Nyakati za dhiki na dhima aliyonayo Shein | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nyakati za dhiki na dhima aliyonayo Shein

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Kakke, Mar 2, 2012.

 1. Kakke

  Kakke JF-Expert Member

  #1
  Mar 2, 2012
  Joined: Dec 4, 2010
  Messages: 1,797
  Likes Received: 389
  Trophy Points: 180
  Posted on March 2, 2012 by zanzibaryetu

  Na Ahmed Rajab

  RAIS Ali Mohamed Shein ana dhamana kubwa kushinda kiongozi yeyote mwengine wa Zanzibar, tangu nchi hiyo iungane na Tanganyika kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dhamana yake ni kubwa hivyo kwa sababu Wazanzibari wenzake wanasubiri kwa hamu matokeo ya mchakato wa kuipatia Jamhuri ya Muungano Katiba mpya.

  Imepangwa kwamba kazi hiyo imalizwe Aprili, mwaka 2014 wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Jamhuri ya Muungano. Miaka 50 ni muda mwingi, uhai wa mtu wa kuzaa na kujukuu ingawa kwa kipimo cha kihistoria huo ni muda mfupi sana kama wa kufumba na kufumbua macho.

  Shein ana bahati. Bahati yake ni kwamba hakabiliwi na upinzani licha ya shida za kiuchumi na za kijamii zilizozagaa huko Visiwani. Kama wapo wenye kumpikia majungu chini kwa chini basi hawathubutu kujitokeza. Hali iliyopo Visiwani haiwaruhusu.

  Shein anaiongoza nchi wakati ambapo Wazanzibari wameungana baada ya kuziyayusha chuki zao za kisiasa na kukubaliana, Novemba mwaka 2010 kuwa na suluhu ya kitaifa kwa Maridhiano ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
  Maridhiano hayo ndiyo yaliyosababisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuibuka kwa ile iitwayo Ajenda ya Zanzibar. Na ni umoja huo uliosababisha pasiwepo upinzani dhidi ya Shein, si wa dhahiri si wa shahiri.
  Hiyo ni bahati kubwa kwa Shein na inampa fursa adhimu ya kuongoza taifa lilioungana. Lakini pia ni changamoto kwake yeye na serikali yake. Ni changamoto kwa sababu Wazanzibari kwa pamoja wanataraji mengi kutoka kwake. Awali ya yote wanamtaka awe na msimamo ulio imara wa kumwezesha kuyatetea vilivyo maslahi ya Zanzibar.

  Ni matumaini yao kwamba hatoteteleka wala kuyumba-yumba atapohitajika kuwasilisha na kuyasimamia maoni yao kuhusu mustakbali wa nchi yao na hususan suala la iwapo Muungano uendelee kama ulivyo au la. Kwa ufupi, tegemeo lao ni kwamba hatowaendea kinyume kwa kutoyapigania matilaba yao.

  Wengi wa Wazanzibari wanataraji kwamba mfumo wa Muungano utaochomoza baada ya kumalizika hiyo shughuli ya kutunga Katiba utakuwa tofauti kabisa na ule wa sasa wa serikali mbili zisizo na mamlaka sawa wala haki zilizo sawa.

  Siku hizi Wazanzibari wana kiu cha kutamani ya kale wanapoukumbuka ufanisi waliokuwa nao wakati wa kupigania uhuru kutoka kwa Waingereza. Juu ya migawanyiko ya kisiasa ya zama hizo hali zao za maisha kwa jumla zilikuwa za juu na uchumi wa nchi yao haukuathiriwa na mchafuko wa kisiasa.
  Hizo zilikuwa nyakati za maisha ya raha na furaha kinyume na sasa ambapo pameingia maisha ya dhiki.
  Sisemi kwamba ufanisi huo ulikuwa timilifu au kwamba haukuwa na kasoro, la. Nisemacho ni kwamba licha ya taksiri zake - na zilikuwa nyingi -dosari hizo hazikuufanya uchumi wa Zanzibar uzorote. Nchi ilikuwa na neema, watu wakipata ajira, sekta ya kilimo ilistawi na pakipatikana vyakula vya kila aina tena kwa bei rahisi.

  Siku hizo angalau kila Mzanzibari akimudu kula vyakula mbalimbali si kama sasa ambapo waliobahatika siku nenda siku rudi wanakula ugali na maharagwe mara tatu kwa siku. Huo ndio mlo wa wengi wa Wazanzibari siku hizi na wapo baadhi yao wasiobahatika hata kuumudu mlo huo.

  Ingawa utawala wa ukoloni Wakiingereza ulikuwa wa kimabavu, ulikuwa hivyo dhidi ya wale waliokuwa wakiupinga na waliokuwa wakidai uhuru. Wananchi kwa jumla walikuwa na uhuru wao wa kiraia ingawa hawakuwa na uwakilishi wa kisiasa. Zanzibar ikitawaliwa moja kwa moja na Uingereza.

  Kinyume na wanavyofikiri wengi tangu mwaka 1890 masultani walikalia kiti cha enzi huko Zanzibar lakini hawakuwa na nguvu za kutawala na kuendesha nchi. Mabwana waliokuwa na amri walikuwa wakoloni Wakiingereza na si masultani. Wao walikuwa wanyenyekevu kwa Waingereza.

  Hii leo Wazanzibari wana mapato ya kujikimu tu, wengi wao hususan vijana hawana ajira. Kuna mfumuko mkubwa wa bei na mapato, bei za vyakula ni za kuruka, huduma za lazima ni duni kama vile za afya, maji, umeme na kumekosekana mfumo wa kuchimba mitaro ya kuchukua maji machafu.

