Nini kinachangia kushuka kwa ubora wa elimu nchini? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nini kinachangia kushuka kwa ubora wa elimu nchini?

Discussion in 'Jukwaa la Elimu (Education Forum)' started by kilimasera, Apr 17, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Apr 17, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  tangu mwaka jana,suala la kushuka kwa kiwango cha ubora wa elimu inaotolewa katika shule za msingi na sekondari hasa za serikali limekuwa likijadiliwa katika vinywa vya wananchi wengi na hasa wadau wa elimu walioko katika makundi mbalimbali ya kijamii nchini.
  Baadhi ya wadau wanaona kuwa ubora wa elimu inayotolewa katika shule hizo, umeshuka kiasi kwamba wahitimu wanaomaliza darasa la saba au kidato cha nne wanahitimu pasipo kuwa na ubora wa stadi za masomo wanayopaswa kuwa nao.
  Hata hivyo wadau wengi wanaona kuwa suala la ubora wa elimu kuwa umeshuka si la mjadala tena, ila mjadala uko katika kuangalia sababu zilizosababisha hali hiyo na hatua za kuchukua ili hatimaye shule zetu ziweze kutoa wahitimu wanaoweza kusoma kozi mbalimbali zinazotolewa na vyuo vya elimu ya juu.
  Septemba mwaka jana, Shirika la Uwazi,chini ya Mtandao wa Elimu Tanzania (Ten Met), ulitoa utafiti ulioonyesha kuwa kiwango cha uelewa wa wanafunzi (ubora wa elimu) katika shule za msingi ulikuwa duni kwa kulinganisha na ngazi za madarasa waliyofikia wanafunzi waliofanyiwa utafiti.
  Utafiti ulionyesha kwamba, mwanafunzi mmoja kati ya watano wanaohitimu elimu ya msingi, huwa hawezi kusoma Kiswahili cha darasa la pili, na kwamba inawezekana mhitimu huyo asijue kabisa kusoma endapo hatapata sehemu nyingine ya kusoma ,baada ya kuwa amemaliza elimu yake.
  Utafiti uligundua kuwa maendeleo katika somo la Kiingreza ni ya chini, na kwamba mpaka kufikia darasa la tano, ni mtoto mmoja tu kati ya wanne ndiye anaweza kusoma Kiingreza cha darasa la pili. Watoto wengi hufika darasa la saba bila ya kuwa na ujuzi wa somo la Kiingreza.
  Utafiti ulionyesha kwamba asilimia 49.1 ya wahitimu wa darasa la saba hawawezi kusoma Kiingereza cha darasa la pili na kwa hali hiyo ni wanafunzi wachache sana wanaoweza kusoma Kiingereza cha darasa la saba. Utafiti ulihitimisha kuwa, watoto wengi wanaoingia sekondari huwa hawana stadi ya Kiingereza,lugha ambayo ndiyo inatumika katika masomo yote yanayofundishwa huko na vyuo vya elimu ya juu isipokuwa Kiswahili.
  Kwa upande wa somo la Hisabati,utafiti ulionyesha kwamba wanafunzi watatu kati ya kumi walio darasa la saba huwa hawawezi kufanya hesabu za kuzidisha za darasa la pili na kwamba mmoja kati ya kumi wanaomaliza darasa la saba huwa hana kabisa maarifa ya somo la Hisabati.
  Maana ya hali hiyo ni kwamba watoto wengi wanaoingia sekondari huwa hawana msingi wa kutosha wa somo la Hisababti, somo ambalo ni muhimu kwenye masuala ya kujifunza na kuchanganua mambo hususani katika nyanja za sayansi, teknolojia na biashara.
  Kama hiyo haitoshi, matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana yalikuja kuthibitisha kuwepo kwa tatizo la ubora wa elimu inayotolewa katika shule zetu baada ya wahitimu wengi hasa katika shule za serikali kufeli mitihani hiyo.
  Kwa kuangalia hali hio wadau mbalimbali wanatoa sababu zinazochangia kuwepo kwa hali hiyo huku baadhi yao wakiwa wanatofautiana na wengine. Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi nchini (Tamangosco) wanasema sababu inayochangia kufeli kwa wanafunzi wengi haikutokana na kushuka kwa ubora wa elimu.
  Walizitaja sababu hizo kuwa ni kitendo cha Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) kutumia muda mfupi wa kusahihisha mitihani hiyo,baraza kuwa na bajeti finyu iliyotengewa na serikali na hasa baada ya serikali kuondoa ada za mitihani kwa wanafunzi wa shule za serikali na kitendo cha baraza kutunga mitihani kwa kutumia mitaala mipya.
  Hata hivyo afisa kutoka NECTA ilizikataa sababu zilizotolewa na Tamangosco,ikisema ilikuwa na fedha za kutosha kama bajeti ya mitihani ilivyokuwa na kuwa lile pengo linalotokana na kufutwa kwa ada za mitihani lilikuwa linafidiwa na serikali yenyewe. Aidha lilisema kwamba muda wa kusahihisha mitihani ulikuwa wa kutosha na kwa mwaka jana muda uliongezwa kwa kuwa kulikuwa na shule nyingi zilizokuwa zinatoa tolea la kidato cha nne kwa mara ya kwanza.
  Machi 23 hadi 25 Mwaka huu,mtandao wa elimu Tanzania uliandaa mdahalo wanne wa ubora wa elimu uliowashirikisha wadau mabalimbali wa elimu ndani na nje ya nchi, ambapo mada mbalimbali zilitolewa na wawakilishi wa Taasisi ya elimu Tanzania(TIE),Necta na watu toka Ten Met.
