Nimechoka na vya ofisini na ruzuku.. | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nimechoka na vya ofisini na ruzuku..

Discussion in 'Jukwaa la Lugha' started by Sooth, Jul 12, 2011.

 1. Sooth

  Sooth JF-Expert Member

  #1
  Jul 12, 2011
  Joined: Apr 27, 2009
  Messages: 3,773
  Likes Received: 4,491
  Trophy Points: 280
  1. Kauli zao asali, bado kushika utamu,
  Kama kifaru wakali, wakishashika hatamu
  Taanguka chini chali, wakati wao karamu,
  Nimechoka na vya ofisini na ruzuku, nasubiri vya porini

  2.Tamaa yao ni raha, si kwa umma utumishi,
  Raia hana furaha, wao ofisi ubishi,
  Maskini ana karaha, huduma mpaka bakshishi
  Nimechoka na vya ofisini na ruzuku, nasubiri vya porini

  3. Wakionjeshwa ruzuku, subiri yao mateke,
  Usoni wanajishuku, hawaji tena Makete,
  Sisi zuzu zumbukuku, acha sana watucheke,
  Nimechoka na vya ofisini na ruzuku, nasubiri vya porini

  4. Vyama sasa kama shamba, binafsi mtu anacho,
  Tayari kufunga kamba, kila asiye na macho,
  Raia ni kama famba, wanabeba watakacho,
  Nimechoka na vya ofisini na ruzuku, nasubiri vya porini

  5. Wa Vunjo anamiliki, ni mrema kashika mpini,
  Ana mikiki mikiki, chafua watu makini,
  Dovutwa shika mkuki, tayari kula maini,
  Nimechoka na vya ofisini na ruzuku, nasubiri vya porini

  6. Kila leo nazozana, keki yetu wagawane,
  Wanachama hukinzana, ruka ruka ka senene
  Baadae hupozana, gawia vyeo vinene
  Nimechoka na vya ofisini na ruzuku, nasubiri vya porini

  7. Vyama kama mama kuku, hanyonyeshi mpaka kesho,
  Tumaini letu kuu, limekuwa kichekesho,
  Sikio kama kifuu, moyo wao wa korosho,
  Nimechoka na vya ofisini na ruzuku, nasubiri vya porini

  8. Vinachipua kwa nguvu, kufa kwake kwa vurugu,
  Tunabaki na mafuvu, fikra zao za ukungu,
  Kwa umbea vimefuzu, wengine wana majungu,
  Nimechoka na vya ofisini na ruzuku, nasubiri vya porini

  9. Vya ofisini meshindwa, tusubiri vya porini,
  Hawa sio wa kufundwa, uroho wamesheheni,
  Wanataka kudundwa, yaingie akilini,
  Nimechoka na vya ofisini na ruzuku, nasubiri vya porini

  10. Vya porini ni mikono, midomo haihusiki,
  Ni mageuzi ya mfano, uongo hausikiki,
  Wasaliti kwenye mbano, banikwa kama samaki,
  Nimechoka na vya ofisini na ruzuku, nasubiri vya porini
   
Loading...