Nyerere alivyoling'oa baraza dhaifu la Mwinyi

Shebbydo

JF-Expert Member
Feb 12, 2015
1,174
1,937
KUITWA Ikulu enzi za utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuliweza kusababisha aliyeitwa kukosa usingizi usiku kucha. Enzi hizo Ikulu iliheshimika mithili ya mahali “Patakatifu” kwa mtu kuvua viatu kabla ya kuingia kuitika wito.

Na ukishaingia, kutazamana ana kwa ana na Mwalimu, macho yake yasiyo na doa la dhambi, kauli zake zisizo na matege kwa kila neno kubeba hoja na tafsiri nzito, tena kwa msisitizo kuweza kukujenga au kukubomoa, ungeweza kujikuta ukijibu swali ambalo hukuulizwa.

Na pale mambo yalipoisha kwa aliyeitwa, ama ilikuwa ni kicheko cha furaha na kupumua kwa tuzo na pongezi kwa utendaji mwema; au kutoka kichwa chini, moyo ukilia na kujuta kwa kukiuka dhamana kwa Taifa na umma ukaridhika kwa kipigo hicho pasipo shaka yoyote.

Mwalimu alikuwa hamchukulii hatua mtu kwa kubahatisha; alijiridhisha kwanza na kile kinachosemwa au kupendekezwa kabla ya kuchukua uamuzi; mfumo wa inteligensia yake ulifanya kazi nzuri. Lakini kutokana na mambo kufanyika ki-shaghalabaghala baada ya Mwalimu, ni kusema kwamba idara makini ya Usalama wa Taifa iliondoka na Mwalimu.

Tofauti na kuitwa Ikulu kikazi enzi hizo, mwaliko kwenye chakula cha jioni lilikuwa jambo la faraja; mazungumzo yalikuwa ya kufurahisha, yenye “michapo” tele kukufanya ufarijike lakini bado mwenye wajibu kwa nchi yako, na hasa katika ujenzi wa Taifa lenye watu wenye usawa. Mwalimu alichukia starehe zisizozalisha mali – thamani. Leo, kama Mwalimu angekuwa hai Ikulu, nina shaka kama angeweza kumwalika Msanii wa “Bongo Fleva”, Diamond Platnum, au Miss Tanzania, akamwacha Mfugaji Bora wa Kiteto.

Nakumbuka enzi hizo, Mwalimu aliagiza kila waziri awe na asome kitabu cha Mchumi – Kilimo wa Kifaransa, Rene Dumont, “False Start in Africa” (Afrika Inakwenda Kombo), ili kujua chimbuko la umasikini wa Mwafrika na vihunzi mbele katika kufikia maendeleo ya kweli.

Leo, hakuna anayejishughulisha na mambo hayo, kazi pekee ni kuongoza harakati za kuingia au kubakia madarakani, kuanzia kumalizika kwa uchaguzi mmoja hadi uchaguzi unaofuata. Chama cha siasa [tawala] ambacho enzi hizo kazi yake ilikuwa ya kuwasemea watu, kimetelekeza jukumu hilo na kuwa chama kwa ajili ya chaguzi za kisiasa tu, kama tutakavyoona hivi punde katika makala haya, hususani, kuhusu ugomvi wa Mwalimu na Rais Mwinyi kufikia Baraza la Mawaziri kung’olewa.

Mwalimu alifanikiwa kushikilia utaratibu mzuri wa kushtukiza na kwa wakati mwafaka, katika kuteua au kubadili viongozi na Baraza la Mawaziri kwa ufanisi mkubwa. Sifa zimwendee Msaidizi binafsi wa Mwalimu, Mama Joan Wickens, na baadaye Mzee Joseph Butiku, kwa ushauri wao makini uliomwezesha Mwalimu kuongoza Ikulu kwa ufanisi, tija na heshima kubwa.

Nakumbuka sakata la uteuzi wa Waziri Mkuu Aprili 1984, kufuatia kifo cha Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine, pale Mwalimu alipowashangaza akina “Thomas Mchunguliaji”. Awali, minong’ono ya uteuzi iliwaelekea aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, hayati Brigedia [baadaye Meja Jenerali] Muhidin Kimario; aliyekuwa Waziri wa Madini na Nishati, hayati Paul Bomani; na aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano, Ujenzi na Uchukuzi, John Samwel Malecela.

Kimario na Malecela walipewa nafasi kubwa na wengi; lakini Malecela alifahamika zaidi kutokana na utumishi wa muda mrefu wa miaka 14 kama Waziri Serikalini na katika Jumuiya ya Afrika, ikilinganishwa na Kimario ambaye alikuwa ndiyo mwaka mmoja tu amehamia kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda Wizara ya Ulinzi.

