Siku ya leo nimeitumia kutazama maadhimisho ya Siku ya Nyerere jinsi yalivyoendelea huko Kigoma. Halaiki ya vijana haikusisimua mpaka Rais Kikwete alipofika, naye kama kawaida hakufika mapema.
Lakini baada ya kumalizika, nimejiuliza hivi kwa nini Serikali yetu imeamua kuadhimisha Tarehe 14 Oktoba kama ndiyo siku ya kumkumbuka Baba wa Taifa? Tarehe 14 Oktoba,1999 ndiyo siku Mwalimu alifariki akipata matibabu katika Hospitali ya St. Thomas, London.
Kwa Mama Maria Nyerere na watoto wake, Makongoro na Madaraka, wajukuu na kwa wote waliompenda na ambao wanajisikia wamepoteza kipenzi chao, leo ingekuwa siku ya kwenda Kanisani kusali, ili Mwenyezi Mungu aipokee roho yake. Leo ndiyo siku ambayo wangekwenda pale kaburini waweke maua ya kumkumbuka.
Lakini, lo leo ndiyo Watanzania baada ya gwaride na halaiki ya kitaifa, wanamiminika katika nyumba za starehe, kunywa, kufurahi na kucheza nyimbo za kizazi kipya!!!!!!.
Ningekuwa mshauri wa Serikali ningependekeza ile siku ambayo familia ya Mwalimu ilikuwa ikiadhimisha kuzaliwa kwake, iwe ndiyo hiyo na sisi Watanzania tunafarahia na kumshukuru Mungu kwamba Baba wa Taifa letu alizaliwa. Tuwaulize familia ya Mwalimu, watuambie ni siku gani.
Mataifa mengi huadhimisha "Founders' Day" kama ni ile ama Mkombozi wao alizaliwa, au siku aliyotiwa mbaroni kutokana na kuongoza harakati za ukombozi na kupinga utawala dhalimu wa nchi yake au utawala wa kikoloni. Sijapata kusikia nchi inaadhimisha siku aliofariki "hero" wao, isipokuwa hii ya kwetu.
Napendekeza Serikali ijayo, itafakari suala hili na kuamua kiustaarabu. Hii haimaanishi kwamba tarehe 14 Oktoba isahaulike. Ikumbukwe ni siku ya huzuni, tulipompoteza Baba wa Taifa. Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi. Amina.