  Mkurugenzi wa Idara ya Ubunifu na uboreshaji mitaala wa (TIE) ,Angela Katabalo kwa upande wake anasema kuwa kipimo cha ubora wa elimu unahusisha mambo mengi na si matokeo ya mitihani peke yake. Alisema kwamba ubora wa elimu unajumuisha ubora wa wananfunzi wanaofundishwa, ubora wa walimu wanaowapatia taaluma na mazingira ya eneo taaluma hiyo inapotolewa.
  Aidha Katabalo anasema kwamba kuwepo kwa miundo mbinu ya kutosha ni eneo lisiloepukika kama kuna nia kweli ya kutoa elimu iliyo bora. Alitaja miundo mbinu ya vitabu vya kiada na ziada, maktaba na maabara kwa ajili ya mafunzo ya vitendo.
  Kwani anasema , ili kuiboresha elimu ,serikali inaendelea kujenga miundo mbinu inayotakiwa na kufundisha walimu walio bora kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
  Kwa upande wake, Mary Soko,Afisa wa programu ya elimu ya msingi wa Oxfam GB Tanzania aliongelea suala la vikwazo vinavyowakabili walimu vilivyo nje ya uwezo wao kama moja ya sababu zinazosababisha kushuka kwa ubora wa elimu. Anavitaja vikwazo hivyo kuwa ni mazingira ya darasa, shule na mazingira ya muundo.
  Ambapo anasema mazingira ya darasa yanajumuisha ukubwa wa darasa, rasilimali za kufundishia kama vitabu,menejimenti ya darasa na vivutio anavyopewa mwalimu. Alisema matokeo ya ukubwa wa darasa yanaweza kuonekana kwenye mahusiano ya mwalimu na mwanafunzi.
  Kwa upande wa mazingira ya shule anasema kwamba ni muhimu shule ikaeleweka kama kitega uchumi kinachozalisha mapato ya baadaye kwa watu. Hivyo ni muhimu watu wakaelewa shule si majengo na watu waliomo ndani yake, bali ni mfumo wa shule unaojumuisha mahusiano, Idadi ya wanafunzi na kiwango cha maarifa na ujuzi wa walimu
  Suala la mazingira ya muundo yanaletwa na suala la mgao na mahitaji ya walimu ambayo hutofautiana kati ya nchi na nchi. Katika hali hiyo basi tatizo la mgao haliletwi na wingi wa wanafunzi peke yake lakini pia mambo ya vivutio vya taaluma ya ualimu kwa kilinganisha na zingine.Alisema kwa mfano walimu wengi wako mjini kuliko vijijini,
  Soko anasema kuwa wao walishafanya utafiti juu ya vikwazo hivi kwa kuongea na baadhi ya walimu, ambapo baadhi ya walimu katika utafiti huo walionyesha ugumu uliopo katika kumfukia kila mwanafunzi hasa darasa linapokuwa kubwa.
  "Si rahisi kupanga njia ya ufundishaji itakayoweza kumfika kila mwanafuzi kwenye darasa la watu wengi.Mfano kutengeneza makundi ni njia isiyo na matunda kwa darasa lenye watu wengi.Na hata nikitengeneza makundi, yatakuwa ya wanafunzi wengi kuweza kuhusiana.Na hata nikiweka makundi ya watu watano watano sitaweza kuwafikia wote ndani ya dakika 40 za kipindi" hayo ni baadhi ya maelezo ya walimu aliofanya nao utafiti ambapo mwalimu aliyetoa maelezo hayo alikuwa na darasa la mwanafunzi 88.
  Wakati mwalimu mwingine aliyehusika pia kwenye utafiti ambapo Soko anamtaja kwa jina moja tu la mwalimu Tabu aliyekuwa na wanafunzi 83 anasema kuwa :
  "Kikwazo cha ukosefu wa vifaa vya kufundishia na hasa vitabu unaathiri ujuzi wa kufikiri ,ujuzi wa msingi wa kujifiunza wa wanafunzi na utamaduni wa kufanya mazoezi. Wanafunzi wanakosa fursa ya kuwa na vitabu na matokeo yake ni kuwa wategemezi wa notisi wanazopewa na walimu siku zote, na wakizikosa wanakuwa hawana kitu kichwani na mtihani ukija lazima wafeli" alisema.
  Hivyo Soko anasema kwamba ili kuongeza tija katika utoaji wa elimu, nmkazo utiliwe kwanza kwa kuwawendeleza walimu ili wafikie ubora unaotakiwa kwa kuwapa mafunzo wakiwa kazini kupitia semina na kozi fupifupi.Lakini pia wawape fursa ya kujiendeleza zaidi ili wapate shahada na stashada ili wayamiliki masomo yao kwa ufanisi.
  Hata hivyo anasisitiza juu ya umuhimu wa kuboresha miundo mbinu ya majengo ili darasa liwe na idadi ya wanafunzi ambao mwalimu atawamudu, watoe vitabu kwa ajili ya walimu na wanafunzi na kujenga maktaba na maabara.Aidha alihimiza wazazi kama wadau muhimu kufuatilia watoto wao ili kuona wanachofundishwa shuleni.
   
 2. K

  Kitefure New Member

  #2
  Apr 18, 2011
  Joined: Apr 17, 2011
  Messages: 3
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Mawazo mazuri. Kuna na hii paper ingine ukiwa na muda uisome. Jamaa naye kachambua elimu ya Tanzania kweli.Anaulzia maana na shule za YeboYebo, yaani shule za serikali zilizoanzishwa holela. It is a very interesting kwakweli

  Struggle to Regain Glory in Education: A Lasting Solution or just a Relentless Skirmish of a Drowning Person?
  Link:
  https://www.jamiiforums.com/internati...ss-skirmi.html
   
Loading...