Hata hivyo, miezi michache kabla ya mchakato huo, mng’aro wa nyota ya Malecela ulikuwa umeingia dosari baada ya kutoa tamko hasidi na kwa kiburi kwa Watanzania kwamba, wale waliolalamikia ufanisi duni wa Shirika la Reli nchini lililokuwa chini ya Wizara yake “waende kuzimu”.

Kauli hiyo ya kudharau umma, licha ya kuzua gumzo na ghadhabu miongoni mwa Watanzania, ilimchukiza Mwalimu pia. Mwalimu alichukia uongozi wa mabavu, lugha chafu na dharau kwa umma. Alisema, moja ya kazi za viongozi ni kuwaelimisha wananchi juu ya jambo tena na tena hadi waelewe, badala ya kutoa majibu ya mkato na ya dharau.

Kwa hilo, Malecela alikuwa amejijeruhi, na nyota ya Naibu wake, Henry Mnyashi Limihagati ilianza kung’ara taratibu kuweza kumshitua aombe radhi, lakini hakufanya hivyo.

Waswahili husema mkasa huzaa mkasa: pengine kilichomponza zaidi Malecela ni kuvujishwa kwa siri na mmoja wa wanandani wake katika familia, kwamba alikaribia kuukwaa Uwaziri Mkuu bila ya shaka yoyote. Nyerere akanusa upepo, akabadili karata, na hivyo orodha ya watarajiwa.

Mwalimu alimteua Waziri wa Mambo ya Nje, Dakta Salim Ahmed Salim kuwa Waziri Mkuu, na kumrejesha Benjamini William Mkapa Wizara ya ya Mambo ya Nje. Watanzania hawakujutia uteuzi wa Dakta Salim ambaye jina lake bado linang’ara gizani hadi leo.

Kung’atuka kwa Mwalimu Urais mwaka 1985 kulimweka madarakani Ali Hassan Mwinyi na kumwona Joseph Sinde Warioba akikamata nafasi ya Waziri Mkuu. Mwinyi, tofauti na mtangulizi wake ambaye alishika nafasi zote mbili – Urais na Uenyekiti wa Chama tawala [CCM], alikuwa Rais tu ambapo Uenyekiti wa Chama ulibakia kwa Nyerere kwa muda hadi alipomaliza kipindi cha kutumikia nafasi hiyo.

Kilikuwa kipindi kigumu mno kwa wote wawili; Mwinyi, mwenye kushikilia dola kwa mujibu wa Katiba ya nchi kwa tiketi ya Chama; na Mwalimu, kama Mwenyekiti wa Chama tawala ndani ya mfumo wa Chama kimoja, lakini asiye na mamlaka ya Katba ya nchi.

Ilikuwa wakati mgumu pia kwa Warioba ambaye, kama Waziri Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Serikali, alipashwa kuzingatia Katiba na maelekezo ya Rais bila kujali kwamba yeye [Warioba] alikuwa mpwa wa Mwalimu kiukoo. Isitoshe, Mwinyi hakuwa mtu wa kuchukulia kwa uzito mambo ya kiutawala hata akapewa jina la “Mzee Ruksa”, kwa maana ya “yote sawa tu” bora liende.

Hatimaye siku ikawadia kwa wawili hao, Nyerere na Mwinyi, kupimana ubavu. Tatizo lilianza na Mwalimu kuona kwamba sera zake za Usoshalisti alizoziasisi, zilikuwa hazitekelezwi ipasavyo na Serikali ya Mwinyi, licha ya Mwinyi na Warioba kutoonesha kupingana wazi wazi na chama, ishara ambayo Mwalimu aliitafsiri kama “mgomo baridi”.

Ukweli, ukimya wa jiwe wa Mwinyi na Warioba walioonesha wakati wakimsikiliza Mwalimu ndani ya vikao vya Kamati Kuu [CC] na Halmashauri Kuu [NEC] ya Chama akiishambulia Serikali, ulitafsiriwa kama uamuzi wa makusudi wa kutotaka kuingizwa katika malumbano waliyojua wasingeshinda, hatua ambayo iliwaudhi wajumbe wa NEC.

Mashambulizi ya Mwalimu kwa serikali kupitia hotuba zake nyingi, yalikuwa ni juu ya uchumi wa nchi, na hasa juu ya uhusiano wa Serikali na Shirika la Fedha la Kimataifa [IMF] na ukosefu wa dira kwa upande wa Baraza la Mawaziri juu ya nini kifanyike wakati wa kujadiliana na IMF na Benki ya Dunia [WB], Mashirika yanayofahamika kunyonya na kudidimiza uchumi wa nchi changa.

