''Tanzaphilia.''

Kufika hapa nikamwambia kuwa na yeye Prof. Khalil yumo.

Kalamu yake ni upanga mkali.

Mazrui aliwaeleza Wakenya nini aliamua pale alipoambiwa hawezi kukubaliwa kuzungumza kuhusu Demokrasia na Katiba Kenya katika ukumbi aliopangiwa labda abadilishe mada yake.

Huu ulikuwa wakati wa shinikizo kwa nchi za Kiafrika kuweka demokrasia na kuruhusu vyama vingi cha siasa.

Serikali ya Kenya ilikuwa katika hofu kubwa ukijaribu kumzuia Prof. Mazrui kuzungumza ndani ya ukumbi mashuhuri wa Islamic Centre labda ikiwa atabadili anuani ya mada yake.

Mazrui akawaeleza Wakenya waliokuja kumsikiliza kwenye ukumbi mwingine kuwa yeye kaamua kubadilisha ukumbi hakukubali kubadilisha mada.

Hii ni bahari kubwa hawa wasomi kutoka Mombasa ni wajukuu wa mshairi wa sifa Muyaka bin Haji na wamechukua ukurasa kutoka kweke.

Huu mukadama mrefu nimeuleta kwa makusudi ili utufikishe kwenye kituo tusimame tumsikilize Prof. Ahmed Muhidin alivyombadilishia Mwalimu maneno yake katika jina lake la uandishi la kupanga (pen name), ''Shija Msafiri,'' Prof. Muhidin akalibadili akamwita Mwalimu, ''Shujaa Msafiri.''

Siku hizo Mwalimu akiandika makala zake zikichapwa na Nationalist, gazeti la TANU ambalo Mhariri wake alikuwa Benjamin Mkapa.

Bila shaka mhariri na mwandishi wa makala walicheka waliposoma jina jipya la "Shujaa Msafiri."

Prof. Muhidin ni mwingi sana kupita kiasi.

Yeye ndiye aliyenigusia kuhusu uhusiano wa Mwalimu na Prof. Mazrui na kunieleza kuwa Mwalimu alikuwa na chumba chake pale nyumbani kwake Msasani ambacho funguo zake akikaa nazo mwenyewe kibindoni na chumba hiki haingii mtu mwingine ila wale wandani wake, yaani wale anaowapenda kama Prof. Muhidin.

Prof. Muhidin akaninong'oneza kuwa baada ya kutoka Ikulu Mwalimu alimuomba amsaidie kuandika historia ya maisha yake.

In Shaa Allah hiki ni kisa cha kujitegemea ikipatikana fursa tutakizungumza.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom