Nipe Rambirambi zangu!

Robert Heriel Mtibeli

Platinum Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
40,330
Reaction score
93,427
NIPE RAMBIRAMBI ZANGU!

Anaandika, Robert Heriel
Taikon wa Fasihi,
Maandishi ya Robert Heriel Kwa Lugha ya Kiswahili.

Andiko Huru;
(Nachukua kiberiti na mshumaa, nawasha mshumaa, kunakuwa na Nuru hafifuf ya mshumaa, kisha naenda kuchukua Daftari alafu naanza kuandika)

Sitaki maua, maua mpelekee nyuki au Roma mkatoliki.
Mimi ni Farasi wa vita, kisiki kijukuu cha mpingo sing'oleki, sichomoki na ukinichoma sichomeki. Unanijua, unanitambua na kunifahamu Mimi ni Dudu liumalo; nang'ata bila kupuliza, nameza bila kumung'unya, Janalaidana mwenye sanaa ya Kifo.

Ni kweli Kabisa niliondoka, ukanipa mikono yako tukaagana, lakini moyo wangu haukukuacha popote nilipoenda ulikuwa pamoja nawe, kama Mwili na kivuli changu, nilipoenda ulienda pamoja nami, nilipokaa ulikaa pamoja nami.
Tazama macho yako, yanaona nini?
Tazama Mikono yako, imeshika nini?
Macho yako yaliona upepo! Na mikono yako ikaushika na kuuzuia usiende wala usirudi. Ili nisizipate taarifa Huku nilipo, nawe usizipate taarifa huku ulipo.

Ni kwanini uliuona upepo? Na uliwezaje kuushika upepo Kwa viganja vyako viwili?
Farasi mwendakasi ndiye Farasi wa vita, lakini vipi kuhusu mpanda Farasi?

Nikaenda ukadhani nisingerudi, mbona tulikubaliana na Kwa ahadi nilisema ningerejea. Nchi za mbali nilienda, kutafuta uzuri WA Maisha.
Nikafika huko nilikokwenda wala sikujua ninaenda wapi, lakini nilipofika nikaambiwa na wenyeji kuwa nilipofika hakuna huo uzuri wa Maisha. Nchi Ile ilikuwa ya ajabu Sana,
Ajabu ya kwanza, ilikuwa Sura za Wanawake wake, walikuwa Wanawake wenye nyuso za kuangusha ngome za mioyo ya wanaume, zilikuwa Sura zenye kuvutia kwa nguvu kama Kani ya Gravitational force. Kila utakapowatazama Wanawake wale ungevutwa Kwa nguvu kwao, wala usingekuwa na uwezo wa kujizuia.
Katika Ajabu kubwa hiyo zilikuwepo ajabu ndogondogo ambazo kama nitazisema itanichukua siku Saba kwani zile ajabu zilikuwa Saba kama siku za majuma.

Huko nilijionea Siri zilizofichwa katika Nyuso za Wanawake, hiyo nayo ilikuwa sehemu ya ajabu. Labda ungefikiri ni aibu na fumbo lake, labda ungedhani tabasamu na mitego yake. Lakini Mimi sikusudii kueleza hayo.
Mimi ninachotaka ni haki yangu, Haki? Ndio Haki yangu I wapi?

Nisikilize vizuri, ajabu ya pili katika Nchi Ile ilikuwa, Lugha ya Watu wake, sikuwahi kufikiri kama kuna Lugha kama Ile. Ilikuwa Lugha ya kimaajabu, bila kusema walisema na kuelewana, bila kufanya yalifanyika yakatokea, uzuri WA Maisha ungepatikana kama ningeijua Lugha Yao, lakini Lugha yao ilikuwa kama msimbo wa Siri uluounganisha moja Kwa moja na nafsi ya kila mmoja wao. Labda walikuwa kama wanyama, wasioongea lakini wanaelewana. Ajabu hii ilinikatisha tamaa, kwani sikuwaelewa, nao hawakunielewa Kwa sababu ati Lugha Yao na yangu zilipishana Kwa maelfu na maelfu ya utofauti.

Ajabu ya mwisho ya nchi Ile ilikuwa, Tabia ya nchi, sijui kama ilikuwa baridi au ni joto, manyunyu au Mvua, jangwa au msituni. Tabia ya nchi ulitegemeana na vile utakavyofikiria, ukifikiri ujangwa Tabia ya nchi inakuwa jangwa, halikadhalika na tabia zingine kadiri ya fikra zako. Hiyo ilinitatiza Sana, sio Mimi tuu Bali hata wenyeji wa nchi Ile. Kwani Wakulima wakiwaza Mvua hapohapo inanyesha lakini Wakati huohuo Wafanyabiashara wakichukia Mvua inaacha Hali iliyopolekea mvurugano mkali WA shughuli za kiuchumi na kijamii pamoja na tabia ya nchi. Hii ilisababisha nchi Ile kukosa Maendeleo Kutokana na wenyeji wake kushindwa kukaa pamoja na kujadiliana kipi kianze Kwa wakati gani na kipi kifuate ili kutimiza mahitaji ya watu wote.