Baadhi ya mambo ambayo hayakumfurahisha Mwalimu, ni pamoja na kuzikwa kwa Azimio la Arusha kwa koleo la Azimio la Zanzibar na ubinafsishaji usiojali, hata akaonya akisema, “msipokuwa makini mtabinafsisha hata magereza”

Lingine alilopigia kelele Mwalimu, ni udhaifu wa uongozi katika kusimamia maadili ya Taifa na uwajibikaji wa viongozi kwa nafasi zao na kwa wananchi, akaonya akisema; “Ikulu ni mahali patakatifu; sio pango la wevi na wanyang’anyi”, kwa maana kwamba mhimili wa nchi ulikuwa umeingiliwa na dumuzi wa ufisadi na kutowajibika kwa kulemazwa na dhana ya “Ruksa” na kwa kila mtu kuishi kwa ukali wa meno yake.

Waziri Mkuu Warioba alijitahidi kadri alivyoweza kumshauri bosi wake juu ya hatari ya nchi kufungua mlango kwa IMF na WB hadi bawaba ya mwisho; lakini alinyamazishwa kwa kuambiwa aache kuleta “maagizo kutoka Butiama kwenye utawala wa nchi”.

Na pale NEC ilipokutana mjini Dodoma, Februari 7 – 12, 1990, ilikuwa na agenda tatu tu; muhimu kati ya zote ilikuwa juu ya “rushwa” ambayo machoni mwa NEC lilikuwa tatizo lililopashwa kukomeshwa hima kama nchi ilitaka kuona maendeleo, demokrasia na malengo mengine ya Taifa yakifanikiwa.

Miaka miwili kabla ya hapo, Tume ilikuwa imeundwa kukusanya ushahidi juu ya rushwa na taarifa iliyotolewa kwa wajumbe wa NEC ilitia uchungu.

Wakati wa mjadala, wajumbe waliilaumu serikali kwa kunyamazia rushwa; ambapo mjumbe mmoja [jina tunalo] alitaka Mawaziri wote, Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya na Wajumbe wa Sekretarieti, Makatibu wote wa Mikoa na Wilaya, wajiuzulu ili kuwapa nafasi Rais na Mwenyekiti wa Chama wateue wengine wenye maadili na tabia njema isiyoweza kutiliwa shaka.

Hata hivyo, mjumbe huyo alizomewa na wenzake akituhumiwa kujilimbikizia mali za kutosha kutostahili kutoa pendekezo kama hilo.

Taarifa ya Tume ilitaja taasisi 12 zilizokithiri kwa rushwa; miongoni mwa hizo zilikuwa Wizara za Afya, Mambo ya Ndani, Sheria na Wizara ya Ardhi.

Ni kwa sababu hii, Mwenyekiti Nyerere alitaka Mawaziri wenye dhamana ya Wizara hizo – Mambo ya Ndani [Meja Jenerali Kimario], Afya [Aron Chiduo] na Sheria [Damian Lubuva], waitwe kwenye Kamati kuu, waelezee hali ya mambo katika wizara zao na vipi walitarajia kukomesha rushwa.