  Zama hizo zilizopita, mfumo wa elimu Visiwani ulikuwa wa kupigiwa mfano. Mwaka 1961 Zanzibar ilikuwa na wahitimu wengi wa chuo kikuu waliopata digrii au shahada kulinganishwa na wale wa Tanganyika.

  Huo ndio ukweli uliokuwepo. Siku hizo Zanzibar ikitajwa kuwa na nafasi ya pili baada ya Afrika ya Kusini katika mizani ya maendeleo miongoni mwa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara. Si leo.

  Mfumo wa leo wa elimu hauwezi kamwe kufananishwa na ule wa kale. Kwa sababu ya mfumo wa elimu uliopo sasa ni muhali kupata wataalamu wataoiwezesha serikali ya Zanzibar iendeshwe kistadi na ipasavyo bila ya ulaji rushwa au kupendeleana wakati wa kuajiri watu katika kazi za serikalini.

  Badala yake tunaona kwamba watu wasio na elimu ya kutosha au ujuzi na uzoefu unaohitajika wanapewa madaraka makubwa serikalini ama kwa sababu za kisiasa au za kupendeleana. Hawa ndio wenye kuhodhi nyadhifa nyeti serikalini na kushika kwao nyadhifa hizo kunaleta madhara makubwa kwa jamii kwani wanakuwa wanazitumia vibaya rasilmali za nchi na wanapoteza fursa ya kuziinua hali za maisha Visiwani kwa kuwapatia watoto elimu bora na kuwapatia wananchi kwa jumla huduma zote za lazima.

  Ingawa hii leo Zanzibar kuna umoja wa kitaifa pamoja na suluhu na hali tulivu ya kisiasa uchumi wake si wa kuridhisha. Isitoshe huduma zake za kijamii hazikidhi mahitaji ya kila Mzanzibari hasa wale walio maskini na wasiojiweza ambao ndio walio wengi Visiwani.
  Tumekumbushana kidogo hali ya mambo ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi na Muungano na Tanganyika na tukagusia hali ilivyo sasa. Na hatuna budi kusema kwamba hali iliyopo sasa hairidhishi hata kidogo na ni lazima ibadilishwe ili Zanzibar iweze tena kuwa nchi ya neema.

  Kwa bahati nzuri, mchakato utaopelekea kupatikana kwa katiba mpya unawapa Wazanzibari na viongozi wao fursa ya kuweza kujipatia ukombozi na maendeleo kwa kuachana na hali ya sasa ilivyo.

  Kwanza ili Zanzibar iweze kuendelea na kujipatia mamlaka yake ndani ya Muungano na Tanganyika utaokuwa wa Mkataba na si wa Katiba, kuna mambo mawili yanayohitaji kuzingatiwa na kutanzuliwa. La kwanza linahusika na hali ya ndani Visiwani kwenyewe na la pili linahusika na uhusiano wa baadaye kati ya Zanzibar na jirani wake wa kidugu Tanganyika.

  Hali ya ndani inatokana na kuzuka kwa utawala wa kisiasa wa kinasaba (political dynasty). Hali hiyo nayo ni chanzo cha kuwako utawala mbovu. Wanaonufaika katika mazingira hayo ni hao watawala wa kinasaba na walio wao pamoja na wafanyabiashara wachache walio matajiri sana na wakubwa wengine. Wao ndio wenye kustarehe ilhali wengi wa wananchi wanahangaika kila uchao kutafuta chakula na uwezo wa kulipia huduma za afya au wa kuwasomesha watoto wao.

  Mustakbali wa Zanzibar, ndani au nje ya Muungano na jirani yake Tanganyika, utaamuliwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo. Inavyoonyesha ni kuwa Wazanzibari hawatokubali zoezi la utungwaji wa Katiba mpya lifanyiwe uzembe na kuachiwa lipindukie mwaka 2014 kwa sababu wana hamu kubwa ya kuona kwamba serikali yao inarejeshewa mamlaka yake yote ya kisiasa, kiuchumi na ya kijamii kutoka serikali ya Muungano.

  Wao wanaamini kwamba kurejeshewa mamlaka na madaraka hayo kutawawezesha kuufyeka au angalau kuupunguza kwa kiwango kikubwa umaskini uliopo sasa na kujipatia maendeleo na ufanisi.

  Rais Shein na viongozi wenzake kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa wanayaelewa hayo kwa sababu kila siku Wazanzibari wa itikadi tofauti za kisiasa, kuanzia wananchi wa kawaida hadi viongozi wao, wanashauriana na kujadiliana kuhusu mustakbali wa nchi yao.

  Suala kuu linalowashughulisha nilile la kuamua ni Zanzibar aina gani waitakayo. Ni muhimu kwamba Shein ahakikishe ya kuwa Wazanzibari wanaitumia kikamilifu haki yao ya kidemokrasi ya kushauriana na kulijadili vilivyo suala la Katiba bila ya kuwekewa mipaka na hususan haja ya kuujadili Muungano kwa ukamilifu bila ya woga.

  Hilo ndilo jukumu kubwa alilonalo Shein na wenzake. Wazanzibari wenzao wameshikamana na hadi sasa wako nyuma yao lakini wanachotaka hasa ni kuwaona viongozi wao wakisema kwa kauli moja na kuitetea Ajenda ya Zanzibar. Wanasema kuwa Shein na wenzake ndio ambao ama watainusuru au wataitosa nchi yao. Hilo si jukumu dogo.

  CHANZO: RAIA MWEMA
   
Loading...