Ndio nikaamua kuondoka na kwenda nchi nyingine ambayo nayo sikuijua, hata Ile niliyotoka sikuijua inaitwaje kwani nilishakuambia kuwa hatukuelewana Lugha.

Kiguu na njia, safari ya kipofu, kutafuta uzuri wa Maisha ikaendelea.
Kutembea nilitembea, uliwahi kutembea mpaka miguu naa misuli ya mapaja ikauma? Uliwahi? Vipi kama umewahi Hali yako ilikuwaje?

Yangu ilikuwa Mbaya zaidi kuliko yako, unabisha sio, nakuambia Mimi nilitembea kama ngamia mkiwa aliyetelekezwa jangwani, ningepanda Gari kama unavyofikiria lakini nauli ningeipata wapi? Nauli niliitumia kufika katika hiyo nchi niliyoitoka yenye maajabu.
Sasa nilikuwa natembea kama mtembezi wa kutafuta Mali za kale.

Nikafika nchi ya pili, ulikuwa mwendo WA siku arobaini Usiku na Mchana kufika katika Nchi Hii, Lugha yake ilikuwa kidogo inafanana na Lugha zetu. Sijasema nilikuwa naielewa Bali nilikuwa nawasikia wakiongea Kwa namna ya Sauti zetu Ila maana ndio nilikuwa siipati. Hawa walikuwa Watu wa kushangaza, wenye macho ya ugunduzi, na midomo inayotoa Sauti ya utawala.
Baada ya kutangatanga Kwa Siku kadhaa katika miji ya nchi Hii nikakutana na ajabu nyingine,
Wakati naongea na wenyeji wa nchi, mwenyeji mmoja aliponisikia nikizungumza alinishika mkono na kunikokota kama kiroba cha kokoto, mpaka kwenye kibanda cha mbao, kisha alipobisha akatoka mwanaume mmoja,, wakawa wanaongea mambo nisiyoyaelewa, lakini ni kama walikuwa wananizungumzia Mimi.
Ghafla bila taarifa nilishangaa Yule mwanaume niliyemfuata akijitambulisha Kwa Lugha yangu, jina lake aliitwa Jafa.

Nilifurahi Kupata MTU anayejua Lugha yangu, unajua Maisha yanahitaji mambo yafuatayo;
1. Wazazi watakaokuzaa, hawa watakuleta Duniani kisha kukupa miongozo na sapoti.
2. Afya ya mwili, hisia, Roho na Akili
3. Lugha
4. Shabaha(malengo na kusudi)
5. Kazi
7. Mali
6. Familia.
Kama hautapata mtu mnayeelewana basi Maisha yanaweza yakakusumbua,

Nikiwa natafuta uzuri wa Maisha nikiwa na Jafa, sikumoja nikasikia Kutoka mbali taarifa ya Msiba wangu. ATI Mimi nimekufa, unajua Yule mtangazaji wa lile tangazo sikuwa nimemwelewa, lakini Akili yangu ikaniambia labda mtu akifa ndivyo anavyokuwa haelewi kuwa amekufa.

Sasa Mimi ni Nani? Pengine ni mzimu. Nikawa najiona kama mzimu unaotembea.

Baada ya miaka mingi kupita nikiwa nimekusanya sehemu ya uzuri wa Maisha, nikagundua uzuri WA Maisha haukamiliki bila familia, na sehemu pekee ya kuipata familia ni Kwa Yule niliyekuwa nampenda Kwa dhati yote, si mwingine ni wewe kipenzi changu.

Nimerudi nyumbani, katika Nchi yangu, Kwa Mpenzi wangu, nimesikitika Sana, moyo wangu umejaa uchungu.
Mpenzi wangu kawapa wageni Milki yangu.
Sio moyo wake, sio mwili wake, sio hisia zake, sio Roho yake, sio mtoto niliyemuacha akiwa tumboni Mwake, sio Mali au Ardhi wala chochote, vyote amewapa Watu wageni.

Alichonionyesha ni Kaburi langu, Kaburi la Taikon ambaye linaonyesha nimekufa miaka mingi iliyopita, Kaburi lenyewe lipo katika shamba la muwekezaji, Kaburi lenye urefu wa futi sita Kwa sita, na upana wa futi nne.
Juu ya Kaburi langu nilikuta kibao kimeandikwa Kaburi linakodishwa.
Hii iliniambia kuwa Ardhi yote inamilikiwa na wageni na wenyeji wamekosa hata maeneo ya kuzikia.
Hivyo nchi yangu imefikia hatua mpaka ya kukodisha makaburi.

Nipeni RAMBIRAMBI zangu, Pesa zote mlizokula kwenye Msiba wangu nipeni. Najua kabisa sio Pesa yangu lakini hamuwezi kubisha kuwa waliochanga walikuwa wananipenda.
Nipeni RAMBIRAMBI zangu.

Namaliza kuandika, nazima mshumaa kunakuwa Giza.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
Kwa sasa Dar es salaam
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…