Lubuva, alisoma mapema alama za nyakati, akaandika barua sawia kwa Waziri Mkuu Warioba ya kujiuzulu, badala ya kukubali kile alichokiona kuwa ni kudhalilishwa kusikostahili. Wakati huo huo, Waziri Mkuu Warioba, naye alikuwa amekabidhi barua kwa Rais ya kujiuzulu.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Kimario, yeye alikuwa tayari kukabiliana na Kamati Kuu ya Chama kwa minyukano, akiapa kuwa kile ambacho angekisema, kingemwaibisha na kumtahayarisha kila mtu.
Agenda nyingine kwenye NEC ilikuwa Rasimu ya mwisho ya Uwekezaji [Investment Code] ambapo serikali ililaumiwa kwa kutozingatia maagizo ya Mwenyekiti wa Chama kwa niaba ya NEC, ya kufanyia marekebisho Rasimu ya Kwanza ili kutoa kipaumbele kwa wazawa badala ya wawekezaji wa kigeni. Rasimu nzima ilitupiliwa mbali. Kwa hili na kwa serikali kutotekeleza maagizo ya chama, Serikali iliwajibishwa.
Na pale Rais Mwinyi alipoitisha Baraza lake la Mawaziri, Machi 12, 1990; nao wakafika kizembezembe na “ki-ruksa” walivyozoea bila kuhisi kitu, hotuba yake kwao safari hii ilikuwa fupi na ya kukanganya; iliishia kwa kuwataka wote wajiuzulu.
Ukweli hawakuhitajika kuandika barua za kujiuzulu kwa sababu tayari walikuwa wamekwishaandikiwa barua za kufuta uteuzi wao.
Swali, ni kwa nini Baraza zima la Mawaziri lilitakiwa kujiuzulu wakati ni mawaziri wanne tu ndiyo waliobainika wizara zao kuongoza kwa rushwa?. Na kwa nini iwe hivyo wakati ilibakia miezi minne tu kufikia Uchaguzi Mkuu wa 1990?
Majibu ya maswali haya yalijengeka kwenye siasa tete za nchini wakati huo. Ni kwamba, kuruhusu Lubuva kujiuzulu ili akatae wito wa Kamati Kuu, kulikuwa hakukubaliki kwa kiongozi kujiponya dhambi kwa njia hiyo; kama tu ambavyo ilikuwa haikubaliki kwa Meja Jenerali Kimario kuruhusiwa kutaka kunyukana na chama.
Kwa hiyo, kwa kuvunja Baraza lote la Mawaziri, pasingekuwa na waziri wa kujiuzulu au kukidhalilisha chama, bali dawa ilikuwa ni kunyukwa katika ujumla wao.
Machi 15, 1990; Rais Mwinyi alitangaza Baraza jipya la Mawaziri na kumwona Warioba akirejea ulingoni kama Waziri Mkuu kwa mara nyingine kwa mshangao wa wengi, lakini si kwamba Warioba alikuwa “fisadi”, bali kwa sababu wengi walitarajia Mwinyi angeleta sura mpya zote.
Uadilifu wa Warioba ulikuwa hauhojiki kiasi cha Mwinyi kukosa Waziri Mkuu mbadala, licha ya kulalama kwamba Warioba alikuwa akileta“maagizo kutoka Butiama” dhidi ya baadhi ya sera za serikali.
Lakini kama ilivyotarajiwa, Mawaziri wa Mambo ya Ndani, Afya na Sheria na wengine wanne: Waziri wa muda mrefu, Al-Noor Kassum [Nishati na Madini], Arcado Ntagazwa [Ardhi, Mali Asili na Utalii], Christian Kisanji [Maji] na mama Getrude Mongella [asiye na Wizara Maalum], hawakuwamo katika orodha ya uteuzi mpya.
Shinikizo la Mwalimu lilishinda
Nyuso tatu mpya zilikuwa ni Nalaila Kiula [Mambo ya Ndani], Charles Kabeho [Afya] na Marcel Komanya [Ardhi]. Waliobaki walibadilishwa Wizara, huku Cleopa Msuya akitolewa Wizara nzito ya Fedha, kwenda Wizara ya Biashara na Viwanda.
Akitangaza mabadiliko hayo, Rais Mwinyi, kana kwamba alikuwa ameamshwa na Mwalimu kutoka usingizini kuhusu yale yaliyokuwa yakiikabili nchi, aliliambia Taifa kwamba, alifanya hivyo ili kuliwezesha Taifa kukabiliana na matatizo ya Uchumi, Uwajibikaji Duni na Rushwa; lakini licha ya mabadiliko hayo, uchumi uliendelea kuporomoka, uwajibikaji kuyoyoma na rushwa kuitafuna nchi kwa ari mpya na kasi ya kutisha.
Kwa miaka iliyofuata, kuendelea kwa udhaifu katika utendaji wa Chama na Serikali na kutowajibika, kulimfanya Mwalimu afikirie zaidi dhidi ya ukuu wa Chama katika kudhibiti hali kwa kutangaza nia yake kuona demokrasia pana zaidi kwa mfumo wa kugawana madaraka [power sharing] kwa njia ya vyama vingi vya siasa akisema, “Chama madarakani ambacho kinapashwa kuwasemea watu, kimetelekeza wajibu wake na kugeuka chama cha kampeni za uchaguzi tu”.
Akaongeza kusema: “ Chama kinapotelekeza madhumuni ya kuwapo kwake, hicho si chama tena,bali ni gofu la kuficha wevi wachache dhidi ya wengi kwa kero kubwa kwa jamii; na inapokuwa hivyo, mimi si mwenzenu tena; wala chama si mama yangu, mama yangu yuko kule Butiama….”
Misingi ya utawala bora iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ilianza kubomolewa tangu Serikali ya Awamu ya Pili. Ni nani kati ya wanaojifaragua leo kudai kuyatetea na kuyalinda mema yote ya Mwalimu;yuko tayari kuikarabati na kuiimarisha misingi hiyo kwa manufaa ya Taifa?
 
Baadhi ya mambo ambayo hayakumfurahisha Mwalimu, ni pamoja na kuzikwa kwa Azimio la Arusha kwa koleo la Azimio la Zanzibar na ubinafsishaji usiojali, hata akaonya akisema, “msipokuwa makini mtabinafsisha hata magereza”.

Mwalimu angekuwa hai asingekuwa ikulu
 
Back
Top Bottom