Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,284
Kumekucha ni salama, ahsante mungu wangu,
Japo dede nasimama, na tete hatua zangu,
Nina kuomba Karima, nifike safari yangu
Nimezama fikirani, nawaza mie nawaza.
Jana sikupe hasira, leo sipate karaha,
Tena sifanye harara, kesho upate furaha,
Kiumbe fanya subira, kama wazitaka raha.
Nimezama fikirani, nawaza mie nawaza.
Aliyeumba kinyonga, ndiye kaumba farasi,
Lumbwi siwezi jinyonga, kulilia kwenda kasi,
Karima ndiye hupanga, ndogo nyingi na kiasi,
Nimezama fikirani, nawaza mie nawaza.
Namtazama jongoo, kunako miguu yake,
Ilivyo kama pongoo, ajabu ni mwendo wake
Kamzidi kangaroo, lakini si mbio zake,
Nimezama fikirani, nawaza mie nawaza.
Sijaona uwaridi, lisilo kuwa na miba,
Ama jambo maridadi, baya liwate kubeba,
Jua kuna kujirudi, ndio ikawepo toba,
Nimezama fikirani, nawaza mie nawaza.
Mja usiwe bahili, pia usifanye ria,
Ila sianguke chali, asama kusaidia,
Moyo usizidi hali, Mola alokujalia,
Nimezama fikirani, nawaza mie nawaza.
Kaditama namaliza, hapa natia kikomo,
Shika nilo yawaza, huenda tapata somo,
Kuuliza unaweza, zingatia yaliyomo,
Nimezama fikirani, nawaza mie nawaza.
Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
Whatspp/call 0622845394 Morogoro